Tuesday, July 31, 2018

MFUKO MPYA WA HIFADHI YA JAMII PSSSF KUANZA KAZI AGOSTI MOSI MWAKA HUU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitangaza rasmi leo Jijini Dodoma tarehe ya kuanza  kufanya kazi kwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  ambapo mfuko huo unaanza kazi Agosti Mosi mwaka huu.Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera na Uratibu Prof. Faustine Kamuzora.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge  Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  unaanza kutekleza majukumu yake bila kuathiri huduma kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma  (PSSSF) Bw. Eliud Sanga (katikati) akisisitiza kuhusu hatua watakazochukua kuhakikisha kuwa mfuko huo mpya unatatua changamoto zilizokuwepo awali katika mifuko iliyounganishwa kuunda mfuko huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kutangaza tarehe ya kuanza rasmi kufanya kazi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF) leo Jijini Dodoma.Kulia ni Mkurugenzi mkuu wa SSRA Dkt. Irene  Isaka.
Na Mwandishi wetu
Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) kuanzia Agosti 1, mwaka huu.
Akizungumza  na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali imekamikisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.
"Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF", alisisitiza mhe. Mhagama
Waziri Mhagama amefafanua kuwa, kutokana na hatua hiyo wafanyakazi wote watakaoajiriwa katika sekta ya umma watasajiliwa katika Mfuko wa PSSSF na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF.
Anaongeza kuwa, Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile.
Akizungumzia rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa  Waziri Mhagama amesema itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.
Pia Waziri Mhagama amewatoa hofu ya kupoteza ajira watumishi wote wa mifuko iliyounganishwa  kwa kuwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa taasisi.
Kuondoa sintofahamu Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) imeandaa mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria na kanuni za PSSSF ili kuhakikisha kwamba wanachama na wadau wote wa sekta ya hifadhi ya jamii wanakuwa na uelewa sahihi wa sheria hizo na mabadiliko yaliyofanyika.
Mbali na hayo, Waziri Jenista ameteua wajumbe wa Bodi ya Mfuko huo ambao ni Bi. Leah Ulaya, Bw. Rashidi Mtima, Dkt. Aggrey Mlimuka, Bi. Stella Katende, Bw. Thomas Manjati, Bw. Henry Katabwa, Bi. Suzan Kabogo pamoja na Bw. Jacob Mwinula.

Read More

Monday, July 30, 2018

AGIZO LA RAIS MAGUFULI KUHUSU FEDHA ZA MASHUJAA KUTUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA LATEKELEZWA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora akiongea na Mkandarasi wa kampuni ya Mionzi Jua, Christopher Athumani, wakati alipofika kukagua kazi inayofanywa na  kampuni hiyo ya kuweka taa kwenye barabara ya Emmaus-African Dream jijini Dodoma, wengine ni Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe (mwenye koti).

Muonekano wa baadhi ya Taa za barabarani zinazowekwa katika barabara mpya ya Emmaus-African Dream jijini Dodoma, Taa hizo zinawekwa kufuatia agizo la Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, aliyetaka fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa mwaka huu, kiasi cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara za jiji hilo.

Muonekano wa taa ya kuongoza magari katika makutano ya barabara mpya ya Emmaus-African -Dream jijini Dodoma. Taa hiyo imewekwa kufuatia agizo la Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, aliyetaka fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa mwaka huu, kiasi cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara ya jiji hilo. 

NA MWANDISHI WETU

Mnamo mwezi Juni, mwaka 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitoa taarifa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza) fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa kiasi cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara   jijini Dodoma.


Kufuatia agizo hilo, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), walipata kiasi cha Shilingi milioni 288 kwa ajili kuweka taa 57 kwenye barabara ya Emmaus-African Dream na taa 42 kwenye barabara ya Kisasa. kiasi cha shilingi milioni 20 walipewa Wakala wa Barabara Dodoma (TANROADS), kwa ajili ya kuhamisha taa ya kuongoza magari kutoka njia panda ya Area D na kuwekwa kwenye makutano ya barabara ya  Emmaus.

Tayari TARURA wameanza kutekeleza agizo hilo kwa kuweka taa kwenye barabara ya Kisasa na Emmaus-African Dream. Kwa upande wa TANROADS-Dodoma, zoezi la kuhamisha taa ya kuongoza magari limetekelezwa, ambapo wakandarasi watakabidhi kazi hizo rasmi mwezi Agosti mwaka huu.

Akiongea wakati wa ukaguzi wa kazi hiyo katika barabara ya Emmaus-African Dream Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora alifafanua kuwa, kuwekwa kwa taa kwenye barabara hizo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais aliyetaka miundombinu ya barabara jijini Dodoma kuboreshwa, hali inayoongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hizo pamoja na kupandisha hadhi ya jiji na makazi ya maeneo husika.

“Taa hizi ni za kisasa na zitasaidia uhifadhi wa mazingira kwakuwa zinatumia mwanga wa jua, Serikali inajitahidi kuboresha miundo mbinu ikiwemo barabara hii, hivyo wananchi ambao barabara inapita katika makazi yao hawanabudi kuilinda miundombinu ya taa hizi. Fedha za walipakodi zimetumika hapa itasikitisha kuona miundo mbinu ya taa hizi kukuta imeharibiwa” amesisitiza Kamuzora.

Awali, akielezea shughuli zinazoendelea katika barabara ya Emmaus-African Dream, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe alibainisha kuwa taa hizo ni za kisasa na zina uwezo wa kuhifadhi umeme hivyo zitasaidia kupunguza ghrama za uendeshaji na uhakika katika matumizi ya barabara hizo.

Kampuni ya Mionzi Jua Ltd ndiyo inayofanya kazi ya kuweka taa katika barabara za Kisasa na Emmaus-African Dream, ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 287.1 zitatumika kukamilisha kazi hiyo.

Read More

TAKUKURU CHUNGUZENI UJENZI WA HALMASHAURI YA BUHIGWE-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, Bw. Raphael Mbwambo afuatilie ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe, baada ya kutilia shaka makadirio ya ujenzi huo.

Amesema mbali na ujenzi wa ofisi hiyo ambayo msingi wake ulikadiriwa kutumia sh milioni 205 lakini Halmashauri imetumia zaidi ya sh, milioni 400, pia halmashauri hiyo imeweka makadirio makubwa ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo utekelezaji wake ni mgumu.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 30, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Buhigwe pamoja na wananchi wa wilaya hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo inayojengwa kwenye eneo la Ruheta.

“Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma fuatilia ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe na tunataka tujue ni nani aliyetengeneza makadirio hayo kwa sababu makadirio aliyoyafanya ni makubwa ulinganisha na mradi husika,” amesema.

Waziri Mkuu amesema “Hospitali mnayojenga ni ya kawaida, haiwezekani mkaweka makadirio kama hayo ya kujenga wodi moja kwa sh milioni 851 wakati kuna baadhi ya maeneo nchini Serikali imetumia sh. milioni 500 kujenga kituo cha afya chenye majengo zaidi ya matano,”.

Kufuatia hatua hiyo , Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kupitia upya makadirio waliyoyaweka katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza kwa kuwa makadirio waliyoyaweka ni makubwa na yatakwamisha miradi yao.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa idara wahakikishe wanasimamia vizuri majukumu ya idara zao na kuyatekeleza ipasavyo. “kila mtumishi wa wilaya hii awajibike kwenye eneo lake na si vinginevyo,”.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya wahamiaji haramu, ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja wamekamata wahamiaji haramu 1,054.

Mkuu huyo wa wilaya alisema zoezi la kuwasaka wahamiaji hao limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharifu pamoja na matukio ya utekaji wa kutumia silaha unaofanywa na raia wa nchi jirani wanaoingia nchini kinyume cha taratibu kwa kushirikiana na wananchi wasiokuwa waaminifu.
Read More

FUATILIENI MADAI YA WAKULIMA WA KAHAWA-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kasimu Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Omary Mgumba afuatilie sh. milioni 150 walizotakiwa kulipwa wakulima wa kahawa wa chama cha msingi cha  Kalinzi Organic Coffee Grower   zilizolipwa kwenye kikundi kingine.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 30, 2018) wakati alipotembelea shamba la kahawa katika kata ya Nyarubanda  Wilayani Kigoma, akiwa njiani kuelekea wilaya ya Buhigwe kwa ajili ya kuendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Ametoa metoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba kumuomba awasaidie kutatua changamoto ya malipo ya wakulima wa chama Kalinzi Organic Coffee Grower ambayo hayajalipwa baada ya kuuza kahawa yao katika chama cha kahawa moshi miaka saba iliyopita.

Waziri Mkuu amesema  wakulima  hao wanatakiwa kulipwa fedha zao kwa wakati, hivyo amemuagiza Waziri Mgumba kuhakikisha anafuatilia ni kwanini fedha hizo zililipwa kwa wakulima wa kikundi kingine. Pia ahakikishe wakulima hao wanapata haki yao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaomba wakaulima hao kupanda miche mipya na kuachana na ya zamani kwa kuwa uzalishaji wake ni mdogo na inashambuliwa sana na magonjwa ukilinganisha na miche ya kisasa.

Aidha, Naibu Waziri huyo wa Kilimo Omary Mgumba alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na ni kweli kuwa fedha hizo zililipwa kimakosa na Bodi ya Kahawa kwenda kwa chama cha Msingi cha Kalinzi Farm Coffee badala ya chama cha Kalinzi Organic Coffee Grower.  Ameahidi kufuatilia suala hilo. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kalinzi Organic Coffee Grower , Bw. Said Mchachu alisema chama chao kina wakulima 447 ambao tangu wapeleke kahawa yao Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuiuza mwaka 2012 mpaka sasa wanaendelea kufuatilia madai yao bila mafanikio.

Alisema madai hayo yamesababisha migogoro ndani ya chama chao kufuatia baadhi ya wakulima wakiwatuhumu viongozi kuwa wao ndio wamekula fedha zao jambo ambalo si kweli, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia ili waweze kupata fedha zao.
Read More

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WATATU KASULU

*Ni wale wanaotuhumiwa kwa wizi wa dawa 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu wa hospitali ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa tuhuma za wizi dawa na vifaa tiba.

Pia Waziri Mkuu ameahidi kuyafunga maduka yote ya dawa yanayodaiwa kununua dawa kutoka kwa watumishi wa hospitali hiyo wasioukkuwa waaminifu na kuziuza kwa wananchi.

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi watumishi leo (Jumatatu, Juni 30, 2018) wakati alipotembelea hospitali ya wilaya hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Amewataja watumishi wanaotuhumiwa kuhusika na wizi huo kuwa ni Mfamasia wa wilaya Bw. Michael Nindi, mtumishi wa maabara Bw. Tilas Mbombwe na Bibi. Venansia Batega  ambaye ni muuguzi.

“Watumishi hawa nimewasimamisha kazi kuazia leo hii, ili wapisha uchunguzi wa upetevu wa dawa na vifaa tiba zikiwemo darubini mbili. Hospitali hii inamatatizo makubwa sana ya wizi,”.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kutenga siku tatu katika wiki na kuwafuata wananchi waishio vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi hao waondoe urasimu wanaouweka kwa lengo la kupokea rushwa na pia wawatumikie wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote. 

“Sitarajii kusikia jambo hilo kwa sababu halina nafasi. Vyombo vinavyosimamia maadili ya utumishi vitimize wajibu wake ili kuwalinda wananchi wasiingizwe katika utoaji rushwa,”.

Read More

Sunday, July 29, 2018

MAJALIWA ATEMBELEA HOSPITALI YA WILAYA YA KASULU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Bibi Pendo Lilola  kwa kujifungua salama  mtoto wa kiume katika  wodi ya wazazi kwenye Hospitali ya wilaya ya Kasulu Julai 29, 2018.  Mheshimiwa Majaliwa aliitembelea Hospitali hiyo  akiwa  katika ziara ya mkoa wa Kigoma Julai 30, 2018.

Read More

ZIARA YA MAJALIWA WILAYANI UVINZA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Ilagala wilayani Uvinza baada ya kutembelea kiwanda kidogo cha kukamua mafuta ya mawese Julai 29, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mchikichi baada ya kukagua shamba la zao hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora wilayani Uvinza, Julai 29, 2018.  Wapili kulia ni mkewe Mary.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama mchikichi wakati walipotembelea shamba la Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora wilayani Uvinza, Julai 29, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama mikungu ya matunda ya  michikichi yanayosubiri kukamuliwa kuwa mafuta ya mawese katika kiwanda kidogo kilichopo kwenye kijiji cha Ilagala  wilayani Uvinza, Julai 29, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama mikungu ya matunda ya  michikichi yanayosubiri kukamuliwa kuwa mafuta ya mawese katika kiwanda kidogo kilichopo kwenye kijiji cha Ilagala  wilayani Uvinza, Julai 29, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama matunda  ya michikichi yaliyokuwa yakichambuliwa kabla ya kukamuliwa kuwa mafuta ya mawese katika kiwanda kidogo kwenye kijiji cha Ilagala wilayani Uvinza, Julai 29, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama kazi ya kukamua mafuta ya mawese kwenye kiwanda kidogo  katika kijiji cha Ilagala wilayani Uvinza Julai 29, 2018. Kulia ni Mbunge wa Kigoma Kusini, Hasna Mwilima na watatu kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.


Read More

Thursday, July 26, 2018

JIJI LA DAR ES SALAAM

Sehemu ya jiji   la Dar es salaam linavyoonekana katika picha iliyopigwa kutoka angani  hivi karibuni.

Read More

Wednesday, July 25, 2018

HALI YA USAFI COCO BEACH HAIRIDHISHI - WAZIRI MKUU


*Ataka Mamlaka za Serikali za Mitaa husika zisimamie fukwe zote nchini  

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usafi Coco Beach hairidhishi na amewataka viongozi wa Manispaa ya Kinondoni wajipange ili eneo hilo liweze kuvutia.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa eneo hilo pamoja na wananchi na watendaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo hufanyika Julai 25, kila mwaka.

Waziri Mkuu ambaye aliambatana na mke wake, Mary Majaliwa, alishiriki zoezi hilo kwa kufyeka nyasi, kuzoa takataka na kupanda miti kwenye ufukwe huo.Zoezi hilo limefanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea Police Officers’ Mess.

“Eneo hili nimelitembelea, bado haliridhishi kwa usafi. Nimeenda kwenye fukwe pale na kukuta takataka nyingi zimelundikwa mahali pamoja. Ni vema Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka zote zinazosimamia usafi ziwaratibu wanaotoa huduma na wanaopata huduma ili    kuendeleza usafi wa maeneo haya nchini kote,” amesema.

Amesema Manispaa ya Kinondoni haina budi kuratibu eneo hilo kwa kupanga eneo la maegesho, la watu kupumzikia, la huduma za chakula na kuongeza kupanda miti ili wananchi waone ni maeneo mazuri yanayovutia.

“Muandae shughuli za burudani zitakazofanyika kila Jumamosi na Jumapili. Karibisheni watu wa kuleta michezo ya baharini kama vile viboti na vibaiskeli vya majini, wekeni bembea ili fukwe ivutie zaidi. Wazazi wataleta watoto wao kwenye michezo wakati wao wakikaa pembeni na kupumzika,” amesema.

Amesema vibanda vilivyoko kwenye ufukwe huo havipendezi na ikibidi waangalie uwezekano wa kuweka makontena ili kuongeza mvuto. “Vibanda hivi havileti picha nzuri sana, hivyo mnaweza kuweka makontena kutoka Pepsi au Coca-Cola ili kuleta muonekano sawia.”

“Jambo hilo linaweza kuwa ni chanzo cha mapato kwa Manispaa hii. Uongozi wa Manispaa tengenezeni haya wakati mkisubiri andiko lenu lipitishwe na muweze kupata fedha za kuboresha ufukwe huu,” amesema.

Alisema eneo jingine linalopaswa kuangaliwa katika ufukwe huo ni kuimarishwa kwa ulinzi ili watu wanaokwenda kupata huduma wasihofie usalama wao.

Waziri Mkuu amesema usafi siyo uishie kufanyika tarehe 25 tu, na akawataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye fukwe zote. “Hii ni changamoto kwenye Mamlaka ya Halmashauri ya Kinondoni, lakini pia Ilala, Temeke, Bagamoyo hadi Tanga, zinapaswa aihakikishe hizi fukwe ziwe safi,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Ally Hapi alisema mbali ya wananchi wa kawaida, walikuwepo pia askari polisi 100 na wanajeshi 150 ambao walishiriki zoezi hilo la usafi.

Alisema Manispaa ya Kinondoni wameanza kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu juu ya uboreshaji wa fukwe ya Coco kwa kuandika andiko maalum na kulipeleka Ofisi ya Rais – TAMISEMI. “Manispaa kupitia miradi ya kimkakati, tumeandaa andiko la kuomba sh. bilioni 11 za kutengeneza na kuboresha ufukwe wa Coco, na tumeshalipeleka TAMISEMI na mazungumzo yanaendelea,” alisema.

Juni 29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.

Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.

Aliitaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari kwenye makutano ya barabara ya Kisasa na barabara kuu ya Dodoma Dar es Salaam na kuweka taa za barabarani kwenye barabara mpya ya mchepuko kutoka Emmaus hadi African Dream iliyojengwa ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam.

Read More

MAJALIWA AADHIMISHA SIKU YA MASHUJAA KWA KUSHIRIKI KATIKA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA ENEO LA COCO BEACH JIJINI DAR.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitembea kwa miguu kuelekea kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam ambako Julai 25, 2018 waliadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy baada ya kuwasili katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam  kuadhimisha siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo hilo Julai 25, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary  wakifyeka nyasi kwenye  eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam  wakati waliposhiriki  katika maadhimisho ya   Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo , Julai 25, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakiadhimisha  Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakipeleka uchafu kwenye gari la takataka wakati waliposhiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua  eneo la Coco Beach baada ya kushirika katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo Julai 25, 2018. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwagilia mti alioupanda baada ya Kuadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salam Julai 25, 2018. Kushoto ni mkewe Mary na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwashukuru mamia ya watu  walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na mkewe Mary wakizungumza na Bibi Amina Fadhili (kulia) baada ya kuadhimisha siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye  eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mashine ya kukamua juisi ya miwa, mali ya Abdillah Issa (kulia) wakati alipotembelea eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam baada ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo hilo Julai 25, 2018.

Read More

Tuesday, July 24, 2018

WAZIRI MKUU KUONGOZA ZOEZI LA USAFI COCO BEACH


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa kesho (Jumatano, Julai 25, 2018) anatarajiwa kushiriki zoezi za usafi eneo la Coco Beach pamoja na wananchi na watendaji mbalimbali.

Zoezi hilo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Juni 29 mwaka huu kwamba Watanzania wafanye usafi kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo huadhimishwa Julai 25, kila mwaka. 

Kwa muhibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, wananchi wanatakiwa wafike eneo hilo kuanzia saa 12:30 asubuhi ili waanze shughuli hiyo. Usafi huo utafanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea maeneo ya Police Officers’ Mess.

Juni 29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Rais Dkt Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.

Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.

Aliitaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari katika barabara ya Kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya kutoka Emmaus hadi African Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.

Read More

Monday, July 23, 2018

WAZIRI MKUU AFUNGUA KONGAMANO LA PILI LA BIASHARA LA KOREA NA TANZANIA


*Aalika wawekezaji kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya mazao
*Ataka waangalie fursa za uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya utalii

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaalika wafanyabiashara kutoka Korea Kusini waanzishe miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani.

Ametoa mwaliko huo leo (Jumatatu, Julai 23, 2018) akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati akifungua Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Korea lililofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kongamano la kwanza lilifanyika jijini Seoul, Februari 2018.

Amesema Serikali inahamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vinavyotumia rasilimali za ndani ambavyo vitasaidia kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo, misitu, madini na bahari.

“Tunakaribisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo ya uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za walaji (consumer goods), pamoja na viwanda vya kuunganisha bidhaa mbalimbali, yaani (assembling plants) kama vile magari, simu na majokofu,” amesema.

Waziri Mkuu pia aliwaalika wafanyabiashara kutoka Korea waliohudhuria kongamano hilo waje kuwekeza kwenye sekta ya utalii ambako alisema kuna vivutio vya mbuga za wanyama kama Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Olduvai Gorge na fukwe za bahari za Tanzania bara na Zanzibar.

“Tanzania ina kilometa 1,200 za fukwe kuanzia Tanga hadi Mtwara, ziko pia fukwe za Zanzibar, ziko fukwe kwenye maziwa yetu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ambazo ni kivutio kingine cha utalii,” amesema.

Amesema ili kusimamia matumizi ya fukwe hizo, Serikali inakamilisha uundaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Fukwe kama ilivyo ile ya Ngorongoro ambayo alisema taratibu zikikamilika, itaanza kazi hivi karibuni.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-yon aliwapongeza viongozi wa Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mageuzi ya kiuchumi hadi kuiwezesha nchi hii kuwa mojawapo ya nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka.

“Mapema mwaka huu, Benki ya Dunia imeitambua Tanzania na kuitangaza kuwa ni miongoni mwa nchi 10 ambazo uchumi wake unakua kwa haraka duniani. Nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Serikali hii pamoja na wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchi hii,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaeleza wafanyabiashara na wenye makampuni kutoka Korea ambao wanashiriki kongamano hilo kwamba amepokea maombi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ambaye ameyaalika makampuni ya Kikorea yashiriki kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji.

“Ukiondoa mradi wa ujenzi wa daraja la Salender ambao mkataba wake umesainiwa leo, Rais Magufuli ameomba makampuni ya Kikorea yashiriki kwenye miradi mikubwa ya kiuchumi na hivi karibuni, taratibu zikikamilika, kuna kampuni moja itasaini mkataba wa kujenga meli kubwa kwenye Ziwa Victoria, na siyo huko tu, hata kwenye Ziwa Tanganyika,” alisema.

Alieleza kuridhishwa kwake na ujenzi unaofanywa kwenye miradi ya kituo cha data cha NIDA (Kibaha) na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo aliitembelea jana jioni.

Waziri Mkuu wa Korea Kusini anatarajiwa kuondoka nchini leo jioni (Julai 23, 2018).
Read More

WAZIRI MKUU WA KOREA AMALIZA ZIARA NCHINI


WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku tatu hapa nchini na kusindikizwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo wa Korea ambaye ameondoka leo (Jumatatu, Julai 23, 2018) saa 9.14 alasiri, ameelekea Oman ambako atakuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili. Aliwasili nchini juzi akitokea Kenya ambako pia alikuwa na ziara ya siku mbili.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius  Nyerere, Waziri Mkuu wa Korea Kusini alisindikizwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam

Kabla ya kuondoka alishuhudia burudani kutoka vikundi vya ngoma na matarumbeta uwanjani hapo.

Mara baada ya mgeni wake kuondoka, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na wasanii waliokuwepo uwanjani na kuwapongeza kwa kujitokeza kutoa burudani kila wakati wageni wanapoitembelea Tanzania.

“Tunawashukuru sana wasanii kwa sababu mlikuja wakati wa mapokezi ya mgeni wetu na sasa mmekuja tena kumsindikiza. Mgeni wetu amefurahia sana ngoma zetu na amesema atarudi tena Tanzania.”

“Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, tunatambua kuwa mnajitoa muda wenu kila mnapokuja kupokea na kusindikiza wageni ili kuweka sura nzuri ya Taifa letu wakati wa kupokea wageni wetu, tunawashukuru sana,” amesema.

Read More

WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA KOREA LEE NAK-YON AONDOKA NCHINI BAADA YA ZIARA YA SIKU TATU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - yun wakifurahia burudani ya kikundi cha matarumbeta kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere wakati mgeni huyo alipoondoka nchini Julai 23, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati alipoondoka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya ziara ya siku tatu nchini, Julai 23, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati alipoondoka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya ziara ya siku tatu nchini, Julai 23, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati alipoondoka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya ziara ya siku tatu nchini, Julai 23, 2018.

Ndege iliyombeba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - yun ikiruka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere baada ya kiongozi huyo kumaliza ziara yake ya siku tatu nchini Julai 23, 2018. 

Ndege iliyombeba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - yun ikiruka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere baada ya kiongozi huyo kumaliza ziara yake ya siku tatu nchini Julai 23, 2018. 

Read More