Saturday, April 27, 2024

WANANCHI WAPEWA SHIME KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI NCHINI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ametoa shime kwa Baraza la Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali kutambua mawanda makubwa ya uwekezaji yaliyo katika nchi yetu.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya kimkakati na uwekezaji lilofanyika katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Jijini Dar es salaam.

Waziri Mhagama amesema kuwa sekta binafsi na wadau mbalimbali waendelee kutoa mapendekezo kwenye fursa mbalimbali zinazojitokeza za kiuchumi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kiuchumi kufikia malengo yaliyopo.

Ameongeza kusema wananchi wa Tanzania wako tayari, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ameonesha kwa vitendo kwamba yuko tayari hivyo ni vyema kumuunga mkono kwa kufanya kazi ili kujenga uchumi wa Taifa.

Aidha jukwaa hilo litasaidia kujenga uelewa wa pamoja juu ya mafanikio yaliyopatikana na katika uwekezaji na ustawi wake wa kiuchumi.

Waziri aliongezea dhana ya kongamano hilo lenye  kauli Mbiu ya “Wekeza Tanzania kuongeza thamani ya ziada” linatumika kujenga uchumi imara ambao umeshirikisha Watanzania wengi.

“Na itatutengenezea mazingira mazuri ya biashara ambayo yatachochea wananchi wengi katika uwekezaji na ushiriki wao katika kujenga uchumi,"alisema Waziri Mhagama

Baraza la Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi limeingia makubaliano na taasisi ya serikali inayosimamia manunuzi ya umma, katika moja ya kipengele katika sheria ya manunuzi ya umma kinachosisitiza kila asilimia 30 ya manunuzi ya umma ya kila mradi yaende kwa vijana, wanawake wazee na watu wenye ulemavu ambayo ni sehemu ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

 

Kwa upande wake Bibi, Beng’i Issa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi wa Kiuchumi (NEEC) amesema moja ya mambo wanayosimamia ni kuangalia kampuni zinazopata kazi kwenye miradi ya kiuchumi na bidhaa zinazouzwa katika miradi hiyo  zinatoka nchini.

Aidha kwenye ajira Baraza la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi linaangalia ajira za moja kwa moja na ajira ambazo sio za moja kwa moja katika uhaulishaji wa teknolojia kwa kusimamia teknolojia nchini na mipango ya kutoa mafunzo ya kuhaulisha inafanyika

Akizungumzia kuhusu kongamano amesema kongamano hilo la Nne limelenga katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini pamoja na kushirikishana mafanikio na changamoto zilizopo katika ushiriki wa watanzania katika uwekezaji.

Read More

Friday, April 12, 2024

WAZIRI MHAGAMA “AWATAKA WANANCHI KUONDOKA MAENEO HATARISHI”


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amewataka  wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi  ili kujikinga na mafurikio ya mvua za vuli zinazoendelea kunyesha.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelea na kujionea maeneo yaliyokubwa na mafuriko ya mvua katika Halmashauri  ya Mlimba Mkoani Morogoro ambapo amewaomba wananchi kuendelea kufuatilia na kusikiliza ushauri wa serikali.

Niwaombe wananchi tuendelee kushikamana ili kupambana na majanga ya Mvua na Mafuriko, ambayo yameleta kadhia kubwa sana kwa wananchi.

“Serikali imetengeneza Mpango wa Dharura wa kukabiliana na mvua za El Nino na mvua za Masika, ambapo serikali itafanya kila linalowezekana kuzuia madhara yasitokee na hasa maisha ya watanzania,” alisema Waziri Mhagama

Ameongeza kusema mafuriko ya maji yamesababisha udongo kumomonyoka na kuharibu miundo mbinu ya reli na kuleta madhara mengine mengi niwaombe wanamlimba tuendelee kuangalia na kusikiliza ushauri wa serikali.

“Serikali itaendelea kuhakikisha inapambana dhidi ya magonjwa ya Mlipuko na uhaba wa chakula  na madhara mengine ambayo yameathiri wananchi, serikali itakuwa pamoja na nyinyi katika kutatua kadhia hizo alibainisha,” Waziri Mhagama

Niwaombe wananchi tuendelee kumuomba mwenyezi Mungu hali iliyopo mbele yetu iweze kupita kwa haraka na ipite kwa usalama mkubwa.

 Ameeleza kwamba katika utabiri wa hali ya hewa unaoendelea kutolewa unaonesha mvua hizi zinaendelea kunyesha hivyo ni vyema tukaendelea kujichukulia tahadhari sisi wenyewe.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mhe. Dustan Kyobya amesema changamaoto ya Mawasiliano ya barabara kwa watu wa Masagati na Utengule kwao wamekuwa kisiwa kutokana na miundo mbinu ya barabara kutopitika, lakini pia Mawasiliano kati ya Jimbo la Ifakara na Mlimba ambazo zinatengeneza wilaya ya kilombero nayo ni magumu.

Aidha Miundo mbinu ya reli ilidondokewa na udongo na kusababisha kukatika kwa makalvati ya reli hivyo kusababisha usafiri wa kutoka Mlimba kuelekea makambako kutokuwepo.

“Nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ndege kwa ajili ya kuokoa watu waliokwama na kuruhusu treni ya Mwakyembe  kuanza kubeba abiria ili kurahisisha mawasiliano,” alisema Mkuu wa wilaya

 

Awali Bi, Zainabu Makenjula Mkazi wa Mlimba ameomba serikali kushughulikia swala la barabara kwa wakati ili kurahisisha mawasiliano na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa sababu kuna maeneo magari wala pikipiki haviwezi kupita.

 

Read More