Sunday, October 17, 2021

Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI yatembelea Mradi wa Timiza Malengo Iramba


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Fatma Taufiq (katikati) walipotembelea kuona utekelezaji  shughuli za mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na TACAIDS, tarehe 16 Oktoba, 2021 Wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida.

Na: Mwandishi Wetu - SINGIDA

Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI imefanya ziara ya kukagua utekeleaji wa shughuli za Mradi wa kinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, mradi wa Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) unaotekelezwa katika Wilaya ya Iramba mkoa wa Singida.

Kamati ilitembelea mradi huo tarehe 16 Oktoba, 2021 ili kujionea maendeleo ya mradi huo kwa lengo la kuona namna miradi inayotekelezwa na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

Mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na kutekelezwa na Serikali kupitia Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine kama TAMISEMI, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknoloji, Taasisi ya Elimu, Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) ,TASAF, AMREF na TAYOA.

Mradi huo umetekelezwa kwa muda wa miaka 3 tangu Januari 2018 hadi Disemba 2020 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na walengwa wakiwa wasichana balehe na wanawake vijana waliopo kwenye vijiji 50 vinavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Wilayani humo.

Hadi sasa mradi umeifikia mikoa mitano ya mfano ikiwemo; Morogoro, Dodoma, Singida, Geita na Tanga ambapo wamelenga kundi la wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walio ndani ya mfumo wa shule, kuendelea na masomo na kufikia ndoto zao wakiwa salama bila maambukizi ya VVU/ UKIMWI.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatma Taufiq akizungumza wakati wa kikao cha ufunguzi alisema ni muhimu kwa Serikali kuendelea kutoa elimu na kuyafikia makundi ya wasichana balehe kwa kuzingatia ndilo kundi lililo katika hatari ya kupata maambukuzi ya VVU huku akiwaasa vijana kuitumia miradi hiyo kama chachu kujikwamua kiuchumia na kutimiza ndoto zao huku wakichangia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Tumetembeela kuona jinsi Serikali inavyotekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kundi la vijana linalotajwa kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU na UKIMIMWI yanahudumiwa ipasavyo na kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya”

Aliongezea kuwa, miradi hiyo inapaswa kufanyika kwa usahihi ili kuwa na tija katika jamii zetu na kuhakikisha inakuwekewa mipango endelevu na kuifikia mikoa yote ili kuwa na vijana wenye kujitambua na kutimiza ndoto zao.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wasichana balehe na wanawake vijana kwa wingi kwa kuhakikisa mradi huu wa Timiza Malengo unafika katika mikoa yote nchini.

“Mradi huu umeanza katika mikoa hii mitano ya mfano, ni malengo kuwafikia vijana wetu wa Kitanzania ili waweze kupatia elimu itakayowasaidia kujitambua na kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwapekelea katika maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,”Alisema Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha jamii inabadili mitazamo kuhusu kundi hili la wasichana balehe na wanawake vijana ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili wajikwamue na kuinua wengine.

Aidha aliwaelekeza watendaji wa Wilaya ya hiyo  kuhakikisha wanakuwa na kanzi data ya wanufaika hao, kusaidia uendelevu wa programu na kuhakikisha waelimisha rika wanapatiwa ushirikiano wa kutosha ili wafikie kundi kubwa lililoachwa nyuma.

“Serikali imelilenga kundi hilo kwa kuzingatia  takwimu za mwaka  2017 ambapo zinaeleza vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 40 ya maambukizi mapya na kati yao asilimia 80 ni watoto wetu wa kike, hii ni dalili kwamba lazima mapambano haya yazidishwe katika makundi haya hatarishi”alisema Waziri Mhagama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Mwenda aliishukuru kamati hiyo kutembelea na kuona utekelezaji wa programu ya TIimiza Malengo na kuendelea kuahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maeneo yote muhimu yanayohusu mradi yanaendelea vyema huku akimshukuru Waziri Mhagama kwa kutoa kipaumbele kwa wilaya hiyo na kusema wataendelea kutunza kanzi data ya wanufaika wa mradi ili matunda yanayotokana na mradi huo yasipoteee.

“Wilaya itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha kunakuwa na bajeti ya kutosha katika kuyahudumia makubdi haya muhimu kwenye jamii,”alisema Mwenda.

Wakitoa shukrani na shuhuda zao tangu kuanza kwa mradi huo wanafunzi wa shule za  sekondari za Lulumba na New Kiomboi waliishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo huku wakisema umewawezesha kuongeza hali ya ufaulu, kujikimu kiuchumi na kupata mahitaji yao kwa wakati na kuwasaidia familia zao katika mahitaji mbalimbali.

AWALI

Mradi wa timiza Malengo unahusisha ugawaji wa taulo za kike kwa wasichana walio ndani ya mfumo wa shule, kugawa kondom na kufunga visanduku vya kondom  katika maeneo husika, kutoa elimu kwa viongozi wa dini kuhusu masuala ya UKIMWI, Utoaji wa mafunzo kuhusu uandaji wa mpango rahisi wa biashara na ujasiriamali, elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi au walezi wa wasichana, kuhamasisha wasichana kupima afya zao kwa hiari kupitia huduma ya mkoba na Vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao kupitia mabonanza, kuwawezesha wasichana kwa kuwapatia ujuzi wa jinsi ya kujikinga na maambukizi pamoja na kutoa elimu kwa njia ya simu kwa kupitia namba 117/15017- bure ambapo wanapokea na kupata fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.