Saturday, October 30, 2021

Mkutano wa Tano wa Mawaziri EAC wanaoshughulikia sekta ya Kazi na Ajira wafanyika Jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi akizungumza wakati wa Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wanaohusika na sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Oktoba 29, 2021.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobasi Katambi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wanaohusika na sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wa Sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika Oktoba 30, 2021 jijini Dar es Salaam huku Mawaziri wakikubaliana kuendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na mikutano ya Wataalamu na Makatibu Wakuu ili lenga kupitia na kujadili utekelezaji wa miradi na programu katika sekta ya kazi na ajira pamoja na utekelezaji wa maagizo na maamuzi mbalimbali ya jukwaa hilo la Mawaziri linalohusika na kazi na ajira.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni muendelezo wa usimamizi wa sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yam waka 1999 katika utengamano wa jumuiya hiyo.

“Utekelezaji wa maagizo, mapendekezo na maamuzi mbalimbali yaliyotolewa yatasaidia kuboresha maeneo mbalimbali katika sekta hii ili kuleta mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ustawi ya jamii kwa nchi wanachama,” alisema Katambi

Aidha, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa katika vikao vilivyotangua vya Makatibu Wakuu na Wataalam kwa majadiliano mazuri ya utekelezaji wa mapendekezo, maagizo na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na kuamuliwa katika mikutano ya ngazi mbalimbali na vyombo vya kisera vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sambamba na hayo Naibu Waziri Katambi alitumia fursa hiyo kuelezea namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyojizatiti katika kukuza sekta ya kazi na ajira kupitia miradi na programu mbalimbali zinazoanzishwa nchini.

Kikao hicho kimejadili na kukubaliana masuala yafuatayo ikiwemo Kuimarisha sera ya kuratibu masuala ya uhamaji nguvukazi ambayo itatoa fursa kwa vijana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujiajiri na kuajiriwa; Kuimarisha program ya kubadilishana wafanyakazi vijana ndani ya nchi wanachama; Kuimarisha na kuainisha Sheria za kazi ndani ya Jumuiya ili kulinda haki za wafanyakazi wageni ndani ya jumuiya hiyo na Kukamilisha mchakato wa kuratibu masuala ya uhamishaji wa mafao ya hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wanaohamia au kurudi nchini mwao.

Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi na wawakilishi kutoka nchi zote wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia Wataalamu na Wadau wa Utatu wa sekta ya kazi na ajira walishiriki, ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa Mawaziri uliongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrik Soranga, Katibu Mkuu kutoka ofisi hiyo Tixon Nzunda pamoja na Wakuu wa Idara zinazojishughulisha na sekta hiyo.

Read More

Thursday, October 28, 2021

Waziri Mhagama ahimiza matumizi ya Dawa kwa wanaoishi na VVU



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiangalia mikeka iliyotengenezwa na umoja wa wanakikundi cha Faraja kinachojumuisha WAVIU kutoka kwenye Konga mbalimbali Wilaya ya Mbeya, anayetoa maelezo ni Bi. Adella Charles.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amekea vitendo vya baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini kukwepa na kusitisha matumizi ya dawa za kupunguza makali ya ugongwa huo huku wakipatwa na madhara zaidi.

Ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua shughuli za watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kutoka katika Konga Jiji Mbeya, kukagua ujenzi wa Kituo cha Tiba na Matunzo (CTC) Chimala pamoja na ujenzi wa Kituo cha Tiba na Matunzo cha Zahanati ya Igawa Mbarali oktoba 27, 2021 Jijini Mbeya.

Waziri alieleza kuwa, kumekuwa na kesi za watu kutoroka na kusitisha matumizi ya dawa hizo huku akieleza kuwa ni changamoto inayokwamisha mapambana dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.

“Wanaoishi na VVU wote acheni kutoroka dawa bali endeleeni kutumia dawa hizo ili kuendelea kufubaza makali na kuwa afya njema,”alisema waziri Mhagama

Alisema ni wakati sasa jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa dawa hizo kwani zimeendelea kusaidia watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI huku wakiimarika na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila kuathiriwa na jambo lolote.

Aidha aliwakumbusha kuendelea kulindana wao kwa wao na kukumbushana matumizi sahihi ya dawa za kufubaza na kupunguza makali ya ugonjwa huo huku akiwasii kuendelea kujiandikisha na BIMA ya Afya ili kusaidia kupata huduma za afya.

“Hakikisheni kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake kwa kusisitiza matumizi sahihi ya dawa bila kukwepa na endeleeni kuhakikisha kila anayeishi na VVU anakuwa na Bima ya afya kwani itarahisisha kupata huduma za afya, mkakati huu ni mzuri napongeza sana,”alisema

Aidha alitumia fursa hivyo kuendelea kuwasihi wanaume kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwani imeonekana ni kundi ambalo lipo nyuma katika kujitokeza kujua hali zao.

Aidha aliagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kuendelea kuunga mkono mapambano hayo huku akimtaka kutoa kipaumbele kwa WAVIU katika utoaji wa mikopo isiyo na riba ili kuwakwamua na changamoto za mitaji.

“Halmashauri endeleni kuchangia jitihada za watu wanaoishi na VVU na hakikisheni mnakuwa na kanzi data itayosaidia kuwafahamu na kuwafikia kwa wakati hii itasaidia katika shughuli za kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao,”alieleza waziri.

Akitoa taarifa ya hali ya masuala ya UKIMWI, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Mbeya, Bw. Douglas Kisunga alisema Halmashauri ina jumla ya konga kata 32 na vikundi wezeshi 54 vya shughuli za mwitikio wa masuala ya UKIMWI na kuhamasisha upimaji na kuwaunganisha WAVIU kutambuana na kusaidiana katika kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao.

Aliishukuru Serikali kuendelea kuwatambua na kuwaunga mkono katika shughuli zao za kila siku huku akieleza mafanikio ya konga hiyo, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji wamefanikiwa kuwa na umoja wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, na kupata huduma za tiba na matunzo na kuhamasisha watu kujitokeza zaidi.

“Mwanzo WAVIU waliojitokeza kwa uchache ambapo walikuwa 53 tu, hadi sasa wamejitokeza na kufikia 1129 na wapo huru, wanaishi kwa raha na wanafuata maelekezo ya Serikali huku wakifurahia maisha,”alisema Kisunga

Aidha alieleza kwa kipindi cha Juni hadi Julai konga imefanikiwa kurudisha watoro wa dawa 132 ambapo wanaume ni 58 na wanawake 74 na kuhakikisha wanabaki katika huduma za tiba na matunzo.

Alifafanua kuwa, Konga zimefanikiwa kuwa mstari wa mbela katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kuendelea kuhamasisha upimaji wa hiari na matumizi ya dawa kwa kujilinda na kulinda wengine na kumekuwa na uwazi wa watu kujitokeza kueleza hali zao.

“Katika kujitokeza kupima na kujua hali wanaume wamekuwa na mwitikio mdogo ambapo kwetu waliojitokeza ni 622 wanaume na wanawake 1407 hivyo kundi la wanaume bado lipo chini tuendelee kuwahamasisha kujitokeza kujua hali zao ili wakikutwa na maambukizi wajiunge katika huduma za tiba na matunzo,”alisema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Leonard Maboko alitoa rai kwa kila mtanzania kutambua kuwa ugonjwa huu upo, watu wajitokeze kupima na kujua hali zao ili kuendeleza mapambano hayo na kupunguza hali ya maambukizi mapya nchini.
Read More

Saturday, October 23, 2021

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria yatembelea Kiwanda cha Kuchakata Bidhaa za Ngozi KILCL







Na: Mwandishi Wetu - Kilimanjaro

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imewataka wawekezaji na wafanyakazi wa kiwanda cha kimataifa cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro Leather International Co. Ltd (KLICL) kufanya kazi kwa juhudi, weledi na maarifa ili makusudio ya kuanzishwa kwake yafikiwe na kuleta manufaa kwa watanzania.

Hayo yalisemwa Oktoba 23, 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Giga wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo aliwataka watumishi wa kiwanda hicho kuwa wabunifu na waaminifu katika kulinda miundombinu ya kiwanda ili kiendelee kuzalisha bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya watanzania wote na kukabili soko la ushindani ndani nan je ya nchi.

“Kamati itaendelea kusimamia na kushauri uongozi wa kiwanda ili kiwe endelevu na kilete tija nchini na ni jambo la faraja kuwa na kiwanda kama hiki kwa sababu mpango wa Serikali umejidhatiti katika kufufua viwanda ili tuwe na bidhaa zetu za ndani na zitakazokuwa na ubora wa kuuzika katika soko la nje,” alisema Mhe. Gigga

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.  Patrobas Katambi alishukuru kamati hiyo kwa kutembelea kiwanda hicho na kusema hoja zote zilizotolewa na wajumbe zimepokelewa na zitafanyiwa kazi vyema huku akisisitiza kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha inawajengea uwezo vijana kupitia fursa mbalimbali za miradi mikubwa iliyopo nchini.

“Kiwanda hiki kimefanikiwa kukuza ujuzi kwa vijana na mmeshuhudia pale kwenye mashine asilimia 80 ya wafanyakazi ni vijana na wanajifunza kutengeneza soli za viatu, mikanda, mikoba ya kina mama na bidhaa nyingine za ngozi,” alieleza

Hata hivyo aliwasisitiza watazania kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje akisema bidhaa zinazotengenezwa nchini zina viwango vyenye ubora huku akihimiza vijana kutumia fursa za uanzishwaji wa viwanda kupata ajira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba alisema hadi kukamilika mradi huo utagharimu zaidi ya Bilioni 126.19.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda, Mhandisi Masud Omari alisema kiwanda kimeanza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za ngozi imara na zenye ubora.

“Tumeanza uzalishaji, hivyo tunatoa wito kwa watanzania wote kuvaa viatu vya kiwanda chetu, kwani ni bora na imara na vinapatikana kwa bei nafuu” alisisitiza Mhandisi Omari.

Katika hatua nyingine wajumbe wa kamati wamepongeza mipango ya kiwanda hicho na kushauri kilenge kuwa na viwango vya kimataifa na kutoa ajira kwa watanzania wengi ikiwemo vijana na wanawake na kushauri elimu zaidi itolewe kuhusu bidhaa za kiwanda hicho na maduka yasambae nchi nzima.

Aidha Mbuge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Tarimo alisema wakazi wa Moshi wapo tayari kulinda kiwanda akisisitiza kuzingatiwa kwa sheria ya udhibiti wa uinizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kuepuka bidhaa feki.

MWISHO


Read More

Waziri Mhagama Apongeza Kampuni ya JATU PLC Kukomboa Vijana Nchini


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akizindua rasmi mradi wa Ufugaji, Bima na Bank ya kampuni ya JATU PLC. Wa tatu kutoka kushoto ni Mhe. Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Miaka Mitano (5) ya Kampuni ya JATU PLC iliyofanyika katika hoteli ya Morena, Jijini Dodoma.



Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya JATU PLC, Dkt. Zaipuna Yonah ikiashiria mchango wake mkubwa katika malenzi ya vijana wakati wa hafla ya maadhimisho ya Miaka Mitano (5) ya Kampuni ya JATU PLC iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage hoteli ya Morena tarehe 23 Oktoba, 2021, Jijini Dodoma.



Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa wanachama katika kampuni ya JATU PLC na namna inavyowakomboa vijana kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Pongezi hizo zilitolewa jana Oktoba 23, 2021 na Waziri Mhagama wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 5 ya kampuni hiyo toka ianzishwe mwaka 2016.

Alieleza kuwa, Kampuni ya JATU PLC imekuwa kiuongo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia miundombinu thabiti iliyojiwekea ambayo imejikita katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko hivyo zimekuwa ni msaada mkubwa kwa wanachama kuondokana na umaskini.

“JATU PLC ni kampuni iliyoanzishwa na vijana, nafurahi kuona mmeweza kushiriki katika juhudi hizi za Serikali kwa kuhakikisha mnazalisha malighafi na kuongeza thamani ya Mazao mnayozalisha kupitia Viwanda kwa lengo la kuwa na mnyororo wa kuongeza thamani na kulinda ajira za vijana wetu ili kupitia mnyororo huo wa thamani muweze kutoa ajira nyingi na kujipatia kipato,” alisema  

“Nipongeze kampuni ya JATU PLC kwa namna imekuwa ikiwasaidia vijana kuondokana na changamoto mbzlimbali zinazowakabili kwa kuwashirikisha katika kilimo, ufugaji na miradi mbalimbali inayoratibiwa na kampuni hiyo maana imewawezesha vijana kuleta mageuzi ya maendeleo katika Taifa lao,” alieleza Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa utafiti wa nguvukazi uliofanyika 2014 ulibainisha asilimia 56 ni vijana hivyo kupitia fursa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni ya JATU PLC ni vyema ikatumika kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwashiriki katika miradi ambayo itawaletea matokea yenye tija.

“Serikali itaendela kuhakikisha kuwa inawawekea vijana mazingira mazuri kupitia program zake mbalimbali ambazo zitawawezesha kupata elimu, ujuzi na mitaji ambayo itawasaidia kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema Mhagama

“Serikali pia itaendelea kuwasadia vijana wa JATU ili kuhakikisha wanafikia malengo yao,”

Alifafanua kuwa, Malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Vijana yameainishwa katika nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2020 -2025, Dira ya maendeleo ya Taifa (vision 2025), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030; Agenda ya Umoja wa Nchi za Afrika 2063; Sera ya Maendeleo ya Viwanda; Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana wote nchini wahitimu wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, Sekondari na hata msingi kujiunga katika vikundi na kusajili Kampuni au vikundi vyao ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na waweze kutimiza ndoto zao.

“Vijana mnapaswa kuiga kazi nzuri zinazofanywa na vijana wenzenu waliopo JATU PLC. Ili kuliwezesha taifa letu kufikia azma yake ya kufikia uchumi wa kati wa juu,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo Waziri Mhagama ameutaka Uongozi wa kampuni ya JATU PLC kuendelea kuwa mfano mzuri kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu kwa kuwaelimisha kuwa mali na ajira vipo shambani. Pia ametaka Mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao wanaomaliza vyuo kujifunza kilimo bishara kinavyoendeshwa na faida zake kwani vijana wengi hawatambui kuwa unaweza kufanya kilimo cha kidijitali. Kuwepo na nidhamu ya kazi ili kuwa na mafaniko yenye tija kwa kampuni.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama aliwapongeza wakezaji katika kampuni hiyo na aliwasihi kuendelea kuongeza mtaji na kupanua wigo wa biashara zao.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda alisema kuwa kutokana na ukubwa wa kampuni ya JATU PLC ni mafanikio iliyonayo vi vyema vijana wakachangamikia fursa hiyo ili wajikwamue kiuchumi.

“Katika hafla hii tumejifunza mengi kwa kuona kampuni ya JATU PLC inavyotekeleza mikakati yake kwa ufasaha hivyo Vijana mkawekeze JATU,” alisema

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Mwanahamisi Munkunda alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama kwa namna ofisi yake imekuwa mlezi mzuri kwa kampuni hiyo ya JATU PLC ambayo imepelekea mafanikio hayo yaliyofikiwa katika miaka mitano.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya JATU PLC, Bw. Peter Gasaya alisema kuwa falsafa ya kampuni hiyo imejikita katika uchumi shirikishi ambao unatoa fursa kwa wanachama kuishi bila kuwa na changamoto ya kipato kupitia fursa zinazowazunguka katika kujiendeleza kiuchumi.

“Katika miaka mitano JATU PLC inajivunia mafanikio iliyoyapata ambayo yamewezesha kampuni kufungua rasmi mradi wa Ufugaji, Bima na Bank ambayo itatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na usalama,” alisema Gasaya

 

MWISHO


Read More

Naibu Waziri Ummy awataka Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa Mikopo inayotolewa na Halmashauri




Na: Mwandishi Wetu - Same

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka wenye Ulemavu nchini kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 2 inayotolewa na Halmashauri kujiinua kiuchumi. 

Naibu Waziri Ummy alitoa kauli hiyo Oktoba 22, 2021 alipotembelea wilaya ya Same, Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro na kuzungumza na watu wenye ulemavu ambapo alisema kuwa, Serikali kupitia uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwajali watu wenye ulemavu kwa kupunguza masharti ya ukopaji wa mikopo hiyo ambapo awali ilikuwa ikitolewa kwa kikundi lakini kwa sasa anakopeshwa hata mmoja.

“Katika fedha ambazo serikali imetenga kwa kila halmashauri nchini asilimia mbili ya mapato ya ndani imetegwa kwa ajili ya kuwakopesha Watu wenye Ulemavu, hivyo tunawajibu wa kuchangamkia fedha hizo na kuzitumikia katika kukuza uchumi wetu” alisema Naibu Waziri Ummy.

Alisema kuwa, zipo baadhi ya halmashauri nchini Watu wenye Ulemavu wamekuwa na muamko kidogo katika kuchangamikia fursa hiyo ikiwemo wilaya ya Mwanga na kutoa wito kwa maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo kuendelea kuhamasisha ili wajitokeze kwa wingi. Aliongeza kuwa, Watu wenye Ulemavu wamekuwa wakichukua mikopo ya halmashauri na kurejesha kwa wakati.  

Sambamba na hayo Naibu Waziri Ummy alisema kuwa, Watu wenye Ulemavu wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi ambapo alikipongeza kikundi cha watu wenye ulemavu cha Thunga group kwa jinsi walivyotumia mkopo walioupata halmashauri kuanzisha duka la rejareja na wakala wa kutoa hela kwenye simu.

“Watu wenye Ulemavu hatupaswi kukata tamaa pindi tunapozarauli na wala tusibweteke wala kuvunjika moyo kwani viongozi wapo mstari wa mbele kututetea na kutuunga mkono” alisema Naibu Waziri Ummy.

Naibu Waziri Ummy alisema kuwa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 ya wanafunzi wenye Ulemavu ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro umepata mabweni mawili yatakayojengwa wilaya ya Mwanga na Moshi.

“Watu wenye ulemavu tunamshukuru sana Rais Samia kwa jinsi ambavyo anatujali na mara nyingi ameonyesha kutufariji na kutufanya na sisi tujione ni sehemu muhimu kwake na katika serikali” alisema.

Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuziomba halmashauri zilizopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kuhakikisha wanazingatia mahitaji ya walemavu katika ujenzi wake pamoja na kusimamia fedha hizo ili thamani ya majengo iendane na thamani ya fedha.

Akisoma taarifa ya mikopo ya Watu wenye Ulemavu katika wilaya ya Same, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Anastazia Tutuba alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 halmashauri hiyo ilitoa mikopo jumla ya Tsh milioni 229 katika vikundi vya Vijina, Wanawake na Wenye Ulemavu. Aidha Mkurugenzi huo alieleza kuwa, jumla ya vikundi 10 vya Watu wenye Ulemavu vilipewa mikopo yenye thamani ya milioni 35.8.  

Kw upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya Mwanga, Salehe Mkwizu alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu ili kuwasaidia kuwajengea uwezo wa kukuza vipaji walivyonavyo.

Read More

Friday, October 22, 2021

Matukio katika Picha Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahala Pa Kazi

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Vijana, Kazi na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akifafanua jambo katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama mahala pa kazi katika UKumbi wa Bunge, Jijini Dodoma, Oktoba 21, 2021.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia mada mbalimbali zil;izokuwa zikiwasilishwa katika kikao cha kamati hiyo na Wataalam kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika UKumbi wa Bunge, Jijini Dodoma, Oktoba 21, 2021.


Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Emmanuel Mwakasaka (Mb.) (kushoto) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge akieleza jambo wakati wa kikao hicho walipokutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama mahala pa kazi katika UKumbi wa Bunge, Jijini Dodoma, Oktoba 21, 2021.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo katika kikao hicho. Katikati ni Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana, Kazi na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi  na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa sheria ya afya na usalama mahali pa kazi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Jijini Dodoma, Oktoba 21, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana, Kazi na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi.


Read More

Thursday, October 21, 2021

Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Namba 7 ya Mwaka 2015 Bungeni Dodoma

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi akitoa ufafanuzi juu ya hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa maafa Namba 7 ya mwaka 2015 Bungeni Dodoma tarehe 20 Oktoba, 2021.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Nagma Giga akiongoza kikao cha kamati hiyo walipokutana kwa lengo la kujadili masuala ya Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa maafa Namba 7 ya mwaka 2015 Bungeni Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kaspar Mmuya akijibu hoja za wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokutana kujadili masuala kuhusu Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa maafa Namba 7 ya mwaka 2015 Doodma.


Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Charles Msangi akiwasilisha taarifa kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kilichofanyika Bungeni Dodoma.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi akinukuu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kilichofanyika hii leo.

Read More

Wednesday, October 20, 2021

Majaliwa: Rais Samia anafikisha Maendeleo kwa Watanzania Wote


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kwenye Baraza la Maulidi lililfanyika katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. Oktoba 19, 2021. 


Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia kwenye Baraza la Maulidi Kitaifa, lililofanyika Kitaifa katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania wakati alipowasili katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba mkoani Kageta, wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye Baraza la Maulid Kitaifa. 

Na: Mwandishi Wetu: KAGERA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeonesha kwa vitendo kuongoza Taifa  na kufikisha maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali tofauti za kidini na ukabila.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kusimamia mshikamano, haki na umoja wa Taifa, hivyo amewasihi Watanzania wote waendelee kumuombea  Rais Samia  ili aendelee kuiongoza vyema nchi yetu.

Ameyasema hayo leo Jumanne (Oktoba 19, 2021) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia katika Baraza la Maulid lililofanyika Kitaifa katika uwanja vya Kaitaba mjini Bukoba Mkoani Kagera.

Waziri Mkuu amewataka waumini wa dini ya Kiislam nchini watumie maadhimisho hayo kama fursa muhimu kwao kuyasoma na kuyatafsiri kivitendo maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) katika mfumo wao wa maisha ya kila siku.

“ Tafakuri hiyo ituwezeshe kuishi maisha ya undugu, kupendana, kuheshimiana na kushikamana miongoni mwetu  Waislam pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.”

Akizungumzia suala la amani na utulivu Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amani ni tunu adhimu ambayo Mwenyezi Mungu ametukirimia kwani kuishi kwa amani ni kumfanya ibada Mwenyezi Mungu.

“Kudumisha amani iwe ni wajibu wa kila mmoja wetu kwani amani ndiyo kila kitu. Bila amani hatuwezi kupata maendeleo, hatuwezi kufanya ibada, watoto wetu hawawezi kwenda shule na mambo mengine mengi”.

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa kinara katika kuenzi na kudumisha amani, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuendelea kuitunza amani hiyo kwa kuwafundisha vijana na watoto misingi ya amani ili nao waidumishe.

“Serikali inatambua umuhimu wa madhehebu ya dini katika kudumisha amani. Viongozi wa dini mmekuwa mabalozi wema na kudumisha amani yetu kwa miongo kadhaa. Jitihada zenu zote zimewezesha nchi yetu kupata utulivu kila wakati na aghalabu kuwa kimbilio la majirani pindi wanapopata machafuko.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa  ametumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao  kufanya maandalizi kwa ajili ya kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyika Agosti mwakani.

 “Zoezi hili litaiwezesha nchi kupata takwimu za msingi zinazotumika katika kutunga sera, kupanga mipango na programu za maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kuchanja chanjo ya kujikinga na UVIKO 19. “Suala la afya ni muhimu na si la kufanyia maskhara.Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia ameshazindua kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO 19. Tumuunge mkono.”

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally amewasihi wananchi waendelee kuwaheshimu na kuwatii viongozi wao wa dini na Serikali  kwa sababu hiyo ndiyo tabia njema ambayo inachangia Taifa kuwa na maendeleo.

Naye, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Sheikh Nuhu Jabir ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia kwa namna inavyowahudumia wananchi kwa kutoa takribani trilioni moja kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Read More

Tuesday, October 19, 2021

Waziri Mhagama: Rais Samia atenga zaidi ya Tsh. Bilioni 600 Ujenzi Awamu ya Pili Majengo ya Serikali Mtumba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama  akichapia tofali kuashiria kuanza rasmi kwa ujenzi wa Majengo ya Ofisi yake katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma Tarehe 18 Oktoba, 2021.Kulia kwake ni Naibu Waziri wake (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi na kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Tixon Nzunda.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma Tarehe 18 Oktoba, 2021 wakati wa kikao cha uzinduzi huo kilicho jumuisha timu ya menejimenti ya ofisi yake, wakandarasi wa ujenzi na washauri elekezi.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda akifafanua jambo wakati wa kikao hicho.


Na: Mwandishi Wetu - DODOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametenga zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali awamu ya pili ili majengo hayo yaanze kutumika kwa haraka.

Ameyasema hayo hii leo Oktoba 18, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa majengo mapya ya Ofisi ya Waziri Mkuu awamu ya pili katika  Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alisema kuwa, toka Serikali ilipotangaza azma ya kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya nchi, mwezi Septemba, 2016, hadi kufikia Juni, 2021 jumla ya Watumishi 18,300 wamekwisha hamia Jijini Dodoma na katika kipindi hicho shilingi bilioni 655, 886, 878, 308.83 zilitumika kuhamisha watumishi  pamoja na kuwezesha ujenzi wa majengo ya Ofisi za Awali za awamu ya kwanza na miundombinu muhimu katika Wizara 23.

“Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza nia na maamuzi ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kwa vitendo pamoja na kuridhia mpango mkakati wa ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali awamu ya pili,” alisema Waziri Mhagam 

Alifafanua kuwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia jumla ya shilingi bilioni 600, 884, 941, 784.70 katika kuhakikisha awamu ya pili ya ujenzi wa mji wa Serikali yanakamilika.

“Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 300 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo ya serikali,” alisema

 Aliongeza kuwa, ujenzi wa majengo katika mji wa Serikali awamu ya pili yatakuwa na muundo wa ghorofa na kila jengo litakuwa na ghorofa 6 kwenda juu na hapatakuwa na  jengo lenye idadi ndogo ya ghorofa hizo.

“Kipekee Ofisi ya Waziri Mkuu tunampongeza Mhe. Rais kwa kupata fursa ya kujenga majengo mawili kupitia ujenzi huu wa majengo haya ya Serikali katika awamu hii ya pili,” alisema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa Wizara zote kukamilisha kwa haraka utaratibu wa kupata wakandarasi kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mikataba yote ya ujenzi ihakikishwe inazingatia thamani ya fedha na viwango katika ujenzi unaotarajiwa kuanza, Taasisi zinazohusika na huduma na miundombinu zihusishwe katika ujenzi na utekelezaji wa Mradi  Taasisi ikiwemo, DUWASA, TANESCO, TTCL, Zimamoto, NEMC, OSHA, TFS na GSO na pia amezitaka kamati za ndani za ufuatiliaji na usimamizi kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi na changamoto zinazojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi.

Aidha, Waziri alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wa jiji la Dodoma kuchangamikia fursa mbalimbali wakati wa ujenzi wa majengo hayo ya Serikali katika awamu hii ya pili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Tixon Nzunda aliahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Waziri huku akimuhakikishia kusimamia mradi huo kwa viwango vinavyo hitajika na kukabidhi mradi huo kwa wakati.

“Tumesha saini mkataba na kumaliza taratibu za manunuzi na kukabidhi rasmi kazi za ujenzi kuanza na hadi sasa kazi za awali zinaendelea ikiwemo kusafisha eneo la mradi. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 16 badala ya miezi 24 kama ilivyokuwa awali,” alisema Nzunda

Read More