Thursday, February 23, 2023

TANZANIA YA KWANZA KUSAINI MKATABA WA KITUO CHA HUDUMA YA DHARURA CHA MAAFA MIONGONI MWA NCHI ZA SADC

 


Tanzania imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na oparesheni za dharura za kanda.

Akizungumza mapema hii leo wakati wa hafla ya utiaji Saini iliyofanyika Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.

Aliongeza kuwa, Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa  na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.

“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa.” Alifafanua.

Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi; Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.

 

Awali mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.

“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu” Alifafanua Dkt Matto.

Read More

Friday, February 17, 2023

DKT.JINGU:WAKULIMA TUONGEZE MSUKUMO WA KUFANYA KILIMO CHENYE TIJA.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri zaidi.

Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Saalam.

Dkt. Jingu amesema dhamira ya Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.

Aliongezea kuwa Serikali itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

“Mwelekeo ni kwamba shughuli wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi ni biashara,” alisema Dkt.Jingu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema Uvuvi wetu bado tunatumia mbinu za zamani lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa zitakazofanya wavuvi waongeze tija.

Ameongeza kusema kuwa, jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.

“Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” alisema Dkt.Madalla

Aidha Serikali itaenda kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.

"Tunaimani zao hili litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili,"alisisitiza Dkt. Madalla

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi  ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na uwekezaji.

 

Read More

Thursday, February 16, 2023

MEJA JENERALI MBUGE: TUTAENDELEA KUJIPANGA KATIKA KUKABILANA NA MAAFA NCHINI


 SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini ili kuhakikisha inapunguza madhara yatokanayo na maafa.

 

Kauli hiyo imetolea na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha wadau cha kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya African Dream Jijini Dodoma.

 

Kikao kazi hicho kililenga kupitia na kujadili rasimu ya mpango huo wenye malengo ya  kusimamia mawasiliano na kuweka utaratibu wa matumizi ya huduma za mawasiliano ndani ya Serikali, Umma, Wadau wa Mawasiliano na Mashirika Binafsi.

 

Meja Jenerali Mbuge alisema, upo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa dharura.

 

“Hakikisheni kuwa mpango unazingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 na Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa 2022 ili kurahisisha utekelezaji wake,”alisisitiza Meja Jenerali Mbuge.

 

Akieleza kuhusu Mpango huo, alisema utarahisisha mawasilino ya haraka, sahihi na kwa wakati unaohitajika kwa kuzingatia mfumo huo uliojikita kidijiti na unahusisha vyombo vya habari ikiwemo matumizi ya radio, televisheni na mitandao ya kijamii.

 

Katika hatua nyingine Idara imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta. Juhudi hizi zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali.

 

“Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inajukumu la kuratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini,”alisema.

 

Idara ya maafa ilizindua nyaraka za usmamizi wa maafa nchini ikiwemo; Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 ambao umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa


Read More

Friday, February 10, 2023

WAZIRI MKUU AZINDUA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.

Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, wakati akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022).

Nyaraka nyingine ni Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

Amesema miongozo na mipango hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.

Waziri Mkuu amesema nchi bado inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.

“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.

Pia, Waziri Mkuu amezielekeza wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao. “Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.

Kwa upande wake, Muwakili Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi Veronica ameihakikishia Serikali kuwa UNDP pamoja na wadau wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na maafa.

Amesema nyaraka hizo zilizozinduliwa leo zitasaidia katika upatikanaji wa taarifa za maafa kwa wakati na hivyo kuwawezesha wahusika kuchukua hatua haraka.

 

Read More

Tuesday, February 7, 2023

WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA.

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa nchini tarehe 09 Februari, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage uliopo Hazina Jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya habari Bungeni Dodoma kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi.

Waziri Simbachawene alisema, katika kuendeleza juhudi za kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa Nchini, Serikali imefanya mapitio ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2012), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2012) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2015-2020). Hivyo, mapitio hayo yamewezesha kuandaliwa kwa nyaraka tano zitakazozinduliwa ikiwemo;Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022),Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa (2022) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027),Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

“Nyaraka zote tano zimeandaliwa kwa kushirikisha wadau ndani na nje ya Serikali. Nyaraka zinazozinduliwa zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na baadaye katika mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa,”alisema Waziri.

Alifafanua kuwa, mipango na mikakati iliyoandaliwa itaimarisha usimamizi wa maafa yanayosababishwa na majanga ya nguvu za asili kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi na majanga yanayochochewa na shughuli za kibinadamu.

Aidha, Majukumu ya utendaji yanazingatia taasisi yenye wajibu wa kisheria, ujuzi pamoja na rasilimali zinazohitajika. Mfumo uliopo umezingatia wajibu wa sekta kutambua hatari za maafa katika eneo lake, kutenga rasilimali za kisekta kabla ya tukio kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabili maafa endapo yatatokea.

Aliongezea kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha shughuli za kuratibu na kusimamia shughuli za maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na Kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na miongozo, mikakati na taratibu za kiutendaji zinazowezesha utekelezaji wa majukumu na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano wa wadau.

Read More

Friday, February 3, 2023

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU NAMMA YA KUPATA CHAKULA CHA MSAADA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema maswala ya upungufu wa chakula yanachukuliwa kama maafa kwa mujibu ya sheria ya maafa iliyopo.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati akifafanua hoja iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahaya Ally Mhata Bungeni  katika Mkutano wa Kumi Kikao cha Nne cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu za kufuata ili kupata chakula cha bei nafuu.

Alisema kuwa, Ofisi yake inajukumu ya kuratibu upatikanaji wa chakula cha msaada kwa kushirikiana na sekta tofauti tofauti ikiwemo hatua zote muhimu za uzalishaji, upatikanaji hadi matumizi kwa walaji.

Alifafanua Ofisi ya Waziri Mkuu inajukumu la kutoa kibali kwa ajili ya chakula cha bei nafuu au msaada linaratibiwa kwa kuielekeza Wizara ya Kilimo kuchukua hatua kupitia NFRA.

 “Kimsingi jukumu la kutoa chakula cha bei nafuu au msaada ni jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo inalitekeleza kwa kuelekeza Wizara ya Kilimo ili ielekeze NFRA kupeleka eneo la kukipeleka kile chakula na kwenda kukiuza kwa bei nafuu iliyopangwa,” alisisitiza waziri.

Read More

KATIBU MKUU KASPAR MMUYA ATETA NA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU

 


Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wametakiwa kutumia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali pamoja na Busara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Hayo yamesema na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bw. Kaspar Mmuya.

 

Bw. Mmuya alisema ameitumikia Ofisi hiyo na kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa lengo la kuleta matokeo chanya.

 

“Kwa majukumu ya Ofisi hii jinsi yalivyo yalitupa nafasi sisi wengine ya kujua wizara nyingine zinafanya nini katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ujumla,”alisema Katibu Mkuu huyo.

 

Pia amewahimiza  watumishi wa Ofisi hiyo kuishi kwa upendo na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu hatua itakayochochea maendeleo ya Taifa na shughuli za Serikali kufanyika katika hali ya ubora na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Sambamba na hilo, Bw. Mmuya alimshukuru Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu kwa kumfundisha, kumuongoza na kumpa ushirikiano wakati wote alipokuwa akitumikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu katika ofisi hiyo.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  Dkt. John Jingu alisema kuwa Katibu Mkuu Mmuya alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa matokeo hivyo  watumishi kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa  kufanya kazi kama timu katika kuitumikia Nchi, kuishi na watu vizuri.

 

 “Tujitahidi kila wakati kufanya kazi kwa matokeo, uliyaishi matokeo na unaendelea kutukumbusha tuyaishi hayo, kila mtu ana nafasi yake lakini lazima kuheshimiana na kujua umuhimu wa kuwajibika, tuendelee kufanya kazi kwa matokeo weledi ushirikino na nidhamu sisi ni timu moja tushirikiane.” Alisisitiza Dkt. Jingu.

 

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Katibu wa  TUGHE tawi la  Ofisi hiyo Bw. Dotto Kyaolang amemshukuru Katibu Mkuu Mmuya kwa kutoa dira ya utendaji kazi na kumtakia afya njema na utendaji mwema katika kituo chake kipya cha kazi.

 

 

Read More