KAIMU
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw. Salum Kimbau amesema maandalizi ya Mpango wa
Afya Moja kwa mkoa wa Kagera utaunufaisha mkoa huo kwa kuzingatia malengo yake
ya kuboresha uratibu na utekelezaji wa Dhana ya Afya ya Moja na kuendelea
kutatua changamoto zilizopo na zenye mwingiliano kati ya binadamu, wanyama
na mazingira
Amezungumza
hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa masuala ya Afya Moja kutoka
sekta mbalimbali zikiwemo za afya, mifugo, mazingira, wanyamapori na kilimo
ambao wamekutana katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kwa siku
tano kuanzia tarehe 27 Aprili hadi 01 Mei, 2026 ili kuandaa Mpango huo
utakaotumika kubaini rasilimali zitakazosaidia kutatua changamoto na
vihatarishi vya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Bw.
Kimbau amesema kuwa, mkoa utanufaika kwa uwepo wa Mpango huo kwani utaongeza
tija katika kutatua changamoto zinazokabili sekta hizo hususan katika kuendelea
kutatua changamoto za mwingiliano wa magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa
binadamu na binadamu kwenda kwa wanyama.
“Tunashukuru
kuufikia mkoa wetu wa Kagera, tunajua kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanatokana
na mwingiliano ulipo kati ya wanyama na binadamu, hivyo kuandaliwa kwa mpango
kutasaidia utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja kwa kushirikiana pamoja, hivyo
utatusaidia kutatua changamoto zilizopo na kuwa na jamii salama,” alisema Bw.
Kimbau
Aliongezea
kuwa ufanisi wa mpango huu unategemea ushirikishwaji wa sekta zote zinazohusika
ili kuleta matokeo chanya.
Naye
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa sehemu ya Afya Moja
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Valentina
Sanga amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika lisilo la
Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeratibu
maandalizi ya uwepo wa mpango huo huku akisihi kuunganisha nguvu ya pamoja
katika kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matunda yanayotarajiwa.
Aidha,
aliwasihi wataalamu wa Masuala ya Afya Moja kutumia fursa hiyo kuja na Mpango
utakaoinufaisha Kagera, kwa kuzingatia ni miongoni mwa Mikoa inayokumbwa na
majanga ya mlipuko mengine yakichangiwa na mwingiliano wa wanyama na binadamu.
“Dhana
ya Afya Moja (One Health) inatoa fursa ya kutambua uhusiano wa karibu kati ya
afya ya binadamu, wanyama, na mazingira. Inasisitizwa kuendelea kujifunza zaidi
dhana hii ili kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za milipuko ya magonjwa na
kuweza kuyakabili endapo yanatokea katika maeneo yetu,” alisisitiza Bi.
Valentina
Aliongezea
kuwa, Mpango huo utasaidia kutatua changamoto za masuala ya kiafya zinazotokea
katika Halmashauri za mkoa wa Kagera, kujiandaa na kukabili majanga hayo ili
kuwa na jamii salama kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Shirika la CIHEB Tanzania, Bw. Mark Lwakatare alisema
mradi wa Usalama wa Afya Duniani utaendelea kushirikiana na mikoa husika katika
kuimairisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja ili nchi iweze kukabiliana na
vihatarishi vya majanga mbalimbali.
“Mradi
huu unashirikiana na Serikali kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa afua
mbalimbali kupitia dhana ya Afya Moja nchini, hivyo mradi utaendelea
kushirikiana katika kujiandaa na kukabili athari katika afya ya binadamu,
manyama na mazingira,” alisisitiza Lwakatare.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.