Thursday, April 30, 2026

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA MFUMO WA PD-MIS MKOANI ARUSHA


 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu imehimiza watendaji wa Halmashauri zote za Jiji la Arusha matumizi ya Mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu.

Hayo yamesemwa katika Mafunzo yavitendo yaliyofanyika katika kata nne za jiji hilo ikiwa ni muendelezo na hitimisho la mafunzo ya mfumo wa PD-MIS yaliyowakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na maafisa ustawi wa jamii na TEHAMA jutoka Halmshauri zote za jiji la Arusha, yaliyochukua siku tatu ambapo makundi ya watu mbalimbali ya watu wenye ulemavu yamejitokeza kuitikia wito wa kujisajili katika mfumo.

Akizungumza wakati wa kilele cha mafunzo hayo, Afisa kutoka kitengo cha huduma kwa watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Gerold Komba ametoa shukrani za dhati Uongozi wa Mkoa na Maafisa ustawi wa jamii na Maafisa TEHAMA kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo tangu siku ya kwanza, Aidha aliwapongeza baadhi ya watu wenye ulemavu waliojitokeza kushiriki .

Amesisitiza kuwa ujuzi uliopatikana utakuwa nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya msingi ya ukusanyaji wa na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu.

Mafunzo haya yanatazamwa kama hatua ya kimkakati ya kuhakikisha Maafisa na Watendaji  wanakuwa na uelewa mpana wa kutekeleza majukumu yao katika kuwahudumia watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kukusanya na kusimamia taarifa za watu wenye ulemavu mkoani humo,jambo litakalosaidia kuimarisha  upatikanaji wa takwimu sahihi na kuimarisha na kuobresha upatikanji wa huduma kwa watu wenye ulemavu na kuinua Uchumi kwa watu wa Kundi hili.



Read More

Wednesday, April 29, 2026

SERIKALI YASISITIZA USHIRIKI WA VIJANA KATIKA UKUAJI WA UCHUMI


Serikali imesisitiza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele cha pekee kwa ushiriki wa vijana katika maendeleo, kwa lengo la kuinua vipaji, uwezo, na ari yao katika kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi,  leo jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la kwanza la kisayansi la vijana kuhusu VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jinsia na masuala mtambuka. Kongamano hilo limeandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Kabudi alisisitiza kuwa dhamira kuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kujenga taifa lenye nguvukazi iliyoelimika, yenye ujuzi na maono.

"Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele kwa vijana kwa kutumia vipaji na uwezo wao katika kufanikisha maendeleo endelevu. Nguvukazi hii itajengwa katika misingi imara ya ubunifu, ujasiriamali, na uwajibikaji," amesema Prof. Kabudi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia na afya ya akili.

Ameeleza kuwa, serikali imeanzisha madawati maalum ya ulinzi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo shuleni, vyuoni, na kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha huduma za kinga na msaada zinawafikia wahitaji kwa wakati.

Awali, akimkaribisha Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, amebainisha umuhimu wa kongamano hilo kwa ustawi wa vijana.

"Kongamano hili ni chachu ya mabadiliko ya fikra na utendaji, tunatarajia elimu watakayopata itakuwa mwanzo wa safari ya kujenga jamii yenye afya, matumaini, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wao," amesema  Dkt. Kilabuko.

Kongamano hilo la siku mbili linaongozwa na kaulimbiu; ‘’Kuunganisha Sayansi na Ubunifu katika Kukabiliana na Janga la VVU, Afya ya Uzazi na Jinsia, Kukuza Ustawi Kuelekea Dira 2050”.




Read More

KAGERA KUNUFAIKA NA MPANGO WA MKOA WA AFYA MOJA

KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw. Salum Kimbau amesema maandalizi ya Mpango wa Afya Moja kwa mkoa wa Kagera utaunufaisha mkoa huo kwa kuzingatia malengo yake ya kuboresha uratibu na utekelezaji wa Dhana ya Afya ya Moja na kuendelea kutatua changamoto zilizopo na zenye mwingiliano kati ya binadamu, wanyama na mazingira

Amezungumza hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa masuala ya Afya Moja kutoka sekta mbalimbali zikiwemo za afya, mifugo, mazingira, wanyamapori na kilimo ambao wamekutana katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kwa siku tano kuanzia tarehe 27 Aprili hadi 01 Mei, 2026 ili kuandaa Mpango huo utakaotumika kubaini rasilimali zitakazosaidia kutatua changamoto na vihatarishi vya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Bw. Kimbau amesema kuwa, mkoa utanufaika kwa uwepo wa Mpango huo kwani utaongeza tija katika kutatua changamoto zinazokabili sekta hizo hususan katika kuendelea kutatua changamoto za mwingiliano wa magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na binadamu kwenda kwa wanyama.

“Tunashukuru kuufikia mkoa wetu wa Kagera, tunajua kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanatokana na mwingiliano ulipo kati ya wanyama na binadamu, hivyo kuandaliwa kwa mpango kutasaidia utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja kwa kushirikiana pamoja, hivyo utatusaidia kutatua changamoto zilizopo na kuwa na jamii salama,” alisema Bw. Kimbau

Aliongezea kuwa ufanisi wa mpango huu unategemea ushirikishwaji wa sekta zote zinazohusika ili kuleta matokeo chanya.

Naye Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa sehemu ya Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Valentina Sanga amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeratibu maandalizi ya uwepo wa mpango huo huku akisihi kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matunda yanayotarajiwa.

Aidha, aliwasihi wataalamu wa Masuala ya Afya Moja kutumia fursa hiyo kuja na Mpango utakaoinufaisha Kagera, kwa kuzingatia ni miongoni mwa Mikoa inayokumbwa na majanga ya mlipuko mengine yakichangiwa na mwingiliano wa wanyama na binadamu.

“Dhana ya Afya Moja (One Health) inatoa fursa ya kutambua uhusiano wa karibu kati ya afya ya binadamu, wanyama, na mazingira. Inasisitizwa kuendelea kujifunza zaidi dhana hii ili kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za milipuko ya magonjwa na kuweza kuyakabili endapo yanatokea katika maeneo yetu,” alisisitiza Bi. Valentina

Aliongezea kuwa, Mpango huo utasaidia kutatua changamoto za masuala ya kiafya zinazotokea katika Halmashauri za mkoa wa Kagera, kujiandaa na kukabili majanga hayo ili kuwa na jamii salama kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la CIHEB Tanzania, Bw. Mark Lwakatare alisema mradi wa Usalama wa Afya Duniani utaendelea kushirikiana na mikoa husika katika kuimairisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja ili nchi iweze kukabiliana na vihatarishi vya majanga mbalimbali.

“Mradi huu unashirikiana na Serikali kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa afua mbalimbali kupitia dhana ya Afya Moja nchini, hivyo mradi utaendelea kushirikiana katika kujiandaa na kukabili athari katika afya ya binadamu, manyama na mazingira,” alisisitiza Lwakatare.

Read More

Tuesday, April 28, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MATUMIZI YA MFUMO WA PD-MIS KWA WATENDAJI ARUSHA


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imeendelea kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kutoa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji na Usimamizi wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu (PD-MIS) kwa watendaji wa mkoa wa Arusha.

Mafunzo hayo yametolewa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kwa Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa TEHAMA kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha matumizi ya mfumo huo katika ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa taarifa sahihi za watu wenye ulemavu yamefanyika, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Gerold Komba, alisema Serikali inaendelea kuhakikisha inaendelea kuweka mipango yake vizuri katika kuhakikisha kwamba kundi hili la watu wenye ulemavu linahudumiwa ipasavyo nchi nzima.

Alisema Mfumo huu wa PD-MIS kwasasa umeshasambazwa katika mikoa mbalimbali ambapo kwasasa mikoa yote ya Kanda ya ziwa, Magharibi na Kanda ya Kusini imeshafikiwa na Mfumo huu, na kwasasa Mfumo umeanza kanda ya kaskazini katika mkoa wa Arusha.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Arusha Bw. Dennis Mgie ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo haya kwani kupitia Mfumo huu takwimu za mkoa zinakua zenye ufanisi lakini pia zitawaongoza kwenye kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.

"Takwimu hizi zitatusaidia kuweza kuwaunganisha watu wenye ulemavu na huduma na fursa mbalimbali ambazo serikali inawezesha watu wenye ulemavu ambao tutawatambua kwa hali zao na kazi zao kupitia mfumo huu". Amesema Bw. Mgie.

 

 





 

Read More

Saturday, April 18, 2026

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WAJENGEWA UWEZO UENDESHAJI HUDUMA NATIONAL CALL CENTER

Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) wamejengewa uwezo katika usimamizi wa mawasiliano kwa wananchi na mbinu bora za kuhudumia wananchi pamoja na matumizi ya mifumo ya kisasa ya National call centre.

Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dar es Salaam ambapo Muwezeshaji Bw. Willynevilline Msamo kutoka Benki ya NMB alieleza umuhimu uwezo wa kushughulikia mawasiliano kwa ufanisi na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma ili kuhakikisha kila mwananchi anayewasiliana na taasisi anapata msaada unaostahili kwa wakati.

“Uanzishwaji na uimarishaji wa huduma za call centre, Ofisi ya Waziri Mkuu unalenga kutatua changamoto za wananchi kwa haraka kwa kuweka mfumo rahisi na wa moja kwa moja wa kupokea na kushughulikia maoni, malalamiko na mapendekezo yao,” alifafanua

Aidha huduma hii itawawezesha wananchi kupata mrejesho kwa wakati, kufuatilia masuala yao kwa ufanisi, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za serikali.

Bw, Msamo alisema, “hatua hii inaonesha dhamira ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya kuendelea kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa viwango vya juu zaidi”.


Read More

Friday, April 17, 2026

SERIKALI YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MIKAKATI YA KUIMARISHA MASLAHI YA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA

 


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imekutana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa watu wenye ulemavu nchini.

Kikao hicho kilichofanyika Jijini Dar es salaam, kimelenga kujadili na kuimarisha uelewa kuhusu Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu,kujadili rasimu ya Mwongozo wa Kitaifa wa Viwango vya Ufikivu, pamoja na kuongeza uelewa juu ya utekelezaji wa fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum.

Akifungua kikao hicho, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU), Bw. Bruno Mwakibibi, amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa kushirikiana na vyama vya watu wenye ulemavu ili kuongeza ustawi wa kundi hilo.

Aidha,amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuhakikisha malengo ya kuwainua watu wenye ulemavu yanafikiwa sambamba na hilo amebainisha kuwa lengo kuu la hivyo ni kuwaunganisha wanachama, jamii na Serikali kwa manufaa ya pamoja.

Aliendelea kusema kuwa, mwongozo huo, pamoja na sera, sheria na kanuni zilizopo, unalenga kuongeza ushiriki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ajira, siasa na afya, huku ukihakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.

Akiwasilisha rasimu ya Mwongozo wa Viwango vya Ufikivu, Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Jacob Mwinula, amesema kuwa ufikivu unahusisha kuboresha mazingira, huduma na taarifa ili ziwe rafiki na kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii.

Aliongeza kuwa, mwongozo huo wa kitaifa wa Viwango vya ufikivu unalenga kuweka viwango mahsusi vya ufikivu katika sekta mbalimbali, kuchochea ushiriki jumuishi na wenye tija, pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa fursa kwa watu wenye ulemavu badala ya vikwazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, Bi. Tungi Mwanjala, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo kwa watu wenye ulemavu na kupokea maoni yao kuhusu changamoto wanazokutana nazo.

Amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma ili kuboresha hali zao za maisha na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.



Read More

Monday, April 13, 2026

DKT. MANYATTA:NGUVU YA PAMOJA YATAKIWA KATIKA MAFANIKIO YA DHANA YA AFYA MOJA


 Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Afya Moja kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta, amesema kuwa Mpango Mkakati wa Afya Moja umejikita kuhakikisha wananchi wananufaika kuanzia ngazi ya  Kaya hadi Taifa kupitia utekelezaji shirikishi wa sekta mbalimbali nchini ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa na kuwa na tija kwa jamii kwa ujumla.

Dkt. Manyatta ameyasema hayo mkoani Tanga wakati wa kikao kazi cha wataalam cha kuandaa Mpango wa Mkoa wa Afya Moja kilichoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sehemu ya Afya Moja kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.

Amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuwajengea uwezo Watalamu ngazi ya mkoa kuhusu utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja na kuwawezesha kutengeneza Mpango wa Utekelezaji wa Afya Moja wa Mkoa ambacho kitafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili 2026 katika Halmashauri ya Mji wa Korongwe, Mkoani Tanga.

Dkt. Manyatta ameeleza kuwa, lengo la dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta/taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.

“Ushirikiano huu pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kimsingi unaongozwa na sekta/wizara za msingi (lead Ministries) ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote,” alifafanua Dkt. Manyatta.

Alifafanua kuwa, uwepo wa Mpango Mkakati ni muhimu kwani unatarajiwa kuweza kujibu na kutatua changamoto zilizopo katika Mkoa wa Tanga, hivyo utumike kama fursa ya kuhakikisha mkoa unakuwa na uelewa wa pamoja wa masuala ya Afya Moja kwa kuunganisha nguvu ya pamoja na kuweza kufanya kazi pamoja kwani hii ndiyo maana halisi ya dhana ya Afya Moja.

Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala, ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo amepongeza uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoendelea kutoa elimu ya masuala ya Afya Moja, na kueleza kuwa mkoa wa Tanga utanufaika kwa uwepo wa Mpango Mkakati wa Afya Moja na kusisitiza kuwa Tanga itautekeleza kwa vitendo na kufanya mkoa  huo kuwa wa mfano

“Ifike mahali tutoke katika mambo ya concept to Action, yaani kuwa na mipango na mikakati ya namna hii na kuitekeleza na hiyo ndiyo umuhimu wa dhana Afya Moja,” alisisitiza Dkt. Simeo

Kwa upande wake, Msimamizi wa  Afya Moja na Mratibu wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na Shirika lisilo la Serikali la  CIHEB Tanzania Dkt. Irene Massawe amesema kuwa, ushirikiano uliopo utasaidia kufanikisha malengo yaliyopo kwa nguvu ya pamoja na kuhakikisha matarajio ya uwepo wa mpango huo yanafika hadi ngazi za chini.

Aliongezea kuwa, sekta husika zikiungana kwa pamoja katika kutekeleza dhana ya Afya Moja itasaidia kudhibiti vihatarishi vya afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko hasa yale yanayoweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, yakiwemo ya kimeta, kichaa cha mbwa kwani itarahisisha na kuleta ufanisi katika kukabiliana na changamoto hizo.

“Tunaamini kuwepo kwetu ndani ya siku tano hizi Korogwe kutazaa matunda kwa washiriki wote kisha kuyaleta haya katika utekelezaji wa kila siku na kuhakikisha tunaleta matokeo chanya  ya mipango hii,” alisema Dkt. Irene.

AWALI

Afya Moja ni Dhana ya Kimataifa iliyoridhiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP) kupitia “Global Health Security Agenda” (GHSA) na wadau wengine wa Afya duniani kote. Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamekuwa yakishirikiana duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kuongeza na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ili kuboresha ufanisi katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na yanayovuka mipaka; tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa na changamoto zingine zinazokabili afya ya jamii zinazohitaji nguvu ya pamoja.

 

Read More

Thursday, April 9, 2026

PROF. KABUDI AKUTANA NA MJUMBE MAALUM WA KATIBU MKUU JUMUIYA YA MADOLA


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe.  Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Lazarus Chakwera jijini Dar Es Salaam.

Mjumbe Maalum huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo atakutana na wadau mbalimbali jijini Dar Es Salaam, Dodoma na Zanzibar.

Wakati wa ziara hiyo ambayo itahitimishwa Aprili 16, 2026. Mhe. Chakwera amepangiwa miadi ya kukutana na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na viongozi wastaafu.

Mhe. Chakwera aliwasili nchini Aprili 08, 2026 na kupokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na alianza ratiba yake kwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo Aprili 09, 2026 jijini Dar EsSalaam.



Read More

MAKATIBU WAKUU WAKUTANA KUJADILI HALI YA UPATIKANAJI WA MAFUTA

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu kilicholenga kujadili hali ya upatikanaji wa mafuta nchini, hususan petroli na dizeli.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma, kimejadili kwa kina changamoto zinazoikabili sekta ya mafuta pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo muhimu unaendelea kuwa wa uhakika.

Aidha, kikao hicho kilipokea na kuchambua taarifa ya kitaalamu kuhusu hali ya soko la mafuta, ikiwemo athari za mabadiliko ya kimataifa yaliyotokana na vita ya Iran, ambayo imeathiri mwenendo wa upatikanaji na bei za mafuta.

Washiriki wa kikao hicho walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa akiba ya mafuta na kuongeza ufanisi katika mifumo ya usambazaji.

Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la mafuta duniani ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kwa lengo la kulinda uchumi wa nchi na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa bila usumbufu.

Read More

SERIKALI YAZINDUA KIKOSI KAZI CHA TAIFA CHA UFUATILIAJI, TATHMINI NA UTOAJI TAARIFA

 


Serikali imezindua Kikosi Kazi cha Taifa cha Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa (ME&R National Task Force) kwa lengo kuratibu utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini katika kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko  wakati akifungua Kikao Kazi Cha Kikosi Kazi cha Taifa cha Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa (ME&R National Task Force) kilichofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Kilabuko amesema, Ufuatiliaji na Tathmini ni dhana muhimu ya usimamizi inayotumika kwa lengo la kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa afua za maendeleo.

“Kikosi Kazi hiki kitakuwa chombo cha kitaalamu cha kusaidia kuratibu utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa U&Tc, kuoanisha mifumo ya kitaifa ya utendaji, kuimarisha ubora wa takwimu na taarifa za Serikali na  kuandaa mapendekezo ya sera na maboresho ya kiutendaji” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Ameeleza kuwa, kikao kazi hicho ni fursa ya kipekee ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya  Ufuatiliaji na Tathmini nchini.

“Matarajio yangu ni kwamba, baada ya kikao hiki tutaboresha uratibu na kuoanisha viwango vya kitaifa vya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) katika Wizara, Idara na Wakala (MDAs), Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwiano na ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo” amefafanua.

Vilevile, Dkt. Kilabuko amebainisha kuwa ipo haja ya  kuoanisha viashiria vya taasisi na maeneo muhimu ya matokeo ya Kitaifa ili kuhakikisha kuwa juhudi za taasisi mbalimbali zinaendana na vipaumbele vya Taifa.

 “ Katika hili, ni muhimu kuimarisha mwingiliano na utangamano wa Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS), PIPMIS na Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo na Programu (NPMIS) ili kuwezesha mtiririko mzuri wa taarifa na matumizi ya data kwa ufanisi” ameeleza.



Read More

Wednesday, April 8, 2026

WATENDAJI OFISI YA WAZIRI MKUU WAKUMBUSHWA KUIMARISHA WELEDI KUTIMIZA DIRA YA TAIFA 2050

Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekumbushwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kujituma ili kuhakikisha wanachangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050, hususan katika maeneo ya sera, uratibu na usimamizi wa utekelezaji wake.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba J.A. Kabudi, wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kuwasili rasmi na kupokelewa na uongozi na watumishi wa Ofisi hiyo katika Jengo la Ngome Jijini Dodoma.

Prof. Kabudi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubunifu miongoni mwa watumishi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

“Ni muhimu tushirikishane mawazo na kufanya kazi kwa pamoja ili kumsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanikisha adhima ya maendeleo yenye kuleta ustawi na furaha kwa Watanzania," alisema Prof. Kabudi

Aliongezea kuwa upo umuhimu wa kushikamana ili kuendelea kuimarisha utendaji wetu ili kumwezesha Mheshimiwa Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Waziri Kabudi alibainisha kuwa mazingira ya kazi yenye mshikamano na mahusiano ya kifamilia hayapaswi kuwa chanzo cha uzembe au utovu wa nidhamu, bali yawe kichocheo cha kuongeza uwajibikaji na kufikia viwango vya juu vya utendaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi aliwataka watumishi kuendelea kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Marehemu William Vangimembe Lukuvi, ili Mwenyezi Mungu amrehemu na kumpa pumziko la milele.

“Nitaendeleza, kadri nitakavyoweza, misingi na jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wangu katika kuijenga Ofisi hii,” aliongeza.

Awali, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Ummy Nderiananga, alimpongeza Prof. Kabudi kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo, akiahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa watumishi wote katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, naye alimpongeza Waziri Kabudi kwa uteuzi huo na kusisitiza kuwa watumishi wako tayari kuongozwa na kushirikiana naye katika kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.





 

Read More

WAZIRI KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE MHE. ZUNGU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi (Mb), amekutana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), katika Ofisi ya Spika Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), alihudhuria na kushiriki katika mazungumzo hayo.

Read More

Wednesday, April 1, 2026

MAKATIBU WAKUU OFISI YA WAZIRI MKUU WAKIFUATILIA HOTUBA YA BAJETI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt. Jim Yonazi (kushoto), Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Bi. Mary Maganga  pamoja na  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Bw. Sospeter Mtwale(kulia) wakifuatilia Hotuba ya Bajeti inayotolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa Mwaka 2026/2027 tarehe 1 Aprili, 2026 Bungeni Jijini Dodoma.

Read More