Sunday, August 25, 2019

MAJALIWA AENDA JAPAN KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Agosti 25, 2019 ameondoka nchini kwenda Japan kwa ziara ya kikazi ya siku saba. Pichani, Mhe. Majaliwa akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako (kushoto)  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.  Avemaria Semakafu (wapili kushoto) kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  kabla ya kuondoka.

Read More

Friday, August 23, 2019

WAZIRI MKUU: ZIARA MKOANI LINDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Rutamba, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Wananchi wa Kata ya Rutamba, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.


Read More

Thursday, August 22, 2019

MATUKIO KATIKA PICHA VIJANA MKOANI GEITA WAPATIWA ELIMU YA UJASIRIAMALI

Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Silas Daudi akitoa mada kuhusu Mpango wa Biashara kwa vijana wanajihusisha na shughuli mbalimbali za biashara na ujasiriamali katika Mkoa wa Geita ikiwa ni awamu ya tatu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 yanayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Baadhi ya Wajasiriamali wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa na mmoja ya watoa mada wakati wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Julius Tweneshe akielezea mada kuhusu taratibu za kufungua kampuni wakati wa mafunzo hayo.
Sehemu ya wajasirimali kutoka Mkoa wa Geita wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Afisa Uwezeshaji kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bw. Halidi Mbwana akitoa mada kuhusu masuala ya utafutaji wa vyanzo vya mapato kwa vijana walioshiriki mafunzo hayo Mkoani Geita.
Baadhi ya Wajasiriamali walioshiriki kwenye mafunzo hayo wakijadiliana kazi kwenye vikundi.
Sehemu ya Sekretarieti wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wawezeshaji wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Geita Agosti 22, 2019.


Read More

Wednesday, August 21, 2019

UN YAIPONGEZA TANZANIA KWA MATUMIZI MAZURI YA RASILIMALI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,anaye maliza muda wake hapa Nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez kwa ajili ya kumuaga Waziri Mkuu  Ofisini kwake ,Magogoni jijini Dar es Salaam leo Agosti 21,2019.

UMOJA wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za ndani na hivyo kuiwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.

Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumatano, Agosti 21, 2019) na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Mratibu huyo Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu, amesema kuwa Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.

“Katika kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na taasisi zake nchini.”

Katika hatua nyingine, Bw. Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza kuandaa na kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu.

Mbali na kuisifu Serikali pia kiongozi huyo amevipongeza vyombo vya habari kwa jinsi vilivyoshirikiana na Serikali kuripoti matukio mbalimbali ya mkutano huo. “Nawapongeza na wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wote wa mkutano wa SADC.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemshukuru kiongozi kwa pongezi alizozitoa ambazo ni ishara kwamba anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kutumia vizuri rasimali zake.

Waziri Mkuu amesema “maelezo yaliyotolewa na Bw. Rodriguez yanaakisi kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Tanzania si nchi masikini na inayo uwezo wa kutoa misaada kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo. Watanzania waendelee kuiunga mkono Serikali yao.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kiongozi huyo kwani alikuwa kiungo kizuri kabaina ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. Pia atakumbukwa sana kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kipindi cha utumishi wake nchini Tanzania.

Awali, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Balozi Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania.

Waziri Mkuu alimpongeza Balozi huyo kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa Serikali ya Tanzania katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo za kiuchumi, elimu, afya, maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya nchini mbili hizo.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mseleku ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa uliompatia katika kipindi chake cha utumishi akiwa nchini na kwamba alitamani aendelee kubaki Tanzania.

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Balozi wa Afrika Kusini, Thamasanqa Dennis Mseleku   kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania amekutana naye   ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam leo Agosti 21.2019.
Read More

Friday, August 16, 2019

TUPO TAYARI KUSHIRIKIANA NA AFRIKA KUSINI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Amesema Tanzania inahitaji uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususan katika kipindi hiki ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati..

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 16, 2019) wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro.

Ameyasema kwa kuwa changamoto zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali zinafanana kwa kiasi fulani na zile za Afrika Kusini kwani historia za nchi hiyo na jiografia vinafana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mazimbu, Waziri Mkuu amesema kuwa lina uhusiano mkubwa na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.

Waziri Mkuu amesema eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

“Mheshimiwa Rais, Tanzania ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele (Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”. 
                                                       
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sera za ubaguzi wa rangi zilikoma mwezi Februari 1994 na kufuatiwa na uchaguzi huru na wa haki uliopelekea kupatikana kwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Hayati Mzee Nelson Mandela mwezi Mei 1994.

“Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote tutawakumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyerere na Hayati Mzee Nelson Mandela kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya umoja katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”.

Amesema misingi imara iliyojengwa na wazee wetu hao, imekuwa chachu ya ushirikiano kwenye majukwaa ya Kimataifa hususani katika kupambana na ubaguzi wa kiuchumi na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema namna pekee ya kuwaenzi viongozi wetu hao ni kuendelea kujenga umoja na kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa ulioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.

Rais huyo wa Afrika Kusini amesema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Serikali Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza teknolojia.

Pia amesema watairisha chuo cha SUA kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ili kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa. “Tutaboresha na shule katika eneo hili na kuweka utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika Kusini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.”

Rais Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na Waziri Mkuu. Kisha alitembelea campus ya Solomon Mahlangu na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.

Pia kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo alitembelea campus ya Mazimbu na kujionea sehemu ambazo waliishi wapigania uhuru wa nchi yake na kisha aliweka shada la maua kwenye makaburi ya wapigania uhuru. Ameondoka uwanja wa ndege wa Morogoro na kuelekea jijini Dar es Salaam saa 1.59 mchana.(mwisho)
Read More

RAMAPHOSA ,ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA SOKOINE(SUA)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, wakati alipowasili katika Mkoa wa Morogoro, akiwa kwenye ziara ya Kiserikali nchini. Agosti 16.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro, kabla ya kumkaribisha Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa kuzungumza. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akizungumza na wananchi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoroalipotembelea Kampasi hiyo. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiwa amesimama katika moja ya picha ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini, kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akizungumza na mwenyeji wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwasili katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiwa kwenye picha ya pamoja, kwenye ofisi ya Utawala, iliyotumika na Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019. 
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akifafanuliwa jambo kwenye moja ya jengo la Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiangalia moja ya kaburi la Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakiangalia makaburi ya Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, katika kambi ya Mazimbu mjini Morogoro. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akipanda mti, wakati alipotembelea Kambi ya iliyotumika na Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, iliyopo Mazimbu mjini Morogoro. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiweka shada la mauwa, katika mnara wa kumbukumbu ya Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, wakati alipotembelea Kambi ya iliyotumika na Wapigania Uhuru hao, iliyopo Mazimbu mjini Morogoro. Agosti 16.2019.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, baada ya kutembelea Kambi ya Mazimbu, mkoani Morogoro, akiwa kwenye ziara ya Kiserikali nchini. Agosti 16.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).. Agosti 16.2019.


Read More

Wednesday, August 14, 2019

WAZIRI MKUU AZINDUA MWONGOZO WA UWEKEZAJI KAGERA


*Azitaka halmashauri nchini kuondoa urasimu, vikwazo kwa wawekezaji

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwaamezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kagera wenye lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji na hivyo, kukuza maendeleo ya mkoa huona ameziagiza halmashashauri zote za wilaya nchini ziondoe urasimu na kupunguza vikwazo kwa wawekezaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 14, 2019) wakati akizindua Kongamano la Wiki ya Kagera na Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Kagera, lilifanyika Bukoba mjini.Amewataka Watanzania wahakikishe wanachangamkia fursa za biashara zilizopo. 

Amesema Watanzania wanao uwezo wa kutumia fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini kwa kushirikiana na taasisi za kifedha na kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini, badala ya kuachia fursa hizo kuchukuliwa na wageni.

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kukuza uchumi kupitia sekta ya na kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025 itaendelea kutekelezwa, hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nje nao waje kuwekeza.

“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda Awamu ya Tatu (2010/2020) na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/2016 2020/2021) ambao lengo lake ni kuendeleza uchumi wa viwanda”.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Uwekezaji Kagera, Waziri Mkuu amesema yamelenga kuwakutanisha wadau wa uwekezaji, ambao ni pamoja na Wafanyabiashara kutoka ndani ya mkoa na nchi jirani zinazozunguka Mkoa wa Kagera.
“Ni ukweli usiofichika kwamba tunahitaji wawekezaji watakaosaidia uchumi wa mkoa huu kukua kwa kasi kupitia fursa zilizopo kwenye nyanja za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, maliasili na utalii”. 

Waziri Mkuu amesema ukuaji mzuri wa uchumi wa mkoa utakuwa na manufaa katika kuongezeka kwa pato la mwananchi wa Kagera, pato la mkoa na hata pato la Taifa nalo litakuwa kwa kasi ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Amesema mkoa wa Kagera ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa kahawa nchini, ambapo zaidi ya nusu ya kahawa yote huzalishwa katika mkoa huo. Wastani wa uzalishaji wa kahawa kwa mwaka ni kati ya tani 50,000 hadi tani 65,000 kutegemea na hali ya hewa ya mwaka husika. 

Hivyo, mkoa huo una fursa kubwa ya uwekezaji kwenye viwanda vya kukoboa na kusindika kahawa.Pia mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa michache Tanzania yenye fursa nyingi za uwekezaji ambazo kwa namna moja au nyingine hazipatikani katika mikoa mingine ya nchini. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na soko kwani unapakana nan chi nne za Afrika Mashariki.

“Kagera imepakana na Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya. Kupakana na nchi hizo zenye idadi kubwa ya watu katika ukanda huu wanaokadiriwa kufikia takriban milioni 190 ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018 ni fursa ya uwepo wa soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa au zinazoweza kuzalishwa katika mkoa wa Kagera”. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafiri ukiwemo wa anga na wa barabara ili kurahisisha usafiri kutoka Bukoba makao makuu ya mkoa wa Kagera kufika katika nchi hizo. 

“Kwa mfano, umbali kutoka Bukoba hadi Kampala ni km. 340, Bujumbura km. 550 na Kigali km. 490. Kadhalika, itakuwa ni rahisi kufikia masoko ya nchi za Sudan Kusini pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC)”.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema dhamira ya kuandaliwa kwa wiki ya uwekezaji mkoani Kagera ina lengo la kuhakikisha kwamba mkoa huo unafanya vizuri katika sekta ya uwezekezaji na biashara, hivyo kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Alisema mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo inamchango mdogo katika pato la Taifa, hivyo wanataka watoke kwenye kuchangia asilimia 3.9 hadi wafikie asilimia 10.

Kwa upande wao, viongozi mbalimbali wakiwemo Magavana kutoka na wafanyabiashara kutoka nchi za Rwanda na Burundi waliahidi kutumia fursa zilizopo nchini, pamoja na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza katika nchi zao.(mwisho)
Read More

Sunday, August 11, 2019

MAJALIWA AZUNGUMZA NA WAOMBOLEZAJI WA VIFO VYA WATU WALIOFARIKI DUNIA KATIKA JALI YA LORI LA MAFUTA MOROGORO

Baadhi ya waombolezaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kushiriki katika maadalizi ya kutambua miili na mazishi ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji  wakati aliposhiriki  katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto  katika  eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.
Baadhi ya waombolezaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kushiriki katika maadalizi ya kutambua miili na mazishi ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji  wakati aliposhiriki  katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto  katika  eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya Mawaziri na viongozi wa mkoa wa Morogoro walioshiriki katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alikuwa  kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Morogoro, Innocenti Kalogelisi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephene Kebwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe na kulia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.

Read More

WAZIRI MKUU AUNDA TUME KUCHUNGUZA AJALI YA MOROGORO


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameunda tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 hadi mchana huu na wengine 70 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka, mjini Morogoro.

“Hii tume inaanza kazi leo (Jumapili, Agosti 11, 2019), Hadi ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii si mara ya kwanza ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi Watanzani pale gari linapoanguka tusitume kama fursa twende tukaokoe binadamu waliopo pale”.

Waziri Mkuu ameunda tume hiyo leo (Jumapili, Agosti 11, 2019), wakati akizungumza na waombolezaji waliofika katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao. Niko mbele yenu nikimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli aliyenituma kuja kuungana nanyi kwenye siku hii ya huzuni”.

Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake kwa sababu ajali imetokea saa mbili asubuhi katikati ya mji, hivyo tunataka kujua ajalj ilipotokea kila mmoja alitumiza jukumu lake.

Amesema ajali imetokea karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi na kuna polisi sasa je hawa wananchi waliopata ajali walienda na madumu ya kuchotea mafuta inamaana waliamka asubuhi wakijua ajali itatokea. “Najua pale ajali inapotokea trafiki wana wahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia.Je lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani”.

Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe ndani ya Serikali kama wamewajibika. “Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake. Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu. Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika kuwapoteza Watanzania”.

Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha kwamba zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, Rais Dkt. Magufuli tayari ameshatoa kibali cha kutolewa fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa zinazohitajika.

Akizungumzia kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo inatangazwa kupitia vyombo mvalimvali vya habari, Waziri Mkuu amesema ni vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Stephen Kebwe.

“Kwenye vyombo vya habari tuelewane kwenye takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini yake. Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyinginyingi mnajenga hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa mtafuteni mkuu wa mkoa”.

 Wakati Huo huo, amesema Rais Dkt. Magufuli alipokea taarifa mapema ya ajali ya lori la mafuta na kusababisha vifo vya Watanzania 69, ambapo alimtaka aende mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwasilisha salamu za pole kwa wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kufuati tukio hilo la kuhuzunisha.

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawaombea marehemu na majeruhi lakini pia amawataka wafiwa na wananchi wote wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao.

“Mheshimiwa Rais amehuzunishwa sana na msiba huu ndio maana amenituma nilete ujumbe huu kwenu.Lakini pia nimekuja na salamu za pole kutoka kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Jambo hili si dogo ni kubwa kwani tumepoteza ndugu zetu wengi. Kwa idadi hii kubwa ya ndugu zetu waliotangulia mbele za haki na wale waliopo kwenye maumivu si jambo la faraja”.

Waziri Mkuu amesema wananchi wasipeleke miili kwanza makaburini ili waweze kupitia na kutambua ndugu na rafiki kwa ajili ya  kuwa na kumbukumbu ya kudumu. “Hali si nzuri ndugu zetu wameungua sana wapo wengine mnaweza msiwatambue lakini mnaweza kutambua kwa alama. Wapo wengine walivaa bangili, heleni, mkanda havijaungua”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kama hawajawatambua Serikali imeweka utaratibu wa vipomo vya vinasaba, ambapo  kumbukumbu hizo zimechukuliwa na wataalamu wetu wa afya. “Kama ukipita ukishindwa kumuona bado tunakuruhusu kukupima vinasaba na kulinganisha na vyakwako. Bado haki ya kumpata ndugu yako iko pale pale madaktari wapo, mitambo ipo tutachukua vinasaba na kuainisha tutatoa nafasi leo hadi saa 10 kufanya utambuzi”.

Amesema Serikali inaratibu vizuri jambo hilo lakini kuanzia saa 10 itaruhusu wale waliotambuliwa kuchukua mwili lakini kama hawajajipanga vizuri itauzika na kama kuna jina litaliandika na kama hakuna jina wataandika namba ya vinasaba ili kutoa fursa kwa ndugu siku nyingine waende wakapimwe na kuoneshwa kaburi la ndugu yao.

 (mwisho)
Read More

MAJALIWA AWAJULIA HALI MAJERUHI WA AJALI YA MOTO WA LORI LA MAFUTA LILILOPINDUKA MOROGORO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole , Shukuru Fabian ambye ni mmoja wa majeruhi wa ajali ya moto wa lori la mafuta lililopinduka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro. Aliwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo kwenye hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimjulia hali, Hans Kifah ambaye ni mmoja wa majeruhi wa ajali ya moto wa lori la mafuta lililopinduka kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Aliwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo kwenye hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.

Read More

MAJALIWA AZUNGUMZA KATIKA IBADA YA KUWAOMBEA MAREHEMU WA AJALI YA MOTO WA LORI LA MAFUTA LILILOANGUKA ENEO LA MSAMVU MJINI MOROGORO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali ya moto wa lori la mafuta lililoanguka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro. Ibada hiyo ilifanyika  kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019.

Read More

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS MAZISHI YA WALIOKUFA KWA AJALI MORO

*Huzuni, simanzi, majonzi na vilio vyatawala mjini Morogorogo


HUZUNI, simanzi, majonzi na vilio vimetawala mjini Morogoro leo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwaakiongoza umati wa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 71 huku wengine 59 wakijeruhiwa.

Mazishi hayo yameanza kufanyika leo (Jumapili, Agosti 11, 2019) katika eneo la makaburi la Kola Hill mjini Morogoro ambapo Waziri Mkuu amemwakilisha Rais, Dkt. John Magufuli. Ametoa pole kwa wafiwa wote na amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo.

Akizungumza na wananchi katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro iliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliouonesha wakati huu wa amajonzi.

Kufuatia ajali hiyo iliyotokea jana saa 2 asubuhi baada ya lori lenye shehena ya mafuta ya petrol kupinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki. Rais Dkt, Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa kuanzia jana Jumamosi Agosti 10,2019 na bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isac Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Morogoro.


(mwisho)
Read More