Tuesday, August 29, 2023

DKT. YONAZI: GLOBAL FUND YAIMARISHA SEKTA YA AFYA NCHINI

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameupongeza na kuushukuru Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa mchango mkubwa unaoutoa katika kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu nchini.

 Ametoa pongezi hizo wakati akifungua mkutano wa Uundwaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa kipindi cha mwaka 2024- 2026 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa hoteli ya APC Bunju Dar es Salaam.

 Mkutano huo ulioudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sekretarieti ya TNCM, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Pamoja na Asasi za Kiraia.

 Akieleza kuhusu mchango wa Mfuko wa Dunia katika sekta ya afya nchini, Dkt. Yonazi alisema kuwa, nchi imeendelea kupiga hatua kwa kuzingatia ufadhali wanaoutoka kwa lengo la kugharamia miradi ya Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI na Uimarishaji wa Mifumo ya Utoaji wa Huduma za afya.

 “Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kupitia ushirikiano thabiti na misaada mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Mfuko wa Dunia yaani Global Fund,”.Alisisitiza

 Aidha alisema kuwa Tanzania bado ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na changamoto za magonjwa hayo na yameendelea kusababisha vifo kwa wananchi walio wengi hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

 Alitumia jukwaa hilo kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

 “Ushirikishwaji wa Wadau Watekelezaji wa Nje ya Serikali (PR2) katika mapambano haya ni kipaumbele cha Serikali yetu. Niwaombe wadau wetu kwa pamoja tushirikiane kufikisha huduma hizi katika jamii yote inayotuzunguka.Ninawasihi muendelee kushirikiana na Serikali katika kuleta uzoefu hususan pale tunapohitajika kuongeza ufanisi na tija katika miradi na huduma za afya,”.Alisema Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tanzania Natioanal Coordinationg Mechanism (TNCM) Dkt. Rachel Makunde alimshukuru Katibu Mkuu ambaye pia ni mwenyekiti wa TNCM kwa usimamizi wake na mchango anaoutoka katika kuyafika malengo ya chombo hicho.

 Naye Dkt. David Sando, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la MDH aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Program hizo ili kuimarisha huduma za afya nchini.

 “Tumeendelea kusupport zaidi ya wagonjwa laki tatu wanaotumia dawa za kufubaza Makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) na kupitia miradi ya HIV, tumeweza kuwafikia wagonjwa wengi katika mikoa 12 tunayoihudumia ambapo ni zaidi ya nusu ya wagonjwa wote nchini,” alieleza Dkt. Sando


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.