Friday, October 15, 2021

Rais Mwinyi: Tuilinde Amani Iliyopo Nchini


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amewaasa Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini ili Tanzania iendelee kuwa kitovu cha amani katika bara la Afrika na mfano wa kuigwa duniani.

Hayo ameyasema leo Oktoba 14, 2021, Chato mkoani Geita katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Bikira Maria, wakati alipokuwa akihutubia wakati wa  maadhimisho ya misa maalum ya kuwaombea Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.

Pamoja na viongozi waliopo madarakani wakiongozwa na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

” Nawashukuru viongozi wetu wa dini na waumini mbalimbali kwa kushiriki katika tukio hili maalum kwa nchi yetu kwa kuzingatia kuwa viongozi wetu walijituma katika kuijenga nchi na sisi hatuna lolote la kuwalipa kwa kutufanya kuwa na Taifa lenye haki, usawa na uhuru, hivyo sisi hatuna budi kuwaombea ili wapumzike kwa amani”. Alisema Rais Mwinyi

Aidha, alisisitiza “Pia Watanzania tudumishe utaratibu huu wa maombi ili kuiombea nchi yetu, Tanzania ni mfano pekee wa kuigwa duniani kutokana na amani iliyopo hivyo hatuna budi kuilinda”.

Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Rulenge  Ngara, Severine  Niwemgizi alisema kuwa ni jambo jema na la hekima kwa viongozi kuanza na sala na maombi kabla ya kuadhimisha sherehe za kilele cha Mwenge.

“Namshukuru, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi na Serikali kwa ujumla kwa kutupa heshima ya kusali pamoja nasi asubuhi hii” alisema Askofu Niwemgizi

Aliongeza kuwa Watanzania waendelee kuwaombea viongozi waliotangulia mbele za haki na waliopo madarakani kwa kufanya matendo mema ambayo viongozi wamekua wakiwaasa.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.