Saturday, December 2, 2017

MARY MAJALIWA: WAZAZI WEKEZENI KWENYE ELIMU YA WATOTO

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewaomba wazazi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wahakikishe wanatumia sehemu ya kipato chao katika kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao.

Amesema elimu ndiyo jambo pekee linaoweza kumsaidia mtoto katika kutimiza ndoto zake za maisha pamoja na kumtoa katika kundi la wategemezi.

Mama Mary aliyasema hayo jana (Jumamosi, Desemba 2, 2017), katika maafali ya shule ya awali na msingi ya Wonder Kids, iliyopo wilayani Ruangwa, Lindi.


Mke wa Waziri Mkuu alialikwa katika maafali hayo kama mdau wa elimu. Maafali hayo yaliyohusisha watoto wa awali ambao wanaingia darasa la kwanza.

“Walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanafunzi hao wanajua kusoma vizuri, hivyo wazazi watumie kipato chao kuwekeza katika elimu kwani faida watakuja kuiona baadaye.”

Alisema kitaaluma yeye ni mwalimu hivyo anatambua kuwa walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanafunzi hao wanajua kusoma vizuri na wanakuwa na tabia nzuri, hivyo wazazi hawana budi kushirikiana nao.

Pia Mama Mary alitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi wawatie moyo walimu kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa. “Wote ni mashahidi watoto wetu tulivyowaleta na sasa ni tofauti.”

Alisema ni vizuri wazazi wakashiriki kikamilifu katika suala la elimu kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya masomo yao badala ya kuwaachia walimu peke yao.

Kwa upande wake ,mgeni rasmi katika maafali hayo ambaye ni Muwakilishi Mkazi wa Children in Crossifire Bw Craig Ferla aliwapongeza wanafunzi hao kwa  kutimiza moja ya hatua katika safari yao ya elimu na aliwasihi waendele kupenda kwenda shule na kusoma kwa bidii.

Pia aliwapongeza wazazi kwa kutambua umuhimu wa elimu ya awali na kuwapeleka watoto wao kwenye shule hiyo ya Wonder Kids. “Wonder Kids ni mahali sahihi ambapo mtoto anapata  elimu na malezi bora.

Alisema elimu ya awali ninzuri kwa mtoto kwa kuwa inawawezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, hivyo aliwaeleza Wanaruangwa kutumia vizuri fursa ya uwepo wa shule  hiyo katika wilaya yao.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bibi Nancy Tausi alisema  Wonder Kid ilianzishwa Januari, 2017 ikiwa na wanafunzi 117 ambao ni wa kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu.


Alisema lengo la kuanzisha shule hiyo ni kuhakikisha watoto wanapata kujua kusoma vizuri na kwamba wanatarajia kuanzisha darasa la kompyuta kwa ajili ya watoto kujifunza TEHAMA pamoja na kuanza kufundisha lugha ya Kifaransa.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.