Saturday, June 29, 2019

WAZIRI KAIRUKI AUTAKA UONGOZI WA KIWANDA CHA GOOD WILL KUZINGATIA USTAWI WA WAFANYAKAZI WAKE.


NA.MWANDISHI WETU - OWM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchi Mhe. Angellah Kairuki ameutaka uongozi wa Kiwanda cha kutengeneza marumaru cha GoodWill Tanzania ceramic ltd  kuzingatia ustawi wa wafanyakazi wake kwa kuzingatia kanuni na sheria mbalimbali za ajira nchini ili kuendelea kuwa mazingira mazuri ya wafanyakazi wake.
Ametoa kauli hiyo alipofanya ziara yake mwishoni mwa wiki katika kiwanda hicho kilichopo katika Kijiji cha Mkiu kata ya Nyamato Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Waziri Kairuki alieleza kuwa, upo umuhimu wa kujali wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia usalama na afya mahala pa kazi ili kuondokana na mazingira mabaya yanayoweza kukwamisha uzalishaji unaotarajiwa.
“Ikiwa kiwanda kimeweza kutoa ajira zipatazo 3000 ni idadi kubwa hivyo lazima myatazame mahitaji yao na kuendelea kuzingatia sheria na haki za wafanyakazi wawapo kazini,”Alisema Waziri Kairuki.
Aliongeze kuwa miongoni mwa maeneo muhimu kwa wafanyakazi wenu ni kuhakikisha mnawapa mafunzo kazini ili kuongeza ujuzi katika fani mbalimbali zinazoendana na uzalishaji kiwandani hapo.
Aidha aliwataka kuendelea kuwapa motisha na kuwa na njia za ubunifu katika kuhakikisha kila mfanyakazi anakuwa mwenye ustawi na kufurahia mafanikio ya uwepo wa kiwanda hicho.
“Ni lazima kujali masuala ya usalama wa afya zao wawapo kazini, kujali stahiki zao, kuwapa kazi zenye staha kwa kulingana na kanuni na sheria za kazi zilizopo,”alisisitiza Waziri Kairuki
Naye Meneja Mwajiri wa kiwanda hicho Bw. Figa Msaphiry alimpongeza Waziri kwa Ziara yake kiwandani hapo na kuahidi kuendelea kuyatekeleza maagizo hayo ikiwemo la kuhakikisha wanaendelea kujali masuala ya Afya na Usalama Mahala Pa Kazi kwa kuzingatia mchango unaotolewa na wafanyakazi hao katika kiwanda hapo.
Alifafanua kuwa, kiwanda kimefanikiwa kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa watanzania 936 kati ya hao wanaume 887 na wanawake 49, lakini pia kiwanda kimetengeneza ajira zisizo rasmi Zaidi ya 1,500 na kwa siku wanapokea vibarua ambao wapatao 40 hadi 50 na hii kupeleekea kuongeza fursa za ajira nchini.
Aliongeze kuwa wafanyakazi wamechangia matokeo chanya katika uzalishaji ambapo kiwanda kinazalisha marumaru mita za eneo 40,000 mpaka 50,000 kwa siku kuwa ambapo soko la ndani ni kwa asilimia 30 hadi 40 na soko la nje ni  kwa asilimia 60 hadi  70.
“Kiwanda chetu kimeweza kupanua soko la marumaru kwa kuuza katika nchi za nje, kwani kwasasa kiwanda kinauza marumaru katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Congo kwa kuzingatia ubora wa bidhaa zetu,”alieleza Figa .
kiwanda cha Good Will Company Limited kilijengwa mwezi Machi, 2016 na kuwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hiki na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kasimu Majaliwa, na kuanza uzalishaji wake mnamo Mwezi Aprili Mwaka 2017.Kiwanda kinazalisha marumaru za sakafuni (floor tiles) na marumaru za ukutani (wall tiles)  kwa saizi zote na “scating”, Katika uzalishaji wa marumaru kiwanda kinatumia malighafi tofauti tofauti ambapo 95% ni malighafi toka hapahapa Tanzania na 5% kutoka China ambazo ni kemikali.Malighafi zinazotoka Tanzania ni felidisper ambayo inatoka Tanga – Handeni, Morogoro na Dodoma, nyingine ni Soap stone kutoka Dodoma na Morogoro, Magnesite kutoka Same Moshi, Udongo wa mfinyanzi (clay soil) na udongo mwekundu (red soil) kutoka Mkuranga – Pwani, Limestone kutoka Mavuji – Kilwa  na Kaolin kutoka Kisarawe Pwani. Mradi huu wa ujenzi wa kiwanda umegharimu jumla ya fedha za kigeni dola milioni 50.
=MWISHO=
Read More

WAZIRI MKUU: UJENZI WA NYUMBA BORA WAONGEZEKA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kaya zinazoishi kwenye makazi bora zimeongezeka kwa asilimia 16 katika kipindi cha miaka sita ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2011/2012.

“Kaya zinazoishi kwenye nyumba zenye paa la kisasa zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2017/2018 wakati kuta za kudumu zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 79 mwaka 2017/2018,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumamosi, Juni 29, 2019) wakati akizungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu lililoko Makulu, Manispaa ya Jiji la Dodoma.

Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Dkt. John Pombe Magufuli, pia alizindua ripoti ya matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara ya mwaka 2017/18.

Waziri Mkuu alisema takwimu hizo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na zinaonyesha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kujenga Tanzania ya Viwanda zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa zinagusa moja kwa moja katika sekta ya ujenzi kama vile viwanda vya saruji, mabati, nondo, na vinginevyo.

Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuona kila Mtanzania anaishi kwenye makazi bora kwani makazi bora huimarisha afya za wakazi na afya bora ni mtaji wa msingi kwa kila mwanadamu kwa kufanya kazi na hivyo kukuza uchumi.

“Tuendelee kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje waje wawekeze kwenye viwanda vya saruji, mabati, na marumaru ili kuongeza uzalishaji na kuleta ushindani wa bei ambao utawanufaisha watu wengi na kuwapatia fursa za kujenga makazi bora ya kuishi,” alisema.

Waziri Mkuu alisema mbali na makazi bora, utafiti huo umebainisha uwepo wa ongezeko la kaya zilizounganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa kutoka asilimia 18 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 29.1 mwaka 2017/2018. “Jitihada za Serikali chini ya Mpango wa Umeme Vijijini (REA), zinaendelea na utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini unaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2016/17 na unategemewa kukamilika mwaka 2020/2021,” alisema.

Akizungumzia hali ya umaskini barani Afrika, Waziri Mkuu alisema kiwango cha umaskini wa kipato cha Watanzania hakitofautiani sana na nchi nyingine ndani ya bara hilo. “Tukiangalia hali ya umaskini katika nchi nyingine za Bara la Afrika kwa miaka ya hivi karibuni, nikianza na Kenya kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi ni asilimia 36.8 (mwaka 2015), Afrika ya Kusini asilimia 55.5 (mwaka 2015), Rwanda asilimia 38.2 (mwaka 2016), Zambia asilimia 54.4 (mwaka 2015), Ethiopia asilimia 23.5 (mwaka 2015) na Zimbabwe asilimia 72.3,” alisema.

Alisema kupunguza umaskini kwa nchi yoyote ile kunapaswa kuhusishwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine za kiuchumi ambazo hugusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi. “Nitumie fursa hii kusisitiza kuwa umaskini ni changamoto kwa dunia nzima na hasa kwa nchi zinazoendelea. Nchi zilizo na hali mbaya zaidi ni zile zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kama takwimu rasmi zinavyoonesha.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ni lazima Serikali iimarishe upatikanaji wa takwimu kwa kuajiri maafisa takwimu wanaowajibika moja kwa moja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu badala ya kumtegemea mtu anayewajibika kwa Mkurugenzi wa Halmashauri.

“Leo hii hatuna Afisa Takwimu katika kila Halmashauri, na matokeo yake hatuna mfumo mzuri wa kupata taarifa kuanzia ngazi ya chini. Tuweke utaratibu ili hawa watu wawepo na kila Afisa takwimu awajibike kupeleka taarifa yake kwa Mtakwimu Mkuu kila wakati.”

“Nilipokuwa Naibu Waziri TAMISEMI ninayeshughulikia elimu, nikiagiza takwimu fulani, kuzipata ilikuwa inachukua zaidi ya wiki mbili, na hiyo ni kwa Halmshauri moja tu. Na wakati mwingine, taarifa inakujia wakati umeshasahau kuwa ulitoa agizo uletewe.”

Mapema, akitoa taarifa juu ya utafiti huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo kiwango cha umaskini kimeendelea kushuka na kufikia tarakimu moja.

Alisema utafiti huo uliofanywa na ofisi yake kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, baadhi ya balozi na mashirika ya Umoja wa Mataifa ulilenga kupata makadirio ya viwango vya umaskini ili kufuatilia, kupima na kutathmini mipango mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Alisema katika utafiti huo, walitumia teknolojia ya kisasa iitwayo survey solution ambayo imesaidia kupunguza gharama za utafiti za kupeleka madodoso na magari. “Tulitumia vishkwambi (tablets) na kupunguza mzigo wa kubeba na makaratasi au kukaa kujumlisha taarifa,” alisema,

 (mwisho)
Read More

SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA HUDUMA KWA WATU WENYE ULEMAVU

Na; Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau imedhamiria kuboresha huduma na upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa kundi la Watu wenye Ulemavu lilikosa baadhi ya fursa hapo awali kutokana na changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo.
“Tunafahamu watu wenye ulemavu wanauhitaji wa huduma bora na vifaa saidizi vitakavyo wawezesha kumudu mazingira ili nao waweze kujumuika katika nyanja zote,” alisema Mhagama
Alifafanua kuwa takwimu na Sensa ya Taifa ya Watu wenye na Makazi ya mwaka 2012, imekadiria idadi ya watu Tanzania ni zaidi ya milioni 44 ambapo milioni 2.5 ni Watu wenye Ulemavu.
Waziri Mhagama alisema, Serikali imeazima kuboresha huduma kwa Watu wenye ulemavu ikimemo kutoa elimu bure na kuimarisha elimu jumuishi, kujenga vituo vya afya na hospitali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa watu wenye ulemavu wasio na uwezo.
Mbali na hayo, alihimiza wadau pamoja na makampuni kuona umuhimu wa kuhudumia kundi la watu wenye ulemavu wakiwa wanatoa huduma mbalimbali za kijamii.
Aidha, alipongeza Kampuni ya Singara Tanzania (TCC) kwa msaada huo na kuwashauri waendelee kukumbuka kundi hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TCC, Bw. Godson Killiza alisema kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa na nijukumu kama wadau kuwasaidia na kuwaunga mkono kwenye masuala mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Ummy Nderiananga alieleza kuwa juhudi za Serikali katika kushirikiana na wadau itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto za Watu wenye Ulemavu katika kufanikisha masuala yao.

MWISHO
Read More

Friday, June 28, 2019

WAZIRI KAIRUKI AUTAKA UONGOZI WA KNAUF KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAMII INAYOWAZUNGUKA.

NA.MWANDISHI WETU – OWM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuka ameutaka uongozi wa kiwanda kinachotengeneza bidhaa za cha za jasi (Gypsumboard) cha KNAUF kuendelea kushirikiana na jamii inayowazunguka katika kujiletee maendeleo.
Ametoa kauli hiyo mapema mwishoni mwa wiki hii alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani ili kukagua shughuli za uzalishaji zinazoendela pamoja na kusikiliza changamoto za wawekezaji hao na kuweza kujadili masuala ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Waziri Kairuki aliwataka kuona umuhimu wa kuchangia katika shughuli za kimaendeleo katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho hususan katika uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa misaada itakayofikia jamii kwa sehemu kubwa na si mtu mmoja mmoja ili kuleta maendeleo katika eneo kubwa na kuondoa tofauti kubwa za kimaendeleo zisizoendana na maendeleo ya maeneo kiwanda hicho.
“Ni muhimu sana, na ni busara kuona ni kwa  namna gani mnashirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hili katika kuleta maendeleo ili kuhakikisha mnakubalika , na kuleta maendeleo ya eneo husika na kuondoa tofauti za kimaendeleo kati ya ustawi wa kiwanda na jamii inayowazunguka”alieleza Waziri Kairuki
Waziri aliutaka uongozi huo kushiriki kimalilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuchangia kuboresha miundombinu inayozunguka mazingira ya kiwanda ili kuendelea kushiriki kwa vitendo na kuunga mkono jitihada za kuendelea eneo hilo.
Sambamba na hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jumaa Abeld aliomba uongozi wa kiwanda kuona namna ya kuchangia katika maendeleo ya eneo lao kwa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya msingi ya Kitangwi pamoja na madarasa manne  katika shule ya msingi ya Kisemvule zilizopo Wialya ya Mkuranga katika mkoa huo.
“Ombi letu ni kuona namna kiwanda hiki kinavyoweza kuchangia katika maendeleo kwa kutujengea vyumba sita vya madarasa katika shule zinazotuzunguka ili kusaidia uhaba uliopo na kusaidi watoto wetu kujifunza katika mazingira mazuri,”alisema Jumaa.
Aidha Meneja Masoko wa Kiwanda hicho Bi. Zainab Mwasara aliahidi ifikapo Julai 05 mwaka huu uongozi wa kiwanda utatoa taarifa za utekelezaji wa maombi hayo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 6.
“Tunaahidi kukutana kama uongozi wa kiwanda ili kujadili na kutekeleza masuala ya msingi ikiwemo hili la ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuendelea kuleta tija kwa uwepo wa kiwanda katika eneo hili,”alisema Mwasara.
Naye, Meneja Fedha wa kiwanda hicho Bi. Wema Mboga alishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji nchini na kumpongeza ziara ya Waziri katika kutatua na kuahidi kufanyia kazi masuala yaliyoelezwa kuwa ni changamoto kiwandani hapo ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika, kutokamili kwa leseni za uchimbaji kwa wakati, tozo kubwa za malighafi na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kiwandani hapo.
AWALI
Kiwanda cha KNAUF kilianzishwa mwezi Novemba mwaka 2015 kwa lengo la kuzalisha bidhaa za jasi (Gypsum board), gundi za jasi, pamoja na chuma za jasi (metal profile) kufanya kazi na usambazaj.Kiwanda kinafanya kazi katika nchi zaidi ya 80 ambapo katika nchi za kusini mwa Janga la Sahara, Tanzania ni nchi pekee ambayo ina uwekezaji huo kutokana na sababu za mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji pamoja na sababu za kijiografia.Kampuni imeajiri wazawa 150 katika Nyanja zote kwa kulenga ifikapo 2020 kiwanda kiweze kuendeshwa na wazawa pasipo kutegemea wataalam kutoka nje.
=MWISHO=

Read More

WATENDAJI DUMISHENI NIDHAMU KATIKA UTENDAJI WENU-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatakaviongozi wote na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi wizara kuwajibika ipasavyo na kudumisha nidahmu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.

Amesema ili kufikia lengo na dhamira ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 kwa ufanisi, viongozi hao wanatakiwa waendelee kuwasisitiza wananchi washiriki ipasavyo kulinda miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge,  Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Septemba tatu mwaka huu.

Pia, Waziri Mkuu amezitaka mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa misitu, uchafuzi wa bahari, mito na maziwa na taka za plastiki ili kulinda mazingira asilia.

Akizungumzia kuhusu bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 33.11, kati yake sh. trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63. “Aidha, sh. trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. 
                                                                                                  
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania pamoja na Washirika wa Maendeleo waiunge mkono Serikali katika kutekeleza vipaumbele vilivyowekwa kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango wa haraka katika maendeleo ya uchumi na ya watu.  

Wakati huo huo,Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha maandalizi hayo ikiwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

“Uboreshaji huo, unatarajiwa kuanza tarehe 18 Julai, 2019 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambapo litafanyika kwa muda wa siku 7 kwa kila kituo na kuendelea hadi tarehe 5 Machi, 2020 litakapohitimishwa katika mkoa wa Dar es Salaam.” 

Waziri Mkuu amesema uboreshaji huo hautahusisha wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 isipokuwa utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu ujao. 

Ametaja kundi lingine litakalohusika na zoezi hilo kuwa ni pamoja na wale watakaoboresha taarifa zao, kama waliohama jimbo au kata na kuhamia katika maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza au kadi zao kuharibika, watakaorekebisha taarifa zao pamoja na kuwaondoa waliopoteza sifa kama vile kufariki.

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Novemba mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao ni sehemu muhimu katika kuimarisha utawala bora na demokrasia ambayo imeendelea kunawiri nchini. Amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza wakati utakapofika.

Amesema Serikali imeendelea kutumia mbio za mwenge kuhamasisha wananchi washiriki uchaguzi huo kupitia kaulimbiu isemayo “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.

Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla hususan wale wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi huo.”

Kwa wananchi wenye nia ya kugombea katika uchaguzi huo, Waziri Mkuu amesema ni lazima wajue majukumu wanayoomba kwamba yanahitaji umakini mkubwa na uchapaji kazi kwa sababu Serikali imewekeza miradi mingi kote nchini, hivyo wanahitajika watu walio tayari kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili itoe matokeo yanayokusudiwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira salama na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.

(mwisho)
Read More

MPANGO WA BLUEPRINT KUANZA JULAI MOSI MWAKA HUU-MAJALIWA

WAZIRI MKU Kassim Majaliwa amesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint) kwa lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, jijini Dodoma. Amesema wakati kazi hiyo inaendelea Serikali itafanya ufutialiaji kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kutathmini kama lengo limefikiwa.

”Utekelezaji wa mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, unaojidhihirisha kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa kwenye mpango huo.”

Waziri Mkuu ametaja tozo zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Maji

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta tija, ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu kusambaza blueprint pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa wizara zote kwa ajili ya kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.

Amesema kupitia mpango wa bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na shughuli nyingine jumuishi.

Wakati huohuo,Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na kilimo tegemezi cha mvua hususani kwenye zama hizi za mabadiliko ya tabia nchi, Serikali kwa sasa inaboresha kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuwatoa wananchi katika kilimo hicho.

Amesema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni pamoja na kuunda upya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo inalenga kuiwezesha tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji. Pia Serikali imehamishia tume hiyo Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza kilimo nchini.

”Ili tuweze kufikia lengo la kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025, tayari nimeielekeza Wizara ya Kilimo isimamia kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.”

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo inatakiwa ihakikishe inasimamia vema miradi 22 ya umwagiliaji inayoendelea sasa pamoja na miradi mipya minane itakayojengwa nchini katika pindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.


(mwisho)
Read More

HOTUBA YA WAZIRI MKUU YA KUAHIRISHA BUNGE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye  mimbali kuwasilisha hotuba yake ya kuahirisha Bunge, jijini Dodoma Juni 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba yake ya kuahirisha  Bunge,  jijini Dodoma Juni 28, 2019.

Read More

Thursday, June 27, 2019

MIFUKO YA UWEZESHAJI IPIMWE KWA MATOKEO YA KIUCHUMI-MAJALIWA


*Asema uboreshwaji wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ni muhimu

SUALA la uwezeshaji wananchi kiuchumi ni jambo muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani, kwa kuwa litawatawezesha kutambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi na hatimaye wataweza kujitegemea na kuondokana na umasikini wa kipato.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo ya Serikali na ya sekta binafsi ambayo inaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

NEEC imekuwa ikiandaa makongamano ya kukutanisha wadau wa masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004, ambapo pia hutoa fursa muhimu ya kupeana taarifa mbalimbali za uwezeshaji.

Kongamano la Nne la Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika Juni mwaka huu katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma ambalo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alieleza umuhimu wa uboreshwaji wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile, kamilisheni na hakikisheni mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya uwezeshaji kwa matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya.”

Alisema uwezeshaji wananchi kiuchumi ni suala mtambuka, sekta mbalimbali za kiuchumi na sekta binafsi zinajihusisha moja kwa moja katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo ni muhimu sana masuala ya uratibu, ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yakafanywa mara kwa mara ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendelee kuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015 - 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

Mbali na agizo hilo, pia Waziri Mkuu alilitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuratibu mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo ya Serikali na ile ya binafsi ili kujua ipo mingapi na inamnufaisha nani na kisha wampelekee taarifa. 

Alisema ni muhimu ikajulikana idadi ya mifuko hiyo ili kujua ipo maeneo gani na namna inavyoendeshwa na kama kweli walengwa wananufaika kwa kiwango gani na je wanajijua, hivyo italiwezesha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuiratibu vizuri.

Alisema Serikali inatambua kuwa kuwawezesha wananchi kiuchumi ni hatua ya msingi katika kujenga Taifa lililoimarika kiuchumi na lenye lengo la kujitegemea hususan katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. 

“Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuhakikisha kuwa fursa ya mikopo kwa ajili ya mitaji inapatikana bila ya urasimu na kwa masharti nafuu ikiwa ni pamoja na kuwafikia wananchi wengi mijini na vijijini.”

Alisema katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa, Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu sambamba na kubuni shughuli za kuwawezesha wananchi katika maeneo yao kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 pamoja na Sheria yake. 

Waziri Mkuu aliongeza kuwa, kwa upande wa sekta binafsi, serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara ili kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. 

Alisema mfano mzuri wa utekelezaji wa jambo hilo ni maboresho ya sheria na mifumo mbalimbali ili kuboresha mazingira kwa sekta binafsi kufanya biashara ikiwemo pamoja na kutekeleza Blue Print. 

“Nyote mtakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Rais ameipa uzito wa kipekee sekta binafsi, miongoni mwa hatua alizozichukua ni kuhakikisha kuwa masuala ya uwekezaji yanakuwa chini ya ofisi ya waziri mkuu ili kushughulikia wawekezaji ambao kwa sehemu kubwa ni sekta binafsi. kadhalika, mifumo ya kodi na tozo mbalimbali imeangaliwa sambamba na sera na sheria husika.”

Pia Waziri Mkuu alizitaka mamlaka husika za serikali zihakikishe zinashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla ili sera, mipango na shughuli zao za kila siku zitoe kipaumbele katika uwezeshaji wananchi kiuchumi. 

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuitaka mikoa na halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama kile cha Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi. 

Waziri Mkuu alitoa muda wa mwaka mmojakwa viongozi wa mikoa ya Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ambayo haijakamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji (Investment Guide) ihakikishe kuwa inakamilisha.

Kadhalika, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu matokeo ya tafiti zilizofanywa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu biashara na uwekezaji nchini kuwa yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya miradi mikubwa inayopendekezwa na shirika hilo.

“Miradi hiyo ni pamoja na ule wa “Harmonized Innovation Solutions for Local Economic Development” ambao upo katika hatua za maandalizi. Lengo la UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi inatekelezwa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.” 

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuziagiza mamlaka zote zishirikiane na NEEC kuhakikisha kuwa fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti za UNDP zinafanyiwa kazi. “Aidha, hakikisheni kuwa miradi mikubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inatokana na tafiti hizo.” 

Alisema ana imani kubwa kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, malengo mbalimbali ya nchi kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi yatafikiwa. Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa ya Miaka 25; na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya umoja wa Mataifa (SDGs).

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, SeraUratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema lengo la mkutano ni kuwakutanisha wadau wote wanaotekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.

Alisema kupitia mkutano huo wanapata mrejesho wa yaliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kujadili, kupima mafanikio, kuona changamoto zilizopo na kujiwekea malengo na mikakati ya kufanya vizuri zaidi kwa mwaka unafuata. 

Waziri huyo alisema katika kukutanisha wadau wa uwezeshaji, Ofisi yao imeanza kutengeneza National Economic Empowerment FrameWorkitakayoelekeza vipaumbelele vya kitaifa vya kisekta kutokana na shughuli za uchumi zilizopo.

Awali,Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’ Issa alisema jukumu la baraza hilo ni kuratibu, kuongoza, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini.

Alisema baraza hilo limeendelea kufuatilia na kutathmini shughuli za mifuko ya uwezeshaji, kiwango cha huduma kwa wananchi na matokeo ya uwezashaji unaotolewa kwa wananchi.

“Hadi kufikia februari mwaka huu mifuko inayotoa mikopo moja kwa moja kwa kushirikiana na ile inayotoa dhamana imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 3.1 kwa wajasiriamali 5,031,219.”

Alisema mifuko inayotoa ruzuku na programu za uwezeshaji zimesaidia kuwezesha kiasi cha zaidi ya sh. trilioni 12 kwa wananchi pamja na kufadhili miradi mbalimbali ya kijamii nchini.

 (mwisho)
Read More

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

WAZIRI MKU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji na biashara.

Amesema mpaka sasa, hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini. 

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 27, 2019) jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la uwekezaji la mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

”Miongoni mwa hatua hizo ni uwepo wa usafiri wa uhakika na wa haraka wa abiria na mizigo kwa kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (Standard GaugeRailway).”

Pia, Waziri Mkuu amesema uwanja wa ndege wa Dodoma umeboreshwa na kuruhusu ndege kubwa na ndogo kutua usiku na mchana. 

”Mashirika ya ndege yanayotoa huduma yameongezeka na maandalizi ya awali ya ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege katika eneo la Msalato yanaendelea.”

Waziri Mkuu amesema mkoa wa Dodoma una barabara za kuaminika za kiwango cha lami zinazoiunganisha na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha huduma za afya na Dodoma kuna hospitali ya Benjamin Mkapa yenye uwezo kama wa Muhimbili na Mloganzila.

Amesema ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji ‘Stiegler’s Gorge’wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115, utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.

“Mradi huo utaongeza upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda na uwekezaji nchini ikiwemo na katika mkoa wa Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (The Blue Print) utakaoanza Julai mosi mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema anatarajia kuwa kongamano hilo litawezesha kupatikana kwa wawekezaji mahiri kwa maendeleo ya uchumi na wananchi wa Tanzania.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge alisema katika azma ya Selikali ya kujenga uchumi wa viwanda wameandaa kongamano hilo ili kutangaza fursa zilizopo.

Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Dodoma Fursa Mpya Kiuchumi Tanzania, Wekeza Dodoma Tukufanikishe’, inatanabaisha nafasi ya mkoa huo kwa sasa na baadaye.

Dkt. Mahenge alitaja baadhi ya fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Dodoma kuwa ni pamoja na uwepo wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, viwanda na taasisi (afya, elimu).


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akioneshwa mkoba uliyobuniwa na Wajasiriamali wa Kitanzania na Meneja Mzalishaji wa Fay Fashion Gregory Mlay, kwenye Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Dodoma, lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma Juni 27.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, wakati akikagua mabanda, kwenye Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Dodoma, lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma Juni 27.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, wakati akikagua mabanda, kwenye Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Dodoma, lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma Juni 27.2019.  

Read More

Wednesday, June 26, 2019

WAZIRI MHAGAMA APOKEA MSAADA WA VIFAA SAIDIZI NA CHEREHANI KUTOKA UBALOZI WA CHINA


NA; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amepokea cherehani na vifaa siadizi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu vilivyotolewa na Ubalozi wa China nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi ndogo za ubalozi huo zilizopo Jijini Dodoma, Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inatambua haki za Watu wenye Ulemavu nchini hivyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao stahiki ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi.
“Vifaa saidizi ni muhimu kwa kundi hilo maalumu kwa kuwa vinawawezesha kumudu mazingira yanayowazunguka na kuwasaidia kufanya shughuli zao za kila siku bila kukabiliana na changamoto,” alisema Mhe. Mhagama
Alieleza kuwa kutokana na vifaa hivyo kuwa ni ghali na upatikanaji wake umekuwa mgumu na kupelekea watu wenye ulemavu kushindwa kuvinunua, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo.
Aliongeza kuwa, katika ujenzi wa uchumi wa viwanda Serikali kupitia Shirika la kuhudumia viwanda Vidogovidogo (SIDO) kushirikiana na wadau imejipanga kuimarisha utengeneza wa baadhi ya vifaa hivyo, vitakavyokuwa vinapatikana hapa nchini.
Aidha alitoa wito kwa jamii kubadili mtazamo na fikra potofu juu ya watu wenye ulemavu, bali watambue kundi hilo linaweza na linamchango mkubwa katika jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke alisema kuwa Serikali ya China itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya wenye uhitaji.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa aliwataka wadau ndani na nje ya nchi kuendelea kujitokeza na kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Katika hafla hiyo pia aliudhuria Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza Mhe. Kemilembe Lwota.
 
Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke akielezea namna Serikali ya China imekuwa ikisaidia masuala mbalimbali nchini wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Vifaa saidizi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu na Cherehani kwa ajili ya wakina Mama iliyofanyika Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiteta jambo na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Vifaa saidizi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu na Cherehani kwa ajili ya wakina Mama iliyofanyika Jijini Dodoma katika Ofisi ndogo za Ubalozi huo Juni 26, 2019.

Sehemu ya washiriki katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi ndogo za Ubalozi wa China zilizopo Jijini Dodoma. 
Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke akimkabidhi cherehani kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke (katikati). Wa tatu kutoka kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza Mhe. Kemilembe Lwota na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq.
Baadhi ya Viongozi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama. Kushoto ni Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq(kulia).
Baadhi ya Wadau walioshiriki kwenye hafla hiyo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) pamoja na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke (katikati) wakimkabidhi Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa (kulia) Kiti Mwendo “Wheelchair” ikiwa ni sehemu ya maabidhiano wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akimkabidhi Fimbo Nyeupe “White Cane” mmoja wa wanafunzi wasioona kutoka Shule ya Msingi ya Buigiri. Wa tano kutoka kulia ni Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke. Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa.
Read More