Friday, January 31, 2020

BUNGENI LEO TAREHE 31.01.2020

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kushoto) akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Bungeni jijini Dodoma, Januari 31, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini, bungeni jijini Dodoma, Januari 31, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Sikudhani Chikambo, Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini, bungeni jijini Dodoma, Januari 31, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula, bungeni jijini Dodoma, Januari 31, 2020. 

Read More

Thursday, January 30, 2020

SERIKALI ZA MITAA BADO ZINA WAJIBU WA KUMHUDUMIA MWANANCHI - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema licha ya kuwepo kwa ugatuaji wa madaraka (D by D), Serikali za Mitaa bado zina wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa sababu ziko karibu nao zaidi kuliko Serikali Kuu.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Bi. Ruth Mollel, kwenye kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni. Mbunge huyo alisema dhana ya ugatuaji wa madaraka inakinzana na hali halisi kwani utekelezaji wake haujaenda sawasawa kwa vile Serikali inakusanya fedha kutoka kwenye vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile kodi ya majengo na mabango.

“Wajibu wa kumhudumia mwananchi ni wa Serikali za Mitaa kwa sababu iko karibu nao zaidi. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kuwa tunashirikiana na Serikali za Mitaa kumhudumia mwananchi lakini hatujaondoa wajibu wa Serikali za Mitaa kuwahudumia wananchi,” amesisitiza.

Amesema Serikali Kuu bado inalo jukumu la kusimamia mapato na imeamua kudhibiti ukusanyaji wa mapato na imekuwa ikihakikisha mapato haya yarudi tena kwa wananchi. “Tunaporudisha kwa wananchi, tunawapelekea hao hao Serikali ya Mitaa kwa mahitaji yao ili watekeleze hilo jambo, hatujawaondolea mamlaka ya kusema tunahitaji darasa, tunahitaji kituo cha afya, tunahitaji uboreshaji wa miundombinu.”

“Tumeongeza hata taasisi kwa kuunda TARURA ili isimamie miundombinu; sasa hivi tunaenda kwenye maji, kutakuwa na taasisi ya kusimamia utoaji wa maji. Pale ambapo kuna mahitaji, Mamlaka ya Serikali za Mitaa iseme inahitaji shilingi ngapi, kwa ajili ya nini, nasi tunawapelekea, ndiyo kwa sababu leo tunaona huduma zinatekelezwa mpaka vijijini. Hii ni kwa sababu tunashirikiana na Serikali za Mitaa katika kuratibu.”

“Ule udhaifu wa usimamizi wa makusanyo, na udhaifu wa usimamizi wa matumizi ambao ulikuwa umejitokeza sasa tunaendelea kuutibu na ndiyo kwa sababu unaona wakati wote tunapokwenda huko kwenye ziara, kwanza tunauliza ukusanyaji na kama makusanyo yoyote yamehifadhiwa na matumizi yake yako sawa, na pale ambapo matumizi yanakuwa si sahihi tunachukua hatua,” amesema.


Amesema kutokana na muundo uliopo, zipo Serikali za Mitaa ambazo zina majukumu yake yaliyoainishwa rasmi na kuna Serikali Kuu ambayo pia inawajibika kuzihudumia Serikali za Mitaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema haitaleta maana endapo Serikali italazimika kutengua matokeo ya uchaguzi wote wa Serikali za Mitaa wakati wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo hayo walikuwa na fursa ya kukata rufaa.

“Chaguzi zote nchini zinatawaliwa na kanuni na sheria zake. Kila mmoja aliyeshiriki kama aliona kuna ukiukwaji wowote, alikuwa na fursa ya kukata rufaa na kama hajaridhika, alikuwa na fursa ya kwenda mahakamani,” alisema.

Alisema chaguzi zote zina sheria zake na kanuni zake na hata wakati wa kuandaa kanuni za Serikali za Mitaa, vyama vyote vya siasa vilishirikishwa katika kutengeneza kanuni zao na moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo inatoa fursa kwa yeyote ambaye hajaridhika huko anakogombea, anaweza kukata rufaa na atakapoona rufaa hiyo kwenye ngazi inayofuata haikutenda haki, aende mahakamani.

“Kwa hiyo kulichukua hili kwa ujumla ujumla, inaweza isiwe sahihi sana kwa sababu kila mmoja kule alipo, alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo fursa ya kwenda kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na utekelezaji wa jambo hilo. Na vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni ya kukata rufaa, kwa hiyo ni wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo kwenda kukata rufaa,” alisema.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Mbozi, Bw. Pascal Haonga, aliyetaka kujua kama Serikali iko tayari kurudia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kwa sababu ule uliopita uligubikwa na dosari nyingi.

“Mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, uligubikwa na dosari nyingi sana zikiwemo za wagombea kutoka vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi kufungwa kwa muda wote, hivyo kupelekea baadhi ya wagombea hasa wa upinzani kushindwa kupata fursa za kugombea. Serikali haioni kwamba ni vema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu?” alihoji.
Read More

TUTAENDELEA KUWA WAKALI KAMA MAMBO HAYAENDI - MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kukemea utendaji usioridhisha pale inapoona mambo hayaendi sawa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na Zanzibar.

Maagizo aliyoyatoawakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda, wilaya ya Kaskazini ‘A’, mkoa wa Kaskazini Unguja ni sahihi kwa kuwa yanalenga kuboresha maendeleo na kulinda wawekezaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub (BLW) katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini Serikali itaruhusu sukari inayozalishwa na kiwanda cha Sukari Zanzibar iuzwe Tanzania Bara.

Amesema alipofanya ziara Januari 18, 2020 katika kiwanda hicho, alikuta tani 3,200 zikiwa hazijanunuliwa. “Nilipofika kiwandani hapo nilikuta sukari nyingi kwenye bohari kwa madai kuwa imekosa soko. Ingawa mbunge amesema anahitaji soko la Tanzania Bara lakini mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka na kiwanda kinazalisha 6,000.”

Waziri Mkuu amesema mpango wa uagizaji sukari kutoka nje ya nchi hauko sahihi kwani wanunuzi walitakiwa kwanza wanunue sukari inayozalishwa ndani ndipo waagize nje kiasi kinachopungua.“Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hii inawavunja moyo wawekezaji wetu,” amesema.

Hivyo, amesema yeye na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ndio wenye jukumu la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba suala la viwanda limo katika utekelezaji wa ilani hiyo.

“Ninapokuta Ilani haitekelezeki popote pale nchini lazima niwe mchungu, lazima tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani na kuwahakikishia masoko na tunajua masoko hayo tunayo,” amesema.

“Pale wapo waagizaji wa sukari watatu tu, sasa kwanini wasipewe masharti rahisi ya kuanza kununua sukari ya ndani na kiasi kinachopungua ndio waagize. Lazima tulinde viwanda vyetu… halafu mtu anasema nimewachefua Wazanzibari. Hivi nimewachefua Wazanzibari ama nimewachefua wanunuzi?” amehoji.

Amesema sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika.

Waziri Mkuu amesema viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika. “Kiwanda kile kimeajiri watu 400 na Serikali inapata kodi zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”

Amesema: “Mwekezaji asipozalisha, wale wananchi hawana ajira. Asipozalisha, atakosa mishahara ya kuwalipa wafanyakazi wake. Atashindwa kulipa kodi. Kutokana na kodi hizi, tumeona maabara inajengwa Bwejuu na kituo cha mama na mtoto pale Bambi; hivyo tutakuwa wakali pale ambapo mambo hayaendi.”
Read More

SERIKALI YATOA AGIZO KWA WANAOSOMA CHINA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma China ambao wapo nchini kwa likizo wasiwaruhusu warudi hadi hapo Serikali itakapotangaza.

Hatua hiyo inatokana na China kukumbwa na mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. “Tunawasihi watoto wasirudi hadi hapo tutakapopata taarifa za kidiplomasia kuhusiana na maendeleo ya ugonjwa huo.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mheshimiwa Cosato Chumi katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na homa hiyo pamoja na baa la nzige.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni kweli China kuna mlipuko wa homa hiyo ya mapafu ambayo hadi sasa imepoteza maisha ya watu wengi na tayari baadhi ya nchi jirani nazo wananchi wake wameanza kupata maambukizi. “Watoto wasirudi hali ikikaa vizuri warudi China kuendelea na masomo na ikiwa vinginevyo Serikali itatafuta utaratibu mwingine.”

Amesema tayari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameshatoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo na aliwahakikishia Watanzania kuwa homa hiyo haijaingia nchini.

Waziri Mkuu amesema: “Katika kukabiliana na homa hiyo, Serikali imejipanga kwa kuimarisha mawasiliano na ubalozi wetu huko China ili kujua hali inaendeleaje, na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki anafanya kazi hiyo ya kutoa mrejesho wa kila siku wa hali ilivyo huko.”

Amesema licha ya kutuma mrejesho, pia Balozi huyo anafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Watanzania kwa kutafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza ugonjwa huo na kuwaelimisha Watanzania waliopo nchini China namna ya kujikinga na homa hiyo.

Akizungumzia baa la nzige lililoikumba nchi jirani ya Kenya, Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Serikali imeshachukua tahadhari ambapo Wizara ya Kilimo ya Tanzania inashirikiana na ya Kenya kumaliza tatizo hilo. Pia amewataka wananchi wanaoishi kwenye mikoa, wilaya na vijiji vilivyo mipakani, watoe taarifa mara watakapowaona wadudu hao.

Read More

WAZIRI MKUU AKIJIBU MASWALI YA PAPO KWA PAPO BUNGENI LEO 30.01.2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Katimba kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Januari 30, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mbunge wa Momba, David Silinde kwenye viwanja vya bunge jijini Dodoma, Januari 30, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mbunge wa Momba, David Silinde kwenye viwanja vya bunge jijini Dodoma, Januari 30, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa  (kushoto) kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Januari 30, 2020. Kulia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi,  Jaku Ayoub. 




Read More

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI WAFANYABIASHARA WA MADINI WANAOFUATA SHERIA WALINDWE-MAJALIWA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinawalinda wafanyabiashara wa madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata sheria na kujiepuka kamata kamata zisizo na tija.

“Katika kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu.”

Ametoa agizo hilo leo (Jamapili, Januari 26, 2020) wakati akifunga semina ya ushiriki wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatakiwa vitumie Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuviagiza vyombo vya Dola kusimamia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha kuwa masoko yote ya madini  nchini yanalindwa.

“Nyote mtakubaliana nami kwamba kila taasisi ina utaalamu na wataalamu wake. Kwa hivyo, hatunabudi kufanya kazi kwa kuheshimu na kutambua utaalamu ama taaluma za wengine tunaoshirikiana nao.” 

“Sasa ni vema tukaondoa tofauti zetu na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuimarisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali madini. Aidha, tutambue kuwa kuna nyakati hatuhitaji kutumia nguvu nyingi bali ushauri tuu ili kutatua changamoto husika.”  

 Waziri Mkuu ameelekeza kwamba kuanzia sasa  wadau wote wanaopatikana na madini wapewe utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza madini hayo badala ya kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni. 

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa yote ya Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema walikosa msaada wa kitaalamu. “Ni wajibu wetu sote kama watumishi wa umma kujenga mazingira rafiki ya kazi, kuaminiana na kufanya kazi kwa ushirikiano.” 

Wakati huo huo,Waziri Mkuu amesema kuazia sasa suala la migodi kutegemea bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi lifikie ukomo kwa kuhakikisha kuwa, kila huduma inayohitajika migodini, inapatikana nchini. 

Waziri Mkuu amesema nchi inawajibu wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa madini kwa maana ya kutoa huduma kwa ubora stahiki na kwa wakati muafaka. 

Amesema sekta ya madini inazalisha ajira ila kuna changamoto ya ubora wa ajira, mishahara na stahiki katika kazi zinazofanana na suala la unyanyasaji wa wafanyakazi. 

Waziri Mkuu amesema masuala mengi hapo yanaweza kuonekana haraka kwenye maeneo yao ya kazi, hivyo ni vyema wakawa na taarifa hizo kwa wakati na kuwasilisha kwa wahusika ili mambo yawekwe sawa na kuipeleka sekta mbele.  

Akizungumzia kuhusu suala la unyanyasaji wa wafanyakazi wazalendo amesema si suala la kufumbiwa macho kama ilivyo suala la usalama wa watenda kazi katika migodi.  

Kadhalika, suala la udhibiti wa wageni kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania wenzetu pia ni jukumu letu na hivyo ni wajibu wetu kusimamia mikataba tuliyoingia na wawekezaji hususani eneo  la urithishaji wa madaraka na ujuzi kwa wazawa. 

Kwa upande wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Waziri Mkuu amewaagiza watafute suluhu ya changamoto ya usalama wa wafanyakazi kipindi wakiwa kazini na baada ya kumaliza muda wa kazi kwa hiari au kwa kustaafu au kumaliza mkataba. “Tumepokea malalamiko mengi sana katika eneo hilo.” 

“Hivyo, ni wajibu wetu kushirikisha wadau wote wanaohusika na masuala ya ajira, bima za wafanyakazi, afya za wafanyakazi na usimamizi wa stahiki za wafanyakazi kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto hii ili isiendelee kukomaa.”

Vilevile, Waziri Mkuu ameagiza suala la utunzaji wa mazingira liwekewe mkazo wa kipekee maana nje ya mazuri yote yaletwayo na Sekta ya Madini, uharibifu wa mazingira unaweza kugharimu maisha ya binadamu, wanyama na mimea. 

Waziri Mkuu amesema “mazingira yetu ndio uhai wetu sisi na vizazi vijavyo, hivyo ni wajibu wetu kama Wizara kuhakikisha wawekezaji wetu ni watu wema kwa mazingira yetu.” 

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu mkubwa alioufanya ambao umeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya madini.

“Hili linadhihirishwa na kitendo cha utiaji saini makubaliano ya uanzishwaji wa Kampuni ya Twiga Minerals uliofanywa juzi Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Januari 2020 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017.”

Awali, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja kwenye masuala ya usimamizi wa sekta ya madini nchini.

Alisema suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini linafanyika kwa kushirikiana kati Wizara ya Madini na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwamba wanaendelea kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kutuma salamu kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa madini bandia pamoja na wanaotaka kuuza madini nje ya mfumo kuwa zama zao zimekwisha.

Read More

Wednesday, January 29, 2020

KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA MIKOA YA MRADI BOMBA LA MAFUTA ZASHAURIWA KUUWEKA MRADI KWENYE MPANGO WA KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MAAFA.






Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa Maafa katika  mikoa 8 na vijiji 184  vinavyopatikana   katika wilaya 24 zilizopo katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, ambapo Mradi wa Bomba la Mafuta utatekelezwa kuuweka Mradi huo katika Mipango yao ya kujiandaa na kukabiliana na Maafa ili kuhakikisha mradi huo hauthiriwi na majanga yanayoweza kutokea.

Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha majukumu ya  kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika, Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji  wilaya au mkoa, pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika.

Akiongea mara baada ya kutembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amefafanua kuwa Kamati za maafa zinalo jukumu la kuchukua tahadhari ya namna ya kuhakikisha majanga yanayoweza kuuathiri mradi huo yanakuwa katika mipango yao ya menejimenti ya maafa ili faida zitakazotokana na utelelezaji wa mradi huo zinakuwa endelevu.

Kwa upande wake,  Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa watanzania hivyo ni dhahiri kuwa eneo la Chongoleani litakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zitakuwa zikiendeshwa, kwa kuwa wananchi ni wadau wa menejimeti ya maafa kupitia kamati za menejimenti  za maafa kuanzia ngazi ya vijiji, wataendelea kuelimishwa juu ya majanga  yanayoweza kuuathiri mradi huo ili waweze kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Tovuti rasmi ya Kampuni inayojenga mradi huo, East African Crude Oil Pipeline www.eacop.com. Kampuni hiyo inabainisha kuwa wanao mpango unaohakikisha utelezaji wa mradi huo unazingatia majanga na maafa wakati wa kupanga, kujenga na kuendesha Bomba, ambapo Mpango huo unahakikisha kwamba, katika tukio la dharura linaloweza kutokea, hatua za haraka, zinachukuliwa.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi unatekelezwa kwa ubia wa ujenzi na uendeshaji kwa kushirikisha kampuni za Total ya Ufaransa, CNOOC ya China, Tullow ya Uingereza na Serikali za Tanzania na Uganda. Mafuta ghafi yatasafirshwa kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania. Mradi wa Bomba hilo una umbali wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 298 zitakuwa nchini Uganda, na kilometa 1,147 zitakuwa nchini Tanzania.
MWISHO.
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akisisitiza umuhimu wa Mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa ya Mikoa linakopita Bomba la Mafuta, kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri Mradi huo, wakati alipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa. 
Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto, akimueleza Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe umuhimu wa Mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa wa Mkoa huo linakopita kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri Bomba la Mafuta ,  wakati walipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa.
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe na  Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto, wakisoma Jiwe la uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la mafuta, wakati walipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa na kushauri mipango ya menejimenti ya maafa ya mikoa linakopita bomba hilo  izingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri mradi huo.
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akiangalia sehemu ya peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga wakati alipotembelea eneo la utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta, ambapo ameshauri mikoa linakopita Bomba hilo kuzingatia Mradi  huo katika mipango ya menejimenti ya maafa kwa athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri mradi huo.


Read More

Tuesday, January 28, 2020

BUNGENI LEO 28.01.2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Manonga, Seif Khamis Gulamali, Bungeni jijini Dodoma Januari 28, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf  Masauni (kushoto) na Mbunge wa Manonga, Seif Khamis Gulamali Bungeni jijini Dodoma, Januari 28, 2020.

Read More

BUNGENI LEO TAREHE 28.01.2020

Wanakwaya wa Bunge  wakiimba Wimbo wa Taifa wakati Spika wa bunge, Job Ndugai  alipoafungua Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge jijini Dodoma, Januari 28, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Bungeni jijini Dodoma, Januari 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Bungeni jijini Dodoma, Januari 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Kuteuliwa, Janet Masaburi, Bungeni jijini Dodoma, Januari 28, 2019.
Spika wa Bunge, Job Ndugai  (wa pili kulia) akimvalisha Joho, Spika  wa bunge Mstaafu, Pius Msekwa katika hafla ya kukabidhi majoho kwa Maspika Wastaafu iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma, Januari 28, 2019. Kulia ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa bunge Job Ndugai  (aliyekaa wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Maspika na Mawaziri Wakuu wastaafu katika hafla ya kukabidhi majoho kwa Maspika wastaafu iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma, Januari 18, 2019.  Waliokaa kutoka kushoto ni Mbunge wa Urambo, Magaret Sitta ambaye pia ni Mke wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sitta, Spika wa Bunge Mstaafu, Pius Msekwa na kulia ni Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda. Waliosimama ni Maziri Wakuu Wataafu, kutoka kushoto ni Frederick Sumaye, Edward Lowassa na John Malecela.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana  na wananchi kutoka Urambo walioambatana na mbunge wao, Margaret Sitta katika hafla ya kukabidhi majoho kwa Maspika wastaafu iliyofanyika Bugeni jijini Dodoma, Januari 28, 2019.


Read More

Monday, January 27, 2020

WAZIRI KAIRUKI ATIKISA WILAYA 6 ZA MKOA WA PWANI, AWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI.

NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki amewahakikishia wafanyabiashara na Wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya Uwekezaji nchini.
Pia, Amesema Serikali imejipanga kuboresha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali zenye tija katika kuliingizia pato taifa.
Ameyasema hayo hivi karibu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 6 katika Wilaya 6 za mkoa wa Pwani ikiwemo; Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga, Mafia na Rufiji pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Akieleza lengo la ziara hiyo Mhe.Kairuki amesema mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali; Uvuvi, kilimo na ufugaji na amefanya  ziara hiyo ili kujionea mazingira  pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akitoa majumuisho ya ziara hiyo Mhe. Kairuki amezitaja changamoto zilizojitokeza katika maeneo mengi aliyotembelea kuwa ni ukosefu wa maji ya kutosha, ubovu wa barabara, ucheleweshwaji wa vibali vya kazi, kukosa umeme wa uhakika na utitiri wa tozo.
Mbali ya changamoto hizo, Mhe. Kairuki ametaja vikwazo vingine kuwa ni kutotengwa kwa maeneo ya uwekezaji, Taasisi wezeshi kutokuwa karibu na wawekezaji, ukosefu wa mitaji ya uhakika na utoaji wa adhabu zisizo za lazima.
Ameongeza kuwa uelewa mdogo wa wawekezaji katika kujiunga na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ni moja ya  changamoto na kuwataka  wawekezaji kwa hiari yao waone umuhimu wa kujiandikisha katika kituo hicho ili kutumia fursa zinazopatikana.
“Wawekezaji tunawakaribisha TIC ili mjue fursa ziliopo nchini zaidi na kuona namna mnavyoweza kunufaika na kituo hiki,”alisisitiza Waziri Kairuki.
Ameongoza kuwa, ipo haja ya kila Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ili kutoa fursa zaidi kwa watu kuwekeza na kuhakikisha miundombinu muhimu inakuwepo.
“Natoa rai kwa kila Halmashauri kuhakikisha kila kijiji kinatenga walau heka 20 za maeneo ya uwekezaji na kuwasilisha taarifa zao TIC” alisema Waziri.
Aidha, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji kuzingatia sheria na taratibu za uwekezaji nchini ili waweze kunufaika na mitaji yao waliyowekeza.
“Endeleeni kuwekeza pasipo kuvunja sheria na kanuni zilizopo ikiwa ni kulipa kodi au kulipa vibali mbalimbali mfanye hivyo tena kwa wakati ili isitokee mmewekeza kwa mitaji mikubwa halafu ikawa kwa hasara,”alisisitiza Waziri Kairuki
Aliwahakikishia wawekezaji kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua mchango wao na imedhamiria kuhakikisha inaboresha miundombinu muhimu ikiwemo uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika, barabara bora, upatikanaji wa maji safi, kuboresha mifumo ya mawasilino na upatikanaji wa huduma bora za mamlaka zinazosimamia masuala yanayohusu uwekezaji nchini.
AWALI
Waziri Kairuki alifanya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa siku 6 na kuzitembelea  Wilaya 6 ambapo jumla ya viwanda 22 alivifikia ikiwemo; Kiwanda cha KEDS, EUROPLASTIC, Samaki investment, KAMAL LTD, Hiill Packaging Company, Tan Choice, Global Packaging Ltd, Hester Bioscience Africa ltd, Chilambo Investment, Sabai Cash nut Processing, SHAFA Investment, Everwell Cable, Ice Drop ltd, Lodhia Group ltd, Waja Mabati na Waja General, Abajuko Enterprises, Tanpesca na kiwanda cha maziwa cha Mather Dairies. Aidha alipata fursa ya kutembelea mashamba ya uwekezaji mbalimbali pamoja na Shamba la Utunge, Sah janand, shamba la Utamaduni, Kigomani na shamba la kuku la AKM.
Wawekezaji wa maeneo hayo walipata fursa za kueleza changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na mapendekezo kwa Serikali ya namna bora ya kuendelea kuwa na ushirikiano ili kufikia dhamira ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na timu aliyoongozana nayo katika ziara yake wakiangalia namna ya ufugaji wa samaki wa kisasa katika shamba la samaki la Utunge lililopo Rufiji mkoa wa Pwani, anayetoa maelezo ni Meneja wa samaki wa shamba hilo Bw. Abdallah Mtutuma.
Mshauri mwelekezi wa Shamba la Utunge Bw. Uwesu Msumi akitoa maelezo ya uwekezaji wake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea shamba hilo lililopo katika Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili shambani hapo.
Mshauri mwelekezi wa Shamba la Utunge Bw. Uwesu Msumi akiwasilisha taarifa ya shamba hilo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea katika Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani kukagua mazingira ya wawekezaji nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na timu yake wakiwa katika shamba la Utunge lililopo katika eneo la Rufiji mkoa wa Pwani, wakati wa ziara yake.
Muonekano wa moja ya bwawa la kufugia samaki kati ya mabwawa 30 yaliyopo katika shamba la Utunge Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo akiwasilisha taarifa ya wilaya yake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea katika Shamba la Utunge lililopo kijiji cha Utunge Wilayani humo ili kukagua maeneo ya uwekezaji na kusikiliza changamoto zao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mwenye t-shirt ya pink) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa shamba la Utunge pamoja na timu aliyoambatana nayo katika ziara yake, mara baada ya kutembelea maeneo ya uwekezaji huo.


Read More

KATIBU MKUU TIXON AONGOZA KIKAO CHA KUJADILI UJENZI WA MAJENGO YA OFISI ZA WIZARA AWAMU YA PILI ENEO LA MTUMBA



Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Bw. Tixon Nzunda akizungumza neno la ufunguzi wakati wa kikao kazi cha wadau wa ujenzi walipokutana Januari 27, 2020 kujadili mpango kabambe wa Ujenzi wa Ofisi za Wizara Awamu ya Pili katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.Kikao kilifanyika katika Ukimbi wa Mkutano wa ofisi yake Dodoma, wa kwanza kushoto ni Katibu wa kikosi kazi cha kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga akichangia jambo wakati wa kikao kazi cha wadau wa ujenzi walipokutana Januari 27, 2020 kujadili mpango wa Ujenzi wa Ofisi za Wizara Awamu ya Pili katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.
Sehemu ya  wajumbe wa kikao cha kujadili mpango kabambe wa ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali kwa Awamu ya Pili wakifuatilia hoja za kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kujadili mpango kabambe wa ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali kwa Awamu ya Pili wakifuatilia hoja za kikao hicho.

Read More