Saturday, October 23, 2021

Waziri Mhagama Apongeza Kampuni ya JATU PLC Kukomboa Vijana Nchini


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akizindua rasmi mradi wa Ufugaji, Bima na Bank ya kampuni ya JATU PLC. Wa tatu kutoka kushoto ni Mhe. Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Miaka Mitano (5) ya Kampuni ya JATU PLC iliyofanyika katika hoteli ya Morena, Jijini Dodoma.Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya JATU PLC, Dkt. Zaipuna Yonah ikiashiria mchango wake mkubwa katika malenzi ya vijana wakati wa hafla ya maadhimisho ya Miaka Mitano (5) ya Kampuni ya JATU PLC iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage hoteli ya Morena tarehe 23 Oktoba, 2021, Jijini Dodoma.Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa wanachama katika kampuni ya JATU PLC na namna inavyowakomboa vijana kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Pongezi hizo zilitolewa jana Oktoba 23, 2021 na Waziri Mhagama wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 5 ya kampuni hiyo toka ianzishwe mwaka 2016.

Alieleza kuwa, Kampuni ya JATU PLC imekuwa kiuongo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia miundombinu thabiti iliyojiwekea ambayo imejikita katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko hivyo zimekuwa ni msaada mkubwa kwa wanachama kuondokana na umaskini.

“JATU PLC ni kampuni iliyoanzishwa na vijana, nafurahi kuona mmeweza kushiriki katika juhudi hizi za Serikali kwa kuhakikisha mnazalisha malighafi na kuongeza thamani ya Mazao mnayozalisha kupitia Viwanda kwa lengo la kuwa na mnyororo wa kuongeza thamani na kulinda ajira za vijana wetu ili kupitia mnyororo huo wa thamani muweze kutoa ajira nyingi na kujipatia kipato,” alisema  

“Nipongeze kampuni ya JATU PLC kwa namna imekuwa ikiwasaidia vijana kuondokana na changamoto mbzlimbali zinazowakabili kwa kuwashirikisha katika kilimo, ufugaji na miradi mbalimbali inayoratibiwa na kampuni hiyo maana imewawezesha vijana kuleta mageuzi ya maendeleo katika Taifa lao,” alieleza Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa utafiti wa nguvukazi uliofanyika 2014 ulibainisha asilimia 56 ni vijana hivyo kupitia fursa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni ya JATU PLC ni vyema ikatumika kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwashiriki katika miradi ambayo itawaletea matokea yenye tija.

“Serikali itaendela kuhakikisha kuwa inawawekea vijana mazingira mazuri kupitia program zake mbalimbali ambazo zitawawezesha kupata elimu, ujuzi na mitaji ambayo itawasaidia kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema Mhagama

“Serikali pia itaendelea kuwasadia vijana wa JATU ili kuhakikisha wanafikia malengo yao,”

Alifafanua kuwa, Malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Vijana yameainishwa katika nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2020 -2025, Dira ya maendeleo ya Taifa (vision 2025), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030; Agenda ya Umoja wa Nchi za Afrika 2063; Sera ya Maendeleo ya Viwanda; Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana wote nchini wahitimu wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, Sekondari na hata msingi kujiunga katika vikundi na kusajili Kampuni au vikundi vyao ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na waweze kutimiza ndoto zao.

“Vijana mnapaswa kuiga kazi nzuri zinazofanywa na vijana wenzenu waliopo JATU PLC. Ili kuliwezesha taifa letu kufikia azma yake ya kufikia uchumi wa kati wa juu,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo Waziri Mhagama ameutaka Uongozi wa kampuni ya JATU PLC kuendelea kuwa mfano mzuri kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu kwa kuwaelimisha kuwa mali na ajira vipo shambani. Pia ametaka Mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao wanaomaliza vyuo kujifunza kilimo bishara kinavyoendeshwa na faida zake kwani vijana wengi hawatambui kuwa unaweza kufanya kilimo cha kidijitali. Kuwepo na nidhamu ya kazi ili kuwa na mafaniko yenye tija kwa kampuni.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama aliwapongeza wakezaji katika kampuni hiyo na aliwasihi kuendelea kuongeza mtaji na kupanua wigo wa biashara zao.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda alisema kuwa kutokana na ukubwa wa kampuni ya JATU PLC ni mafanikio iliyonayo vi vyema vijana wakachangamikia fursa hiyo ili wajikwamue kiuchumi.

“Katika hafla hii tumejifunza mengi kwa kuona kampuni ya JATU PLC inavyotekeleza mikakati yake kwa ufasaha hivyo Vijana mkawekeze JATU,” alisema

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Mwanahamisi Munkunda alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama kwa namna ofisi yake imekuwa mlezi mzuri kwa kampuni hiyo ya JATU PLC ambayo imepelekea mafanikio hayo yaliyofikiwa katika miaka mitano.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya JATU PLC, Bw. Peter Gasaya alisema kuwa falsafa ya kampuni hiyo imejikita katika uchumi shirikishi ambao unatoa fursa kwa wanachama kuishi bila kuwa na changamoto ya kipato kupitia fursa zinazowazunguka katika kujiendeleza kiuchumi.

“Katika miaka mitano JATU PLC inajivunia mafanikio iliyoyapata ambayo yamewezesha kampuni kufungua rasmi mradi wa Ufugaji, Bima na Bank ambayo itatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na usalama,” alisema Gasaya

 

MWISHOEmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.