Sunday, December 31, 2017

TAFUTENI TAKWIMU MPYA, WAZIRI MKUU AAGIZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Kilimo kutoka mikoa inayolima korosho, washirikiane kupata takwimu mpya za wakulima wa zao hilo.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi.

“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mkisimamiwa na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, mshirikiane na kusimamia kwa umakini upatikanaji wa takwimu za wakulima na maeneo yanayolimwa, haiwezekani kila mwaka takwimu ziwe ni zilezile tu,” alisema.

“Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je hao wakulima wako, kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana miche mingapi, na je ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alisema.

“Pia nilikwishawaagiza maafisa ushirika na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) mpaka chama kikuu cha ushirika, kuwa kila mmoja anapaswa atambue ana wanachama wangapi katika chama chake. Hili litawezekana pia kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata au Mwenyekiti wa Kijiji, kwa sababu wao wana idadi kamili za watu wanaowaongoza,” alisema.

“Ninaamini tukifanya hilo tutamaliza tatizo la takwimu na Serikali itakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wakulima wake, na tutaweza kuweka bajeti ya kutosha kuhudumia mahitaji yao,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alipanda mche mpya wa korosho ili kuanzisha zoezi la upandaji miche hiyo na kisha akagawa miche kwa wakulima 10 kutoka vijiji vya Likunja, Kitandi, Kilimahewa na Nachingwea ambao waliwawakilisha wenzao.

Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikagua vitalu vya miche ya mikorosho vilivyopandwa na Halmashauri ya Ruangwa na kuelezwa kuwa miche hiyo ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile iliyotokana na mbegu na ya pili ni ile iliyotokana na vikonyo (grafting).

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki zoezi hilo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.