Tuesday, September 8, 2026

AFDP YAWA CHACHU YA MAENDELEO YA WANANCHI KIPUMBWI.

Wananchi wa Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga, wameeleza kunufaika na Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

Hayo yameelezwa na wawakilishi wa wavuvi, wachakataji na wafanyabiasha wa mazao ya uvuvi kutoka Kata ya Kipumbwi wakati wa ziara kutathmini utekelezaji wa Programu hiyo katika mapitio ya utekelezaji wa kipindi cha kati (MTR) inayofanywa na Timu ya IFAD.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu wa Umoja wa Wachakata Dagaa Kipumbwi (UWADAKI), Bw. Abdallah Mohamed, amesema AFDP imelenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza kipato, kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi, kuimarisha lishe na masuala ya jinsia.

Amesema kupitia Programu hiyo, makundi mbalimbali yamenufaika, yakiwemo Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Vyama vya Wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo wa mazao ya uvuvi.

Ameongeza kuwa, Programu hiyo imewezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayolenga kuboresha shughuli za uvuvi na biashara ya mazao ya uvuvi, ikiwemo ujenzi wa soko la samaki la kimataifa, vichanja vya kukaushia dagaa, mtambo wa kuzalisha barafu na chumba cha ubaridi.

Miundombinu hiyo inatarajiwa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuongeza upatikanaji wa masoko, kuongeza usalama wa chakula na lishe na fursa za ajira.

Aidha, Bw. Mohamed amesema AFDP imewamepatiwa mafunzo mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya elimu ya fedha na ujasiriamali yaliyolenga kuwezesha wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo wa mazao ya uvuvi kuanzisha na kuendesha biashara zenye mafanikio, usimamizi bora wa fedha hususan mapato na matumizi. 

Mafunzo ya lishe yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto na makundi mbalimbali kulingana na umri, pamoja na uhusiano uliopo kati ya lishe bora, afya na uwezo wa kufanya kazi. 

Pia, mafunzo ya jinsia yamelenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi, maamuzi ya familia na vikundi, pamoja na kuwezesha usawa wa fursa katika uzalishaji, biashara na matumizi ya mapato.

Vilevile, AFDP inalenga kuchochea uvuvi endelevu unaozingatia mabadiliko ya tabia ya nchi na kuongeza upatikanaji wa samaki, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato kwa wananchi katika ngazi ya jamii na Wilaya ya Pangani kwa ujumla. 

 Katika ziara hiyo, wataalamu waliendelea kuhamasisha ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii kwa usawa, kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa mazao ya uvuvi na kuweka mifumo na mipango madhubuti itakayosaidia katika uendeshaji endelevu wa soko hilo la kimataifa la samaki, ili liweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kipumbwi, Pangani na Taifa kwa ujumla.

 

Read More

Sunday, September 6, 2026

RAIS DKT. SAMIA KUZINDUA MIRADI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA, DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua majengo ya Ofisi za Wizara, Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba,Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika jumanne Septemba  nane mwaka huu  katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma leo  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe.Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo.

Alisema uzinduzi huo utahusisha maeneo matatu makuu ambayo ni majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.

Profesa Kabudi alisema kukamilika kwa majengo hayo, kutawezesha watumishi 18,510 kutumia ofisi za Mji wa Serikali, Mtumba.

“Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya Ofisi za muda.ujenzi wa majengo hayo ulianza Novemba 28 mwaka  2018 na kukamilika Machi 22 mwaka 2019, hatua iliyowezesha baadhi ya watumishi wa Wizara na taasisi kuanza kuhamia.

Aliongeza kuwa :” Awamu ya pili ya ujenzi ilianza Oktoba, 2021, ikiwa inalenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya watumishi wote wa Wizara na Taasisi zilizopangwa kuhamia Mtumba.Pia ilihusisha ujenzi wa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo barabara za lami.

Profesa Kabudi alisema mbali na barabara hizo, miundombinu ya kudumu ya mawasiliano pamoja na Uwanja wa Mashujaa imekamilika na itakuwa sehemu ya miundombinu itakayotumika katika shughuli za Serikali.

Hata hivyo, alisema baadhi ya miradi bado iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42.

“Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na uondoshaji wa maji taka, TEHAMA, ufungaji wa mifumo ya usalama ya CCTV Camera, ujenzi wa kituo cha zimamoto pamoja na utekelezaji wa mpango wa upandaji miti na ustawishaji wa Mji wa Serikali nazo zinafanyika, "alisema.

Alisema Rais Dkt.Samia ameendelea kuweka msisitizo katika kuboresha mazingira hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani za Wizara na taasisi 26 zinazohamia katika majengo hayo.

Profesa Kabudi alisema hatua hizo zinaendelea kuifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa alama muhimu za utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.

Alisema uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

Read More

Wednesday, September 2, 2026

SERIKALI YATOA MAELEKEZO 13 KUKABILIANA NA EL-NINO

 


SERIKALI imetoa maelekezo 13 kwa umma, kamati za usimamizi wa maafa, Wizara, Taasisi, Mikoa, Halmashauri na sekta mbalimbali nchini, kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.

Imeelekeza maeneo yote hatarishi yatambuliwe mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike na hatua stahiki zichukuliwe, ikiwemo kuwahamasisha wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama.

Maelekezo hayo yametolewa hii leo  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino.

Profesa Kabudi amesema Serikali imeelekeza kuhakikisha mvua hizo zinatumika kikamilifu kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi.

Aidha, amesisitiza wananchi wanapaswa kuelimishwa na kuhimizwa kuchukua hatua za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama, kuweka akiba ya chakula, kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu bora kwa msimu wa Vuli.

“Kuandaa rasilimali kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa yatakayotokea na kushirikisha wadau wote wa maafa, wakiwemo wananchi, taasisi na sekta binafsi katika maeneo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Serikali imeagiza kuandaliwa na kutekelezwa kwa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea.”

Profesa Kabudi amesema Wizara, Taasisi, Mikoa na wadau wengine wanaohusika na miundombinu wanapaswa kufanya ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha inaimarishwa na kusafishwa, ikiwemo madaraja, makaravati na mitaro.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea, zikiwemo huduma za usafirishaji, maji na umeme.

Serikali pia imeagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka ngumu, usafishaji na uimarishaji wa njia za maji, kingo za mito na mabwawa.

Aidha, imeelekeza kuhakikisha vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vinapatikana na kuwa katika hali ya utayari wakati wote.

Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza kubainisha na kutenga maeneo salama yatakayotumika kwa ajili ya makazi ya dharura pindi maafa yatakapotokea.

Kwa upande wa sekta ya utalii, Serikali imeagiza kufanyika kwa ukaguzi na ukarabati wa miundombinu iliyopo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Jamii ili kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea wakati wote.

“Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote zimeagizwa kufuatilia na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El-Nino zichukuliwe kwa wakati.”

KUHUSU BILIONI 730

Akizungumzia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu makadirio ya matumizi ya Sh. bilioni 730 katika kujiandaa na kukabiliana na El-Niño, Profesa Kabudi amesema taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi wa kina kuhusu shughuli zilizoainishwa katika mpango huo.

Amesema Sh. bilioni 730 ni makadirio ya fedha zinazohitajika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño kabla, wakati na baada ya El-Nino kutokea.

“Kwa mujibu wa Mpango, makadirio ya fedha zinazohitajika kutumika katika kutekeleza Mpango huo ni Sh. bilioni 730,” amesema.

Hata hivyo, amesema fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo katika sekta zote ni Sh. bilioni 10

Read More