Friday, December 31, 2021

Waziri Mhagama: Serikali Kuendelea Kuchukua Hatua Stahiki Dhidi ya Majanga na Maafa Nchini


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watendaji kutoka katika ofisi yake alipotembelea na kukagua Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula kilichopo katika ofisi hiyo hii leo Desemba 31, 2021 Jijini Dodoma.

Na: Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya Majanga na Maafa nchini kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa (Tanzania Centre of Excellence in Disaster Management).  

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea na kukagua Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula kilichopo katika ofisi hiyo hii leo Desemba 31, 2021 Jijini Dodoma kwa lengo la kupokea taarifa na hatua zinazochukuliwa katika kuboresha utendaji wa kituo hicho.

Waziri Mhagama alieleza kuwa kati ya mambo mazuri yaliyofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa katika mwaka wa 2021 ni pamoja na ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa kinachojengwa eneo la Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma.

“Ofisi ya Waziri Mkuu tunajivunia na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa ambacho kitasaidia kuimarisha uwezo wa usimamizi wa maafa katika sekta zote hapa nchini kwa ajili ya maendeleo endelevu,” alisema Waziri Mhagama

“Ujenzi wa kituo hicho ni dhamira ya serikali katika kuhakikisha inazingatia namna njema ya hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na maafa yanapojitokeza,” alisema

Aliongeza kuwa, Katika kutekeleza mpango huo Serikali imeendelea na azma ya ujenzi wa Kituo cha Tiafa cha Usimamizi wa Maafa nchini kwa kuingiza tena mpango wa ujenzi wa kituo hicho katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020 – 2025) katika Ibara ya 107 kipengele (h) ikiwa na lengo la kuhakikisha vyombo vinavyoshughulika na maafa vinakuwa na mpango wa utayari wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa kituo hicho kitasaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa na kuwezesha uwepo wa vifaa na zana za kisasa katika utoaji wa huduma za usimamizi wa maafa nchini, kuwa na mfumo wa kisayansi wa kufuatilia mwenendo wa majanga na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukua kwa wakati kwa ajili ya tahadhari za awali, kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa, kuwa na rasilimali za kutosha na kuimarisha ushirikiano na wadau katika utekelezaji wa dhana nzima ya mzingo wa maafa kwa ajili ya kuwa na jamii yenye uchumi stahimilivu pamoja na kituo hicho cha usimamizi wa maafa kuwa cha mfano kwa ajili ya jamii yenye ustahimilivu na uchumi endelevu nchini.

Akiwa katika ziara hiyo ya kutembelea na kukagua Kituo hicho cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula, Waziri Mhagama amewataka wadau kutoka katika sekta mbalimbali wanashughulikia masuala ya majanga na maafa kuwa na mfumo wa Kanzi Data (Data Base) ili kujua namna walivyorejesha hali katika maeneo yaliyokubwa na majanga na maafa. 

Read More

Monday, December 6, 2021

Serikali kushirikiana na EAC kuendeleza Wajasiriamali Wadogo


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akieleza jambo kuhusu maonesho hayo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza.


Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wa kuratibu vizuri maandalizi ya Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) kwa Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Ally Msaki (kulia) ambaye ni mwenyekiti wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

*******************************

Na: Mwandishi Wetu - MWANZA


Serikali kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejipanga kuwa na sera ya kuendeleza wajasiriamali wadogo kwa lengo la kukuza haraka sekta ya biashara ndogo, kuongeza ajira, vipato vya wajasiriamali, pato la Taifa na kupunguza umaskini katika jamii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati akifungua Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na nchi 5 ikiwemo Burundi, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini na Uganda zimeazimia na kujipanga kuwa na sera itakayosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati sambamba na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa shughuli zao.

“Sekta isiyo rasmi inachukua sehemu kubwa ya Uchumi na Uzalishaji katika nchi nyingi hasa nchi zinazoendelea, hivyo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatekeleza azma ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi ya Wajasiriamali kupata huduma stahiki za usajili na kufanya biashara,” alisema

“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwa kuwa nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi kubwa hali inayopelekea umuhimu wa uwepo wa sera zitakazosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema Waziri Mkumbo

Aliongeza kuwa, Maonesho hayo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali ni kiashiria kuwa serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuwezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata fursa ya kutangaza biashara zao na kutafuta masoko.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alipongeza wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kwa kuwa na bidhaa zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu.

Katika hatua nyingine, alipongeza wajasiriamali wanawake na vijana kwa kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali).

“Biashara ndogo zinafanywa zaidi na Wanawake na Vijana jambo ambalo ni muhimu na katika maonesho haya Zaidi ya asilimia 60 ya wajasiriamali walioshiriki ni wanawake ambapo tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya mapato yatakayopatikana katika biashara zao zitasaidia familia na kutatua changamoto mbalimbali,” alieleza

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa

maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) yamechangia kwa kiasi kikubwa kudumu kwa umoja na mshikamano wa jumuiya hiyo.

“Ni vyema kuendelea kuwaunga mkono na kuwashukuru Viongozi wetu kwa kutuletea mfumo huu wa ufanyaji biashara ambao umewaunganisha wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa wamoja,” alisema Waziri Mhagama

Pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kutumia kama nyenzo ya kubadilishana ujuzi ili kupunguza tatizo la ajira kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nimetembelea mabanda mengi katika maonesho haya na nimefurahishwa na teknolojia ya mashine zilizopo katika banda la Kenya, ninaamini kwamba tukiamua sisi watanzania kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kufundisha vijana kutengeneza mashine hizo tutawawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel alisema kuwa maonesho hayo yamekuwa ni chachu kwa wakazi wa Mwanza na wananchi kutoka maeneo ya jirani kupata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kuimarisha biashara zao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Peter Mathuki amepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maandalizi mazuri na kwa namna ilivyoshirikisha vijana wabunifu katika maonesho hayo.

Read More