Thursday, August 31, 2023

WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA EL-NINO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Octoba hadi Disemba mwaka 2023, baada ya Mamlaka ya hali hewa nchini (TMA) kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli zinazotegemewa kuanza katika kipindi hicho, ambao umeonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa.

Waziri Mhagama ameyasema hayo , alipokuwa akizungumza na waandishi habari katika Ukumbi wa Mkutano wa Ofisi ya hiyo mtaa wa Posta Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama amesema kipindi hicho cha mvua kubwa kinaweza kuendelea mpaka mwezi Januari 2024, na alisema kuwa Msimu wa Vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka unahusisha maeneo ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

“Tunaona madhara kadhaa yanayoweza kutokea katika baadhi ya sekta kutokana na uwepo huo wa El-nino utakaosababishwa na mvua kubwa katika kipindi hicho ambacho kimesemwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini ni kama vile, mafuriko yatakayoleta uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali na maporomoko ya ardhi kuathiri makazi.” Alifafanua Waziri Mhagama

Aidha, aliongeza kusema kuwa madhara mengine yanaweza kutokea katika Sekta ya mazingira ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mashamba, Miundombinu ya usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini pamoja na magonjwa ya milipuko kwa binadamu, wanyama na kuongezeka kwa wadudu waharibifu wa mazao na mimea.

Sambamba na hilo, Waziri Mhagama amesema Serikali inaelekeza kamati za usimamizi wa maafa na sekta, kushirikiana na umma kuchukua baadhi ya hatua kama vile kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madhara na kukabiliana na maafa endapo yatatokea pamoja na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

“Tunazielekeza kamati hizo zisisubiri maafa yatokee, waanze kutambua maeneo yote hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuanza kuandaa mipango ya kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutoka na utabiri huo wa Mamlaka ya hali ye hewa.” Alisisitiza Waziri Mhagama

Pia Ameziagiza kamati hizo kuanza kuandaa na kuainisha rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikiksha zianaendana na maeneo yao.

Awali Waziri Mhagama amezikumbusha kamati hizo kuchukua hatua kwa kuzingatia utabiri wa Hali ya Hewa kwa kuelimisha wananchi kwenye maeneo yao juu ya hatua za tahadhari za kuchukua ili kuokoa maisha pale ambapo jambo lolote litatokea na kukoa mali na kutoa taarifa kwa haraka sana kwa mamlaka Husika kuhusu dalili zozote za kutokea Maafa.

Waziri Mhagama Ametoa wito kwa wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi maeneo ya uwanda wa chini na pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao. 

 

Read More

Tuesday, August 29, 2023

DKT. YONAZI: GLOBAL FUND YAIMARISHA SEKTA YA AFYA NCHINI

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameupongeza na kuushukuru Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa mchango mkubwa unaoutoa katika kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu nchini.

 Ametoa pongezi hizo wakati akifungua mkutano wa Uundwaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa kipindi cha mwaka 2024- 2026 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa hoteli ya APC Bunju Dar es Salaam.

 Mkutano huo ulioudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sekretarieti ya TNCM, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Pamoja na Asasi za Kiraia.

 Akieleza kuhusu mchango wa Mfuko wa Dunia katika sekta ya afya nchini, Dkt. Yonazi alisema kuwa, nchi imeendelea kupiga hatua kwa kuzingatia ufadhali wanaoutoka kwa lengo la kugharamia miradi ya Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI na Uimarishaji wa Mifumo ya Utoaji wa Huduma za afya.

 “Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kupitia ushirikiano thabiti na misaada mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Mfuko wa Dunia yaani Global Fund,”.Alisisitiza

 Aidha alisema kuwa Tanzania bado ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na changamoto za magonjwa hayo na yameendelea kusababisha vifo kwa wananchi walio wengi hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

 Alitumia jukwaa hilo kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

 “Ushirikishwaji wa Wadau Watekelezaji wa Nje ya Serikali (PR2) katika mapambano haya ni kipaumbele cha Serikali yetu. Niwaombe wadau wetu kwa pamoja tushirikiane kufikisha huduma hizi katika jamii yote inayotuzunguka.Ninawasihi muendelee kushirikiana na Serikali katika kuleta uzoefu hususan pale tunapohitajika kuongeza ufanisi na tija katika miradi na huduma za afya,”.Alisema Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tanzania Natioanal Coordinationg Mechanism (TNCM) Dkt. Rachel Makunde alimshukuru Katibu Mkuu ambaye pia ni mwenyekiti wa TNCM kwa usimamizi wake na mchango anaoutoka katika kuyafika malengo ya chombo hicho.

 Naye Dkt. David Sando, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la MDH aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Program hizo ili kuimarisha huduma za afya nchini.

 “Tumeendelea kusupport zaidi ya wagonjwa laki tatu wanaotumia dawa za kufubaza Makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) na kupitia miradi ya HIV, tumeweza kuwafikia wagonjwa wengi katika mikoa 12 tunayoihudumia ambapo ni zaidi ya nusu ya wagonjwa wote nchini,” alieleza Dkt. Sando

Read More

Monday, August 28, 2023

WANANCHI WAPEWA RAI KUSHIRIKI WIKI YA KITAIFA YA UFUATILIAJI NA TATHMINI

 


Wananchi wamepewa wito wa kushiriki katika wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini itakayofanyika Jijini Arusha ambayo itahusisha kutoa elimu itakayowawezesha kutoa taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini na Ufuatiliaji wa Miradi mbali mbali ya kimaendeleo inayofanywa na Serikali katika maeneo yao.

Hayo yameelezwa leo na Mtakwimu Mkuu kutoka Idara ya Ufuatliaji na Tathmini ya Ofisi Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Thomas Saguda, alipokuwa akizungumza na Kituo kimoja cha Televisheni Jijini Dodoma.

Bwn. Saguda Alisema, Wananchi hao wanaweza kushirki kupitia maonesho mbalimbali yatakayoonesha kazi mbalimbali za Ufuatiliaji na Tathmini zilizofanyika ndani ya nchi na kupata kujionea mengine yatayooneshwa na washiriki mbalimbali kutoka nje ya nchi.

“Maonesho haya yatawapa fursa wananchi ya kuelewa namna wanavyopaswa kufanya Ufuatiliajia na Tathmini, wenzetu wataalam wanaita Citizen Science, ni rahisi sana Mwananchi ukimuuliza mradi flani wa maji pale umefanya kazi, atakwambia unafanya kazi, ama atakwambia maji pale yalitoka wiki mbili tuu yakakatika, kwa hiyo yule anakupa taarifa ya uhakika, kwa sababu ndiyo mnufaika na ndiyo mlengwa.” Alisema bwana Saguda.

Aliendelea kusema kuwa Sambamba na Maonesho hayo Kongamano hilo pia litahusisha mafunzo ya kitaaluma, warsha mbalimbali zitakazoendeshwa na wataalamu wabobezi wa masuala ya Ufuatiliajia na Tathmini kutoka ndani na nje ya nchi na kuongeza kusema kuwa mada mbali mbali zimekwisha wasilishwa kwa ajili ya Utekelezaji.

Awali akiongea katika kipindi hicho maalum, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. JohnBosco Quman, alisema Eneo la Ufuatiliaji  na Tathmini linamgusa kila mmoja, aliyepo Serikalini au katika Sekta Binafsi kwani Utekelezaji wa Miradi mingi inatekelezeka katika jamii na inamgusa kila mmoja, “Ukiangalia katika ngazi ya Wizara Sera ndo zinatekelezeka huko, lakini kwenye suala la utekelezaji linashuka kwenye ngazi ya Halmashauri na ndiko kwenye wadau mbalimbali, kwa hivyo kwa kupitia miradi kama vile ya Afya na Maji, Serikali inavyotoa fedha na kusimamia miradi hiyo, matokeo yake yanamgusa kila mmoja.” Alibainisha Bw. Quman

Aliendelea Kufafanua kuwa Idara hii ina jumuku kubwa la kuhakikisha kuwa kile ambacho kinachotolewa na Serikali kinaenda kunufaisha  jamii nzima.

Sambamba na hilo, Kongamano hili la Pili la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha mapema mwezi Septemba, itawalenga zaidi,wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini, Maafisa na Mameneja wa Miradi kutoka katika Taasisi zote za Umma, Taasisi Binafsi, makampuni, Asasi za Kiraia na mashirika ya Kimataifa.

 

Read More

Saturday, August 26, 2023

MWONGOZO WA UANDAAJI NA UANDISHI WA SERA ZA KISEKTA, ZANZIBAR – 2022 WAZINDULIWA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe.Hamza Hassan Juma amezindua Mwongozo wa Uandaaji na Uandishi wa Sera za Kisekta, Zanzibar katika Ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul - Wakili Kikwajuni Zanzibar.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesemea kuwa ni miongoni mwa muendelezo wa utekelezaji wa hati ya kisheria Nambari 14 ya mwaka 2020 iliyoitaka ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi kupitia Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo kusimamia masuala ya Sera za kisekta nchini.

Mhe. Hamza alisema, Ofisi yake imechukua jitihada mbali mbali za kuifanyia kazi hati hiyo ya kisheria ikiwemo kufanya tathmini ya Utekelezaji wa Sera za Serikali ambapo tathmini ya kina kwa Sera 39 ilifanyika na mambo mbalimbali yalibainika yakiwemo mapungufu, mafanikio na changamoto zilizopo katika kusimamia uratibu wa uandaaji na utekelezaji wa Sera nchini.

“Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni kutokulingana kwa miundo ya kisera nchini jambo ambalo linaweza kurejesha nyuma upatikanaji halisi wa utekelezaji wa Sera.Aidha, kupitia Ripoti ya Tathmini hiyo pamoja na mambo mengine Ofisi yangu imeandaa Mwongozo huu ambao utakuwa umetatua changamoto mbali mbali na utaleta matarajio mazuri katika uratibu wa Sera nchini kwa maslahi ya nchi yetu,” alisema Mhe. Hamza

Aliongezea kuwa Mwongozo umezingatia miongozo ya Kikanda na Kimataifa, Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 na Mipango ya Maendeleo Endelevu ya Kitaifa na Kimataifa.

 “Ofisi inaimani kikao hichi chenye ushiriki wa Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Mashirika, Wakurugenzi, Wakuu wa Vyuo, Sekta Binafsi na Maafisa Viungo wanaosimamia Sera ni ishara njema inayoonesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyojali ushirikishwaji wa Taasisi za Umma na za Binafsi katika kusimamia maendeleo ya nchi hii,” alieleza.

Aidha, uzinduzi ulihusisha wajumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni ishara na kielelezo cha Muungano wetu kuhakikisha inaendeleza mashirikiano hasa katika Sera zinazotekelezwa katika pande zote mbili za Muungano kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa Sera zenye sura ya Muungano.

Alitoa wito kwa Wizara zote kutoa elimu stahiki ya Sera zao na kuandaa utaratibu wa ushirikishwaji wa wadau husika katika uandaaji na utekelezaji wa Sera hizo sambamba na kuufanyia kazi mwongozo huu kwa manufaa ya umma.

“Ni muhimu kuzingatia suala zima la kuzifanyia mapitio Sera zote ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa kuzingatia taratibu zilizoainishwa kwenye mwongozo huu,” alisisitiza Mhe. Hamza

Akitoa salamu za Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu ofisi hiyo anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa amesema uwepo wa Mwongozo utaongeza tija na matokeo chanya katika sekta mbalimbali katika kutoa huduma kwa jamii huku akieleza kuwa, ofisi yake itaendelea kuimarisha mashirikiano na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi hususan katika kuratibu masuala ya sera nchini.

“Tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano pamoja na kujifunza kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hususan Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika maeneo yote yanayoratibiwa na Serikali hizi mbili,” alisisitiza

Bw. Mutatembwa aliongezea kuwa uwepo wa mwongozo huu  utaimarisha utekelezaji wa Sera kwa kuwezesha kuwa na sera zilizoandaliwa kwa kuzingatia Sera shirikishi na kuakisi hali halisi.

 

Read More

Friday, August 25, 2023

WAZIRI MHAGAMA, APOKEA MWONGOZO WA KITAIFA WA UFUATILIAJI NA TATHMINI KATIKA TAASISI ZA UMMA.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu nayeshugulika na Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Amepokea Rasimu ya kwanza ya Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali katika Taasisi za Umma.

Akipokea Rasimu hiyo Jijini Dodoma, Waziri Mhagama alisema Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali Nchini, Utasaidia kuwa na matokeo ambayo yanaendana na programu na Miradi iliyopangwa kutekelezeka ndani ya Taifa, na Itasaidia Serikali kujipangia Programu zenye matokeo chanya.

 “Tunaweza tukawa na matokeo yakawa hasi, ama mradi usifanye vizuri, ila tukiwa na Mwongozo mzuri basi utatusaidia ndani ta Taifa kuwa na matokeo mazuri yaliyowekwa kutokana na Utekelezaji wa mradi Husika” alibainisha.

Sambamba na hilo, alisema kuwa, mwongozo huu utafikisha Taifa mahali ambapo dhana ya uwajibikaji wa hiari na uratibu wa Pamoja itafikiwa na kujifanyia tathmini katika usimamizi na utekelezaji wa programu, zilizopo nchini na Usimamizi mzuri wa Rasilimali watu na Rasilimali fedha kwenye Serikali kuu, Taasisi na Serikali za Mitaa.

Aidha, Mhe. Waziri Mhagama Alisema ana Imani kuwa Muongozo huu, utasaidia kuimarisha Utawala Bora na kuendelea kusema kuwa, bila Utawala bora hakuna kizuri kitakachofanyika, katika dhana nzima ya kutelekeza kazi za kila siku akitolea mfano dhana ya uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.

“Tunatarajia kuwa Mwongozo huu Utatusaidia kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu na muda Mfupi.” Alihimiza.

Aliongeza kusema kuwa Mwongozo huu utasaidia kukamilisha programu na miradi Pamoja na  kufikisha huduma kwa wananchi  kwa wakati na viwango vinavyotarajiwa na kuokoa Rasilimali fedha kwa kiasi kikubwa.

“Nauona huu Mwongozo ni kitu cha Muhimu na kipekee,Tunataraji mwongozo huu utusaidie ndani ya Serikali kupanga miradi na program zetu kwa kuzingatia vipaombele tulivyonavyo, kwenye Sekta, Taasisi, Mashirika ya Umma na wakala lakini hata kwenye Sekta Binafsi sababu wale ni washiriki wetu kimaendeleo.” Alifafanua

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha kuandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali Dkt. Fransis Mwaijande, alisema Uandaaji wa Mwongozo huo umetokana na kuiwezesha Ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza jukumu la Kikatiba ambapo limeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungango wa Tanzania Ibara ya 52 fungu cha 1-3 ya mwaka 1977, mbayo inaipa Ofisi ya Waziri Mkuu Mamlaka ya Kusimamia Shughuli za Serikali ikiwemo Ufuatiliaji na Tathmini wa Sera Mipango, Miradi na Programu za Maendeleo na Utendaji wa Shughuli za Serikali kwa Ujumla.

Awali, Akiongea wakati wa wasilisho la Mwongozo huo, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu alisema, rasimu hiyo ya Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni miongoni mwa document ambayo itatumika wakati wa kongamano la pili la Kitaifa Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Mwezi Septemba Mkoani Arusha.

Read More

Tuesday, August 22, 2023

LUTENI KANALI MASALAMADO: TAARIFA NA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KUSAIDIA KUOKOA MAISHA YA WATU NA MALI ZAO

 


Imeelezwa kuwa uwepo wa taarifa na huduma za hali ya hewa zinalenga kusaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa, upepo mkali na vimbunga nchini.

 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado wakati akifungua mkutano wa 22 wa wadau wa utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) (National Climate Outlook Forum, Ncof-22 for October to December 2023 rain season) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Giraffe, Dar es Salaam.

 

Mkutano huo wa Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa kwa msimu wa mvua za Vuli 2023, umebebwa na kaulimbiu inayosema; “matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa wote na kwa wakati”.

 

Alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi ambapo zimeshuhudia athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko haya ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo, kubadilika kwa misimu ya mvua hasa tarehe za kuanza na kuisha kwa mvua.

 

Pia Mamlaka imeendelea kuboresha huduma ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo (Downscaled forecast), kuwa utabiri huu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

 

Luteni Kanali Masalamado ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuendelea kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaosaidia kujiandaa na kujikinga na viashiria vya maafa nchini hivyo kuifanya jamii kuwa na taarifa muhimu za hatua za muhimu zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepuka madhara yatokanayo na maafa nchini huku akisihi kuendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

 

“Ushirikiano huu ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa,”alisema Luteni Kanali Masalamado.

 

Alifafanua kuwa, Mamlaka inaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na wadau ili kuendelea kukusanya maoni na taarifa mtambuka  kwa ajili ya kurahisisha ufungashaji wa taarifa hususani eneo la athari katika ngazi ya wilaya. Hivyo wadau wote ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana na TMA ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa taarifa za kisekta.

 

“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa mvua za Vuli, kwa mwezi Oktoba hadi Disemba, 2023; ni muhimu sana kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta yake”, alisisitiza Luteni Kanali Masalamado.

 

Sambamaba na hilo alihimiza na kuwasihi wadau wote kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Namba 2 ya mwaka 2019, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vituo vya hali ya hewa vinasajiliwa kama ambavyo sheria inaelekeza.

 

Vilevile kwa watumiaji wa taarifa na huduma za hali ya hewa kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa mujibu wa sheria ili kuongeza tija na kupunguza athari za hali mbaya ya hewa.

 

Kwa upande Wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Ladislaus Chang’a alikieleza malengo ya mkutano huo wa wadau kuhusu Utabiri wa Vuli, Oktoba hadi Disemba, 2023 alisema unalenga kujadiliana na kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa mvua za Vuli utakavyoweza kutumika kwa tija katika sekta mbalimbali hapa nchini.

 

“Kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za hali ya hewa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea na jitihada za kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwemo miundombinu na rasilimali watu. Hivyo, tunaishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo,” alisisitiza Dkt. Chang’a.

 

Aidha, akizungumzia kuhusu msimu huu wa Vuli, 2023 mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwepo wa Hali ya El Nino ambayo ilianza kujitokeza mapema mwezi Juni, 2023 na imeendelea kuimarika. El Nino inatarajiwa kuendelea hadi mwanzoni  mwa mwaka 2024.

 

“Sambamba na mifumo mingine ya hali ya hewa, tathmini ya mwelekeo wa msimu wa Vuli 2023 itazingatia pia uwepo wa  hali hiyo ya El Nino na athari zinazoweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini hivyo tuendelee kuchukua tahadhari muhimu ikiwemo kuzingatia taarifa za utabiri zinazotolewa,” alisisitiza

 

Read More

Monday, August 21, 2023

WAZIRI MHAGAMA AHIMIZA MASHIRIKIANO

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ) Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Idara ya Ufutiliaji na Tathimini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini, (TAKUKURU) katika kutumia Mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathimini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali, ili kuweza kuondoa upendeleo, Rushwa na kutoa huduma bora kwa wananchi katika utendaji Serikalini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dodoma alipokuwa katika kikao kazi cha Mapitio kilichohusisha Wakurugenzi, wa Idara na Wakuu wa vitengo wa Ofisi hiyo ambapo, Mamlaka ya Serikali Mtandao imefanya wasilisho la Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa shughuli za Serikali.

Waziri Mhagama Alisema kuwa, eneo la Ufuatiliaji na Tathmini ni eneo ambalo haliwezi kukwepeka “Leo Tumekutana hapa tumefanya kazi nzuri ya kufanya mapitio na kuangalia ramani hii ambayo inaanza na kuwa na mfumo wa Ufuatilia na Tathmini Nchini, kama nyenzo muhimu sana ya Utendaji kazi ndani ya Serikali.” Alisisitiza

Aliendelea kusema kuwa, Mfumo huu utasaidia kushauri namna ya kujipanga na namna ya kufanya kazi ndani ya Serikali ,“Mfumo huu utusaidie kuchakata  kila kitu na kutusaidia kupata matokeo sahihi kwa jambo sahihi na shughuli sahihi, katika kupima utendaji kazi na matokeo yake.” Alifafanua.

Aidha, Alisema pia kwa Mujibu wa Sheria kuna Taasisi ambazo zimekasimiwa majukumu ya kufanya, zinazofanana na Idara hii akitolea mfano Tume ya Taifa ya Mipango, na kusema ni lazima kukutana na Tume hii ya Mipango ili kila mtu afanye kazi kwa kufuata Sheria na Kuzingatia Mifumo iliyopo. “Ni lazima kufanya Tathmini na Ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya fedha katika Utekelezaji wa Miradi na utendaji wa shughuli za Serikali, eneo hili kwenye mfumo liwekwe vizuri na liweze kutusaidia,” Alisema.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga, Alisema Mamlaka ya Serikali Mtandao (Ega) imefanya wasilisho zuri lenye kutoa muelekeo wa Utendaji wa Shughuli za Serikali Utakaosaidia Ofisi ya Waziri Mukuu kuratibu vizuri shughuli za utendaji Serikalini katika kuripoti na kufanya Tathmini.

Akiongea baada ya wasilisho hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Sakina Mwinyimkuu alisema, Idara yake Itajitahidi kufuatilia kwa Ukaribu ukamilishwaji wa mfumo huo kwa wakati, ili Taasisi za Umma ziweze kushirikishwa na mfumo uweze kufanya kazi kwa wakati kwenye upimaji wa Utendaji wa Shughuli za Serikali.

Awali, Akiongea katika kikao kazi hicho, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA cha Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Innocent Mboya alisema, Amepokea maelekezo ya kukamilisha mfumo huo ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/2024.

 “Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao, tunaahidi kwamba ndani ya hizi wiki mbili, tutakuwa tumeandaa mpango kazi ambao utatupeleka kwenye ramani na utelekelezaji wa mfumo huu, na ndani ya miezi mitatu tutakuwa tumekamilisha mfumo huu kwa kufuata matakwa na maelekezo ya Serikali.”  Alisisitiza

Walisisho hili ni Sehemu ya Utekelezaji wa Maelekezo ya Mhe. Waziri Mhagama aliyoyatoa katika kikao cha mazingativu kilichofanyika Mkoani Arusha Mapema Mwezi huu.

Read More

Monday, August 14, 2023

NAIBU WAZIRI UMMY, ATOA WITO KWA WANANCHI KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII.Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia na (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga ametoa rai kwa wananchi, Taasisi na Wizara kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutembelea vivutio vyetu vya utalii wa ndani.

Wito huo umetolewa wakati Viongozi na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, walipotembelea Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro baada ya kutoka katika Mkutano wa Mazingativu Mkoani Arusha.

"Tunamshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa alizozifanya katika sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal tour," alibainisha.

"Tumefika Ngorongoro na tumejionea wageni wamefurika wamekuja kujionea vivutio vya utalii." Alisisitiza.

Aidha, alitoa shukrani nyingi Kwa Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa kutoa ruhusa ya kutembelea eneo hilo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.

Aliongeza Kwa kusema kuwa, ziara hiyo imeimarisha upendo, uongozi na urafiki kati ya viongozi na watumishi na itaongeza hari ya utendaji kazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia na (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amesema, ziara hiyo ni Maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu kwa lengo la kuhakikisha kwamba tuna viongozi wa kusimamia Sera na wanalifahamu eneo la utalii wanaloliratibu Sera zake katika Serikali.

"Tumekuja kuona Mazingira halisi ya Utalii pamoja na Mazingira halisi ya Utendaji kazi, Tumeona Utalii umekuwa kwa kiasi kikubwa wageni ni wengi na sisi kama Serikali tunawajibu wa kuhakikisha tunaweka sera bora za kuwasaidia wageni kuendelea kuja nchini," Alisisitiza

Aliendelea kusema kuwa, eneo la Ngorongoro ni zuri linavutia na Watanzania wana fursa ya kuja kujionea.

Read More

Friday, August 11, 2023

WAKULIMA WATAKIWA KUJIFUNZA MBINU BORA ZA KILIMO KUPITIA MAONESHO YA WAKULIMA NANENANE.


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Muhagama amesema maonesho ya kilimo ya Nane Nane ni njia pekee ya wakulima kuweza kujifunza mbinu bora za kilimo cha  kisasa na matumizi ya zana bora za kilimo  zinazoweza kuleta  mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara nchini.

 

Aliyasema hayo mapema , alilpokuwa katika Shehia ya Dole Kizimbani alipokuwa akifunga Maonesho ya wakulima Nane Nane yaliyo washirikisha wadau kutoka sekta binafsi na wakulima 275 wajasiriamali, taasisi binafsi na za Serikali.

 

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Hussen Ali Mwinyi inafanya   juhudi kubwa katika kuibadilisha nchi ili kuweza kuleta madiliko katika sekta za uzalishaji wa chakula na kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wake” alibainisha.

 

Zanzibar imepiga hatua nzuri na matokeo ya Maonesho yatawezesha wakulima kujifunza vitu vipya na kwenda kuleta mapinduzi ya kilimo ambapo wakulima wataźalisha kwa wingi mazao ya biashara ambayo yataongeza mnyororo wa thamani wa mazao na kuweza kufanya baishara katika soko la ndani na nje ya nchi.

 

Akiongea katika maonesho hayo, katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwangiliaji, Maliasili na Mifugo amesema Maonesho hayo yenye lengo la kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima yamedumu kwa siku 10 na kugharimu kiasi cha Shilingi  Milioni Mia Tano fedha za kitanzania.

 

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Umwangiliaji, Maliasili na Mifugo Mhe. Shamata Shaame Khamis ameishukru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mashirikiano yao na kuyawezesha maonesho ya kilimo kwa mwaka 2023 kufanikiwa

 

Aidha aliwashukuru wadau na wananchi wote waliochangia na kuwaomba wakulima kuzidisha bidii na kuja na mbinu mpya za kilimo katika maonesho yajayo

Read More

WAZIRI MHAGAMA, AHIMIZA KUWEPO MUONGOZO NA MFUMO WA UFUATILIAJI NA UTENDAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, Ameitaka Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali, kuharakisha kutengeneza Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Utendaji wa Shughuli za Serikali Pamoja na kukamilisha na kuzindua haraka Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ndani ya nchi utakaotumika na Seriali kwa ujumla, Wizara, Taasisi na maeneo yote ya Utendaji kazi ndani ya Serikali.

 Ameyasema hayo Jijini Arusha, alipofungua Mkutano wa Mazingativu uliyohusisha, Viongozi, watumishi wa Ofisi hiyo Pamoja na Taasisi zake.

Sambamba na hilo, Pamoja na kuonesha Imani wa Mkurugenzi wa Idara hiyo mpya, Waziri Mhagama aliitaka pia idara hiyo kuwa na Ubunifu “Jaribuni kununua mifumo, miundo na taratibu za kufanya ufuatiliaji na Tathmini kutoka kwenye mataifa mengine, ili tuweze kuitangaza Taifa letu kwa kazi hili kuwa tunaweza kufanya vizuri” Alisisitiza Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama alisema anahitaji kupata taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Ofisi yake na Serikali kwa ujumla wa kila robo mwaka ikiwa ni katika kuboresha Eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu Uchapishaji wa Nyaraka za Serikali, Waziri Mhagama alisema katika eneo hilo, katika mwaka huu Mpya wa Fedha 2023/2034, Serikali imejiwekea mkakati wa kuongeza Maduhuli na mapato ya yake kupitia Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ambapo ujenzi wa Mradi wa Mkakati wa kiwanda kipya cha Mpigachapa Mkuu wa Serikali Umefikia asilimia 97% na “Tumeshaanza kufanya manunuzi ya mashine za kisasa, na tumeshafufua mashine ambazo zilikuwa zimehariba.

Nisisitize Chapa muendeshe kiwanda kwa Ubunifu, jengeni fikra mpya boresheni mifumo miundo na namna ya uhifadhi na uchapaji wa nyaraka za Serikali, nataraji kiwanda hiki kinaweza kikajiuza na kinaweza kikapata soko la nchi za kusini mwa Afrika SADC na katika na Soko la  nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, pale mnalo jambo na kazi kubwa ya kufanya, na mazingativu haya yawasaidie kujiongoza na kupata picha na fikra ambazo zitatuvusha.” Alisisitiza Waziri Mhagama

Akiongea katika Mkutano huo wa Mazingativu, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt Jim Yonazi alisema kuwepo kwa Ofisi hiyo Jijini Arusha katika Mkutano huo  ni kutokana na nia ya Ofisi hiyo kuhakikisha kwamba inatenda majukumu yake kwa umakini na kwa utimilifu ikiwa ni pamoja na Uratibu wa shughuli za Serikali kwa ujumla na kwenye maeneo mengine.

“Tunaweza kujifunza kutoka hapa ndani ya nchi mambo mengi na tukatumia ubunifu na wataalam wa ndani katika utendaji na hakuna mtu anaweza kuwa mbunifu katika mazingira yenye stress, hivyo tunaweza kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi na kukuza na kuongeza uelewa katika utendaji.”Alisema

 Kwa kutekeleza Agizo la Mhe. Waziri Mhagama, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Ofisi Hiyo Bi. Sakina Mwinyimkuu alisema, kikosi kazi kitakaa haraka ili kuweza kuandaa mwongozo wa ufuatiliaji na Tathmini na kuhusiana  na kuwa na Mfumo wa Ufuatiiaji na Tathmini, Mkurugenzi alisema kazi hii inafanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Serikali Mtandao (Ega) na maandalizi ya kujengwa kwa mfumo huo yanatarajiwa kuanza.

 Kwa Upande wake Mpigachapa Mkuu wa Serikali Bw. George Lugome alisema, kama Idara imejipanga hasa kwa watumishi kuhakikisha wanafanya kazi katika ubora wa hali ya juu na kuhakikisha, watumishi watapata mafunzo ya kuendesha mashine mpya za kisasa, kuongeza idadi ya watumishi wenye sifa na ueledi katika endeo hilo la uchapaji “Ili kuweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ni lazima pia tuchape nyaraka za Serikali kwa kufuata Ubora na kuweka alama za usalama kulingana na teknolojia zilizopo,na tumeshaanza mikakati ya namna gani ya kushirikiana wenzetu wenye utaalam wa masuala ya usalama katika nyaraka mbalimbali.” Alifafanua

Mada mbalimbali  zinawalishwa katika Mkutano huu wa mazingativu ni Matarajio  ya washiriki wengi kuwa, mkutano huo utawasaidia, kuboresha utendaji wa kazi, kujifunza, kupata ubunifu  katika maeneo yao ya kazi, kuongeza bidii zaidi na hali ya utendaji katika kazi unaoendana na sayansi na teknolojia.

 

Read More

Thursday, August 3, 2023

MRADI WA UJENZI WA MJI WA SERIKALI MTUMBA, UMELETA AJIRA NA KUCHANGIA CHACHU YA UKUAJI WA UCHUMI.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, amesema mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, pamoja na Miradi mingine ya kimkakati imeleta ajira na kuchangia kasi na chachu ya ukuaji wa uchumi hususan katika Jiji la Dodoma.

Ameyasema hayoalipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Jengo la Mpigachapa Mkuu wa Serikali; Jengo la Kituo cha Taifa cha Usimamizi na Uratibu wa Maafa, Jengo la Wizara Mipango na Uwekezaji, na jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu).

Waziri Mhagama alisema kuwa, ujenzi wa Mradi hiyo mikubwa ya kimkakati inayoendelea umewezesha vijana wengi kupata ajira katika maeneo hayo, na kujiongezea pato binafsi sambamba na kuchangia ukuajia wa uchumi kutokana na manunuzi ya bidhaa zinazotumika katika mradi hiyo kufanyika katika viwanda vilivyopo nchini.

Alipokuwa katika jengo la Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Waziri Mhagama alisema kuwa mradi huo, mkubwa umefikia asilimia tisini na saba (97%) ambapo kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na hadhi na sifa ya kuwa ni kiwanda kikubwa kimojawapo cha Serikali,ambapo mashine mpya zimeagizwa na kiwanda hicho  kitafanya kazi za ndani ya nje na nchi za Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ukanda wa nchi za  Kusini mwa Afrika (SADC).

"Sisi tumejipanga kwa matumizi ya ndani na nje pia, nimefarijika kuona ujenzi kwa awamu, hii ya kwanza umefikia hatua kubwa, na ujenzi wa Ofisi umeanza na unaenda kwa kasi." Alisisitiza Waziri Mhagama.

Alipokuwa katika kituo cha Taifa cha Uratibu na Usimamizi wa Maafa Mhe. Mhagama alisema, ujenzi wa awamu ya kwanza ya kituo hicho pia umekamilika kwa Asilimia tisini na nne (94%) na kufafanua kuwa maghala mawili makubwa na Ofisi za Watumishi zimeshakamilika.

"Tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba katika kituo hicho nchi inafikia malengo ya kitaifa na Maono na maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa Ujumla" Alibainisha Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama  Alisema kuwa katika kituo  hicho cha Maafa kutakuwa na vitu vingine vingi ambavyo vinajenga dhana nzima ya uratibu na usimamizi wa Maafa, ambapo kutakuwa na kiwanja ambacho, kitakuwa kinasaidia utuaji na uondokaji wa Helkopta ambazo zitaweza kwenda kwenye shughuli za maafa, kutakuwa na kituo cha tiba kitakachosaidia dharura za maafa hasa katika magonjwa ya milipuko na kitatumika pia katika masuala ya utafiti na tiba na kituo cha mafunzo kwa wataalam ambao watashughulika na usimamizi na uratibu huo wa dharura.

Waziri Mhagama pia alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) pamoja na Jengo la Wizara ya Mipango na uwekezaji katika Mji wa Serikali Mtumba, na kuagiza kuongezeka kwa kazi ya ujenzi ili majengo hayo yaweze kukabidhiwa kwa wakati.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi Hiyo Bw. Anderson Mutatembwa, alisema Ofisi hiyo itasimamia kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama, ikiwa ni pamoja na kuzifanyia kazi chagamoto zilizojitokeza na kuhakikisha zinatatuliwa kwa wakati.

Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mwakilishi na Msimamizi Mkuu wa miradi ya Ujenzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Mhandisi Anania Saudeni, Alikiri kuyapokea maagizo ya Mhe. Waziri Mhagama na kuyatekeleza kwa wakati, kimkataba na kukamilika katika ubora kulingana na maelekezo na kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na Mchana na kuongeza  nguvu kazi ya kutosha na usimamizi madhubuti.

 

Read More