Thursday, May 31, 2018

WIZARA, TAASISI ZA SERIKALI ZITUMIE NISHATI MBADALA – WAZIRI MKUU


*Aagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wabadilike
*Ataka wasimamie wananchi waachane na matumizi ya mkaa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.

Wizara, taasisi na mashirika yote ya Serikali na binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati mbadala ili matumizi ya mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”

Waziri Mkuu amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Ili kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.

“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.

“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”

“Meya ametoa fursa na amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni bajeti kupitia Mabaraza ya Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa teknolojia hii kwenye maeneo yenu. Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe watengeneze mashine nyingi zaidi na zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze kutumia teknonolojia hiyo kupikia,” alisisitiza.

Amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam wafuatilie kwa karibu usambazaji wa teknolojia hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali ya mazingira hapa nchini ni mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu waishio mijini.

“Hali ya mazingira nchini mwetu ni mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa sababu mahitaji yao yote wanayapata sokoni na madukani,” alisema.

“Wenzetu wa mikoani na vijijii wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba wanataabika kwa sababu kipato chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.  

Alisema mazingira yanafungamana na utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na kwamba maendeleo ya nchi pia yamefungamana moja kwa moja na mazingira. “Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,” alisema.

Waziri Makamba alisema taasisi za Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na shule zinaongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.

Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu kila siku.

“Chuo hiki kina migahawa tisa, kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna mgahawa mmoja mdogo unatumia magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa unatumia magunia mangapi?” alihoji.

Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni siku ya kilele. Pia wiki nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na mjadala wa kitaifa.

Read More

Wednesday, May 30, 2018

MAJALIWA AZINDUA WIKI YA MAZINGIRA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuzindua Maadhisho ya Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuzindua Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na watatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhandisi Evarest Ndikilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutokana na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. katikati ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutokana na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. katikati ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. 

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada ya maonyesho  kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Bibi Nimwagile Mwaijumba wakati alipotembelea banda la Kituo cha Utengenezaji magari cha Nyumbu  na kujionea mashine ya kutengeneza mkaa bora kwa kutumia takataka iliyobuniwa na kutengenezwa na kituo hicho. Waziri Mkuu alitembelea mabanda ya maonyesho  kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Watatu kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Opwani Mhandisi, Evarest Ndikilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya JHS , David Mwendapole  wakati alipotoa maelezo kuhusu majiko makubwa yanayotumia  gesi kidogo  katika maonyesho ya Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Wanne kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. 

Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi baada ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, Mwenyekiti wa CC wa Mkoa wa Dar es alaam, Kate Kamba,Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Matiku Makori  na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Read More

WAZIRI MKUU AIPONGEZA BENKI YA NMB KUCHANGIA HUDUMA ZA KIJAMII


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya NMB kwa kuchangia huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo elimu, afya na michezo.

Ametoa pongezi hizo leo (Jumatano, Mei 30, 2018) wakati akizungumza Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Bi. Ineke Bussemaker ofisini kwake Magogoni jijini Dra es Salaam.

Amesema katika jitihada za Serikali za kufufua ushirika na hasa kwenye mazao makuu matano, wakulima wamehamasishwa wafungue akaunti ili malipo ya fedha zao yafanywe moja kwa moja kweye akaunti zao.

“Tumehamasisha wakulima wote wafungue akaunti ili malipo ya mazao yao yafanywe mojamoja katika akaunti zao jambo ambalo litaepusha wizi au kunyang’anywa fedha wawapo mitaani, na kupitia mawakala walioko vijijini, wataweza kupokea fedha hizo,” amesema.

Amesema uwepo wa mawakala wa benki hadi vijijini, umesaidia kuwafanya Watanzania wasiweke fedha ndani ya nyumba zao.

Akizungumzia mchango wa Benki hiyo kwenye huduma za jamii, Waziri Mkuu amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuchangia vitabu, madawati na michezo ambapo imetoa mchango wa sh.milioni kwa timu ya soka ya Namungo iliyoko wilayani Ruangwa.

“Tumeona Benki ya NMB ikifadhili timu mbalimbali za ligi kuu kama vile AZAM, na sasa wameanza kuchangia timu za daraja la kwanza kwa kuichangia timu ya Namungo shilingi milioni 10. Pia walichangia sh.milioni kwenye ujenzi wa uwanja wa kisasa kule Ruangwa, tunawashukuru sana,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Bussemaker alisema wamefurahi kupata fursa ya kuichangia timu ya Namungo na kwamba wataifuatilia kwa karibu kuona ushiriki wake ukoje kwenye ligi hiyo. “Pia tunaitakia kila la kheri kwenye ushiriki wao wa ligi daraja la kwanza,” alisema.
Read More

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA AKUTANA NA VIONGOZI WA BENKI YA NMB NA KUPOKEA HUNDI YA SH. 10M KWA AJILI YA TIMU YA MPIRA WA MIGUU YA NAMUNGO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bibi Ineke Bussemaker (katikati) na  Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB (Head of Government Business), Bibi Vicky Bishubo, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni  jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bibi Ineke Bussemaker (katikati) na  Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB (Head of Government Business), Bibi Vicky Bishubo, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni  jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 10, 000,000/=  kutoka kwa  Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bibi  Ineke Bussemaker (katikati) ukiwa ni mchango wa Benki hiyo kwa timu ya mpira wa miguu ya Namungo ya wilayani Rungwa. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam Mei 30, 2018. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB,  Bibi Vicky Bishubo.

Read More

NITAZINDUA KAMPENI YA KUPIMA VVU - WAZIRI MKUU


*Lengo ni kuhamasisha wanaume wapime afya zao, wajue hali zao
*Ataka Wakuu wa Mikoa wahamasishe upimaji hadi ngazi za vijiji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mwezi ujao, atazindua kampeni maalum ya upimaji wa virusi vya UKIMWI (VVU) ambayo imelenga kuwahamasisha wanaume wapime afya zao na kutambua hali zao.

“Serikali tumeandaa kampeni maalum ya kuhamasisha upimaji wa VVU na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza VVU mara moja (Test and Treat), hasa kwa wanaume. Kampeni hii itazinduliwa rasmi na mimi mwenyewe jijini Dodoma tarehe 19 Juni 2018,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Mei 30, 2018) wakati akizindua maadhimisho ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (PEPFAR) kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Takwimu zinaonyesha watu ambao wako tayari kupima kwa hiyari yao siku zote ni wanawake. Akinababa wakiambiwa hutoa sababu mara hiki, mara kile. Nitoe wito kwa wanaume wote, tubadilike! Ni vema tushiriki kampeni ya wanaume kujitambua na kupima ili tujue hali zetu,” amesema.

Amewataka wadau wote wanaohusika na masuala ya UKIMWI washiriki kikamilifu katika kampeni hiyo baada ya uzinduzi, na pia akawataka Wakuu wa Mikoa mikoa yote nchini wasimamie kampeni hizo muhimu katika mikoa yao hadi ngazi ya vijiji.

Waziri Mkuu amesema ujio wa PEPFAR umeleta mafanikio makubwa katika vita dhidi ya UKIMWI na kupitia shughuli zake, elimu ya kinga na ufahamu kuhusu UKIMWI ilitolewa kwa watu wa rika na makundi mbalimbali ya jamii.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukubwa wa viwango vya maambukizi na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoambukizwa VVU katika baadhi ya mikoa nchini.

Amesema kuna mikoa 14 ambayo kiwango cha maambukizi kiko juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.7 na akaitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe wenye asilimia 11.4, Iringa (asilimia 11.3), Mbeya (asilimia 9.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5) na Katavi (asilimia 5.9). Mikoa mingine ni Shinyanga (asilimia 5.9), Songwe (asilimia 5.8) Ruvuma (asilimia 5.6) Pwani (asilimia 5.5) Tabora (asilimia 5.1) pamoja na Tanga, Dodoma na Geita ambayo yote ina asilimia 5.0 ya maambukizi.

Waziri Mkuu ameitaja mikoa mingine sita ambayo ina ongezeko kubwa la watu wanaoishi na VVU kuwa ni Iringa (asilimia 11.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5), Tanga (asilimia 5.0), Dodoma (asilimia 5.0) na Manyara (asilimia 2.3).

Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa nguvu na jitihada zaidi zinahitajika katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa kuweka utaratibu thabiti na endelevu wa kutoa elimu na hamasa ya kutumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI nchini. “Kwa hiyo, programu za kinga zinapaswa kuwa endelevu kwenye mikoa yote nchini, hususan mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi. Pia huduma za ARVs ziendelee kupewa kipaumbele katika mipango yetu,” amesisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema Tanzania kwa sasa ina watu karibu milioni moja ambao wako kwenye matibabu ya kufubaza VVU.

“Kutokana na mpango wa PEPFAR, Tanzania imekwishapokea sh. trilioni 10 tangu mfuko huu uanzishwe mwaka 2003 na matumizi ya dawa za kufubaza VVU yamesaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa asilimia 70, yaani kutoka vifo 110,000 mwaka 2003 hadi kufikia 33,000 mwaka 2016,” alisema.

Alisema kutokana na matumizi ya dawa hizo, maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto nayo pia yamepungua kutoka asilimia 12 na kufikia asilimia 4.9 hivi sasa.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani, Bi Inmi Patterson alisema kati ya sasa na Septemba 2019, PEPFAR inatarajia kutumia zaidi ya sh. trilioni moja (dola za Marekani milioni 512) katika kuboresha huduma za kuzuia maambukizi ya VVU, upimaji na matibabu hapa nchini.

Alisema wanapoendelea na utekelezaji wa kazi za mfuko huo na maadhimisho ya miaka 15 ya PEPFAR, kampeni yao itaendelea kwa mwaka wote wa 2018 na imelenga kupunguza unyanyapaa na tabia ya kuwatenga watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

“Kampeni ya PEPFAR15 inalenga kupunguza unyanyapaa, kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma zitolewazo za kukabiliana na VVU. Kila mtu atakayepimwa na kugundulika kuwa ana maambukizi ya VVU, ataanzishiwa matibabu mara moja. Tutafanya kazi na watu wanaoishi na VVU nchini kote ili kusimulia habari nzuri (positive stories) za watu wanaoishi na VVU ambao waliwahi kuwa dhaifu ama wagonjwa lakini sasa wana nguvu na afya; habari za akinamama wanaoishi na VVU na wanapata matibabu ili kuwalinda watoto wao,” alisema.
Read More

MAJALIWA AZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 15 TANGU KUANZISHWA KWA MFUKO WA DHARURA WA RAIS WA MAREKANI WA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI (PEPFAR)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Inmi Patterson wakati alipowasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kuzindua   Maadhimisho ya Miaka 15 Tangu  Kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEPFAR), Mei 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia)  na Kaimu Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Inmi Patterson kabla ya Kuzindua  Maadhimisho ya Miaka 15 Tangu  Kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEPFAR) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza  katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 15 Tangu  Kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEPFAR) kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam,  Mei 30, 2018.Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Maadhimisho ya Miaka 15 Tangu Kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEPFAR) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam,  Mei 30, 2018.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiagana baadhi ya viongozi walioshiriki  katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 15 Tangu  Kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEPFAR) Kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018. Kutoka kulia ni Dkt. Janet Mwambona wa Taasisi HIV/AIDS Treatment Advisor,Walter Reed Army Institute Of Research, Brian Rettmann ambaye ni Mratibu  wa PEPFAR nchini, Dkt. Leonard Maboko, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume yaTaifa ya  Kudhibiti Ukimwi Tanzania na wanne kulia ni Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson.

Read More

Sunday, May 27, 2018

DK. SALEH ALI SHEIKH: TANZANIA NI MFANO WA KUIGWA

*Asifu amani iliyopo nchini, upendo wa Watanzania
*Asema mahujaji wa Tanzania hawana rekodi za uovu


WAZIRI wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ali Sheikh amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine kutokana na amani iliyopo.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumapili, Mei 27, 2018) wakati akitoa nasaha kwa wageni walioshiriki futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

“Ninaomba nipelekewe shukrani zangu kwa umma wa Watanzania kutokana na upendo walionao. Ukiwaona ni watu wa amani, furaha na upendo na hili linathibitishwa na amani iliyopo nchini mwenu,” alisema.

Alisema uwepo wa amani na upendo miongoni mwa wananchi ni kielelezo tosha cha kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa dini ambao ndiyo wanawalea Watanzania. “Kilichofanyika leo ni daraja kati ya Tanzania na Saudi Arabia, ni asubuhi njema ambayo pia ni dalili kwamba kuna mchana mwema unakuja,” alisema.

Alimshukuru Waziri Mkuu kwa ukaribisho aliopewa kushiriki futari nyumbani kwake na kuongeza kuwa hicho ni kitendo cha udugu na utu na kitazidi kujenga mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Alisema tabia hizo njema ni urithi kutoka kwa maulamaa waliotumwa na Mungu ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwatengeneza watu wawe na tabia njema na siyo kuwafundisha junsi ya kurusha ndege.

“Matendo haya yanaonekana wazi kwa Watanzania kwani hata wakati wa hijja kuna nchi nyingi zinakuja kule kwetu, lakini haijawahi kuripotiwa kuwa hujaji wa Tanzania ameingia katika utovu wa adabu,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimshukuru Waziri huyo na ujumbe wake kwa kuitembelea Tanzania na kushiriki kwenye mashindano ya 19 ya kuhifadhi Quran Afrika.


Waziri Mkuu alisema amefarijika na uamuzi wa Waziri huto wa Saudi Arabia na ujumbe wake wa watu 16 kuamua kuongeza siku zaidi za ziara yao hapa nchini hadi Jumatano (Mei 30, 2018) badala ya kuondoka Jumatatu (Mei 28, 2018) ili waweze kutembelea vituo vya watoto yatima na kuona maeneo mengine jijini Dar es Salaam.

“Tumefarijika na ahadi uliyoitoa pale uwanjani kwamba mwaka kesho utahakikisha kwamba Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Makkah, Sheikh Abdul Rahman Abd al Aziz al Sudais anakuja nchini kuhudhuria mashindano ya 20 ya kuhifadhi Quran tukufu,” alisema.

Viongozi wengine waliohudhuria futani hiyo ni Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal, na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mstahiki Meya wa Kinondoni wa Meya wa Temeke.
Read More

MAJALIWA AFUTURISHA KWENYE MAKAZI YAKE JIJINI DAR

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkaribisha, Waziri wa Mambo ya Dini wa Saud Arabia, Dkt. Saleh Alashiek (wapili kushoto) na ujumbe wake wakati alipofuturisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu,  Oysterbay jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkaribisha, Waziri wa Mambo ya Dini wa Saud Arabia, Dkt. Saleh Alashiek (wapili kushoto) na ujumbe wake wakati alipofuturisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu,  Oysterbay jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofuturisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam  Mei 27, 2018. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Dini wa Saud Arabia, Dkt. Saleh Alashiek na kulia ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir.

Baadhi ya waalikwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza katika futari aliyoiandaa kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Mei 27, 2018.Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (kushoto) akiagana na baadhi ya wanawake walioshiriki katika futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.


Read More

MTANZANIA AIBUKA KIDEDEA MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN AFRIKA


*Waziri Mkuu amtaka Sheikh Kishki akaonane na Waziri wa Ardhi atoe maamuzi ya kiwanja
          
KIJANA wa Kitanzania, Shujaa Suleiman Shujaa ameibuka kidedea na kitita cha sh. milioni 15 katika mashindano ya 19 ya Afrika ya kuhifadhi Quran kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.

Shujaa mwenye miaka 23 ambaye ni mkazi wa Morogoro, amejishindia pia laptop, kiwanja chenye hati eneo la Kigamboni kilichotolewa na kampuni ya Property International ya jijini Dar es Salaam pamoja na dola za Marekani 500 kutoka kwa Bw. Ahmed Seif “Magari” aliyetoa dola 500 kwa washindi wote watano.

Akizungumza na maelfu ya waumini na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo mchana (Jumapili, Mei 27, 2018), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuilinda amani iliyopo nchini kwani ikipotea hakuna atakayeweza kufanya ibada.

“Mtakubaliana nami kuwa amani ya nchi yetu, ndiyo inatufanya tutembee vifua mbele dhidi ya wenzetu, ni neema kubwa ambayo kila muumini anapaswa kuilinda kwani ikipotea hata mkusanyiko wetu huu wa leo si rahisi kufanyika mahali kama hapa,” amesema.

“Leo hii tuko hapa uwanjani kwa sababu tuna amani, kama Serikali isingekuwa inashirikisha Watanzania wote kulinda amani, basi tusingeweza kukutanika hapa. Kuna nchi 18 ziko hapa, na watu wake wamekuja hapa uwanjani kwa kuwa wana uhakika na amani tuliyonayo sisi Watanzania,” alisema.

Alisema katika nchi ambazo amani imetoweka, watu wanalazimika kufanya shughuli za ibada majumbani au kwa kujificha. “Wenzetu hao, hawapati fursa adhimu kama hii ya kujumuika pamoja na majirani, ndugu, jamaa na marafiki kusikiliza na kufurahia kisomo cha Quran au kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,” aliongeza.

Aliwataka Watanzania waendelee kubeza na kupuuza kauli za walio wachache ambao kwao kuzungumzia amani ni kujipendekeza kwa Serikali. “Watu hao wamesahau kwamba tofauti katika Uislamu hazikuanza leo, lakini tofauti hizo hazikuwa sababu ya wema waliotangulia kuacha kuheshimiana na kushirikiana,” alisisitiza.

Mshindi wa pili kwenye kundi hilo la juzuu 30 ni Ahmed Noor wa Sudan ambaye ameshinda sh. 12,564,750 pamoja na laptop akifuatiwa na Muzamil Awadh Mohamed wa Sudan alijishindia sh. milion 7.5 pamoja na laptop zilizotolewa na kampuni ya Camara Education.

Mshindi wa nne ni Abdulally A. Mohammed wa Kenya aliyepata zawadi ya sh. 5,711,000 na wa tano ni Ibrahim Maazur kutoka Niger, aliyepata sh. 3,426,000. Washindi hao wote watano walipewa zawadi ya kwenda hijja na Waziri wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ally Sheikh.

Washiriki wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji Djibouti, Kenya, Ethiopia, Congo DRC, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

Washiriki wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu (washindi watatu), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na Juzuu 20 (washindi watatu).

Viongozi wengine waliohudhuria mashindano hayo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kutoka Saudi Arabia, Comoro, Oman, Uturuki, Kenya, Msumbiji na Nigeria, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Sheikh Nurdin Mohammed Ahmad (maarufu kama Sheikh Kishki) akaonane na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi ili atoe maamuzi ya kiwanja chao kilichopo eneo la Matumbi ambacho mwaka jana aliagiza kifuatiliwe taratibu zake na kisha wapatiwe.

“Kuhusiana na suala la kiwanja mlichosema, mamlaka ya awali ni Manispaa ya Temeke na ilishakamilisha taratibu zote za kisheria, ikapeleka kwa Afisa Ardhi wa Mkoa kuona kama limepita kwenye vikao vyote ndipo wanaenda wizarani kupata kibali. Hakuna sababu ya wizara kuikatalia manispaa huku eneo lenyewe likiwa kwenye ramani kuu ya manispaa yenyewe, nenda mumuone Waziri mwenye dhamana, awape ardhi,” alisema.

Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kupewa taarifa akiwa jukwaani kwamba taasisi ya Al-Hikma iliwasiliana na Manispaa ya Temeke, hadi mkoani wakapewa barua zinaonyesha eneo liko sawa lakini walipofika wizarani wamekwamishwa na Afisa mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Mama Mpetula.

Juni 11, mwaka jana katika mashindanio ya 18, taasisi ya Al-Hikma waliomba wapatiwe kiwanja na.118 kwenye kitalu E kilichoshikamana na kiwanja na. 117 chenye shule yao ya Al-Hikma Girls iliyoko Temeke ili waweze kujenga zahanati.
Read More

MAJALIWA AHUTUBIA NA KUKABIDHI ZAWADI KWA WASHINDI WA MASHINDANO YA KUHIFADHI QUR-AAN TUKUFU AFRIKA KWENYE UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwa mgeni rasmi katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur- aan Tukufu  Afrika yaliyoandaliwa na  Taasisi ya Al – Hikima, Mei 27, 2018. Katikati ni Waziri wa Mambo ya Dini wa Saud Arabia, Dkt. Saleh  Alashiek.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir akizungumza katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.

Baadhi ya waalikwa waliohudhuria katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.

Baadhi ya waalikwa waliohudhuria katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir akizungumza katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.

Waziri wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dr. Saleh  Alashiek  akizungumza katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018. 

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akihutubia katika Mashindano ya 19 ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika  yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akimkabidhi Shujaa Suleiman Shujaa zawadi ya shilling milioni 15 baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kwanza wa Mashindano ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mei 27, 2018. Kulia ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir na watatu kulia ni Rais wa Taasisi ya Al- Hikima, Sheikh Shariff Abdukadir.

Read More

Saturday, May 26, 2018

TUJIEPUSHE NA VITENDO VYA CHUKI – WAZIRI MKUU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waumini wa dini ya Kiislamu wajiepushe na vitendo vinavyoweza kupandikiza chuki dhidi yao au kwa waumini wa dini nyingine.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Mei 26, 2018) wakati akizungumza na viongozi na mamia ya waumini wa dini ya Kiislamu walioshiriki mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu kwenye ukumbi wa Mwl. J. K. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama Tanzania (Istiqaama Muslim Community of Tanzania), yalijumuisha washiriki 29 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

“Serikali inatambua na inathamini sana, mchango wa dini katika kuwalea waumini kiimani na kutunza amani ya nchi. Hivyo, tujiepushe na kauli au vitendo ambavyo vinaweza kupandikiza chuki na uhasama dhidi yetu au dhidi ya waumini wa imani nyingine,” amesema.

“Nitoe rai kwenu viongozi wangu na waumini wenzangu, tujenge misingi ya kuvumiliana na kustahamiliana. Hilo pekee ndilo linaloisimamisha nchi yetu kuwa ni mfano wa kuigwa na kimbilio la wale waliovurugikiwa na amani katika nchi zao. Kadhalika, amani inajenga na kutoa fursa ya kuweza kutekeleza majukumu yetu ya kiibada, kiuchumi na kijamii bila hofu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa Surah Al-Imraan Ayah 103, Allah Mtukufu alihimiza umuhimu wa umoja miongoni mwa Waislamu. “Katika umoja huo, Allah amesisitiza Waislamu kuwa wamoja na kutofarakana. Mafundisho na wasia wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam ni kuwa tupendane na tushikamane. Wakati wote Mtume wetu aliheshimu na kuwathamini watu wote hata ambao hawakuwa Waislamu,” ameongeza.

“Kwa msingi huo, kama Waislamu nasi ni vema tukajipamba na tabia njema za Mtume wetu Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam. Katika hili, mtakubaliana nami kuwa tabia njema ni miongoni mwa makusudio muhimu sana ya kuletwa Mtume Muhammad kwetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuwapa elimu watoto kama ambavyo imesisitizwa kwenye Quran tukufu na kama ambavyo imesisitizwa na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) kwamba suala la kutafuta elimu ni la lazima kwa muislamu, awe mwanaume au mwanamke.

“Kama mnavyofahamu, Uislamu umeweka mkazo mkubwa sambamba na kusisitiza umuhimu wa elimu. Hili linathibitishwa na aya ya kwanza kabisa ya Quran kuteremshwa kwa Bwana Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam (SAW) ambayo ilimuamrisha kusoma (Surah Al-’Alaq ayah 1).”

“Kwa msingi huo, kama ambavyo mnatoa msukumo kwa vijana wetu kusomeshwa Quran, msukumo huo huo muutoe pia katika kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapatiwa mafunzo sahihi kuhusu tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka za utawala zilizopo. Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia vijana hawa kuwa raia wema na wazalendo kwa nchi yao,” amesema.

Amesema Quran licha ya kuwa ni kitabu cha dini lakini kimebeba masuala yote muhimu katika maisha ya muislamu ya kila siku. “Hivyo, ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya uadilifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, huna budi kuwekeza zaidi katika elimu. Kwa hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu wanasoma na kuhifadhi Quran pekee, bali pia wanapaswa kupewa fursa ya kujifunza elimu ya mazingira ili waweze kufikia hatua bora za kimaisha duniani na akhera,” amesema.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubei alisema mashindano hayo yamefana na imeshangaza kuona mtoto anatajiwa namba tu ya aya na anaweza kuielezea kuwa iko kwenye sura fulani.

Kama ambavyo nabii Yahya aliamriwa kushika kitabu, nasi pia tushike kitabu na tuyashike yaliyo ndani yake, tusije kuishi katika ardhi yenye rutuba na yenye rasilmali madini halafu na sisi tushindwe kuvuna kile kilichomo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiaya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif alisema jumuiya hiyo yenye matawi 20 Tanzania Bara na Visiwani, ilianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kutoa mafunzo ya kiroho na kuwajengea vijana maadili mema ili Taifa liwe na watu wenye kujali amani, wanaoheshimiana na kupendana kidugu.

Alisema jumuiya hiyo imejenga shule 14 za msingi na sekondari kwenye maeneo mbalimbali nchini na inatarajia kujenga shule kubwa ya kimataifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kufungua shule ya ufundi.

Katika mashindano hayo, kijana Kombo Fakhi Hamad (19) kutoka Istiqaama Pemba aliibuka mshindi wa jumla kwa kuweza kuhifadhi juzuu 30 na kupewa zawadi ya sh. milioni nne. Kombo pia aliibuka mshindi wa kwanza kwenye kundi la kuhifadhi juzuu 30 (tahfidh) akifuatiwa na Ally Said Mohamad (18) aliyepata sh. milioni mbili. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mariam Nassor Said (14) aliyepata sh. milioni 1.5.

Katika kundi la kuhifadhi juzuu 30 (tashdia), Masoud Bakari Ally (18) alikuwa mshindi wa kwanza na alipewa zawadi ya sh. milioni moja akifuatiwa na Mustafa Abdallah Hamad (17) aliyepata sh. 700,000 na wa tatu alikuwa Jumaa Ally Othman (16) aliyepata sh. 500,000.

Katika kundi la kuhifadhi juzuu 20, mshindi wa kwanza alikuwa Hilal Khamis Hamad (14) aliyepata sh. milioni 2.5 akifuatiwa na Ally Suleiman Ally (15) aliyepata sh. milioni 1.3 na mshindi wa tatu alikuwa Salim Khamiis Juma (15) aliyepata sh. milioni moja.
Read More