Wednesday, October 13, 2021

Majaliwa: Vijana Jiepusheni na Matumizi Mabaya ya Tehama

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita.


Baadhi ya Wamanchi wakimsikikliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita  Oktoba 12, 2021. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama Katiba ya Jumuyia ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru (TAUTA) wakati alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

Na: Mwandishi Wetu: CHATO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi hususani vijana wajiepushe na matumizi yasiyo sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama vile wizi na utapeli wa fedha unaofanywa kwa njia ya mtandao.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa vijana nchini wajiepushe na matumizi mabaya ya TEHAMA kama kujiunga na makundi yasiyofaa, kujiingiza kwenye majukwaa ya uchochezi kwani vitendo hivyo vinavuruga amani, utulivu na mshikamano wa Taifa.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 12, 2021) alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa katika Viwanja vya Mazaina wilayani Chato, Geita yenye kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni Msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji.” Pia Waziri Mkuu amezindua Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Tanzania (TAUTA).

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza maadhimisho ya wiki ya Vijana Kitaifa na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru vifanyike katika wilaya ya Chato mkoani Geita ili kumuenzi Muasisi wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere ambaye alitoa mchango mkubwa katika kulikomboa Taifa letu akiwa kijana.  

Kutokana na umuhimu huo Serikali imesisitiza matumizi sahihi ya TEHAMA kwenu vijana kwani ninyi ndio watumiaji wakubwa na wahanga wakubwa wa TEHAMA. Ni ukweli usiopingika kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.”

“Vijana wengi wamefanikiwa kutokana na matumizi sahihi ya TEHAMA hususan kwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao. Vijana wameweza kuanzisha na kuendesha vituo vya huduma za intaneti na pia kuanzisha wakala wa huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu.”

“Hivyo, tukitumia fursa hizi vizuri na maendeleo ya TEHAMA tuliyonayo, tutasonga mbele kwa kazi kubwa zaidi. Tunayo mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, tumieni fursa hizo za mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri zetu kuwekeza katika miradi yenye tija kwa maendeleo yenu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka vijana watumie fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira inayoikabili dunia kwa sasa. “Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini pia tunayo fursa ya uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza vijana watembelee kwa wingi banda la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Foundation) lililopo katika maonesho hayo ili wakajifunze kupitia historia ya baba wa Taifa umuhimu wao kama vijana wa Tanzania katika kujenga misingi ya uzalendo, uwajibikaji na ujenzi wa Taifa.

“Umuhimu wa kujua historia ni dhahiri kabisa kwani itaongeza ari ya uzalendo, kuipenda nchi yetu na kuimarisha muungano wetu ambao asili yake ni udugu wetu. Hii ni namna bora zaidi ya kumuenzi muasisi wa Taifa letu. Ama kwa hakika Kiongozi wetu huyo alikuwa ni mzalendo na muaminifu kwa Taifa.”

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo kuhifadhi kumbukumbu ya historia na kazi za Baba wa Taifa. “Maono yake, falsafa zake, uzalendo wake na bidii ya kazi aliyoifanya Baba wa Taifa kwa Taifa hili katika uhai wake vitaendelea kukumbukwa jana, leo, kesho na kila siku katika uhai wa dunia hii.”

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema katika wiki hiyo ya vijana kitaifa imewawezesha vijana kufanya tafakuri ya kina kuhusu falsafa juu ya maono ya Baba wa Taifa kupitia kazi alizozifanya kwa Watanzania,

Pia, amesema kuwamaadhimisho hayo yamewawezesha vijana kubadilishana uzoefu katika bidhaa na huduma za kiuchumi zinazotolewa na makundi mbalimbali ya vijana nchini. “Kupitia wiki hii tumewawezesha vijana kujitambua na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.”

Kwa upande wake, Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tabia Maulidi Mwita amesema kuwa Wizara hiyo itashirikiana na vijana wate nchini wakiwemo na walioshiriki katika maonesho hayo katika kuulinda na kuudumisha Muungano kwani una faida kubwa.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda amesema wiki ya vijana imeanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha na kuwapa nafasi vijana na wadau wa shughuli za maendeleo yao na kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali yanayowahusu kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Amesema maadhimisho hayo ambayo yalianza Oktoba 8, 2021 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 yamehudhuriwa na vijana zaidi 1.000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambao pamoja na mambo mengine wamepata mafunzo ya aina mbalimbali yakiwemo na ya matumizi bora ya TEHAMA.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.