Friday, May 28, 2021

TAMOBA wafanya wasilisho la mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama wa Bodaboda na Bajaji

 



Kampuni ya Tanzania Motorcycle and Bajaj Association (TAMOBA) imefanya wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu.Lengo la wasilisho hilo ni kuutambulisha rasmi mfumo huo kwa Wizara,  Idara na Taasisi za serikali.


Kwa mujibu wa wasilisho la TAMOBA,liliowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Joseph Kimisha, limebainisha kuwa zipo faida za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na mfumo huo Kurahisisha udhibiti wa uhalifu kwa kupitia mfumo wa kielektroniki katika kupashana taarifa za wahalifu na kihalifu, Kukuza ajira kwa Vijana kwa kurasimisha biashara ya pikipiki (Bodaboda) na bajaji. Pia mfumo huo utaongeza ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za polisi.


Kikao hicho kimeongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Kaspar Kaspar Mmuya, na kuhudhuriwa na Wajumbe kutoka Wizara ya Mambo ya ndani - Jeshi la Polisi, Kamishina wa Ushirikishwaji Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Dkt. Mussa Ali Mussa, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na Ofisi ya WazirI Mkuu – Idara ya Uratibu wa Shughuli za serikali.


Mfumo huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2019 na aliyekuwa makamu wa pili wa Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ally Idd, jijini Dar es Salaam. Aidha, TAMOBA tayari wameandaa Kitabu cha Mwongozo wa kufichua na kuzuia Uhalifu kwa Polisi, Maafisa Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji ambapo wataanza na Usajili wa Pikipiki (Boda Boda) kwa kuanza na mkoa wa Dar es salaam kama mkoa wa majaribio, lengo likiwa ni kuifikia mikoa yote nchini.


Mnamo mwaka 1980 serikali  iliruhusu kampuni binafsi  za ulinzi kutoa huduma za ulinzi hapa nchini, chini ya uangalizi , uratibu na usimamizi  wa Jeshi la polisi kwa mujibu wa Katiba na sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi kwa mujibu wa Sura ya 322, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

MWISHO.

 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Kaspar Kaspar Mmuya akifuatilia wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu, kutoka kwa Kampuni ya TAMOBA, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TAMOBA, Joseph Kimisha, akibainisha faida za kiuchumi na kijamii za mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu, wakati wa wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma.

Kamishina wa Ushirikishwaji Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Dkt. Mussa Ali Mussa akifuatilia wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu, kutoka kwa Kampuni ya TAMOBA, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali (Ufuatiliaji), Devotha Gabriel, akifuatilia wasilisho maaluum kwa Ofisi hiyo, kuhusu mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu, kutoka kwa Kampuni ya TAMOBA Jijini Dodoma, kulia kwake ni Afisa Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi na Idara hiyo, Ewald Bonifasi.


Baadhi ya wajumbe wa kikao wakifuatilia wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama kwa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya moto hasa Pikipiki za miguu miwili na mitatu, kutoka kwa Kampuni ya TAMOBA Jijini Dodoma, Wajumbe hao ni kutoka Wizara ya Mambo ya ndani - Jeshi la Polisi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na Ofisi ya WazirI Mkuu – Idara ya Uratibu wa Shughuli za serikali.


Read More

Thursday, May 27, 2021

Waziri Mhagama: Tatizo la ajira nchini, Tafiti kwenye nguvu kazi na Rasilimali watu kufanyika mwaka huu.


 

Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), imepanga mwaka huu kufanya tafiti mbili kubwa ambazo zitajikita kwenye kubaini nguvu kazi pamoja na rasilimali watu.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.


Ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanaendelea kushirikiana ambapo Wizara hiyo inapitia sera ya elimu na huku Ofisi hiyo ikifanya tafiti.


“Mwaka huu tumeamua kufanya tafiti mbili kubwa ambapo tafiti moja tunaendelea nayo ambayo ni hali ya nguvu kazi nchini. Utafiti huo utatausaidia kujua ni asilimia ngapi ya vijana wanaofundishwa ndani ya  nchi na  wanaweza kuajirika nchini  na kama hawaajiriki ni kwa nini. Aidha Utafiti huo utatusaidia kuelewa sekta ipi yenye fursa nyingi kuliko sekta nyingine ya ajira hii itasaidia mafunzo ya ufundi yaendane na mahitaji yetu ya ajira” Amesisitiza Mhagama


Aidha, Mhe. Mhagama amefafanua kuwa serikali imeshakamilisha utaratibu wa kufanya utafiti wa Hali ya rasilimali watu nchini. Utafiti huo utasaidia kuelewa juu ya watanzania waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kama wanaendana na mahitaji ya ajira kwa sasa.


Ameongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikisimamia vibali vya ajira kwa wageni, hivyo wataelewa sababu ambazo hupelekea wawekezaji kuhitaji kuwaleta watu wao wenye ujuzi ile hali wenye ujuzi wa viwango hivyo wapo hapa Tanzania, lakini pia itaeleweka maeneo gani ambayo nchi haina ujuzi na wangependa ujuzi huo upatikane hapa nchini.


Mhe. Mhagama amewataka wadau wa elimu ya Ufundi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha changamoto za ajira zinashughulikiwa ipasavyo nchini. Amesisitiza kuwa ili kuweza kuwa na uchumi wa kati endelevu hadi kufikia uchumi wa juu tunahitaji kuwa na mfumo rasmi wa kuwandaa vijana katika viwango vya juu vya maarifa, ujuzi, na stadi za kutenda. 


Mhe. Mhagama amefafanua kuwa kwa sasa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwenye sekta ya nishati ya umeme, Reli ya kisasa, kwenye Sekta ya Afya na Elimu pamoja na Barabara na hivi karibuni utatekelezwa mradi wa Bomba la mafuta kutoka Tanzania hadi nchini Uganda. Ameeleza kuwa miradi hiyo ili iwe endelevu ipo haja ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuendeleza uangalizi wa miradi hiyo.


Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la (NACTE), Prof. John Kondoro na Katibu Mtendaji (NACTE) Dkt. Adolf Rutayuga,wamefafanua kuwa  Kongamano hilo litalisaidia Baraza hilo kuwa na mipango ya kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika Elimu ya Ufundi.


Aidha, wamefafanua kuwa wataweza kuwa na suluhisho kwenye masuala ya kupata maeneo ya kutosha ya mafunzo ya vitendo, Upatikanaji wa Takwimu sahihi za wataalamu kwenye sekta za ajira, Kuimarisha uhusiano kati ya Taasissi za Mafunzo na soko la ajira, na hatimaye Elimu na Mafunzo ya Ufundi itaweza kutoa mchango mkubwa katika Maendeleo ya sekta zote za kiuchumi hapa nchini.


Pia, Mkurugenzi Idara ya Wanachama, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Zachy Mbenna ameiomba serikali kushirikiana na sekta Binafsi katika juhudi za kuendeleza kukuza ujuzi kwa kusimamia tozo inayotozwa ya kukuza ujuzi  kwa kuelekezwa kwenye kukuza ujuzi moja kwa moja  kwa kuishirikisha sekta Binafsi kwenye maoni ya matumizi yake.


Ameomba kiwepo chombo cha kitaifa kitakacho ratibu juhudi za kukuza ujuzi kwa kuwaunganisha wanaotoa mafunzo ya kukuza ujuzi. Aidha, ameomba kuwapa motisha waajiri wenye utaratibu wa kukuza ujuzi katika maeneo yao ya kazi kwa kupewa utambuzi wakati wa kulipa kodi, ameomba wadau hao wa sekta Binafsi wanaochangia masuala ya ujuzi kupewa mazingira ya kipaumbele wakati wa uwekezaji. Utekelezaji wa masuala hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wadau wanaotekeleza masuala ya kukuza  ujuzi nchini.


Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda” Wadau hao ni Serikali, Taasisi zinazotoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Waajiri. Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa ushirikiano na Taasisi ya Sekta Binafsi.

MWISHO.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akisisitiza umuhimu wa tafiti za nguvu kazi na Rasilimali watu, wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.

Baadhi ya wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakifuatilia Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma. Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda

Katibu Mtendaji (NACTE) Dkt. Adolf Rutayuga akifafanua umuhimu wa Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo litakavyosaidia kuibua mipango ya kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika Elimu ya Ufundi.

Baadhi ya wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakifuatilia Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma. Wadau hao wamebanisha kuwa  wataendelea kushirikiana na serikali ili Elimu na Mafunzo ya Ufundi iweze kutoa mchango mkubwa katika Maendeleo ya sekta zote za kiuchumi hapa nchini.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la (NACTE), Prof. John Kondoro akieleza umuhimu wa Kuimarisha uhusiano kati ya Taasissi za Mafunzo na soko la ajira, wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.

Baadhi ya wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakifuatilia Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma. Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo mara baada ya  kufungua  Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.







Read More

Wednesday, May 26, 2021

Waziri Mhagama ateta na Viongozi wa Plan International Tanzania


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Plan International – Tanzania, ofisini kwake jijini Dodoma.

 

Ujumbe huo umeongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa Plan International – Tanzania Dkt. Mona Girgis, akiwa na Meneja Miradi wa Plan Interanational Tanzania, Peter Mwakabwale,  pamoja na Meneja wa Uchechemuzi  wa Plan International  Tanzania.

 

Kupitia kikao hicho, Viongozi hao wa Shirika hilo walipata fursa ya kueleza kwa kina mipango yao ya kushirikiana na serika kwenye shughuli wanazozifanya. Wamebainisha kuwa wanayo miradi wanayo tekeleza katika kuchochea maendeleo ya vijana pamoja na kujumuisha watu wenye Ulemavu kwenye shughuli za maendeleo.


Katika Mazungumzo hayo Mhe. Mhagama amewahakikishia kuwa serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana nao katika mikakati ya maendeleo ya vijana na masuala ya watu wenye ulemavu. Amewaeleza kuwa  atawaelekeza Wataalamu wa Ofisi hiyo wakutane na Wataalamu wa shirika hilo ili wapange mipango mikakati ya kushirikiana nao.


Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi,vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu) inaratibu masuala ya Vijana na watu wenye Ulemavu kwa Uhamasishaji wa vijana, malezi na uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii, pia inaratibu masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa kutoa utaalamu na huduma kwa watu wenye ulemavu. 

 

MWISHO

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akiongea na viongozi wa Plan International – Tanzania, ofisini kwake jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na  viongozi wa Plan International – Tanzania, ofisini kwake jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Plan International – Tanzania Dkt. Mona Girgis mara baada ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano na shirika hilo walipomtembelea , ofisini kwake jijini Dodoma.


Read More

Tuesday, May 18, 2021

Serikali Wilayani Kilosa yawataka wanaoishi mabondeni kuhamia Maeneo salama yaliyotengwa

 


Serikali Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro imewataka wananchi  wanaoishi mabondeni kuhamia katika maeneo maalumu yaliyotengwa  na Halmashauri hiyo  ili kuepukana na athari za maafa ya mafuriko.


Hayo yamebainishwa Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi wakati wa ufunguzi wa semina ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko.


‘’Natoa wito kwa wananchi wanaojenga katika mapito ya maji wanazuia  maji kufuata mkondo wake na kusababisha maafa ya mafuriko lakini pia wa mabondeni wahamie maeneo ya miinuko na waliojenga kwenye maeneo ya kilimo na waliogeuza maeneo ya kilimo kuea makazi baadala ya kujenga makambi ya muda kwa ajili ya kusimamia mashamba yao warudi katika maeneo tuliyowapatia’’ amesema Mgoyi.


Mgoyi amebainisha kuwa kumekuwepo na utamaduni wa wananchi kutaka fidia maafa yanapotokea bila kutambua wao ni sehemu ya visababishi vya maafa hayo huku akiwasistiza kutokuwepo fidia kwa mwananchi ambaye atakaidi maagizo ya Serikali.


Sambamba na hayo, amefafanua kuwa Serikali Wilayani humo  imeanza mpango mkakati wa kuhuisha miundombinu ya maji ili kusaidia kukabiliana na kasi ya maji ambayo inaleta athari kwa wananchi Wilayani humo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura, Luteni Kanali,  Selestine  Masalamado, amewataka wananchi wilayani humo kuchukua hatua za kupunguza athari za maafa zikiwemo kutochimba madini kando ya mito, kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji kando ya mito hiyo.


Naye Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu) ambaye pia ni Mratibu wa Usimamizi wa maafa Mkoa wa Morogoro, Anza Ndossa  amebainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi hao kwa kuwa Wilaya ya Kilosa ina kata 40 huku 11 kati ya hizo zinaathirika na mafuriko ambapo kijiji cha Kitete huathiriwa sana na maafa  ambapo Machi 2020 kaya  takribani kaya 791 ziliathirika kwa maafa ya mafuriko.


Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), Reuben Mbugi ameihakikishia Serikali yaTanzania  kuwa wataendelea kushirikiana nao katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa yatokanayo na mafuriko.


Katika hatua nyingine, wananchi wa ya Kichangani, Tindiga na Changarawe wameishukuru serikali kwa kuendesha elimu hiyo ambayo itawasaidia katika kujenga uwezo wa kujiandaa, kuzuia na kukabili maafa ya mafuriko iwapo yatatokea.


Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kilosa chini ya Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), wanatoa elimu kwa umma inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na maafa ya mafuriko katika kata  tano za wilaya hiyo zilizo katika hatari zaidi ya kuathirika na maaafa ya mafuriko.

=MWISHO=

 

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe. Adam Mgoyi akisisitiza  wananchi wanao ishi maeneo hatarishi ya mafuriko kuhama na kuhamia maeneo salama yaliyotengwa kwa ajili yao, wakati wa ufunguzi wa semina ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura,  Luteni Kanali;  Selestine  Masalamado, akifafanua  umuhimu wa wananchi  wa wilayani humo kuchukua hatua za kupunguza athari za maafa zikiwemo kutochimba madini kando ya mito, kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji kando ya mito hiyo.

 

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.
Mratibu mradi, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), Reuben Mbugi akieleza namna ya shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali yaTanzania   katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa yatokanayo na mafuriko.

Mratibu wa Shughuli za serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, akiendelea kuwajengea uwezo Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.

Mratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Msangi akifafanua Utaratibu wa Tathmini za Maafa kwa mujibu wa sheria  ya maafa.

Mtaalamu wa Masuala ya Hali ya Hewa, Kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Suleimani Chilo, akielemisha matumizi sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wilayani Kilosa wakiwemo Viongozi wa dini wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi (Katikati walio kaa)

Baadhi ya wataalamu walioshiriki katika zoezi la kuelimisha jamii juu ya  maafa ya mafuriko kwa kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi (Katikati walio kaa)
Baadhi ya wataalamu walioshiriki katika zoezi la kuelimisha jamii juu ya  maafa ya mafuriko kwa kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko, 
wakiwa wakipata maelezo ya namana mito ya wilayani hivyo inavyosababisha mafuriko kutoka kwa Mratibu wa maafa wilayani humo, Maximillian Ndwangila.

Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura,  Luteni Kanali;  Selestine  Masalamado, akiwakabidhi wenyeviti wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko mabango na miti kwa ajili ya kuendelea na juhudi za kuhifadhi mito.

 



Read More

Sunday, May 9, 2021

Waziri Mhgama aridhishwa na utendaji wa NSSF

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amepongeza kazi inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF kwa kuhakikisha wanahudumia wateja kwa weledi na ufanisi katika kufikia malengo yaliyopo.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa NSSF mapema hii leo Mei 9, 2021 mkoani Morogoro waziri alionesha kufurahishwa na mwenendo wa mfuko ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha na kupata hati safi ya ukaguzi.

 

Waziri alieleza uwepo wa mafaniko hayo yanaenda sambamba na uwepo wa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi hivyo yaendelee kutumika kwa uhumimu wake ili kuimarisha umoja na mshikamano katika utendaji kazi wa kila siku.

 

“Mabaraza ya Wafanyakazi ni vyombo vya ushauri na usimamizi yana wajibu wa kuhakikisha kuwa Waajiri na Watumishi wanatambua wajibu na haki zao, wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji kazi yenye tija, staha na upendo, hivyo tuyatumie kwa tija”. Alisema Waziri Mhagama.

 

Waziri alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wote wa mfuko huo kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na kutimiza wajibu kwa kila mmoja katika eneo lake la kazi.

 

“Ni muhimu wa kila Mtumishi kuonesha juhudi za utendaji kazi kwa kufuata kanuni za maadili ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005. Kanuni hizi zikifuatwa kwa ukamilifu Watumishi watatoa huduma bora na stahiki kwa Wanachama ambao ndiyo waajiri wetu”.Alisisitiza

 

Aidha aliendelea kuwaasa Mameneja wa Mikoa, Wakuu wa Idara na Vitengo wasimamie kwa dhati suala la maadili katika sehemu zao za kazi na kuendelea   kutumia muda wa kazi kuhudumia wanachama kwa kujibu hoja zao na kutatua kero zao kwa haraka na kwa ufanisi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alishukuru na kumhaidi Waziri kuyatendea kazi maelekezo yake na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakiksha malengo yanafikiwa.

 

“Nitafanya kazi kwa jududi na maarifa kwa kushirikiana na watumishi wote ili kukidhi mahitaji ya wanachama na nchi kwa ujumla”Alisema Mshomba.

Aliahidi kuendelea kuboresha huduma kwa kuhakikisha mifumo inakaa vizuri na kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri na kukomboa wakati huku wakifanya kazi kwa umoja.

 

AWALI

Mkutano wa 47 wa Baraza la Wafanyakazi wa NSSF ulilenga kupitia Taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Mfuko kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020; kujadili na kupitisha Mpango wa Mfuko wa Mwaka 2021/2022; na kujadili na kupitisha Bajeti ya Mfuko kwa mwaka 2021/2022.Aidha ulitoa fursa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Taasisi hiyo ili kuendelea kuwa na tija nchini.

 

=MWISHO=

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na meza kuu wakiimba wimbo wa umoja na mshikamano wakati wa mkutano huo.
 Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NSSF wakiimba wimbo wa umoja na         mshikamano kabla ya ufunguzi wa baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Baraza la Wafanyakazi la NSSF lililofanyika Mkoani Morogoro Mei 9, 2021.

Mkurugenzi Mkuu NSSF Bw.Masha Mshomba  ahutubia na kueleza utekelezaji wa ofisi yake kabla ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la NSSF lililofanyika Mkoani Morogoro.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NSSF wakifuatili kikao hicho.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma NSSF Bi. Lulu Mengele akiongoza mkutano wa baraza la wafanyakazi wa ofisi hiyo uliofanyika hii leo Mei 9, 2021 Mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NSSF wakifuatili kikao hicho.


Read More

Saturday, May 8, 2021

Mwongozo wa Uwekezaji Tabora Wazinduliwa

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amezindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora ulilofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike ulipo katika Ofisi za mkuu wa mkoa huo tarehe 8 Mei, 2021.

 

Mwongozo huo umetayarishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Mkoa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

 

“Mwongozo wa uwekezaji ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuzitangaza fursa zilizopo hapa mkoa wa Tabora zipate wawekezaji na kusaidia kuinua hali ya uchumi wa watu wa mkoa huu na Taifa kwa ujumla,”Alisema Waziri Mwambe.

 

Waziri Mwambe amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wetu.

 

“Nimesoma mwongozo kuhusu utajiri na fursa nyingi zilizopo katika mkoa huu zikiwemo za maliasili, madini, mifugo, kilimo cha tumbaku, pamba, alizeti pamoja na shughuli za ujasiriamali mdogo na wa kati hivyo zitumieni kwa tija ya uchumi wa taifa kwa ujumla,”alisisitiza Waziri Mwambe.

 

Aliongezea kuwa, zipo fursa mpya zinazojitokeza katika mkoa huu ambazo ni pamoja na bomba la mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga na kupiti mkoa wa Tabora, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, umeme wa REA, barabara za lami, Maji toka Ziwa Victoria na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali.

 

Aidha Waziri alieleza matarajio yake kuhusu hali ya uwekezaji katika mkoa huo ikiwemo, kuona kila mtendaji wa Serikali ataondokana na urasimu, na vikwazo visivyo na tija ambavyo vinawakwaza wawekezaji wanapofika katika mkoa kuwekeza.

 

Akihitimisha hotuba yake, aliutaka mkoa kuendelea kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji cha Kanda (TIC) kilichopo Kigoma kuanzisha Kituo cha kutolea huduma kwa pamoja (One Top Centre) na kuhakikisha kinakuwa na rasilimali za kutosha.

 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama alisema Mpango huu utawawezesha wakulima hususan vijana kupata pembejeo na masoko ya kuaminika ya bidhaa zao na kuhakikisha wanajikita katika kilimo cha mashamba ya Pamoja.

 

Programu ya Kilimo cha Mashamba ya Pamoja (Block Farming) inaratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha wananchi hususan vijana kufanya kilimo biashara chenye tija na kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo ambapo kupita kilimo cha pamoja vijana watawezeshwa kupata mbolea kwa urahisi, kupata pembejeo za kilimo, kuwekewa utaratibu mzuri na nafuu wa kusafirisha bidhaa zao kutoka shambani hadi sokoni na watawezeshwa kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao,”alisistiza Waziri Mhagama.

Mfumo huu ukisimamiwa vizuri ndio njia sahihi itakayoiwezesha nchi yetu kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo. Mfumo huu unachochea matumizi ya teknolojia za kisasa na kuwezesha tija kubwa katika sekta ya kilimo.

 

Naye Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Philemon Sengati  alishukuru hatua muhimu ya uzinduzi wa mwongozo huo, huku akieleza namna mkoa utakavyohakiksha unatekelezwa kwa vitendo na kukiri ni tukio la kihistoria na la heshima kwa mkoa kwa ujumla.

Alifafanua kuwa, uwepo wa mwongozo huo utasaidia kutangaza fursa na vivutio vya uwekezaji ikiwemo ardhi, idadi kubwa ya mifugo takribani milioni 3.7, utalii wa kihistoria, uwepo wa madini na mapori ya akiba pamoja na misitu ya hifadhi inayofaa kwa ufugaji wa nyuki na uvunaji wa mazao ya misitu.

“Zipo sababu nyingi za kuwekeza Tabora ingawa hili la utashi wa kisiasa limechochea kuvutia wawekezaji katika kuhakikisha changamoto na vikwazo vinaondolewa kwa wakati,”alisema Dkt. Sengati

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP hapa nchini, Bi.Christine Musisi alisema UNDP itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Alisema UNDP itaendelea kusaidiana na Mikoa katika utekelezaji wa miongozo hii kwa kutoa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha panapohitajika.

 

 “UNDP kwa Kushirikiana na Serikali, Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) zimefanikisha kuandaa miongozo katika mikoa 25 na miongozo hiyo ipo katika hatua mbalimbali na itazinduliwa siku za hivi karibuni,”alisema Musisi

 

Mawaziri wengine waliohudhuria na kutoa neno ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.


=MWISHO=

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora, hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.Uzinduzi ulifanyika Mei 8, 2021 Tabora.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe pamoja na viongozi alioambata nao wakionesha kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji kwa Mkoa wa Tabora mara baada ya uzinduzi rasmi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama akihutubia wakati wa uzinduzi huo.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akitoa salamu za Wizara yake wakati wa uzinduzi huo.

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa salamu za wizara yake wakati wa uzinduzi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya KilimoTanzania (TADB), Japhet Justine akitoa salamu za ofisi yake wakati wa uzinduzi huo.

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama akiangalia vikapu zinavyotengenzwa na wajasiriamali wa mkoa wa Tabora wakati wa maonesho yaliyoambatana na uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Tabora.

 

Read More