Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ametoa
rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu
za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri
zaidi.
Wito huo ameutoa katika kikao
cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo
Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika
Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar
es Saalam.
Dkt. Jingu amesema dhamira ya
Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.
Aliongezea kuwa Serikali
itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo
na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.
“Mwelekeo ni kwamba shughuli
wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi
ni biashara,” alisema Dkt.Jingu.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema Uvuvi wetu bado
tunatumia mbinu za zamani lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa
zitakazofanya wavuvi waongeze tija.
Ameongeza kusema kuwa,
jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye
vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya
samaki na chakula cha samaki.
“Lengo ni kuongeza uzalishaji
wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za
uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” alisema Dkt.Madalla
Aidha Serikali itaenda kutoa
mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua
vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.
"Tunaimani zao hili
litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa
kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni
katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo
Awamu ya Pili,"alisisitiza Dkt. Madalla
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na
Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi
unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali
za kilimo na uwekezaji.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.