Monday, December 18, 2017

HOTUBA YA MHE. KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Ndugu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; 

Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin William Mkapa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Wenyeviti Wastaafu wa CCM;

Makamu Wenyeviti wa CCM, Dkt. Ali Mohamed Shein (kwa upande wa Zanzibar) na
Mzee Philip Japhet Mangula (upande wa Tanzania Bara);

Makamu Wenyeviti Wastaafu mliopo hapa;

Katibu Mkuu, Ndugu Abdulrahman Kinana;

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan;

Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais;

Mheshimiwa Mama Maria Nyerere;

Mheshimiwa Mama Fatma Karume;

Itifaki imezingatiwa.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
MAPINDUZI!

1.0.      UTANGULIZI
Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;Serikali ya Awamu ya Tano inatimiza miaka miwili toka iingie madarakani mwezi Novemba, 2015.

Katika kipindi hiki, Serikali imeendelea kutekeleza changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuweka sera madhubuti zinazosaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa mwelekeo wake wakati akifungua Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 hapa Dodoma.

Baada ya maelekezo haya, hatua kadhaa zimechukuliwa na mafanikio dhahiri tumeanza kuyaona.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Mafanikio dhahiri yameanza kuonekana katika kipindi hiki kifupi. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa nidhamu kwa Watumishi wa Umma; mabadiliko ya hali ya uchumi; kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo; kuongezeka kwa mapato ya ndani; kupungua kwa rushwa, kuimarika kwa Muungano wetu na kushughulikiwa kwa migogoro ya ardhi.

Suala la Nidhamu, Rushwa na Dawa za Kulevya.

Serikali iliweka dhamira ya kuwahudumia wananchi wote hususan maskini kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo na huduma muhimu za jamii. Ili kufikia azma hii ilibidi tuanze kujenga nidhamu ya Watumishi wa Umma kwa kubaini wazembe, wabadhilifu, wezi wa mali na fedha za umma, wala rushwa mahali pa kazi na wasio tayari kuwatumikia wananchi na hasa wanyonge; na kusimamia mwenendo wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji mali na kukusanya mapato.

Tulianzisha mapambano ya wazi dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya. Yote haya ilikuwa ni mkakati wa kuwezesha kutekeleza Ilani yetu kwa vitendo na kwa mafanikio. Yote haya tumeyaeleza kwa kirefu kwenye vitabu tulivyowapa.

2.0.      HALI YA UCHUMI

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Mwenendo wa viashiria vya ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu kwa mwaka 2016 na 2017 vinaonesha kuwa uchumi wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa kwa mwaka 2015 na 2016 ulikuwa asilimia saba na hivyo kuifanya Nchi yetu kushika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika. Tafiti na uzoefu kutoka nchi zilizoendelea unaonyesha kwamba, mwenendo huu wa ukuaji wa uchumi utaiwezesha Tanzania kufikia kundi la Nchi zenye Uchumi wa Kati lenye wastani kipato cha Dola za Marekani 1,043 sawa na wastani wa Shilingi Milioni 2.4 kwa mwaka. Wastani wa Pato la Mtanzania umeongezeka kutoka Shilingi Milioni 1.9 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Shilingi Milioni 2.1 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 11. 

Aidha, Serikali imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato. Kutokana na juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa Mwezi mwaka 2015 hadi Shilingi Trilioni 1.3 kwa Mwezi mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 34.6.

Kupitia makusanyo hayo sasa serikali inaendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo katika kila Halmashauri, Idara za Serikali, Wizara kwa kiasi cha Shilingi bilioni 428.5 kila mwezi.
(Sekta ya Uchumi na Fedha imeelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 4 hadi  wa 8 wa vitabu mlivyogawiwa).

3.0.      SEKTA ZA UZALISHAJI

3.1.     KILIMO

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeielekeza Serikali kutilia mkazo kuendeleza sekta ya kilimo ili kukifanya kilimo kuwa cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara ambacho mazao yake yaongezwe thamani. Serikali imeimarisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo, kuimarisha huduma za ugani, kuimarisha huduma za umwagiliaji, kuwezesha upatikanaji wa masoko na kuhamasisha Sekta binafsi, vyama vya ushirika na kanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 Serikali iliingia makubaliano na kampuni za kuzalisha na kuuza mbegu kwa bei ambayo ni rahisi kwa mkulima. Serikali pia imeanzisha mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea ambapo kwa sasa ununuzi wa mbolea hufanywa kwa pamoja. Mfumo huu unaongeza upatikanaji wa mbolea na unapunguza bei kwa asilimia 30 kwa mkulima, mfuko wa mbolea sasa unauzwa kati ya Shilingi 50,000/= hadi 60,000/= na mfumo huo umeanza msimu huu wa kilimo ambapo hadi Septemba 2017 jumla ya tani 55,000 zimeingizwa nchini. Tayari manufaa yake tumeanza kuyaona.

Serikali inaendelea kuhimiza Bodi za mazao ya pamba, korosho, kahawa, ufuta, tumbaku na mazao mengine kuandaa mbegu na madawa ya kuulia wadudu kwa haraka na bei nafuu.

Kwa upande wa zana za kilimo, Serikali imejenga uwezo wa sekta binafsi katika kuwezesha upatikanaji wa zana za kilimo ambapo katika kipindi cha Novemba 2016 na Septemba 2017 jumla ya matrekta makubwa 2,500 na matrekta ya mkono 336 yaliingizwa nchini na sekta binafsi. Kupitia mpango wa kuendeleza viwanda, Tanzania imeanza kuunganisha matrekta ya kilimo kupitia kampuni ya Ursus ambayo tayari imetengeneza matrekta 1894 ya ukubwa tofauti. Pia, Serikali imenunua mashine za kisasa 14 za kusindika mpunga zenye uwezo wa kukoboa kati ya tani 5 hadi 30 kwa siku kwenye skimu 13 za umwagiliaji nchini.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imeongeza Maafisa Ugani kutoka 9,558 mwaka 2015 hadi 13,532 mwaka 2017. Kati ya hao, 8,232 ni Maafisa Ugani wa sekta ya kilimo, 4,283 mifugo, 493 uvuvi na 524 ni Maafisa Ushirika. Vituo vya mafunzo ya kilimo na mifugo vya kata vimeongezeka kutoka 147 mwaka 2015 hadi 322 kufikia Juni, 2017, sawa na ongezeko la asilimia 54.3 kwa sekta zote.

Aidha, Serikali imejenga masoko na maghala ya kimkakati katika mipaka ili kudhibiti wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi kuingia    moja kwa moja mashambani na kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo. Aidha, mfumo wa stakabadhi ghalani umeonyesha mafanikio makubwa na mabadiliko ya Uongozi kwenye Menejimenti ya Bodi umeonesha matokeo chanya katika   zao la korosho. Mfano, katika msimu wa 2015/2017 kiasi cha korosho kilo laki moja na hamsini na tano (155,244,645) ziliuzwa kwa bei ya Shilingi Bilioni mia tatu themanini na nane (388,474,530,906.40).  Mheshimiwa Rais baada ya kutoa pembejeo bure kwa wakulima, uzalishaji umeongezeka na mwaka huu 2017/2018 hadi kufikia sasa kilo laki mbili sitini na tano (265,651,031) zimeuzwa kwa thamani ya Shilingi Trilioni moja nukta moja. Ambapo inatazamiwa kuwa hadi mwisho wa msimu itafikia 300,000 tutapata sio chini ya trilioni 1.4. Wastani wa bei kwa kilo umepanda kutoka Shilingi 1,300 hadi Shilingi 4,000.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Kilimo yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 8 hadi wa 13 wa vitabu mlivyogawiwa).

3.2.      MIFUGO

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Kwa upande wa sekta ya mifugo Serikali inaongeza uzalishaji wa mitamba, kujenga miundombinu ya mifugo ikiwemo malambo na mabwawa, kuzalisha mashamba darasa ya malisho, kuendeleza na kutoa elimu ya teknolojia ya uhamilishaji, kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Katika kutekeleza maelekezo haya ya Ilani, Serikali inatoa elimu kwa wafugaji kufuga mifugo itakayompa tija mfugaji. Tumeanza kutambua mifugo kwa kuweka alama, kujua idadi na mahali ilipo ili kuweka takwimu, tumeagiza Maafisa Mifugo kuhudumia mifugo, tumezuia mifugo kutoka nje ili kuondokana na migogoro ya wafugaji na wakulima, magonjwa, n.k. tumetenga maeneo ya mifugo kila wilaya na mikoa. Hadi sasa, tumetenga jumla ya hekta 519,918 za maeneo ya ufugaji kwenye vijiji 80 katika Wilaya 17 za Mikoa 11 ya Tanzania Bara na kufanya jumla ya eneo lililotengwa hadi sasa kufikia hekta milioni 2.535 katika vijiji 728. Aidha, jumla ya hati za kumiliki ardhi kimila 44 zimetolewa kwa wafugaji katika Wilaya za Monduli, Ngorongoro, Hanang, Simanjiro na Karatu. Pia, Serikali imeanzisha mashamba darasa ya uzalishaji malisho katika Halmashauri za Bunda, Busega, Kiteto na Igunga. Lengo ni kuanzisha mashamba darasa katika maeneo yote ya wafugaji nchini.

Tumetoa mafunzo ya uhamilishaji kwa wahamilishaji 264 yanayohusu mabadiliko ya teknolojia, tumetoa vitendea kazi, ukarabati wa miundombinu, mitambo ili huduma za uhamilishaji ziwe za uhakika.

Pia, tunahamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ili kumpatia faida kubwa mfugaji.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Mifugo yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 14 hadi wa 18 wa vitabu mlivyogawiwa).

3.3         USHIRIKA

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inaendelea kusimamia sekta ya ushirika ambayo ilikuwa imepoteza mwelekeo. Dhana ya ushirika ni nzuri na endapo itasimamiwa vizuri, itamnufaisha mkulima. Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kufufua ushirika nchini kwa kufanya uhakiki wa mali na kusimamia fedha za ushirika.

Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Ushirika, tunaunda ushirika kwenye mazao yanayoendesha ushirika, tunachukua hatua kwa viongozi wanaofuja mali na fedha za ushirika, tulianza na ushirika   wa korosho, tumbaku, chai. Uchunguzi unafanywa kwa ushirika wa Kahawa. Tutaendelea na hatua hizo kwa mazao yote yanayoendeshwa kwa ushirika. Serikali inataka kuona Maafisa Ushirika wanasimamia ushirika ili mkulima mnyonge anufaike na kilimo kupitia ushirika.

3.4        MALIASILI NA UTALII

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Utalii ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa na ajira kwa wananchi. Kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo Serikali inasimamia utekelezaji wa mikakati ya kukuza utalii nchini kwa kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka, kuongeza bajeti ya sekta ya utalii, kuimarisha mafunzo ya utalii, kujenga mazingira ya kuwezesha vijana kuanzisha makampuni ya kitalii na kuhifadhi malikale. Pia tunatatua migogoro ya mipaka kati ya wananchi na mapori yaliyohifadhiwa kwa lengo la utalii.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo kukarabati kilometa 2,571 za barabara zilizopo ndani ya hifadhi, njia za miguu zenye urefu wa kilometa 143.5 na kuongeza matangazo ya utalii ndani na nje ya Nchi. Juhudi hizo zimewezesha idadi ya watalii kuongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,284,279 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 12 na kuliingizia Taifa Dola za Marekani Bilioni 2. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeongeza bajeti ya utalii hadi kufikia Shilingi Bilioni 6.6 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 4.2 zilizotengwa mwaka 2016/2017. Tunaimarisha matangazo ya vivutio vya Kitalii ili kuongeza idadi ya Watalii.

Serikali imehakiki mipaka yote ya maeneo ya hifadhi ikiwemo Ngorongoro kwa kuweka alama za kudumu na mabango ya tahadhari. Hadi mwezi Mei, 2017 vigingi 14,755 vimesimikwa, sawa na aslimia 62.4 ya vigingi 23,638 vinavyohitajika. Serikali inaendelea kudhibiti ujangili na uharibifu wa Misitu ili kulinda maliasili zetu.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Maliasili na Utalii yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 19 hadi wa 23 wa vitabu mlivyogawiwa).

3.5        VIWANDA

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inahakikisha kuwa uchumi wa Nchi yetu unakua kwa kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda. Katika kujenga uchumi wa viwanda, Serikali imehamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa ndani na nje ya Nchi.

Tumeona mwitikio mkubwa wa sekta binafsi kuwekeza katika viwanda. Baadhi ya viwanda vilivyoanzishwa katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 ni pamoja na; kiwanda cha kusindika maziwa cha Milkcom Ltd kilichopo Kigamboni – Dar-es-Salaam ambacho uwekezaji wake ni Shilingi Bilioni 44 na kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 67.5 za maziwa kwa mwaka na kutoa ajira kwa watu 500; kiwanda cha nyama cha Meat King Ltd kilichopo eneo la Moshono - Mkoa wa Arusha kimewekeza Shilingi Bilioni 5.5 kwa ajili ya kusindika nyama ya ng’ombe, kuku na kondoo; kiwanda cha Lakairo Polybagkilichopo Mwanza ambacho uwekezaji wake ni Shilingi Bilioni 4 chenye uwezo wa kuzalisha magunia ya sandarusi milioni 10 kwa mwaka; kiwanda chaGlobal Packaging kilichopo Kibaha – Pwani  kimewekeza Shilingi Bilioni 8 chenye uwezo wa kuzalisha magunia ya sandarusi milioni 11.75 kwa mwaka na ajira ya watu 110. Kiwanda cha Nyama kilichopo hapa Dodoma kinachinja Ng’ombe 350 – 500 kwa siku.

Baadhi ya viwanda vikubwa vinavyoendelea kujengwa hapa nchini ni: Kilua Steel Group – kiwanda cha nondo kinazalisha tani 2000 kwa siku; kiwanda cha marumaru cha Goodwill kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani; kiwanda cha kusokota nyuzi za pamba cha NAMERA kilichopo Gongolamboto, Dar-es-Salaam; kiwanda cha kukausha mbogamboga cha Vegeta Padravka Ltd kilichopo Bagamoyo - Pwani ambacho uwekezaji wake unatarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 9.9 na kiwanda cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch kinachojengwa Mvomero – Morogoro ambacho kitahitaji ng’ombe 50,000 na mbuzi 60,000 kwa mwaka.

Serikali inaweka mkazo wa ujenzi wa viwanda, kila Mkoa ili kuzalisha bidhaa pia kupunguza tatizo la ajira nchini.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Viwanda yameelezwa  kwa kina kuanzia ukurasa wa 24 hadi wa 26 wa vitabu mlivyogawiwa).

3.6        MADINI

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Ili kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia kikamilifu katika kukuza uchumi na ajira, Serikali inaimarisha ukaguzi wa uzalishaji na mauzo ya madini katika migodi mikubwa na midogo nchini ambapo katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Novemba, 2017 jumla ya sampuli 8,497 za mikuo ya dhahabu na makinikia ya shaba (copper concentrate) kutoka kwenye migodi mikubwa zilifanyiwa uchunguzi kwenye maabara ili kujua kiasi na thamani ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa nje. Kaguzi pia zilifanywa katika Migodi ya Tanzanite One na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka ambazo zimeiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa jumla ya Dola za Marekani Milioni 6.99. Aidha, Serikali imefanya ukaguzi katika uzalishaji na mauzo ya madini ya ujenzi na viwandani katika Mikoa mbalimbali chini na kuwezesha malipo ya mrabaha wa Shilingi   Bilioni 9.97. Mrabaha huo unatokana na uzalishaji na mauzo ya tani milioni 20.69 za madini ya ujenzi na viwandani yenye thamani ya Shilingi Bilioni 324. Kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa ukuta wa eneo la Tanzanite ili kudhibiti utoroshaji.

Vilevile, ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia ya “vat leaching” kuchenjua marudio katika Mikoa ya Mbeya, Mwanza, Geita, Shinyanga na Tabora umefanyika. Jumla ya kilo 2,500 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 183 zilizalishwa na wamiliki halali wa leseni katika maeneo hayo. Ukaguzi huo umewezesha malipo ya mrabaha wa kiasi cha Shilingi Bilioni 7.3. Ukaguzi umefanyika pia kwa Wachimbaji Wadogo wa dhahabu katika Wilaya za Chunya, Geita na Mpanda ambapo jumla ya Kilogramu 48.68 za dhahabu na mifuko 100,287 ya mawe yenye madini ya dhahabu yenye thamani ya wastani wa Shilingi Bilioni 6 ilizalishwa na wachimbaji hao na fedha Shilingi Milioni 244 zilikusanywa kama mrabaha. Mapato haya ni sehemu tu ya fedha zinazopatikana, nyingi zinapotea kwa utoroshaji wa madini yetu.

Katika jitihada za kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo Rasilimali za Madini, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM aliagiza kuundwa kwa Tume mbili maalum za uchunguzi wa makontena yaliyokuwa na mchanga wa makinikia yaliyokamatwa bandarini, Dar-es-Salaam, na maeneo mbalimbali nchini na kuagiza kupata taarifa za uchunguzi huo. Aidha, Mheshimiwa Rais alizuia usafirishaji wa makinikia nje ya Nchi baada ya kugundua wizi wa utoroshaji unaofanywa na baadhi ya makampuni makubwa. Serikali ilitoa waraka wa sheria Bungeni wa kutunga Sheria ya Kulinda Rasilimali za Nchi. Tulikamata makontena yapatayo 423 yenye makinikia yaliyokuwa yanatoroshwa kwenda nje ya Nchi.

Serikali imehamasisha wawekezaji wa Smelter na Refinery kujitokeza kwa ajili ya kujenga mitambo hiyo hapa nchini. Jumla ya kampuni 25 zimeonesha nia na Serikali inaendelea na utaratibu wa kutafuta kampuni zitakazofaa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo hiyo. Vilevile, Serikali itaendelea kuisimamia na kuilinda sekta ya madini na itaendelea kujiridhisha kuwa Watanzania wananufaika vizuri.

Ndugu Mwenyekiti  na WanaCCM wenzangu;
Serikali katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Julai, 2017 imetoa jumla ya leseni 4,207 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 74.1 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini kote nchini. Aidha, jumla ya maeneo 11 yenye ukubwa wa hekta takribani 38,951 yenye uwezo wa kutoa leseni za uchimbaji 3,895 yametengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika Mikoa ya Kagera, Singida, Katavi, Ruvuma, Lindi, Tabora na Geita. Pia, Serikali imetoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 2,000 kuhusu teknolojia mbadala za uchenjuaji dhahabu, usalama migodini, ujasiriamali, utunzaji kumbukumbu na utunzaji wa mazingira.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Madini yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 26 hadi wa 32 wa vitabu mlivyogawiwa).

4.0.      SEKTA YA MIUNDOMBINU NA HUDUMA ZA KIUCHUMI
4.1.      ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inatekeleza mipango ya kuendeleza ardhi ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo utakaorahisisha umilikishaji wa ardhi na uhifadhi wa kumbukumbu za ardhi kwa kukamilisha ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi, kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi, kutatua migogoro, kero ya ardhi kote nchini na kuhakikisha kuwa kila mwenye ardhi anapimiwa na kupewa hati.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imeanza kufunga Mfumo unganishi katika Halmashauri za Manispaa za Kinondoni na Ubungo Jijini Dar-es-Salaam. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Juni, 2018 na baadaye Mfumo huo utafungwa katika Halmashauri zote nchini. Aidha, Serikali imeboresha Mfumo wa Ukusanyaji Kodi ya Pango la Ardhi kwa kuweka Mfumo maalumu uitwao Government e-payment Gateway System katika Halmashauri 31 na hivyo kukomesha vitendo vya Maafisa Ardhi kugawa viwanja mara mbili; na sasa ada na tozo zote kulipwa kwa njia ya kielektroniki pia simu za mkononi. Serikali imeunda Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi yenye jukumu la kufuatilia na kuratibu malipo yote ya fidia yatakayofanywa na Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala, Mikoa na Halmashauri. Mwongozo wa namna shughuli za Mfuko wa Fidia ya Ardhi zitakavyofanyika umeandaliwa na kusambaza kwa wadau.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imefanya uhakiki wa mashamba pori yasiyoendelezwa ambapo ukaguzi wa mashamba ya uwekezaji 121 yenye ukubwa wa ekari 552,139 katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Dar-es-Salaam, Lindi, Manyara, Arusha Pwani, Njombe na Kagera umefanyika ambapo mashamba 58 yalibainika kutoendelezwa. Mashamba hayo pamoja na mengine yenye ukubwa wa ekari 429,654 yaliyopo katika Mikoa ya Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa na    Dar-es-Salaam yamefutiwa umiliki na kurudishwa kwa halmashauri husika kwa ajili ya kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na kuigawa kwa kuzingatia mahitaji ya ardhi yaliyopo katika eneo husika. Tutaendelea kubaini mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyagawa kwa wananchi.

 Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imepima vijiji 11,000 kati ya vijiji 12,545 Nchi nzima hadi kufikia Agosti, 2017. Pia, jumla ya hatimilki za kimila 69,208 zimeandaliwa na kutolewa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa upande wa upimaji wa viwanja, jumla ya hatimiliki za viwanja 82,633 na nyaraka za kisheria 122,106 zimesajiliwa na kutolewa. Kazi ya kubainisha viwanja 50,200 vitakavyorasimishwa katika Halmashauri za Manispaa za Musoma, Kigoma Ujiji, Tabora, Singida, Sumbawanga na Lindi inaendelea.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya ArdhĂ­, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 32 hadi wa 40 wa vitabu mlivyogawiwa).

4.2.       UJENZI NA UCHUKUZI
4.2.1.                 Barabara

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu; 
Serikali inaendelea kujenga miradi ya barabara na madaraja kwa kuzingatia vipaumbele kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama chetu. Ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza miradi ya barabara mijini na vijijini, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini -TARURA yenye jukumu la kusimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za mijini na vijijini ambazo ziko chini ya TAMISEMI ambazo hazipo chini ya Wakala wa Barabara Kuu yaani TANROADS.

Aidha, Serikali imeendelea kukamilisha kujenga barabara Nchi nzima. Zipo zilizokamilimika kwa kuunganisha Mikoa na miradi mbalimbali inatekelezwa kwa kiwango cha lami. Hii ni kukamilisha ndoto ya Mheshimiwa Rais ya kuwa Watanzania watasafiri kwa gari aina ya Mark II kutoka Sirari wilayani Tarime mkoani Mara hadi Mbamba Bay – Ruvuma, kwa kupita juu ya barabara ya lami.

Mpaka sasa tumekamilisha na tunaendelea na ujenzi wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,500 kwa zaidi ya Shilingi trilioni 1.8 zikiwemo Barabara za:
(i)              Dodoma – Kondoa – Babati Km. 232; Shilingi Bilioni 335.46
(ii)             Tunduma – Sumbawanga Km. 223; Shilingi Bilioni 350.2
(iii)            Tunduru- Nakapanya- Mangaka – Mtambaswala Km 202.5;
Shilingi Bilioni 175.2

Ujenzi unaoendelea
(i)              Kidahwe –Kasulu Km 50: Shilingi Bilioni 46
(ii)             Nyakanazi – Kakonko Km 50; Shilingi Bilioni 46
(iii)            Mafinga –Igawa Km 137.9; Shilingi Bilioni 235.4
(iv)            Njombe – Makete Km 107.4; Shilingi Bilioni 217.53
(v)             Arusha (Sakina) – Tengeru na mchepuo wa Arusha (Arusha by pass) Km. 56.5; Shilingi Bilioni 145.1
(vi)            Mtwara – Mnivata Km 50; Shilingi Bilioni 89.59. Aidha tunaendelea kutafuta fedha kutangaza zabuni ya kuunganisha Newala – Masasi.

Wakati huohuo tunayo miradi iliyo katika maandalizi ya ujenzi na imetengewa fedha mwaka 2017/2018 yenye urefu wa zaidi ya Km 1,800 kwa thamani ya Shilingi trilioni 2.99  ikiwemo;
(i)           Masasi-Nachingwea – Nanganga Km 91; Shilingi Bilioni 3.5
(ii)          Mbinga – Mbambabay Km 67; Shilingi Bilioni 129.3
(iii)          Tunduma – Sumbawanga, kazi inaendelea hadi Mpanda – Uvinza (mkandarasi yupo kazini).

Vivuko Na Madaraja
(i)           Tumekamilisha ujenzi wa Kivuko cha juu cha Furahisha – Mwanza kwa Shilingi Bilioni 7.076 na Daraja la Mto Kilombero kwa Shilingi Bilioni 56.8,  
(ii)          Sasa tunajenga madaraja ya juu (Flyover) ya TAZARA kwa Shilingi Bilioni 94, Ubungo Shilingi Bilioni 177.4 na tunatarajia kujenga Kivuko cha Mwenge.

Tunaimarisha usafiri jijini Dar-es-Salaam Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na tutajenga awamu tatu nyingine ili kuimarisha usafiri katika Jili la  Dar-es-Salaam kutoka:
§    Katikati ya Jiji – Mbagala
§    Katikati ya Jiji – Gongolamboto
§    Morocco – Mwenge – Tegeta.

Tutajenga pia Bandari Dar-es-Salaam; Bagamoyo; Mtwara.

Serikali inakusudia kutekeleza miradi iliyopangwa kwenye bajeti zaidi ya km 1,300 na tumefanya upembuzi yakinifu kwa kilometa 1,371. Aidha, Serikali inaendelea na ukarabati wa barabara za kwenye Miji na Halmashauri nyingi nchini.
(Kazi za ujenzi wa barabara za lami nchini tumefafanua kwenye Ukurasa 38 – 55)

4.2.2. Usafiri wa Anga

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
 Serikali imeimarisha Shirika letu la Ndege ambapo katika mwaka 2016/2017, Serikali iliingia mkataba wa ununuzi wa ndege mpya sita ambapo ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q 400 ziliwasili nchini Septemba, 2016 na zinaendelea kutoa huduma. Ndege moja, aina ya Bombardier Dash 8 Q 400imekamilika na itawasili nchini wakati wowote. Ndege mbili aina ya C - series na Boeing 787-8 Dreamliner 1 zitakuwa zimeingia nchini ifikapo Juni, 2018.

Serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege. Uwanja wa Kimataifa wa JNIA – ujenzi wa Jengo Jipya (Terminal III) umefikia asilimia 66 na kazi ya ujenzi inaendelea. Tumekamilisha maeneo ya kusimamia ndege katika uwanja wetu wa KIA. Tunakamilisha jengo la kupokelea abiria katika Uwanja wa Ndege wa Songwe. Tumepanua Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa thamani ya Shilingi Bilioni 60 na tunatarajia kuongeza njia kwa kilometa moja zaidi ili kuwezesha ndege kubwa zaidi kutua. Tunakamilisha ujenzi wa eneo la kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa Tabora.

Serikali imesaini mikataba ya ukarabati na upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Shinyanga na Sumbawanga. Fedha zimetengwa mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa Viwanja vya Ndege vya Iringa (Shilingi Bilioni 3.76); Musoma (Shilingi Bilioni 3.85); Songea (Shilingi Bilioni 3.66); na Mtwara (Shilingi Bilioni 3.55). Tutatenga fedha kwa ajili ya Viwanja vya Ndege vya Lindi na Nachingwea. Tunaboresha kwa kuweka taa za kuongozea ndege na mawasiliano katika Uwanja wa Ndege wa Tabora. Tunarefusha njia ya kurukia, jengo la kuongozea ndege na jengo la mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kukamilisha jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma.

4.2.3. Miundombinu ya Reli

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali imeanza ujenzi  wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge kutoka Dar-es-Salaam–Tabora–Kigoma/Mwanza, Tabora–Mpanda, kipande cha Km. 300 kutoka Dar-es-Salaam hadi Morogoro kitakachogharimu Shilingi Trilioni 2.74 umeanza na Mkataba wa kuanza ujenzi wa kipande cha Km. 412 kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora) wenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.328 umesainiwa.  Aidha, kazi ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Uvinza – Musongati imekamilika.

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali za Rwanda na Burundi zinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia mradi huo. Pia, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Mtwara – Songea – Mbamba Bay kwa thamani ya Trilioni 3.99 na matawi ya kwenda Mchuchuma na   Liganga (Km. 1,000) kwa Standard Gauge ilikamilika Juni, 2016. Vilevile, kazi ya usanifu wa kina wa njia ya Reli ya Tanga – Arusha imekamilika Mei, 2015 na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli mpya ya kutoka Arusha hadi Musoma (km 600) na matawi ya Engaruka (km 53), Minjingu (km 35) na tawi kuelekea Dutwa (km 2.8) pamoja na reli ya Tabora – Mwanza (km 120) unaendelea.

Tunatarajia kuongeza urefu wa reli kutoka Mpanda hadi Bandari ya Kalemie ili kuhudumia Ziwa Tanganyika.

4.2.4   Usafiri wa Majini

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;Serikali itaimarisha usafiri wa majini kwa kuwa na miradi ya kipaumbele. Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kuboresha usafiri wa majini kwenye Ziwa Tanganyika, Nyasa na Victoria.

Ziwa Tanganyika, taratibu za ununuzi wa Meli mpya unaendelea na watalaam. Meli ya thamani ya Shilingi Bilioni 24 yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 200 itapatikana.

Ziwa Victoria, mchakato wa kumpata Mkandari kutoka Korea Kusini umakamilika. Meli ya thamani ya Dola za Marekani Milioni 37 yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400 itapatikana.

Kuhusu Ziwa Nyasa, Serikali imeshapata Meli 2 za mizigo zenye uwezo wa tani 1,000 kila moja kwa thamani ya Shilingi Bilioni 11.252 na sasa tunakailisha ujenzi wa Meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo ya thamani ya Shilingi Bilioni 9.119.
(Mafanikio tuliyoyapata katika sekta nzima ya Ujenzi na Uchukuzi yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 41 hadi  wa 69 wa vitabu mlivyogawiwa)

4.3.          NISHATI

4.3.1. Uzalishaji wa Umeme

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
 Serikali inaongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kwa kutekeleza Miradi mikubwa ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I na II ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuzalisha megawati 565 kwa kutumia gesi asilia kwa gharama ya Shilingi Trilioni 1.2 na maandalizi kwa ajili ya miradi ya Kinyerezi III na IV ambayo itazalisha takribani megawati 600 inaendelea. Vilevile, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji wa Staglier’s Gorge ambao utazalisha megawati 2,100. Pia, Serikali imekamilisha Mradi wa Backbone wa kV 400 unaounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga wenye urefu wa Km. 670. Serikali inashughulikia tatizo kubwa linalokabili Mikoa ya Lindi na Mtwara kukosa umeme wa uhakika. Tumeagiza mashine zitakazoziba pengo la mashine zilizoharibika. Pamoja na mashine hizo, Serikali itaunganisha kwenye gridi ya taifa mikoa hiyo kutoka Dar-es-Salaam.

Serikali pia inakamilisha ujenzi wa njia ya umeme kutoka Makambako, Njombe, Madaba, Songea, pia Madaba hadi Ludewa kupitia Liganga. Kazi inaendelea. Serikali inajenga vituo vya kuongeza nguvu ya umeme Njiro – Arusha, Mahumbika – Lindi na Madaba – Songea ili kuwezesha usambazaji umeme wa uhakika hadi vijijini. Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha uzalishaji wa umeme wa jua kwa kutumia gridi ndogo katika maeneo ambayo hayafikiwi na Gridi ya Taifa ambapo hadi sasa kuna takribani MW.10 zinazalishwa. Pia Mradi mkubwa wa Kishapu –Shinyanga MW. 150 unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na Mradi wa Chuo Kikuu cha Dodoma MW. 55 unatarajiwa kukamilika mwaka 2019. Kwa sasa mgao umepungua na matarajio yetu ni kuwa tutauza umeme nje ya Nchi.

4.3.2.  Umeme Vijijini

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Kwa upande wa umeme vijijini, Serikali imekamilisha kwa asilimia 98 Mradi Kabambe wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA Turn-key Projects phase II), jumla ya wateja 172,000 kati ya wateja 250,000 wameunganishwa na kazi inaendelea. Wakala wa Kusambaza Nishati Vijijini (REA) imeongezewa fedha ambapo katika bajeti ya Mwaka 2017/2018, Wakala ilitengewa Shilingi Bilioni 667.48 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 587.61 zilizotengwa katika Mwaka wa fedha 2016/2017. Duru ya kwanza ya Awamu ya Tatu ya Mpango Kabambe wa Kusambaza Umeme ambayo imeanza itahusisha kupatiwa umeme kwa vijiji 3,559 na vijiji vitakavyosalia vinavyofikia 4,314 vitapatiwa umeme katika duru ya pili ya Awamu ya Tatu ikihusisha maeneo yaliyopo nje ya gridi. Pia, umeme utapelekwa katika maeneo ambayo hayakupitiwa katika awamu mbili za mwanzo hii ni pamoja na taasisi za elimu, afya na pampu za maji katika maeneo ya vijijini.

(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Nishati yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 70 hadi  wa 74 wa vitabu mlivyogawiwa).

4.4.      MAWASILIANO

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inahakikisha kuwa Taasisi za Elimu, Ofisi za Wakuu wa Wilaya/Polisi, Hospitali zote za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta 65 ziunganishwe katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Kwa kushirikiana na Kampuni ya VIETTEL hadi kufikia mwezi Septemba, 2017 Serikali imefikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Ofisi za Halmashauri 117, Vituo vya Posta 71, Vituo vya Polisi 129, Hospitali za Wilaya  90, Mahakama 27 na huduma ya intaneti bure kwa miaka mitatu katika shule 425.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inafikisha huduma za simu za viganjani kwa wananachi wote ambapo kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Kata 443 zenye uhitaji wa huduma za mawasiliano zimepata wazabuni wa kupeleka mawasiliano husika. Kati ya kata hizo 443, upelekaji wa mawasiliano umekamilika katika kata 391 na Kata 52 zilizobaki zinategemewa kufikishiwa huduma hiyo kabla ya mwisho wa mwaka 2019. Vilevile, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Serikali imetoa zabuni ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 75 zenye vijiji 154 ambazo zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2018.

Kampuni ya Viattel imepewa zabuni ya kufikisha mawasiliano kwenye vijiji 4,000 vilivyobaki katika mwaka huu wa fedha.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Mawasiliano yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 74 hadi wa 77 wa vitabu mlivyogawiwa).

5.0.      HUDUMA ZA JAMII
5.1.      AFYA

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali inaimarisha huduma za Afya ili ziwafikie wananchi wote hadi vijijini ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Novemba 2017, Serikali imeongeza Vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka Vituo 7,014 mwaka 2014/2015 hadi 7,284 mwaka 2016/2017, sawa na  ongezeko la Vituo 269. Serikali imekamilisha ujenzi wa Hospitali za Mlonganzila, Benjamin William Mkapa na Hospitali za Rufaa kwa ngazi za Mikoa. Wilaya sasa zimeanza kujenga hospitali na ujenzi umefikia hatua mbalimbali katika maeneo tofauti. Hivi sasa Halmashauri 15 zinaendelea na ujenzi wa hospitali za Wilaya, Halmashauri nyingine 15 zipo katika hatua ya kupandisha hadhi Vituo vya Afya kuwa hospitali za Wilaya na Halmashauri 13 zimetenga maeneo na kuanza maandalizi ya ujenzi. Hospitali za Mikoa zote sasa zinahamishiwa Wizara ya Afya.

Aidha, Serikali imehamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ambapo idadi ya watu waliojiunga imeongezeka kufikia asilimia 34 mwaka 2017 kutoka asilimia 19 ya mwaka 2015. Uhamasishaji kwa wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) unaendelea katika Mikoa mbalimbali nchini.

Vilevile, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi kufikia Shilingi Bilioni 260 mwaka 2017/2018. Hadi mwezi Juni, 2017, asilimia 83 ya dawa muhimu zaidi (essential medical items) zinapatikana katika Bohari ya Dawa na hali ya upatikanaji wa dawa kwenye Hospitali kufikia mwishoni mwa mwezi    Julai 2017 ni asilimia 86.3. Lengo la Serikali ni kuondoa tatizo la ukosefu wa dawa, Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali.
(Mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Afya yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa wa 77 hadi wa 89 wa vitabu mlivyogawiwa).

8.3.      ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;Serikali inaboresha Sekta ya Elimu kuwa ya mwelekeo wa Sayansi na Teknolijia ili kufanikisha ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.

Ndugu Mwenyekiti na WanaCCM wenzangu;
Serikali ya Awamu ya Tano  ilianza kutekeleza Mpango wa Elimu Bila Malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari ambapo tangu Januari, 2016 Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia Elimu Bila Malipo. Mwezi Julai 2016, kiasi hicho kiliongezwa hadi kufikia Shilingi Bilioni 23.868, na hivyo kufanya Serikali kutumia jumla ya Shilingi Bilioni 465.6 kugharamia elimu bila malipo hadi mwezi Agosti, 2017. Hatua hiyo imesaidia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa Darasa la I kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi kufikia wanafunzi 2,120,667 mwaka 2016. Changamoto iliyojitokeza ni upungufu wa madawati na Walimu. Madawati yametolewa ya kutosha na ajira za Walimu zimeanza kutolewa.

Aidha, Serikali imeweka juhudi katika kujenga maabara ambapo kwa sasa shule za Serikali zenye maabara ni 2,141 kati ya 3,614 na zisizo za Serikali zenye maabara ni 1,075 kati ya 1,145. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 16.9 kwa Shule za Sekondari 1,696 kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa Masomo ya Sayansi kwa nadharia na vitendo.

Vilevile, Serikali imeongeza Bajeti ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka Shilingi Bilioni 365 mwka 2015 hadi Shilingi Bilioni 483 mwaka 2017 na kuwezesha idadi ya Wanafunzi wanaopata Mkopo wa    Elimu ya Juu kuongezeka kutoka 98,300 mwaka 2015 hadi wanafunzi 125,000 mwaka 2017.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.