Monday, October 30, 2023

PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP) YAMEWEZESHA TAFITI ZA TEKNOLOJIA YA KISASA ZA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI.


 

Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi (AFDP) imewezesha Tafiti za Kiteknolijia kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) katika kuzalisha mbegu za kisasa zenye uwezo wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibi) Mhe. Ummy Nderianaga wakati wa wasilisho la Taarifa ya Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Bungeni Dodoma.

Akitolea mfano aina ya mbegu sita za mahindi ikiwa ni Pamoja na Situka M1, TMV1, STAHA, Bora, T104 na T105, kuwa zikipandwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo zinapelekea kuleta matokeao bora na Tafiti zinaonesha kuwa mbegu hizi zina uwezo mkubwa wa ustahimilivu dhidi ya changamoto mbalimbali za mabadiliko tabianchi.

Akiongelea suala la usalama wa chakula, Naibu Waziri Nderianaga alisema kuwa suala hili linakwenda sambamba na kipengele cha Usalama wa mbengu. “tulimaliza hivi punde mkutano wa Chakula Afrika na Tanzania imeonekana kuwa ni kitovu kwenye suala la chakula hivyo kama hatutakuwa na mbegu Bora na nzuri kufikia malengo itakuwa ni kazi.” Alibainisha

Kwa upande Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Salimu Mwinjaka, alisema katika sekta ya Kilimo, Programu hii ya kimkakati inalenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima, na jitihada kubwa ni kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua sambamba na kuihamasisha jamii ya wakulima, umuhimu wa kutumia mbegu bora katika kuleta tija na mageuzi ya kilimo.

Akiongoza kikao hicho, Kaimu Mwenyetiki wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo Alisema “Tumeona mikakati Mizuri ya Serikali ambayo imewekwa hasa katika suala la mbegu, hii ni kuhakikisha kwamba suala zima la uzalishwaji wa mbegu bora na kwa wakati linafanikiwa.”

Akiongea katika kikao hicho, Mhe. Boniphace Nyangindu Butondo (Mjumbe wa kamati) alishauri Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) kuwa na mkakati wa kuzalisha mbegu zenye tija za kutosha na kuangalia mbegu za mazao mengine kama vile Mtama, Mpunga na Pamba na kuzalisha mbegu za kutosha za Asili ili kuweza kukabiliana na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea kwani mbegu nyingi za kisasa zinaonesha kushambuliwa na wadudu mbalimbali.

 Kwa Upande wake Mhe. Dkt. Alice Kaijage (Mjumbe wa Kamati) Alishauri Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) kuongeza uwanda wa Tafiti hususani katika zao la Alizeti, kama linaweza kustawi bila tatizo katika mikoa mingine tofauti na Singida, akitolea mfano Mkoa wa Pwani.

Awali akiongelea suala la Mbegu la Asili, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) Dkt. Sophia Kashenge Kilenga, Alisema kuna nasaba nyingi sana ya benki ya Mbegu za asili Mkoani Arusha,”Ni kweli kabisa Mbegu za Asili zina sifa ambazo kila mtu anahitaji, na zina nasaba nyingi mchanganyiko zinazopelekea ukuaji wa mbegu kwenda polepole na una mipaka, hivyo kwa ukuaji wa sasa wa idadi ya watu ni vyema kuwa na maeneo maalum ambayo mbegu za asili zitatumika na kwa kulisha idadi kubwa ya watu ni vizuri kutumika kwa mbegu zinazozaa kwa wingi katika eneo dogo.

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.