Sunday, September 30, 2018

WAZIRI MKUU ATAKA WACHIMBAJI WADOGO WAENDE BENKI WAKAKOPE MITAJI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo wa madini waende Benki wakakope mitaji kwa sababu wana uhakika wa kudhaminiwa na Benki Kuu.

“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la kawaida sana. Nenda mkakope ili mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu na madini mengine,” amesema.

Ametoa wito leo (Jumapili, Septemba 30, 2018) wakati akifunga maonesho ya mkoa wa Geita ya dhahabu, madini, teknolojia ya madni na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita. Maonesho hayo yalianza Septemba 24, mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema, wakati akikagua mabanda ya maonesho kwenye viwanja hivyo, ameelezwa kwamba gharama ya mtambo unaohitajika kwa wachimbaji wa kati inafikia sh. milioni 10. “Naomba niwaeleze wanaGeita kwamba mnakopesheka, nendeni mkaombe mikopo ili mnunue mitambo ya kuchenjua dhahabu,” amesisitiza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaeleza wana-Geita kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kwa wao kuunganisha nguvu kwa kujiunga kwenye vikundi ili wawe na malighafi ya kutosha mitambo hiyo.

“Wakuu wa wilaya za Mkoa huu simamieni zoezi hili kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa vikundi na mwende mkawasemee benki pale wanapokwama.”

Akielezea kuhusu makusanyo ya fedha kutokana na mauzo ya dhahabu kwenye mkoa huo, Waziri Mkuu amesema tangu Aprili mwaka huu, mapato yanayotokana na madini yameongezeka kutoka sh. milioni 400 na kufikia sh. milioni 850 Agosti, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wazazi wawapeleke watoto wao kwenye vyuo vya ufundi vya VETA ili wakajifunze taaluma ya uchongaji wa madini na vito kama eneo jipya la ajira nchini.

“Nimemuona binti mmojakwenye banda la VETA akielezea vizuri kuhusu uchongaji wa madini na vito. Nikabaini kumbe jambo hili linaweza kufanyika hapa nchini kwetu. Ninawasihi Wazazi pelekeni watoto wenu kwenye vyuo vya VETA vya Mwanza, Geita na Moshi ambako kozi hii inafundishwa,” amesisitiza.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria maonesho hayo, Waziri wa Madini, Bibi Angella Kairuki alisema sekta ya madini ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 4.8 tu, licha ya kuwa sekta hiyo iliongoza kwa kuingiza fedha za kigeni kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi katika mwaka 2016/2017.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.  

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya thamani ya madini yanayouzwa nje ya nchi ni dhahabu na kwamba mkoa wa Geita unaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu ambapo katika mwaka 2017, asilimia 41.2 ya dhahabu iliyouzwa ilitoka kwenye mkoa huo.

“Kwa upande wa wachimbaji wadogo wanaozalisha dhahabu, mkoa wa Geita unaongoza ambapo tani 1.175 za dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 89 zilizalishwa, na kati ya hizo, asilimia 49 ilizalishwa na wachimbaji wadogo,” alisema.

Alisema takwimu hizo zilipatikana kabla Serikali haijachukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa carbon yenye dhahabu kuvuka mipaka ya mkoa, hali iliyokuwa inachangia utoroshaji, ukwepaji wa kodi na jamii husika kushindwa kunufaika na madini yayiyopo kwenye maeneo yao.

Maonesho hayo yamekutanisha makampuni 250 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na yataendelea hadi Jumatano jioni, Oktoba 3, 2018 kutokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kwa Waziri Mkuu ili wananchi wa mkoa wake wapate fursa zaidi ya kujifunza masuala ya madini, uwekezaji na matumizi ya teknolojia sahihi zinazozingatia utunzaji wa mazingira.

Kaulimbiu ya maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini, inasema: “Teknolojia bora ya uzalishaji dhahabu kwa maendeleo ya kijamii na uchumi wa viwanda”.

(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AHUDHURIA MAONESHO GEITA TAREHE 30.09.2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, mara baada ya kuwasili mkoani humo kufunga maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimuuliza maswali mwanafunzi wa VETA Moshi, Jesca Jonathan (mwenye rasta), kuhusu utaalamu wa kuchonga vito na madini alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Wa pili kulia ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kifungashio cha kopo la kahawa aina ya AMIMZA alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Kulia ni Afisa mauzo wa TANICA PLC, Revina Peter akitoa maelezo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea maelezo ya mtambo wa kuchenjua madini unaoweza kumilikiwa na wachimbaji wa kati alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita, Septemba 30, 2018. Anayetoa maelezo ni Katibu Msaidizi wa UMUMAGE, John Ngenda.

Mwanafunzi wa mwaka pili katika chuo cha VETA Moshi, Careen Vedasto akiendesha kifaa cha kuchimbia madini kilichobuniwa na wanafunzi na walimu wa chuo hicho mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea mabanda kwenye maonesho ya dhahabu, madini, teknolojia ya madini na uwekezaji, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita,Septemba 30, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel.
Read More

Thursday, September 27, 2018

SERIKALI KWA SASA INABORESHA MAENEO YA UTAWALA-MAJALIWA

*Asema lengo ni kuziwezesha halmashauri kujiendesha zenyewe

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri kujiendesha zenyewe. 

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, jijini Dodoma. 

Ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa maombi mengi ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala nchini. “Kama mnakumbuka nimekuwa nikieleza mara kadhaa kwamba tunazishukuru Serikali za Awamu zilizotangulia kwa kuainisha maeneo ya utawala.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanapaswa wajitathmini sambamba na kuainisha mikakati mizuri ili kuhakikisha lengo la kusogeza huduma kwa wananchi linatimia.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2014/15 jumla ya halmashauri 66 na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379 na vitongoji 8,777. Hadi sasa, maeneo hayo hayajaweza kuwa na miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha ili kuwezesha wananchi kupata huduma iliyokusudiwa. 

“Mathalani, mkoa wa Songwe halmashauri zake zote, hata halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo ndiyo makao makuu ya mkoa bado haujafikia vigezo vya kuwa Manispaa. Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na huwezi kuamini kama ni Ofisi za Halmashauri.” 

“Taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari sh. bilioni 120.7 zimepokelewa kwenye halmashauri mbalimbali kati ya sh. bilioni 238.8 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri sawa na asilimia 50.54 ya fedha zote. 

Amesema kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya Serikali na mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo baadhi yake zitapewa fedha za kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki kwa sababu zimekuwa zikipokea fedha kwa muda mrefu. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa halmashauri hizo wahakikishe wanajenga Ofisi za Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji badala ya kuendelea kuanzisha Serikali hizo huku zikiwa hazina hata ofisi. 

Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na zoezi la kuajiri watumishi hususan wa kada za afya na elimu, ambapo kati ya mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya elimu 13,472 na afya 8,238 kwa lengo la kuziba mapengo yaliyopo.

(mwisho)
Read More

JUMLA YA VIWANDA 1,596 VIMEJENGWA NCHINI-MAJALIWA


*Asema ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya viwanda 1,596 vimejengwa ambapo ni sawa na asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 hadi Desemba 31, 2018 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, jijini Dodoma. 

Waziri Mkuu amesema kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa Nchi OR- TAMISEMI kwamba kila Mkoa ujenge viwanda 100.

Amesema tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea uchumi wa viwanda, inaonesha kwamba mpaka sasa jumla ya hekta 367,077 zimetengwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya viwanda vikubwa, viwanda vya kati na viwanda vidogo. 

“Nitoe wito kwenu kwamba mwendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika hili, tujue katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa kwa viwanda vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na kuna mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi zilizozalishwa kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo.” 

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kushiriki katika kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua fursa za uwekezaji.

Pia kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vikubwa ili Tanzania iweze kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. “Tumieni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia vikundi vyao ili wawekeze katika viwanda vidogo vidogo vyenye kuleta tija na kuongeza pato la kaya ili kuutokomeza umaskini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali katika Dira ya Maendeleo ya 2025 ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kujitegemea kimapato kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo 2025. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha lengo hilo linatimia. Serikali imeanzisha utaratibu wa kugharamia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuziongezea halmashauri mapato ya uhakika na kupunguza utegemezi wa ruzuku.

“Hadi sasa, sh. bilioni 131.5 zimeidhinishwa kutekeleza miradi ipatayo 22 katika halmashauri 17 zilizokidhi vigezo kwenye mikoa 10. Hivi ninavyozungumza, tayari kiasi cha sh. bilioni 16.4 zimekwishapelekwa kwenye halmashauri hizo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.” 

Waziri Mkuu amesema kuwa uchambuzi wa miradi mingine zaidi unaendelea na halmashauri zitakazokidhi vigezo zitapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. 

Amesisitiza kwamba fedha hizo zikatumike kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. Amesema kwa sasa, hatutakuwa na utaratibu wa kutoa fedha bila kufahamu kwa kina fedha hizo zinakwenda kufanya nini na zitaleta mabadiliko gani. 

“Nimesikia kwamba katika baadhi ya halmashauri fedha zilizokwishatolewa bado hazijaanza kutumika kikamilifu watu wanaendelea kujadili namna ya kuzitumia, niwakumbushe tu kwamba Mheshimiwa Rais hakutoa fedha hizo ili zikakae benki. Wakurugenzi wa Halmashauri mlisaini makubaliano ya matumizi ya fedha hizo, hivyo, zingatieni hilo.”

Waziri Mkuu amewataka Madiwani wasimamie matumizi ya fedha hizo ili halmashauri zipate miradi yenye ubora unaotakiwa, inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa pamoja na inayokamilika kwa wakati. 

Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 34 inasema Umuhimu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Kutoa Huduma na Ushiriki wa Wananchi Kupitia Fursa na Vikwazo Kuelekea Uchumi wa Viwanda”.

Amesema kauli mbiu hiyo, inatilia mkazo maneno ya awali ya Rais Dkt. Magufuli, kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo karibu zaidi na wananchi na zinapaswa kutoa huduma na kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


(mwisho)
Read More

MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA 34 WA ALAT JIJINI DODOMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete kufungua Mkutano wa 34, wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa, Septemba 27, 2018.  Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo na kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt, Mary Mwanjelwa. Watatu kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Josephat Kandege na watatu kulia ni Meya wa jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu mitambo ya umeme kutoka kwa Kaimu  Mkurugenzi Mtendaji wa Tekinolojia na Masoko wa REA, Elineema Mkumbo (wapili kushoto) wakati alipotembelea banda la maonyesho la REA kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma, Septemba 27, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT)  kwenye ukumbi wa Jakaya  Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT)  kwenye ukumbi wa Jakaya  Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT)  kwenye ukumbi wa Jakaya  Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27, 2018.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Mkutano huo kwenye  ukumbi  wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma, Septemba 27, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiagana na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27, 2018. Kulia ni Mwenyekiti wa ALAT, Gulaam Hafeez 'Mukadam',   wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na wanne kulia  ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa. 

Read More

WAZIRI MKUU: WANAJIOSAYANSI MNA WAJIBU WA KULINDA MADINI YETU

*Ataka waisaidie Serikali kubaini vyanzo vya maji vya uhakika

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanajiosayansi nchini wawe walinzi wa kwanza wa rasilmali za madini, maji na mafuta bila kujali wako serikalini au kwenye sekta binafsi.

“Katika utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuwa wa kwanza kujua kinachoendelea katika sekta zote mnazohusiana nazo, yaani madini, maji na mafuta. Haijalishi unafanya kazi serikalini au shirika binafsi, wewe ni Mtanzania na una jukumu la kulinda rasilimali za nchi yako.” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Septemba 27, 2018), wakati akifungua warsha ya siku sita yaJumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania iliyoanza leo kwenye hoteli ya New Dodoma, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ambaye amefungua warsha hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka wanajiosayansi hao kutoka Serikalini, taasisi binafsi na vyuo vya elimu ya juu wasishiriki kulihujumu Taifa kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wasaliti namba moja.

“Msijihusishe au kushiriki kulihujumu Taifa lenu kwani kwa kufanya hivyo, mtakuwa wasaliti namba moja. Hakikisheni mnakuwa mabalozi wa Serikali katika mashirika haya kwa kutoa elimu juu ya sheria zinazosimamia sekta hizi huku mkisisitiza umuhimu wa kufuata sheria za nchi zenye kusimamia rasilimali zetu adhimu,” amesema.

Amesema mbali ya kilimo, rasilmali miamba na madini ndivyo vyenye mchango mkubwa wa kukuza viwanda kote duniani na kwamba utaalamu wa jiosayansi una mchango mkubwa kwenye malighafi za viwandani, upatikanaji wa maji ya kutosha nchini, mafuta, gesi asilia na uzalishaji wa nishati kupitia jotoardhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wanajiosayansi hao waisaidie Serikali kutafuta vyanzo vya maji vya uhakika ili itumie kihalali fedha zinazotengwa kwenye uchimbaji visima vya maji na kuepuka upotevu wa fedha.

“Ni jukumu la wanajiolojia la kutuambia wapi maji yapatikana. Muandae utaratibu mzuri wa kutunza takwimu kuhusu kiwango cha maji, ni wapi maji yalipo na ujazo wake. Kwenye eneo hili tumepoteza fedha nyingi sana, tumepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri ili tutoe huduma za maji wananchi lakini kwa sababu hatukuwashirikisha wanajiosayansi, wachimbaji wameenda kuchimba visima na wakakosa maji, yakabaki mashimo tu bila maji. Mna jukumu kubwa la kuisadia Serikali ili itumie vizuri fedha inazozitenga kwa ajili ya maji kwa kubainisha wapi kuna maji, yako kiasi gani na yako umbali gani,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri wa Madini, Bibi Angella Kairuki amesema wizara hiyo inakusudia kuanzisha chombo maalum cha usajili cha kuwatambua wanajiosayansi kisheria kupitia Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini (Geoscientists Registration Board -GRB) kama ilivyo kwa wahasibu, wahandisi na mabaraza ya wasajili mbalimbali ili kukabiliana na wataalamu feki wa fani hiyo.

“Wizara ya Madini inategemea wanajiosayansi wawe wazalendo kwa Taifa kwa kutoa taarifa za kitaalamu zinazoendama na uhalisia ili kuondoa malalamiko yanayotokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu hasa wale wanaojifanya wataalamu ilhali wakijua wazi hawana utaalamu wa fani hii,” amesema.

Amesema azma ya Serikali ni kumaliza changamoto zinazoikabili sekta hiyo ya madini zikiwemo ukiritimba uliokuwa ukifanyika katika mlolongo mzima wa utoaji leseni, utafutaji na uzalishaji wa rasilmali madini.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AFUNGUA WARSHA YA WANAJIOSAYANSI. JIJINI DODOMA.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa mwananjiolojia, Batwenge Chakutema kuhusu vifaa mbaIimbali vinavyotumika katika utafiti na upimaji madini wakati alipofungua Warsha  ya Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania  (Tanzania  Geological Society - TGS) kwenye hoteli ya New Dodoma, Septemba 27, 2018 .
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akifungua Warsha   ya Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania  (Tanzania  Geological Society - TGS) kwenye hoteli ya New Dodoma, Septemba 27, 2018 .


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia zawadi ya kinyago cha njiwa wawili kilichotokana na jiwe  wakati  alifungua  Warsha  ya Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania  (Tanzania  Geological Society - TGS) kwenye hoteli ya New Dodoma, Septemba 27, 2018 . Kushoto ni Waziri wa Nishati, Angela Kairuki na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Patrobas  Katambi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Warsha  ya Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania  (Tanzania  Geological Society - TGS) kwenye hoteli ya New Dodoma, Septemba 27, 2018 .

Read More

Tuesday, September 25, 2018

TNBC YAANDAA MWONGOZO WA MAJADILIANO WA KUBORESHA MASUALA YA SEKTA UMMA NA SEKTA BINAFSI NCHINI (PUBLIC PRIVATE DIALOGUE – PPD)

Baraza la Taifa la Biashara Nchini (TNBC) limeandaa mwongozo wa majadiliano utakaosaidia Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kupitia mfumo rasmi wa mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya nchini.
Hayo yamesemwa na Willy Magehema kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwamba lengo la mwongozo huo ni kuimarisha mahusiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii hasa zinazolenga katika kuwezesha ukuaji wa shughuli za biashara na uwekezaji nchini.
“Mwongozo huu utasaidia kuleta tija na ushirikiano wa Sekta Umma na Sekta Binafsi katika kuinua mipango ya maendeleo ya sekta Binafsi Nchini”, alisema Magehema.
Mwongozo huu unaeleza kutoa maelekezo ya mambo muhimu ya kuzingatia katika Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Dhumuni ni kuyaimarisha na kuyawezesha mabaraza ya Biashara ya MIkoa na Wilaya yaweze kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa kuelezea mambo yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa Maandalizi ya majadiliano;Uendeshaji wa majadiliano na baada ya majadiliano.
“Mwongozo huo utashirikisha wadau kutoka katika sekta zote pale inapohitajika ili kutakua kero na changamoto zinazojitokeza katika mabaraza ya biashara kama vile masuala ya ukusanyaji kodi, miundombinu, Afya na mengine yote yanayohusu Sekta ya umma na Sekta binafsi yataainishwa katika mwongozo huo” alisisitiza Magehema.
Pia mwongozo huo utatoa maelezo ya kina ikielezea ni yapi  ya  Kufanya na Kuepuka ili kuongeza ufanisi kwenye majadiliano kati ya Sekta Umma na Sekta Binafsi.
Mapema: Wadau walioshiriki katika kikao kazi hicho, wameeleza kuwa Baraza la Taifa la Biashara liendelee kujenga uhusiano mzuri utakaojenga uaminifu kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, vilevile wakuu wa Mikoa na Wilaya watambue kuwa maendeleo  ya mabaraza ya biashara yanaanzia katika mikoa yao na Wilaya zao kwanza.
TNBC  pamoja na wadau wengine watapitia rasimu ya mwongozo huo  itauhakiki kwa kushirikiana na wadau kwenye mikoa Tanzania bara na baadae kuwasilishwa katika kamati tendaji ya baraza la Taifa la Biashara kwa ajili ya uhakiki wa mwisho kabla ya kuanza kutumika.
Uandaaji wa mwongozo huu umeratibiwa na TNBC kwa msaada wa mradi wa Local Investment Cimate (LIC )na Enabling Growth Through Investment and Enterprise (ENGINE).
Read More

TNBC YAANDAA MWONGOZO WA MAJADILIANO WA KUBORESHA MASUALA YA SEKTA UMMA NA SEKTA BINAFSI NCHINI (PUBLIC PRIVATE DIALOGUE – PPD)

Wadau wakifuatilia uwasilishwaji wa mwongozo wa majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi  kupitia mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya katika kikao kazi kilichoandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) tarehe 25 Septemba, 2018 Jijini Dar es Salaam.

Wadau wakifuatilia kwa karibu uwasilishwaji wa mwongozo wa majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi  katika kikao kazi kilichoandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu tarehe 25 Septemba,2018 Jijini Dar es Salaam.

Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe Tawi la Dar es Salaam Prof. Honest Prosper Ngowi akiwasilisha majadiliano kwa wadau wakati wa kikao kazi cha Baraza la Taifa la Biashara kujadili Mwongozo kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa ngazi ya Mikoa na Wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam  tarehe 25 Septemba,2018.

Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Willy Magehema akifafanua jambo wakati wa majadiliano ya mwongozo baada ya kuwasilishwa na Mshauri mwelekezi katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Waziri Mkuu JijininDar es Salaam tarehe 25 Septemba, 2018

Patrick Mavika kutoka Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) akichangia jambo wakati wa kikao kazi cha majadiliano ya mwongozo kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kupitia mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya kilichofayika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam tarehe 25 Septemba, 2018. Kulia Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mtendaji wa TNBC Willy Magehema.

Read More

Monday, September 24, 2018

WAZIRI MKUU ATANGAZA TUME YA UCHUNGUZI AJALI YA MV NYERERE



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametangaza tume ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo itaongozwa na Jenerali mstaafu, George Waitara.

Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza leo (Jumatatu, Septemba 24, 2018), Waziri Mkuu amesema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Amewataja wajumbe wengine kuwa ni Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.

Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.

Amemwagiza Mkuu wa Majeshi, Jenarali Venance Mabeyo asimamie uundaji wa tume hiyo na kuainisha ni mahitaji gani yanatakiwa kwa haraka na pia afuatilie utekelezaji wake. 

MV Nyerere ilipinduka na kuzama Septemba 20, mwaka huu ambapo hadi sasa jumla ya watu 41 wameokolewa na wengine 227 wamepoteza maisha baada ya miili mingine mitatu kupatikana leo asubuhi. Jana yalifanyika mazishi ya kitaifa ambapo miili tisa ilizikwa kwenye eneo la uwanja wa shule ya msingi Bwisya. Miili 214 ilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao. 

Wakati huohuo,Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza itangazwe zabuni ya haraka ya kutengeneza kivuko kingine kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo na abiria zaidi ya 200.

“Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais, na mimi ninamuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aitishe zabuni hiyo haraka sana. Kazi hiyo ifanywe mara moja ili kivuko kipya kiweze kutengenezwa na kusaidia wananchi wa eneo hili kwa haraka,” amesema.

Amesema kivuko kipya kikikamilika, itabidi kipangiwe ratiba za safari nyingi zaidi badala ya kwenda mara moja kwa siku ili kuondoka kero ilikuwa ikiwakabili wananchi hao.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AKAGUA SHUGHULI ZA UOKOAJI MV NYERERE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya watu walionusurika  katika  ajali ya kivuko cha MV Nyerere wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Bwisya  kisiwani humo Septemba 24, 2018. Wengine ni mwananchi ambao bado wamepotelewa na  ndugu na jamaa katika ajali hiyo wakisubiri kutambua miili endapo itaonekana.

Gari la wagonjwa  likiwa limeegeshwa kwenye jengo la Kituo cha Afya cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara wilayani  Ukererwe ili kuteremsha mwili wa mtoto  ambao waokoaji  waliupata katika kivuko cha MV Nyerere Septemba  24, 2018. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea kituo hicho leo asubuhi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akikabidhi  kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isaack Kamwelwe mchango wa sh. milioni 10 zilizotolewa na CCM kwa ajili ya kusaidia katika  ajali ya Kivuko cha MV Nyerere  kilichozama ktika kisiwa cha Ukara wilayaniu Ukerewe, Septemba 20, 2018.  Makabidhiano hayo yalifanyika  katika kijiji cha Bwisya kisiwani Ukara, Septemba 24, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali, Venance Mabeyo  baada ya kumkabidhi jukumu kuwa msimamizi mkuu wa operesheni ya uokoaji katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, Septemba 24, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali, Venance Mabeyo  baada ya kumkabidhi jukumu kuwa msimamizi mkuu wa operesheni ya uokoaji katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, Septemba 24, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (katikati)  na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Faustine Kamuzora kwenye kijijii cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe baada ya Waziri Mkuu kutembelea eneo kilipozama kivuko cha  MV Nyerere kijijini hapo Septemba 24, 2018.

Read More

Sunday, September 23, 2018

MAJALIWA ASHIRIKI MAZISHI YA WALIOFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA KIVUKO CHA MV NYERERE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama  wakati alipowasili katika kijiji cha Bwasa kwenye  kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe kushiriki katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere, Septemba 23, 2018.

 Askari wakiweka kaburibi miili ya baadhi ya  wananchi walifariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama kwenye  kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati wa   mazishi yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kijiji cha Bwisa kisiwani Bukara, Septemba 23, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula na viongozi wengine walioshiriki katika mazishi ya  baadhi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya meli ya MV Nyerere katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe Septemba 23, 2018.

Wahandisi na mafundi wakifanya juhudi kubwa za kukivuta kivuko cha MV Nyerere ambacho kilizama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe .Baadhi Wananchi waliofariki dunia katika ajali hiyo walizikwa katika mazishi yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye kijiji cha Bwasa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Abood  (wapili kulia) akiungana na Masheikh katika  sala kwenye mazishi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Mazishi hayo yaliongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kijiji cha Bwisa  kisiwani Bukara, Septemba 23, 2018.

Read More

MAJALIWA AONGOZA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI KATIKA MAZISHI YA WANANCHI WALIOFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA MV NYERERE



 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama   katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama  katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bwisa  kisiwani Ukara Septemba 23, 2018.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhusu juhudi zinazofanywa  na wahandishi za kukivuta kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati aliposhiriki katika mazishi ya wananchi waliokufa katika ajali ya kivuko hicho kwenye kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Renatus Nkwande akiomba katika  mazishi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV  Nyerere kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Mazishi hayo yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yalifanyika katika kijiji cha Bwisa kisiwani Bukara, Septemba  23, 2018.




Read More