Thursday, October 14, 2021

Serikali Kuendelea Kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa katika Usimamizi wa Maafa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na Vyombo vya Habari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa hii leo Oktoba 13, 2021 Chato, Mkoani Geita. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Col. Jimmy Matamwe. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Charles Msangi. 

Na: Mwandishi Wetu: CHATO 

Serikali kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa imeendelea kuimarisha ushirikiano katika kufanikisha hatua za usimamizi wa maafa nchini ikiwa ni moja ya mikakati ya kuepusha na kupunguza maafa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Chato mkoani Geita katika Maonesho ya Wiki ya Vijana,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa kwa lengo la kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa katika mifumo ya maisha, afya, uchumi, elimu, jamii, utamaduni, miundombinu na mazingira.

Alitaja tasisisi hizo za kuwa ni Taasisi za Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa, Nchi Washirika, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika.

Aidha, Mhe Waziri Jenista alisema “Serikali ya Awamu ya Sita kwa maono chanya ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza madhara ya maafa ikiwa ni njia muhimu ya kulinda maendeleo ya kisekta ili kufikia matokeo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na utekelezaji wa Makubaliano ya Paris katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi,” alieleza Waziri Mhagama

Alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imekuwa ikiadhimisha siku hii kila mwaka kwa ajili ya kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa na kitaifa, ili kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali katika ubora zaidi pale maafa yanapotokea.

Mhe. Waziri Mhagama, aliongeza kuwa  Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kuanzisha maghala ya kuhifadhi vifaa vya huduma za kibinadamu ambayo yapo kimkakati katika Kanda sita kwa ajili ya kurahisisha upatikananji wa huduma za kibinadamu pindi maafa yanapotokea kwa kushirikiana na kamati za maafa za Wilaya na Mikoa.

Pia, kupitia ushirikiano huo kimeanzishwa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura pamoja na vifaa na muongozo kwa ajili ya uendeshaji wake. Vilevile, vikundi vya wanawake, vijana na watoto katika shule vimekuwa vikiwezeshwa ili kuboresha mifumo ya maisha katika Wilaya ambazo zimekuwa zikiathirika na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Waziri Mhagama alieleleza kuwa Serikali imeandaa mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 zilizoonekana kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na maafa mbalimbali.

Sambamba na hilo, Mhe. Waziri Mhagama, alieleza jitihada za Serikali katika kupunguza madhara ya maafa yanayoendelea kujitokeza ikiwemo changamoto ya kuibuka kwa hatari ya mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona – 19 (UVIKO-19).

“Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja baina ya nchi jirani, marafiki na taasisi za jumuiya ya kimataifa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa wakati huu na siku zijazo, hivyo Serikali imepokea na inaendelea kutekeleza programu ya chanjo kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu ambao ni hatari kwa maisha na kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa nchi yetu na dunia kwa ujumla,” alisema

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha sera, sheria na kuandaa mikakati kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.

Pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na Uwanja wa Mazaina Chato mkoani Geita  ili kupata elimu ya kukabiliana na majanga na kupunguza athari za maafa inayotolewa na wataalamu wetu ili kulinda maisha, mali na uchumi wetu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Col. Jimmy Matamwe alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi zote ili kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na maafa  pale yanapotokea na pia kuzuia viashiria vyake.

Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ilitokana na Azimio Na. 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Desemba, 2009 ambapo iliamuliwa Oktoba 13 ya kila mwaka. Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ikiwa na lengo la Kukuza utamaduni wa kupunguza madhara ya maafa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia, kujitayarisha, kukabili na kurejesha hali kuwa bora zaidi. Kaulimbili ya mwaka huu ni kwa umoja wetu… tunaweza kuokoa dunia


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.