Monday, October 30, 2023

PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP) YAMEWEZESHA TAFITI ZA TEKNOLOJIA YA KISASA ZA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI.


 

Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi (AFDP) imewezesha Tafiti za Kiteknolijia kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) katika kuzalisha mbegu za kisasa zenye uwezo wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibi) Mhe. Ummy Nderianaga wakati wa wasilisho la Taarifa ya Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Bungeni Dodoma.

Akitolea mfano aina ya mbegu sita za mahindi ikiwa ni Pamoja na Situka M1, TMV1, STAHA, Bora, T104 na T105, kuwa zikipandwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo zinapelekea kuleta matokeao bora na Tafiti zinaonesha kuwa mbegu hizi zina uwezo mkubwa wa ustahimilivu dhidi ya changamoto mbalimbali za mabadiliko tabianchi.

Akiongelea suala la usalama wa chakula, Naibu Waziri Nderianaga alisema kuwa suala hili linakwenda sambamba na kipengele cha Usalama wa mbengu. “tulimaliza hivi punde mkutano wa Chakula Afrika na Tanzania imeonekana kuwa ni kitovu kwenye suala la chakula hivyo kama hatutakuwa na mbegu Bora na nzuri kufikia malengo itakuwa ni kazi.” Alibainisha

Kwa upande Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Salimu Mwinjaka, alisema katika sekta ya Kilimo, Programu hii ya kimkakati inalenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima, na jitihada kubwa ni kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua sambamba na kuihamasisha jamii ya wakulima, umuhimu wa kutumia mbegu bora katika kuleta tija na mageuzi ya kilimo.

Akiongoza kikao hicho, Kaimu Mwenyetiki wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo Alisema “Tumeona mikakati Mizuri ya Serikali ambayo imewekwa hasa katika suala la mbegu, hii ni kuhakikisha kwamba suala zima la uzalishwaji wa mbegu bora na kwa wakati linafanikiwa.”

Akiongea katika kikao hicho, Mhe. Boniphace Nyangindu Butondo (Mjumbe wa kamati) alishauri Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) kuwa na mkakati wa kuzalisha mbegu zenye tija za kutosha na kuangalia mbegu za mazao mengine kama vile Mtama, Mpunga na Pamba na kuzalisha mbegu za kutosha za Asili ili kuweza kukabiliana na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea kwani mbegu nyingi za kisasa zinaonesha kushambuliwa na wadudu mbalimbali.

 Kwa Upande wake Mhe. Dkt. Alice Kaijage (Mjumbe wa Kamati) Alishauri Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) kuongeza uwanda wa Tafiti hususani katika zao la Alizeti, kama linaweza kustawi bila tatizo katika mikoa mingine tofauti na Singida, akitolea mfano Mkoa wa Pwani.

Awali akiongelea suala la Mbegu la Asili, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) Dkt. Sophia Kashenge Kilenga, Alisema kuna nasaba nyingi sana ya benki ya Mbegu za asili Mkoani Arusha,”Ni kweli kabisa Mbegu za Asili zina sifa ambazo kila mtu anahitaji, na zina nasaba nyingi mchanganyiko zinazopelekea ukuaji wa mbegu kwenda polepole na una mipaka, hivyo kwa ukuaji wa sasa wa idadi ya watu ni vyema kuwa na maeneo maalum ambayo mbegu za asili zitatumika na kwa kulisha idadi kubwa ya watu ni vizuri kutumika kwa mbegu zinazozaa kwa wingi katika eneo dogo.

 

Read More

Thursday, October 12, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU

 


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo wakati kamati ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) katika katika Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza mara baada ya kukagua vikundi vya vijana vikiwemo  Sitetereki kilichopo Kata ya Old Shinyanga, Jahazi, Kata ya Ibadakuli na Tunaweza katika Kata ya Kolandoto Mhe. Nyongo amesema lengo la ziara ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

“Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kumlinda mtoto wa kike hasa katika gonjwa kubwa la UKIMWI, namna ya kumkomboa mtoto wa kike, kujifunza kazi za ujasiliamali ili kujikwamua katika maisha pamoja  kupaza sauti dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo sisi kama wabunge tumeridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali,”Amesema Mwenyekiti huyo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaomba vijana wa kike kuendelea kujiamini na kufanya kazi vizuri kwani Serrikali ya Awamu ya Sita inawajali vijana na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia ziara hiyo  Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Hassan Mtenga  ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kukamilisha na kujengwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo huku akiipongeza TACAIDS na wadau wa maendeleo kuwa na mwamko wa kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

“Tumejifunza kitu kwasababu  tunao watu wako tayari kupiga vita janga  kuu la UKIMWI na niishukuru TACAIDS, Mawaziri wenye dhamana na hawa wadada ambao  wameamua kutoka kwenye  sughuli za kuuza bar na kuanzisha biashara  zao sasa uwe mfano  wa kuigwa kwa maeneo mengine,”Amepongeza Mhe. Mtenga.

Vilevile Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Christina Mnzava amesema wazazi na walezi wana wajibu wa kusimamia malezi sahihi ya watoto ili kuwakomboa katika tabia hatarishi huku  akiupongeza Mpango wa Dream kwa kuamua  kuwafikia mabinti katika maeneo yao akishauri mradi huo kuongeza wigo na kuwafikia vijana wengine  waliopo Vijijini .

“Sisi kama wazazi na walezi tunaweza kuwakomboa watoto wetu katika tabia hatarishi ambazo wanazipata mtaani kuna wengine walikuwa wanauza miili yao, lakini kutokana na mradi huu wamejikwamua wamefundishwa ujasiriamali, kuwekeza tumeona wasichana wamejitambua wanatengeneza sabuni, batiki, vyungu katika vikundi vya Kata za Old Shinyanga, Ibadakuli na Kolandoto kwa kweli wamefanya vizuri,”Ameeleza Mjumbe huyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Christina Mndeme amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuondoa unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU ambao upo juu, kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi ili muda mwingi wautumie kwenye uzalishaji na sio kwenye mambo yanayoweza kuwasababishai maambukizi ya VVU,kuelimisha jamii kuacha mila potofu ambazo zinasababisha ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) Bi. Agnes Junga amefafanua kuwa lengo la Mpango huo ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa wasichana kuanzia umri wa miaka Tisa hadi 24.

“Mpango huu ulizinduliwa 2014 ukilenga kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Nchi 13 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania ambapo tulianza na Halmashauri Sita na hadi sasa tumefikia Halmashauri 12. Shirika la (FHI360) kwenye mradi wa EPIC tunatekeleza Dreams katika Mikoa miwili ya Shinyanga ndani ya Halmashauri Tano na Iringa katika Halmashauri mbili na tunawafikia wasichana kuanzia miaka 15 hadi 25 walio nje ya shule pamoja na wazazi au walezi na jamii kwa ujumla tuhakikishe msichana anafikia ndoto zake.

Aidha akizungumza kwa niaba ya wanakikundi kutoka Vikundi vya Mabinti Balehe na Wanawake Vijana vya Sitetereki, Tunaweza na Jahazi mwanakikundi Sungi Leonard amesema uanzishwaji wa vikundi hivyo vimewasaidia kama mabinti kujitambua, kufahamu elimu ya afya, kuwajengea uwezo wa kukabiliana na vitendo vya kikatili pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kuwawezesha kiuchumi.

“Nilikutana na mwezeshaji kiuchumi na mwelimishaji rika nikapata elimu ya ukatili wa kijinsia, umuhimu wa upimaji wa afya, matumizi sahihi ya kinga, magonjwa ya ngono na VVU ambayo imenisaidia kujitambua kama binti. Pia nilifanikiwa kujiunga katika kikundi cha Sitetereki nikajifunza kutengeneza batiki kazi ambayo inanipatia kipato na ninamudu mahitaji yangu tofauti na ilivyokuwa awali,” Ameshukuru Mwanakikundi huyo.

Read More

Wednesday, October 11, 2023

WAZIRI MHAGAMA, AZINDUA MUONGOZO WA UWEKEZAJI MKOA WA MANYARA.


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa watendaji wa Serikali; kujipanga na kuhakikisha Muongozo wa uwekezaji kwa Mkoa Manyara unawafikia wananchi wote ili kufanya kazi kwa tija.

Kauli hiyo ameitoa Mkoani Manyara wakati wa Ufunguzi wa wiki ya Kitaifa ya Vijana tukio alilolifanya kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

“Tunataka Muongozo huu uweze kutoa fursa nyingi kwa vijana ili uweze kujenga kizazi ambacho kitatatumia Muongozo huu kwa muda mrefu” alieleza.

Aliendelea kusema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu italeta timu ya baraza la uwezeshaji kiuchumi, timu ambayo itasaidia kujenga uwezo kwenye dhana kutengeneza vitu asilia (Local content) ili kuongeza tija na kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea wanawekezaji.

“Makapuni yaliyowekeza katika Mkoa wa Manyara yaone namna ya kutumia fedha zile zinazorudi kwa jamii, kwa kuwekeza katika vikundi vya vijana wabunifu ili kupitia muongozo wa uwekezaji usaidie kuleta tija kwa vijana na maendeleo ya Mkoa,” alihimiza

Akizungumza kuhusu madhimisho ya wiki ya vijana, Mhe. Waziri Mhagama amesema ubunifu aliyouona wakati alipotembelea Mabanda, hasa uliofanywa na kijana Said Mussa wa kubuni namna ya kutengeneza taa za magari zilozoharibika na kurudisha katika muonekano mpya ni ubunifu mzuri.

“Kijana Huyu wa Kitanzania akifanikiwa kuhuisha teknolojia hiyo basi tutakuwa uwezo huko mbele kujenga viwanda vidogo vidogo vingi vya kuzalisha taa za magari nakusaidia kuongeza pato la kigeni na Kubrand Tanzania ya Mhe. Samia Kupitia Ubunifu wa Vijana,” alisema.

Namshukuru sana Mhe. Mhe. Prof. Joyce L. Ndalichako na Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian John Luhemeja kwa kuridhia kumpatia Mkopo kijana huyu ili kuhakikisha anafanya vizuri katika ugunduzi alioufanya.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi vijana ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Joyce Ndalichako amesema wiki ya vijana inalenga kutambua Mchango wa Waasisi wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekh Abeid Amani Karume.

 

Ameongeza kusema Maadhimisho ya wiki ya vijana Kitaifa ya Mwaka 2023 yanayofanyika Mkoani Manyara, kauli mbiu yake ni,” Vijana na Ujuzi Rafiki kwa Mazingira na Maendeleo Endelevu”. Maadhimisho ya vijana yanakutanisha vijana na wananchi wa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo vijana wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu. Ni fursa kwa Serikali na Wadau kutambua mchango mzuri wa vijana kwa maendeleo ya nchi yetu.

 “Natoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuthamini vijana wa Tanzania kwa matendo kwa kuhakikisha vijana wanapatiwa mitaji ya kuendeleza biashara zao au kwa kuanzisha shughuli za maendeleo,” alibainisha

Awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bi, Queen Sendiga alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuchagua Manyara kuwa Mwenyeji wa Kilele cha Madhimisho ya Siku ya vijana kitaifa, Mwenyeji wa Misa Maalumu ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa, na Mwenyeji wa Killele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.

“Moja ya mambo makubwa yatakayoachwa katika Mkoa wa Manyara, kutokana na kuwa Mwenyeji wa kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru ni pamoja na Ujenzi wa uwanja Mkubwa wa kisasa wa Mpira wa Miguu ambao Umejengwa kwa hadhi,” alisema

Read More

Friday, October 6, 2023

IDARA YA MENEJIMENTI YA MAAFA NCHINI YASHIRIKISHA UJUZI KWA WANAFUNZI NA WAKUFUNZI KUTOKA MALAWI


 

Idara ya Menejimenti ya Maafa Nchini yashirikisha ujuzi wa masuala ya usimamizi wa maafa kwa wanafunzi na wakufunzi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Jeshi la Ulinzi la Malawi walifanya ziara yao ya mafunzo nchini Tanzania.

 Akizungumza wakati wa kikao kilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam kilicholenga kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa maafa kati ya wataalam wa Ofisi ya Waziri Mkuu na ujumbe wa wanafunzi na wakufunzi kutoka chuo hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi wa maafa na kueleza kuwa ujio wao ni moja ya ishara kuwa nchi hizo mbili zimeendelea kuwa na mahusiano mazuri na kupongeza hatua hiyo.

 “Hatua hii ya kukutana pamoja na kupeana uzoefu imetufariji na inaimarisha umoja baina yetu, hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo na Serikali ya Jamhuri ya Malawi katika masuala ya menejimenti ya maafa kwa kuhakikisha tunatumia fursa zilizopo katika kuyafikia malengo hayo,”alisema Kanali Masalamado.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaeleza kuwa, Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kiutendaji katika kukabiliana na maafa huku akisema uwepo wa Teknolojia ya TEHAMA umeendelea kurahisisha masuala ya usimamizi wa maafa nchini hasa upande wa mawasilisno wakati wa dharura kwa kuanzishwa kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharula katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambacho kimerahisisha mawasiliano kwa ajili ya upatikanaji wa taarifa za maafa nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Jeshi la Ulinzi la Malawi na kiongozi wa msafara huo kutoka chuo hicho, Brigedia Jen. Luke Mwetseni amepongeza namna nchi ya Tanzania inavyoendelea na masuala ya menejimenti ya maafa huku akishukuru namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyowasaidia wakati wa maafa ya Kimbunga Freddy kilichotokea Machi, 2023 ambapo Tanzania ilitoa misaada mbalimbali ikiwemo ya kibinadamu na fedha kwa Taifa hilo.

“Serikali ya Tanzania ilitushika mkono wakati wa maafa ya Kimbunga Freddy kwa kutupatia Mablanketi, madawa ya binadamu, fedha pamoja na ndege kutoka jeshi la Wananchi wa Tanzania zilizosafiri kuja Malawi kwa lengo la wokozi, tunashukuru sana kwa namna mlivyojali, hii inaonesha namna mlivyojipanga katika masuala ya menejimenti ya maafa hongereni sana,” alisema Brig Jen. Mwetseni

Aidha alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake makini katika masuala ya Menejimenti ya maafa na kusema kuwa wanaitumia Tanzania kama nchi ya mfano kuja kujifunza kwa vitendo namna inavyoratibu masuala ya maafa ili kuendelea kuwa na jamii stahimilivu katika maafa.

“Kwa kutambua mchango wenu tumekuja na tuzo hii maalum kwa ajili ya kuonesha kuwa tulitambua na kujali Serikali yenu ilivyotutendea sisi watu wa Malawi wakati wa maafa, tunaahidi kuendelea kushirikiana katika kuimarisha umoja huo,” alisisitiza Brigedia Jen. Mwetseni.

Awali alisema kuwa, ujio wao nchini unatija kubwa na utasaidia wanafunzi hao kuongeza ujezi utakao wasaidia wanapoelekea kumaliza mafunzo katika chuo hicho pamoja na kuwaongezea maarifa katika utendaji kazi wao.

 

Read More

Thursday, October 5, 2023

KATIBU MKUU KIONGOZI AIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA USIMAMIZI MZURI WA UJENZI WA MJI WA SERIKALI

 


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Uratibu na Usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Ametoa pongezi hizo mapema leo, alipokuwa katika ziara maalum ya Makatibu Wakuu ya kutembelea mji wa Serikali Mtumba Dodoma ambapo alisema mafanikio ya mradi huu wa ujenzi wa Mji wa Serikali ni kukamilika kwa ukamilifu wake akitolea mfano ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa kuwa ni alama kubwa ambao utatumika kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na wageni kujifunza nini ambacho Tanzania imefanya.

“Tunathamini kazi yenu kubwa sana mnayofanya, kama tulivyosema awali kwenye Wasilisho, hii kazi inahitaji Uratibu kwa Sababu ni kazi ya Serikali, siyo kazi ya mmoja kuwa amemaliza na wengine kujisikia vibaya, tunashukuru kwa kutupitisha kwenye kazi kuanzia mwanzo, tumeona juhudi kubwa za wataalamu wetu na wasimamizi lakini pia tumeona kazi kubwa iliyopo mbele na tunatambua kwamba baadhi ya wadau wanakaribia kumaliza kazi zao.” Alisema Mhe. Balozi Kusiluka.

 Aliendelea kusema kuwa bado kuna muda wa kutosha wa kutatua Changamoto ndogo zilizobainika katika ziara hiyo; na kusisitiza kuutazama mradi huo kwa ujumla wake kama Serikali moja, na kazi ya uratibu ikiendelea lakini pamoja na kuimarisha timu ya wataalamu wa ngazi zote katika ujenzi na kuwasikiliza, “Ni Fursa Pekee ambayo tumepewa ya kujenga Makao Makuu ya Serikali mapya  na Serikali imetoa fedha nyingi kwa hivyo ni lazima sisi wataalam tufanye kazi inavyopaswa.” Alisisitiza.

Alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo, na kuwapa uhuru wataalam kufanya kazi ya kitaalam inavyopaswa, na kushauri wadau wengi kushiriki katika kazi hiyo pamoja na kujadili mambo ya kitaalam ili watu wengi waweze kujifunza

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonaz alisema swala la ushirikishwaji wa wataalam katika ujenzi wa mji wa Serikali ni swala la muhimu sana, na wadau mbalimbali wanashirikishwa kwa ajili ya kuja kuwekeza katika maeneo mbali mbali  ambayo yametengwa katika mji huo wa Serikali,na majengo hayo ya Mji wa Serikali yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.

 

Read More