Tuesday, September 25, 2018

TNBC YAANDAA MWONGOZO WA MAJADILIANO WA KUBORESHA MASUALA YA SEKTA UMMA NA SEKTA BINAFSI NCHINI (PUBLIC PRIVATE DIALOGUE – PPD)

Baraza la Taifa la Biashara Nchini (TNBC) limeandaa mwongozo wa majadiliano utakaosaidia Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kupitia mfumo rasmi wa mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya nchini.
Hayo yamesemwa na Willy Magehema kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwamba lengo la mwongozo huo ni kuimarisha mahusiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii hasa zinazolenga katika kuwezesha ukuaji wa shughuli za biashara na uwekezaji nchini.
“Mwongozo huu utasaidia kuleta tija na ushirikiano wa Sekta Umma na Sekta Binafsi katika kuinua mipango ya maendeleo ya sekta Binafsi Nchini”, alisema Magehema.
Mwongozo huu unaeleza kutoa maelekezo ya mambo muhimu ya kuzingatia katika Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Dhumuni ni kuyaimarisha na kuyawezesha mabaraza ya Biashara ya MIkoa na Wilaya yaweze kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa kuelezea mambo yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa Maandalizi ya majadiliano;Uendeshaji wa majadiliano na baada ya majadiliano.
“Mwongozo huo utashirikisha wadau kutoka katika sekta zote pale inapohitajika ili kutakua kero na changamoto zinazojitokeza katika mabaraza ya biashara kama vile masuala ya ukusanyaji kodi, miundombinu, Afya na mengine yote yanayohusu Sekta ya umma na Sekta binafsi yataainishwa katika mwongozo huo” alisisitiza Magehema.
Pia mwongozo huo utatoa maelezo ya kina ikielezea ni yapi  ya  Kufanya na Kuepuka ili kuongeza ufanisi kwenye majadiliano kati ya Sekta Umma na Sekta Binafsi.
Mapema: Wadau walioshiriki katika kikao kazi hicho, wameeleza kuwa Baraza la Taifa la Biashara liendelee kujenga uhusiano mzuri utakaojenga uaminifu kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, vilevile wakuu wa Mikoa na Wilaya watambue kuwa maendeleo  ya mabaraza ya biashara yanaanzia katika mikoa yao na Wilaya zao kwanza.
TNBC  pamoja na wadau wengine watapitia rasimu ya mwongozo huo  itauhakiki kwa kushirikiana na wadau kwenye mikoa Tanzania bara na baadae kuwasilishwa katika kamati tendaji ya baraza la Taifa la Biashara kwa ajili ya uhakiki wa mwisho kabla ya kuanza kutumika.
Uandaaji wa mwongozo huu umeratibiwa na TNBC kwa msaada wa mradi wa Local Investment Cimate (LIC )na Enabling Growth Through Investment and Enterprise (ENGINE).


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.