Tuesday, June 27, 2023

MUONGOZO WA UTEKELEZAJI WA DHANA YA AFYA MOJA WAJADILIWA

Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Mololo Noah  akiongoza kikao cha Kuthibitisha Muongozo wa Utekelezaji wa  dhana ya Afya Moja. Kikao hiki kilihusisha washiriki kutoka sekta ya Afya, Mifugo, Mazingira, Wanyamapori, BAKITA na mashirika ya Umoja wa Kimataifa. Kikao kilifanyika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya regency  Mkoani Singida

Read More

Saturday, June 24, 2023

KATIBU MKUU DKT. YONAZI AHIMIZA WATUMISHI KUWA NA TABIA YA KUPIMA AFYA .

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu amewakumbusha  watumishi wa ofisi yake kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuyafikia malengo ya Serikali.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao chake na watumishi wa ofisi hiyo kilichofanyika Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma.

Katibu Mkuu huyo amesema upo umuhimu wa kujizoeza kupima afya hususan kwa magonjwa sugu yasiyoambuiza kwani yameendelea kuwa changamoto hasa kwa watu wenye umri mkubwa.

“Ni muhimu tumepata fursa ya kukumbushwa kupima afya zetu, hii ni changamoto inayotukabili, hivyo ni muhimu kuzingatia ushauri wa afya na masharti ya namna ya kuboresha masuala yanayohusu afya zetu, “alisema Dkt. Yonazi

Pamoja na hilo aliwakumbusha watumishi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuendelea kutekeleza majukumu wakiwa wenye afya na kuwa na matokeo chanya.

Aidha aliutumia mkutano huo kuwaasa watumishi hao kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Mkutano huu ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo tulianza kuiadhimisha tarehe 16 Juni, 2023 na leo ndio kilele.Wiki hii tunaitumia kutafakari namna tunavyotekeleza majukumu yetu kwa kipindi kilichopita, kujadili namna ya kutoa huduma bora kwa jamii ya Watanzania, kujifunza mbinu mpya na kuibua changamoto zinazotukabili katika kutekeleza majukumu yetu kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi,”alisisitiza

Pia aliwahimiza Watumishi kuendela kufanya kazi kwa upendo na kuheshimiana kwani kwa kufanya hivyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani.

“Ni falsafa yangu kuona watu ninaowaongoza wanafanya kazi kwa upendo na kushirikiana, ni lazima kuhusiana na kuwa na mashirikiano mazuri, napenda kufanya kazi na watu wanaoheshimiana na wenye amani siamini kama mtu anaweza akafiri vizuri iwapo hana amani ndani”alisisitiza Dkt. Yonazi

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti ya TUGHE wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Numpe Mwambenja alipongeza uwepo wa mkutano huo huku akieleza kuwa ni nyenzo muhimu kwa kuongeza motisha kwa watumishi wa umma, na imeonesha kujali na kuendelea kuleta umoja kazini.

“Mkutano huu umekuja wakati sahihi na muda sahihi, tunawapongeza viongozi wetu kuendelea kutuweka pamoja na kutukumbusha kupendana, kushirikiana na kuishi kwa amani, hili tumelithamini sana na tunaahidi hatuta waangusha tutachapa kazi na kuendele kuhudumia jamii ya Watanzania na kuitumikia nchi yetu kwa ujumla,”alisema Numpe.

 

Read More

Tuesday, June 13, 2023

MEJA JENERALI MBUGE “TUIMARISHE USHIRIKIANO KUKABILI MAJANGA”

 


Serikali  kupitia  Ofisi  ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.

Kauli hiyo imetolewa   Mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge  wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.

Meja Jenerali Mbuge amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwingiliano wa binadamu, wanyama na mazingira ambao  husababisha  kutokea kwa magonjwa mbalimbali yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya   kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana  na majanga hayo.

“Tunahuisha mwongozo huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usimamizi wa Maafa.   Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa husisitiza yakiwemo  Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO),  Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta mbalimbali ili  kuwa na mikakati na sera za  pamoja katika kuimarisha afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.

“Ili kutekeleza dhana ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na utendaji katika ngazi zote. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki utauhuishwa na kutafsiriwa,” Ameeleza.

Aidha amebainisha kuwa   Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina  wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya  Afya Moja kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja 2022-2027.

Read More