Thursday, January 13, 2022

Waziri Mhagama Akabidhi Rasmi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mawaziri Wapya

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi Nyaraka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Mhe. Dkt. Pindi Chana kama ishara ya kumkabidhi rasmi ofisi hiyo, kulia tarehe 13 Januari, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi Nyaraka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako kama ishara ya kumkabidhi rasmi ofisi hiyo, kulia ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Dkt. Pindi Chana tarehe 13 Januari, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama  amekabidhi rasmi ofisi kwa Waziri  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Dkt. Pindi Chana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako  ili kuendelea na majukumu katika ofisi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano  ya ofisi hiyo Januari 13, 2022 Jijini Dodoma  Mhe. Mhagama alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa kuhudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka saba  ambapo  amewashukuru watumishi kwa ushirikiano walioutoa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi kupitia  nafasi aliyoteuliwa kutumikia  ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Ubora kwa kuendelea kutatua changamoto za watumishi wa umma , kusimamia haki za watumishi wa umma kuhakikisha wanatumikia wananchi kwa weledi kwa ustawi wa Taifa.

“Ninajua kiu ya watumishi wa umma ndani ya Nchi yetu, ninajua vilio vya madaraja ninajua vilio vya watendaji ambao wakati mwingine hawataki kutoa haki kwa watumishi wa umma ninajua masuala yote yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma ninaomba niwaambie bado ni sehemu ya utendaji wa kazi wa Serikali ili yale mambo yanayohusiana na utumishi wa umma nipo bado pamoja na nyie,” alisema Mhe. Mhagama.

Hata hivyo aliwasihi watumishi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mawaziri walioteuliwa katika Ofisi hiyo pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla na wananchi wake.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Mhe.  Dkt. Pindi Chana alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na  kumteua kutumikia nafasi hiyo huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na utayari wake kushirikiana na watumishi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

Katika hatua nyingine Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu  Mhe. Prof. Joyce Ndaliachako aliwaomba watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa mshikamano kuhakikisha Taifa linapata maendeleo na wananchi wake na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake aliyekuwa Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu  Tixon Nzunda amekabidhi ofisi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Dkt. John Jingu  na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu.

Akiaga watumishi wa ofisi hiyo Katibu Mkuu Nzunda aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu  Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo alimshukuru Mhe. Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kumuamini na kumruhusu kuendelea kuwatumikia wananchi .

“Nataka niwahakikishie  Makatibu Wakuu wenzangu timu hii mnayoiona ni nzuri na itawapa ushirikiano , timu imara, ni watu wanaofanya kazi usiku na mchana kwa hiyo nawapongeza kwa kuungana na familia ya ofisi ya Waziri Mkuu kwahiyo ninaomba ushirikiano mliokuwa mnanipa mkawape makatibu hawa kuhakikisha ile misingi ya uwajibikaji na weledi inaendelezwa,” alisema Nzunda.

Sambamba na hilo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Dkt. John Jingu alieleza kwamba fursa hiyo kwake ni nafasi muhimu ya kutoa mchango wa maendeleo ya Taifa huku akiwasisitiza watumishi hao  kuwa huru kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha, kujenga na kuimarisha shughuli za uratibu wa Serikali.

“Namshukuru Mhe. Rais kwa kuona naweza kutoa mchango kwa kuhudumu Pamoja nanyi katika ofisi hii niwaombe ushirikiano maana kila mmoja hapa ni gwiji katika eneo lake na nimekuja kufanya kazi na nyie. Moja ya kazi yangu ni kujifunza kutoka kwenu ili twende pamoja mlango uko wazi ukiwa na wazo unalofikiri litachangia katika kuboresha utendaji wetu wa kazi nakukaribisha kutoa maoni yako ili twende na kasi ya Awamu ya Sita,”alibainisha Dkt. Jingu .

Vile vile Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi kuhakikisha ndoto ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafikia wananchi kwa huduma bora inafikiwa.

Aidha Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Bw. Kasper Mmuya alieleza furaha yake ya kuendelea kuhudumu katika ofisi hiyo huku akiwaasa wafanyakazi kutumia muda wao vizuri wawapo kazini kwa kuhudumia na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakizingatia taaluma walizonazo.

Read More

Katibu Mkuu Nzunda Akabidhi Rasmi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Makatibu Wakuu Wapya

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda akizungumza na menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika ukumbi wa Ofisi hiyo Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda akimkabidhi nyaraka Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Dkt. John Jingu wakati wa hafla ya makabidhiano rasmi ya ofisi hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (ngome) Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda akimkabidhi nyaraka Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katibu wakati wa hafla ya makabidhiano rasmi ya ofisi hiyo iliyofanyika katika Januari 13, 2022  Dodoma.

Read More

Thursday, January 6, 2022

Vijana Wahamasishwa Kuwekeza Katika Shughuli za Kiuchumi

 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kaspar Mmuya akizungumza na vijana wakati wa hafla ya Ufungaji wa Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana yaliyofanyika katika Kituo cha Elimu kwa Jamii (Maktaba) Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Januari 6, 2022.

 

Sehemu ya Vijana wakisikiliza hotuba ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Kaspar Mmuya (hayupo pichani) wakati wa Ufungaji wa Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana yaliyofanyika katika Kituo cha Elimu kwa Jamii (Maktaba) Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kaspar Mmuya akikabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa Tipis Masiaya (kulia), mmoja wa vijana walioshiriki mafunzo hayo. 

 


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Julius Tweneshe akieleza jambo wakati wa hafla hiyo ya Ufungaji wa Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana yaliyofanyika katika Kituo cha Elimu kwa Jamii (Maktaba) Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.

 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kaspar Mmuya (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Halmashauri ya Kiteto, Benki ya CRDB, NMB, SIDO na vijana walioshiriki katika mafunzo hayo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara yaliyofanyika katika Kituo cha Elimu kwa Jamii (Maktaba) Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Januari 6, 2022.

 

Na: Mwandishi Wetu – Kiteto, MANYARA

Vijana nchini wahamasishwa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuanzisha miradi au shughuli za uzalishaji mali zenye tija zitakazowawezesha kuchangamkia na kusimamia ipasavyo fursa mbalimbali za kukua kiuchumi na kuchangia pato la taifa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaspar Mmuya ameyasema hayo Januari 6, 2022 wakati wa Ufungaji wa Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.

Naibu Katibu Mkuu alieleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inasimamia utekelezaji wa afua za kushughulikia mahitaji ya makundi maalum ya vijana wakiwemo vijana kutoka jamii ya wafugaji kama ilivyoanishwa kwenye Ibara ya 3.25 ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, hivyo kupitia afua hiyo vijana hupatiwa mafunzo ya ujuzi tepe kulingana na mahitaji yao ambapo huhamasishwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali na kuunganishwa kwenye fursa za uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia asilimia 4% ya mapato ya Halmashauri na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa vijana katika kukuza uchumi wa nchi, hamasa kubwa imekuwa ikitolewa na viongozi kwa vijana wazawa kuanzisha viwanda, makampuni na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zenye tija zitakazowafanya wanakuwa kiuchumi na kujiletea maendeleo katika jamii zao,” alisema Naibu Katibu Mkuu Mmuya  

“Hapa Kiteto mnaongoza kwa uzalishaji wa mahindi bora na alizeti, hiyo ni fursa kwenu vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyo zalisha bidhaa zinazotokana na mazao hayo,” alisema

Alifafanua kuwa, Serikali inatambua vijana ni kundi kubwa linalofanya nguvukazi ya taifa, kwa mujibu wa taarifa za Shirika la takwimu la Taifa (NBS) inakadiriwa kuwa idadi ya vijana nchini ni Milioni 17.7 sawa na ailimia 31.5% ya Idadi ya watu wote nchini ambapo kati ya vijana 17.7 vijana wenye uwezo wa kufanya kazi ni Milioni 14.2 Sawa na asilimia 80.3% (Ripoti ya Matokeo ya utafiti wa Nguvu Kazi ya mwaka 2020/2021).

“Asilimia kubwa ya vijana wanaishi vijijini ambapo wanajishughulisha na kilimo na ufugaji katika kuendesha Maisha yao, hivyo kutokana na takwimu hizo, Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha mazingira katika sekta ya kilimo na ufugaji ili vijana wengi waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kujiletea maendeleo,” alieleza Mmuya

Aliongeza kuwa lengo la mafunzo haya ni kubadilisha mitazamo ya vijana katika kuchangamkia fursa mbalimbali za kuichumi ndio maana mwitikio wa vijana katika Halmashauri ya Kiteto kushiriki mafunzo hayo ni mkubwa sana.

“Katika Mkoa huu wa Manyara, Halmashauri ya Kiteto ambapo mafunzo haya yamefanyika vijana wameonesha uhitaji mkubwa wa kupatiwa mafunzo haya. Hali hii inaashiria kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu kwa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa mafanikio na tija.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alitumia fursa hiyo kuhimiza Halmashauri zote nchini kuwezesha vijana kiuchumi kupitia kupitia mikopo inayotolewa kwa Vijana asilimia 4%, Wanawake asilimia 4% na Watu wenye Ulemavu asilimia 2%.

Sambamba na hayo aliwataka Maafisa Maandeleo ya Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweka mifumo na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji wa vikundi vya vijana vinavyopatiwa mikopo na Halmashauri ili kupata matokeo yenye tija ya maendeleo ya fedha hizo za serikali zinazotolewa moja kwa moja kwa wananchi. Pamoja na hayo amewataka vijana kutumia fursa hiyo kujifunza kwa umakini mkubwa ili muweze kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika kuendesha miradi yenu na kujikwamua kiuchumi.

Pia, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kuendelea kusaidia jitihada za Serikali katika kutekeleza programu mbalimbali za Maendeleo ya vijana nchini.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Julius Tweneshe alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuyafikia na kuyawezesha kiuchumi makundi yote ya vijana yanayojumuisha waliopo mijini, vijijini, wenye mahitaji maalumu ikiwemo vijana wa kike na kiume, Vijana wanaotoka katika jamii za wakulima na wafugaji na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi.

“Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana tumeweka mikakati ya kuwasaidia vijana kwa kuhakikisha kuwa tunayafikia makundi yote maalumu ya vijana likiwemo kundi lenu hili la vijana kutoka kwenye Jamii ya Wafugaji,” alisema

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Kiteto, Bi. Beatrice Rumbeli ambaye ni Afisa Mipango alisema kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa katika shughuli za kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwemo kutoa mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu.

“Katika Mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Kiteto ilitenga kiasi cha shilingi milioni 183 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu ambapo hadi sasa jumla ya milioni 120 zimekwisha tolewa kwenye vikundi,” alieleza Rumbeli

Naye Kijana Mnufaika wa Mafunzo hayo Bw. Marisix Urasa, aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara yaliyoanza kutolewa katika Halmashauri hiyo ya Kiteto kuanzia tarehe 04 hadi 06 Januari, 2022 ambapo alieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni chachu kwa vijana katika wilaya hiyo kubadilika kifikra kwa kuanza kurasimisha na kuboresha biashara zao.

“Sisi vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto tunatambua Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasimamia utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuhusu kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, hivyo sisi vijana kama nguvukazi ya Taifa tunao mchango mkubwa katika kufanikisha jitihada hizo za Serikali na za Viongozi wetu wa nchi ili kufikia malengo ya mpango huo,” alisema Urasa

MWISHO


Read More