Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imekutana
na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, viongozi wa vyama vya watu wenye
ulemavu pamoja na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka Mikoa mbalimbali ya
Tanzania bara kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa watu wenye
ulemavu nchini.
Kikao
hicho kilichofanyika Jijini Dar es salaam, kimelenga kujadili na kuimarisha
uelewa kuhusu Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu,kujadili
rasimu ya Mwongozo wa Kitaifa wa Viwango vya Ufikivu, pamoja na kuongeza uelewa
juu ya utekelezaji wa fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi
maalum.
Akifungua
kikao hicho, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu,
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU), Bw. Bruno Mwakibibi,
amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa
kushirikiana na vyama vya watu wenye ulemavu ili kuongeza ustawi wa kundi hilo.
Aidha,amesisitiza
umuhimu wa viongozi hao kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuhakikisha
malengo ya kuwainua watu wenye ulemavu yanafikiwa sambamba na hilo amebainisha
kuwa lengo kuu la hivyo ni kuwaunganisha wanachama, jamii na Serikali kwa manufaa
ya pamoja.
Aliendelea
kusema kuwa, mwongozo huo, pamoja na sera, sheria na kanuni zilizopo, unalenga
kuongeza ushiriki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali
ikiwemo elimu, ajira, siasa na afya, huku ukihakikisha hakuna kundi linaloachwa
nyuma.
Akiwasilisha
rasimu ya Mwongozo wa Viwango vya Ufikivu, Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu, Bw. Jacob Mwinula, amesema kuwa ufikivu unahusisha kuboresha mazingira,
huduma na taarifa ili ziwe rafiki na kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa
kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii.
Aliongeza
kuwa, mwongozo huo wa kitaifa wa Viwango vya ufikivu unalenga kuweka viwango
mahsusi vya ufikivu katika sekta mbalimbali, kuchochea ushiriki jumuishi na
wenye tija, pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa fursa kwa watu wenye
ulemavu badala ya vikwazo.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, Bi.
Tungi Mwanjala, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu fursa
zilizopo kwa watu wenye ulemavu na kupokea maoni yao kuhusu changamoto
wanazokutana nazo.
Amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma ili kuboresha hali zao za maisha na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.