Sunday, December 31, 2017

WAZIRI MKUU ATOA KADI ZA CHF KWA WAZEE 4,000

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kumudu gharama za matibabu bila kulazimika kuwa fedha taslimu.

Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Ruangwa na vijiji vya jirani katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CWT, mjini Ruangwa, mkoani Lindi.

“Leo hii nimetoa kadi za CHF kwa wazee 4,000 wa wilaya hii. Ninaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutenga fedha na kuwalipia wazee hawa ili wanufaike na bima hii ya afya kama ambavyo imeelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.”

“Ninatoa wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao; yaani mhusika, mwenza wake na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama huna fedha taslimu,” alisema.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi kwa Mzee Issa Juma Ngalapa, mkazi wa kata ya Nachingwea pamoja na Mzee Suleiman Stola Lihepa wa kijiji cha Kilimahewa, kata ya Nachingwea kwa niaba ya wazee wote waliotakiwa kupatiwa kadi hizo.

Akitoa ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Andrea Chezue alisema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya kwa wazee wameuita ‘CHF Endelevu’ kwa sababu walifanya tathmini na kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, dawa zitaisha au wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.

“Katika Halmashauri tulifanya utambuzi wa wazee wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwenye vijiji vyote na kubaini kuwa kuna wazee 4,000. Tukaamua Halmashauri iwalipie sh. 15,000 kwa kila wazee sita kama ilivyo katika kaya ili tuweze kuchangia gharama za matibabu yao,” alisema.

“Mzee akipatiwa kadi hii, inakuwa ni ya kudumu, anaitumia miaka yote. Si ya kulipia kila mwaka kama zilivyo zile nyingine. Hadi sasa tumeshatoa kadi kwa wazee 2,700 na tunaendelea kutengeza kadi hadi tukamilishe zote. Tumepanga kuwa kila mwaka, tutafanya utambuzi wa wazee katika vijiji vyote ili wale wanaofikisha umri huo, nao pia waingizwe kwenye mpango huu,” alisema.

Read More

MAPATO YA KOROSHO YAFIKIA TRILIONI 1.08 HADI SASA

MAPATO kutokana na mauzo ya korosho katika msimu wa 2017/2018 katika mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma yamepanda na kufikia sh. trilioni 1.08 ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Bw. Hassan Jarufu alitoa taarifa hiyo jana jioni (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akitoa ufafanuzi juu ya uzalishaji na mauzo ya zao la korosho nchini hadi kufikia mwisho wa mwaka 2017.

“Ukiangalia msimu wa mwaka 2015/2016, utaona kuwa korosho zilizozalishwa zilikuwa kidogo zaidi. Msimu huo ziliuzwa kilo 155,244,645 zikiwa na thamani ya sh. 388,474,530,906.00 ikilinganisha na msimu wa 2016/2017 ambapo jumla ya kilo 265,237,845.00 ziliuzwa zikiwa na thamani ya sh. 871,462,989,284.00,” alisema.

Alisema katika minada 10 ya msimu wa 2017/2018, mauzo ya korosho yamefikia kilo 285,828,205 zenye thamani ya sh. 1,082,200,383,581.00. “Mnada wa 10 ulikuwa tarehe 21 Desemba, 2017 na minada bado inaendelea kwa msimu wa 2017/2018,” alisema.

Akitoa ufafanuzi wa mauzo hayo kwa kila mikoa hadi kufikia mnada wa 10, Bw. Jarufu alisema Mkoa wa Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya sh. 701,674,466,366.00 ukifuatiwa na mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye thamani ya sh. 247,163,294,296.00.

“Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya sh. 76,173,400,063.00 na mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya sh. 57,189,224,856.00 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia sh. trilioni 1.082,” alisema.

Bw. Jarufu alitoa ufafanuzi huo mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

Bw. Jarufu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za wilaya,imeendelea kutekeleza mpango wa miaka mitatu wa kupanda  mikorosho 10,000,000 kila mwaka.

Katika mpango huu, wastani wa mikorosho 5,000 inatarajiwa kupandwa katika kila kijiji au mikorosho 30 kwa kaya kwa mwaka, sawa na ekari 330,000 kwa mwaka kwa nchi mzima. Lengo la mpango huu ni kuongeza kiasi cha korosho kinachozalishwa nchini kwa kuongeza wigo wa halmashauri zinazozalisha korosho na kupanda miche inayotokana na mbegu bora zenye uzalishaji mkubwa na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu,” alisema.

Alisema katika msimu wa 2017/2018, Bodi ya korosho inaratibu uzalishaji wa jumla ya miche 14,001,820 ambayo imetokana na tani 100 (kilo100, 000) zilizozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele.

“Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: kilo 31,170 za mbegu zitapandwa shambani moja kwa moja ambazo zitatoa jumla ya miche 2,181,900; kilo 68,830 zitazalisha jumla ya miche 11,819,920 kati ya miche hiyo isiyobebeshwa ni 9,636,200 na miche itakayobebeshwa ni 2,183,720.

“Ni matumaini yetu kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2018, miche yote itakuwa tayari imezalishwa, kugawanywa na kupandwa katika mashamba ya wakulima,” aliongeza. 

Mkurugenzi huyo alisema, katika msimu huu eneo la utekelezaji wa mradi limeongezeka kutoka Halmashauri 51 za msimu uliopita 2016/2017 hadi kufikia Halmashauri 90 nchi nzima  ikiwemo mikoa mipya iliyothibitishwa kustawi zao la korosho hapa nchini.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.
Read More

VIJANA JITOKEZENI MLIME KOROSHO - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu lina fursa nyingi.

“Mahitaji ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika mahotelini na kwenye mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa,” alisema.

Ametoa wito huo jana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

Waziri Mkuu alisema anaamini kuwa kijana yoyote mwenye nguvu ya kufanya kazi hawezi kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa. “Kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche 37 hadi 40. Kuna mtu atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” aliuliza.

Waziri Mkuu alisema kilimo cha korosho ni rahisi lakini pia kilimo cha korosho ni rafiki wa mazingira, kwani miti ikikua inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua. Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya Lindi, Mtwara, Ruvuma Pwani na Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika kuwa zao hilo linaweza kustawi bila shida.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.

“Leo tumeanza usambazaji wa miche ya bure hapa Ruangwa ambao najua utafuatiwa na wilaya nyingine hapa nchini. Nimeelezwa kwamba mche wenye kutoa mazao mengi ni wa kuanzia miaka mitatu hadi saba, kwa umri huu miche ya korosho inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama ambavyo mtashauriwa na maafisa kilimo ili wakati wa palizi ya hayo mazao, shamba lako la korosho libakie kuwa safi,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake. 
Mapema, akitoa taarifa ya taarifa ya uzalishaji wa miche ya mikorosho msimu wa 2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. Ramadhani Kaswa alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo uliweka lengo la kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.

“Hadi mwisho wa msimu huu, jumla miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima sawa na asilimia 71.6 ya lengo lililowekwa. Kati ya hiyo, Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri ya Lindi miche 100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale miche 106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya Ruangwa miche 177,862,” alisema.

“Miche hii iligawanywa kwa wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao. Zoezi la tathmini ya miche iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye halmashauri zote za mkoa,” aliongeza.

Bw. Kaswa alisema kutofikiwa kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa, na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.

Alisema kwa msimu huu wa 2017/2018, mkoa uliweka lengo la kuzalisha miche ya mikorosho iliyobebeshwa na isiyobebeshwa 7,132,000. Kati ya hiyo, Wilaya ya Kilwa walilenga miche 1,122,000, Lindi Vijijini 1,550,000, manispaa ya Lindi 1,000,000, Liwale miche 450,000, Nachingwea miche 1,810,000 na Ruangwa miche 1,200,000.

“Hadi kufikia tarehe 29 Desemba, 2017 tayari miche 4,974,425 ilikuwa imezalishwa na iko tayari kwa kupandwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa kama ifuatavyo:- Kilwa miche 772,000, Lindi Vijijini 1,160,455, manispaa ya Lindi 771,440, Liwale miche 266,000, Nachingwea 991,070 na halmashuri ya Ruangwa imezalisha miche 1,013,460,” alisema.

Sherehe hizo za uzinduzi wa upandaji miche mipya zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.
Read More

TAFUTENI TAKWIMU MPYA, WAZIRI MKUU AAGIZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Kilimo kutoka mikoa inayolima korosho, washirikiane kupata takwimu mpya za wakulima wa zao hilo.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi.

“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mkisimamiwa na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, mshirikiane na kusimamia kwa umakini upatikanaji wa takwimu za wakulima na maeneo yanayolimwa, haiwezekani kila mwaka takwimu ziwe ni zilezile tu,” alisema.

“Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je hao wakulima wako, kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana miche mingapi, na je ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alisema.

“Pia nilikwishawaagiza maafisa ushirika na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) mpaka chama kikuu cha ushirika, kuwa kila mmoja anapaswa atambue ana wanachama wangapi katika chama chake. Hili litawezekana pia kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata au Mwenyekiti wa Kijiji, kwa sababu wao wana idadi kamili za watu wanaowaongoza,” alisema.

“Ninaamini tukifanya hilo tutamaliza tatizo la takwimu na Serikali itakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wakulima wake, na tutaweza kuweka bajeti ya kutosha kuhudumia mahitaji yao,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alipanda mche mpya wa korosho ili kuanzisha zoezi la upandaji miche hiyo na kisha akagawa miche kwa wakulima 10 kutoka vijiji vya Likunja, Kitandi, Kilimahewa na Nachingwea ambao waliwawakilisha wenzao.

Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikagua vitalu vya miche ya mikorosho vilivyopandwa na Halmashauri ya Ruangwa na kuelezwa kuwa miche hiyo ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile iliyotokana na mbegu na ya pili ni ile iliyotokana na vikonyo (grafting).

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki zoezi hilo.

Read More

WAZIRI MKUU AMWAGIZA AFISA MADINI AITISHE KIKAO KESHO SAA 4 ASUBUHI

*Ni baada ya kupokea mabango ya wananchi wakidai kunyanyaswa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha wananchi kesho (Jumapili) saa 4 asubuhi.

“Sasa hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho saa 4 asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.

“Hawa ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.

Baada ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.

Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila wanapokutana na viongozi hao.

“Tunanyanyaswa na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.

Alidai hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.

Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.

“Hapa pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,” alisema.

Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba yoyote.

“Yale ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.


Read More

Saturday, December 30, 2017

DC RUANGWA MTAFUTIE JENGO AFISA MADINI AKAE HAPA - WAZIRI MKUU

*Asema ni gharama kutoka Nachingwea kila mara
*Asema migodi mingi iko Ruangwa kuliko Liwale, Nachingwea

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Joseph Mkirikiti atafute jengo haraka kwa ajili ya ofisi ya madini wilayani humo.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017) baada ya kubaini kuwa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale anaishi Nachingwea lakini anahudumia wilaya tatu za Ruangwa, Liwale na Nachingwea yenyewe.

Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo. Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi baada ya kukagua migodi ya wachimbaji wadogo iliyopo kijijini hapo.

“Sisemi ahamie hapa kwa sababu ni nyumbani, hapana. Ni kwa sababu najua ofisi yake iko Nachingwea lakini shughuli nyingi za madini ziko Ruangwa kuliko Liwale na Nachingwea,” alisema.

“Haiwezekani uwe kule, halafu uwahudumie huku wananchi walio wengi. DC mpe ofisi akae hapa, apite maeneo mengi ya huku na kuwasikiliza wachimbaji wadogo ambao ni wengi zaidi. Kule mashimo ni moja moja, ataenda mara moja kwa wiki. Kuanzia sasa, atakuwa Ruangwa ili afanye kazi kwa karibu zaidi na kundi kubwa la wachimbaji wadogo,” alisema.

Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alitembelea mgodi wa dhahabu wa Namungo na kukagua shughuli za uzalishaji pamoja na mitambo inayotumiwa kwenye uchenjuaji wa mchanga wa dhahabu.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Meneja Mitambo ya Uchenjuaji (Processing Plant) wa kampuni ya Gemini inayomiliki mgodi huo, Bw. Emmanuel James alisema kwa sasa wamesimamisha mitambo kwa sababu wanakabiliwa na tatizo la umeme mdogo licha ya kuwa wameweka umeme wa njia tatu.

“Umeme upo wa njia tatu lakini tatizo hautoshi, pia transfoma iliyopo ni ndogo na haihimili umeme wa mgodini,” alisema.

Alipoulizwa wametoa ajira kwa watu wangapi, Bw. James alijibu kuwa wametoa ajira zaidi ya 200, ambapo kati ya hizo, ajira 40 ni za moja kwa moja.

Naye Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Tale alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna mashimo zaidi ya 120 yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo hilo  lakini mashimo 47 yanaendelea na uzalishaji na mengine 32 yalifungwa ama kwa sababu za kiusalama ama kwa kuwa yamekamilisha kazi yake na hayana faida tena.


Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji miche bora na mipya milioni 10.
Read More

WAPINZANI WENGINE 19 WAREJEA CCM RUANGWA

*Wamo 13 kutoka ngome kuu ya CUF Matambarare

WANACHAMA 19 kutoka vyama vya upinzani katika kata za Matambarare na Mnacho wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wamekabidhi kadi zao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).     

Wanachama hao kutoka vyama vya CUF na CHADEMA, walikabidhi kadi zao kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana jioni (Jumamosi, Desemba 30, 2017) wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Matambarare Kusini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.

Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo.

Akiwa katika kijiji cha Matambare Kusini, Waziri Mkuu alipokea wanachama 17 ambao kati yao 13 wanatoka Chama cha Wananchi (CUF) na wanne wanatoka Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA).

Akiwa katika kijiji cha Ng’au kata ya Mnacho, wilayani humo, Waziri Mkuu alipokea wanachama wawili, Bw. Swibert Mwambe kutoka CUF na Bw. Paskali Rogert wa CHADEMA.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake 17, Mzee Said Bakari Makungwa (maarufu kama Ustaadh Makungwa) alisema alikuwa muasisi wa chama cha TANU pamoja na CCM mwaka 1977 kilipozaliwa, na alishika nyadhifa mbalimbali hadi alipoamua kuondoka.

“Jamani nimerudi nyumbani, na mtu akirudi nyumbani huwa haadhibiwi,” alisema Ustaadh Makungwa mwenye umri wa miaka 80 na kuamsha kicheko kwenye mkutano huo.

Alisema yeye anataka kuwakumbusha wananchi waliohudhuria mkutano mambo manne aliyoyasisitiza Baba wa Taifa, hayati Mwl. Julius K. Nyerere ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Kuhusu ardhi, alisema wanaRuangwa wamepewa ardhi na Mwenyezi Mungu ili iwape mazao na madini. “Watu ni sisi ambao tunapaswa tutumie vema rasilmali tuliyopewa katika ardhi,” alisema.
Kuhusu siasa safi, Ustaadh Makungwa alisema: “Kuna siasa safi gani zaidi ya hii tuliyonayo sasa? Utaitafuta wapi zaidi ya kwa Mheshimiwa Magufuli? Safari hii, kafikisha bei ya korosho hadi sh. 4,045 kwa kilo moja. Nani kama Magufuli?” alihoji Mzee Makungwa.

Kuhusu uongozi bora, Mzee Makungwa alisema Mheshimiwa Magufuli ameonyesha njia akisaidiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. “Kazi ya viongozi ni kuonyesha njia. Sasa wewe kugeuka kushoto au kulia unatafuta nini?” alihoji.

“Hebu niambieni Ruangwa ya juzi na ya leo ziko sawa?,” alijohi na kujibiwa kwamba haziko sawa. “Mimi nimerudi nyumbani, ninaomba msamaha pale nilipowaudhi. Kwa sababu ya umri wangu, ninaijua vema historia ya CCM, njooni kwangu mchukue historia ya chama,” alisema huku akishangiliwa.


Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji miche bora na mipya.
Read More

Friday, December 29, 2017

WAZIRI MKUU AWAPOKEA WANACHAMA 60 WA CUF


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama wapya 60 kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wanachama hao wamepokelewa leo mchana (Ijumaa, Desemba 29, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Nkowe kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Kabla ya kuwakabidhi kadi za CCM, Waziri Mkuu alipokea kadi za CUF kutoka kwa vijana saba kwa niaba ya wenzao 60. Vijana hao ni Hamisi Juma, Fatuma Abdallah, Mwajuma Mohammed, Thomas Moto, Zainab Nachiluku, Samia Said na Juma Said.

Vijana hao saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM pamoja na wenzao 53, walikula kiapo cha uaminifu.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau wanachama wote ni vijana ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali na wameridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano.

Bw. Essau alisema wanachama hao wote wametoka vijiji vya Kipindimbi, Nkowe na Mpumbe.

Novemba 5, mwaka huu, Waziri Mkuu alipokea wanachama 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa.

Read More

WAZIRI MKUU AKIWA RUANGWA

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akiwa na mganga mkuu wa kituo cha afya Nkowe Dk. Paul Mbinga,wakati akikagua ujenzi wa nyumba ya daktari, Waziri Mkuu yupo Wilayani Ruangwa kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka ambapo aliamua kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake. Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akipewa maelezo ya ujenzi wa maabara katika kituo cha afya Nkowe na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ruangwa, Waziri Mkuu yupo Wilayani Ruangwa kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka ambapo aliamua kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake. Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Nkowe,baada ya kutembelea na kukagua kituo cha afya Nkowe Wilayani Ruangwa,. Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akipokea wanachama wapya 60 wa Kata ya Nkowe Wilayani Ruangwa, kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM). Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akisalimiana na Sister Nelly Membe wa Shirika la Bikira Maria Msaada wa Wakristu la Ndanda,katika Kata ya Nkowe Wilayani Ruangwa, Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akifungua Tawi la vijana wakereketwa wa CCM la Majaliwa Camp,katika Kata ya Nkowe Wilayani Ruangwa, Desemba 29, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Nkowe,baada ya kutembelea na kukagua kituo cha afya Nkowe Wilayani Ruangwa,. Desemba 29, 2017.

Read More

Thursday, December 28, 2017

HARAKISHENI UMEME KUKAMILISHA MRADI WA MAJI NAMAHEMA ‘A’ - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Meneja wa TANESCO wilaya ya Ruangwa, Bw. Samuel Pyuza ahakikishe umeme unapatikana mapema kwenye pampu ya maji ili kukamilisha mradi wa maji wa Namahema ‘A’.

Ametoa wito huo jana jioni (Alhamisi, Desemba 28, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Namahema ‘A’ na Namahema ‘B’ wilayani Ruangwa, mkoani Lindi waliofika kumsikiliza mara baada ya kukagua mradi wa maji ambao umechukua miezi sita tangu uanze. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Januari 15, mwakani.

Mradi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu sh. milioni 244.52, unatarajiwa kuwahudumia wakazi 2,257 wa vijiji hivyo viwili ambao walikuwa wanasongamana kupata maji kutoka kwenye kisima ambacho kilikuwa kinatumia pampu ya mkono. Kijiji cha Namahema ‘A’ kina watu 1,668 na Namahema ‘B’ kina watu 589.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Jumla ya sh. milioni 189.93 zimeshatumika kwenye mradi huo ambazo ni sawa na asilimia 77.68 ya fedha ziliopangwa kutumika. Fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Maji wa Taifa (National Water Investment Fund).

Kazi ambazo zimekamilika hadi sasa ni ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DP) 32; ujenzi wa mtandao wa mabomba yenye urefu wa mita 6,460; tenki la kuhifadhia maji leye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house); ujenzi wa uzio (fence) kwenye nyumba ya mitambo; ujenzi wa uzio (fence) kwenye tenki la kuhifadhia maji; na ununuzi wa pampu na mota.

Read More

RUANGWA LEO 28/12/2017

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea, kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka ambapo aliamua kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Desemba 28, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mwananchi wa kijiji cha Mibure, Mzee Menrad Kilian, baada ya kukagua ujenzi wa zahanati kijijini hapo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Desemba 28, 2017.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mibure, wakati alipoenda kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho Desemba 28, 2017. Waziri Mkuu yupo jimboni kwake kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa KALIF Construction, Ally Mohamed Libaba akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) wakati wakijaribu kuvuta maji kutoka kwenye pampu ya mradi wa maji wa kijiji cha Namakuku, Desemba 28, 2017. Wa kwanza kulia ni msimamizi wa mradi huo, Bw. Fadhil Ally Libaba.

Read More

Wednesday, December 27, 2017

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora akifurahia maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Geoffrey Kirenga wakati alipotembelea shamba la mahindi la Kiwanda cha Kuzalisha Viranga na chakula cha Kuku, Silverlands mkoani Iringa, wengine ni Mkurugenzi wa Mashamba na Mifugo Kiwanda cha,  Rob Nethersole na Mratibu wa SAGCOT Ofisi ya Waziri Mkuu, Girson Ntimba.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha uendelezaji kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga wakati alipotembelea  shamba la mahindi la Kiwanda cha Kuzalisha Viranga na chakula cha Kuku, Silverlands mkoani Iringa.Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa, Asas Diary Milk, Fuad Faraj, wakati alipofanya ziara mkoani Iringa, kukagua viwanda vinavyofanya kazi na Kongani ya Ihemi inayotekelezwa na Mpango wa uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Sehemu ya mitambo ya Kiwanda cha Kuzalisha Viranga na chakula cha Kuku, Silverlands mkoani Iringa, kiwanda hicho kinahitaji tani 7,000 za Soya kwa siku kwa ajili ya uzalishaji lakini hadi sasa wanapata tani 2,000 kwa siku  hivyo kupelekea kiasi kingine kuagizwa kutoka nje ya nchi. Mpango wa uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari umeanza kuboresha mazingira ya uwekezaji ili wananchi wanufaike na fursa hiyo.Sehemu ya mitambo ya Kiwanda cha Kusindika maziwa, Asas Milk Diary mkoani Iringa, kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika lita 50,000 za maziwa kwa siku lakini kinapata lita 20,000 kwa siku. Mpango wa uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari umeanza kuboresha mazingira ya uwekezaji ili wananchi wanufaike na fursa hiyo.

Katika moja ya jitihada za kuhakikisha mafanikio ya mkakati wa kujenga Uchumi wa Viwanda nchini serikali imeendelea Kuboresha mazingira bora ya biashara kwa  wawekezaji kwa kuendeleza kilimo ili kuchochea maendeleo na sekta ya kilimo kupitia Mpango wa uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Akizungumza baada  ziara ya Kukagua shughuli za SAGCOT mkoani Iringa kwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha vifaranga na chakula cha kuku Silverlands na kiwanda cha kusindika Maziwa cha Asas Diary Milk,   Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora alifafanua kuwa njia ya kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi imara utakaohimili ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa ni kuboresha mazingira ya Uwekezaji.

“Tunaweka  mazingira wezeshi ya kisera na kisheria ili kuhakikisha ukuaji endelevu wa kiuchumi katika sekta ya kilimo hasa kwa kuishirikisha sekta binafsi na kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, tunao Mpango wa SAGCOT tunataka kutumia fursa hizi katika kilimo kukuza uchumi, tuondokane na kilimo cha kujikimu na kuhamia kilimo biashara. Wawekezaji wanahitaji kuona utayari wa wakulima ili wawekeze. Tukumbuke  zaidi ya asilimia 70 ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo”, alisema Kamuzora.

Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Iringa ,Wamoja Ayoub, alifafanua kuwa tayari mkoa huo umeanza kupata mafanikio kwa utekelezaji wa SAGCOT mkoani  humo kwa wakulima kuweza kulimochenye tija , kuongeza thamani mazao yao na kupata masoko ya uhakika.

“Kutokana na ongezeko la matumizi sahihi ya pembejeo kumekuwa na ongezeko la tija kwa mazao kutoka tani 2.2 za mahindi kwa hekta kwa msimu wa mwaka 2014/2015 hadi tani 2.7 za mahindi kwa hekta kwa msimu  wa mwaka 2016/2017na Mpunga kutoka tani 3.2 kwa msimu wa mwaka 2014/2015 hadi tani 4.6 kwa msimu  wa mwaka 2016/2017”, alisema  Wamoja.

Kwa nyakati tofauti wawekezaji katika Kongani ya Ihemi, Mkurugenzi Mtendaji wa Biashara Kiwanda cha kuzalisha Vifaranga na chakula cha kuku  Silverlands, Sean Johnson na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa Asas Diary Milk, Fuad Faraj, walieleza kuwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za kufanya biashara, wameiomba serikali kufanya mapitio ya kodi hasa katika uzalishaji wa bidhaa za viwanda.

Wawekezaji hao walibainisha kuwa  serikali itafanikiwa zaidi katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwa kutaanzishwa kituo kimoja cha kufanyia kazi “One stop Centre”  kwa mamlaka zote za  udhibiti, usimamizi na uratibu wa shughuli hizo  kwa Kongani ya Ihemi (Iringa na Njombe).

Pia walishauri serikali kuweka ruzuku katika mbegu za viazi na alizeti za viazi mviringo na ili kuwezesha wakulima wadogo kumudu kununua mbegu bora  zitakazo ongeza uzalishaji na kuchangia malighafi za viwanda vilivyo katika kongani ya Ihemi (Iringa naNjombe)

Awali, akieleza utekelezaji wa Mpango wa uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha uendelezaji kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga alieleza kuwa wanaendelea kuboresha ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuweza kuboresha mazingira bora ya uwekezaji na biashara katika kongani ya Ihemi
Tunaamini kilimo ni fursa  kwani ni  wazi wawekezaji wanategemea kwa kiasi kikubwa mavuno na mazao bora ili kuzalisha bidhaa nzuri. Uchumi wa viwanda unategemea kilimo chenye tija na ninyi mnatuhakikishia kuwepo tija hiyo.”
Programu ya SAGCOT inatekelezwa katika  mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Katavi  na imegawanywa katika kongani (cluster) sita za Ihemi (Iringa na Njombe), Rufiji, Kilombero, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga. Program hiyo imeanza kutekelezwa mwaka 2011 na mwisho wake mwaka ni 2030. WafadhIli wa SAGCOT ni Serikali ya Tanzania, Shirika la misaada la Uingereza (UKAID), Shirika la misaada la Marekani(USAID), Benki ya Dunia (WBG), Ubalozi wa Norway, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na AGR.

Read More