Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kaspar Mmuya (katikati)
akiwa kwenye picha ya pamoja watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Halmashauri
ya Kiteto, Benki ya CRDB, NMB, SIDO na vijana walioshiriki katika mafunzo hayo
ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara yaliyofanyika katika Kituo
cha Elimu kwa Jamii (Maktaba) Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara,
Januari 6, 2022.
Na: Mwandishi Wetu – Kiteto, MANYARA
Vijana nchini wahamasishwa kuwekeza
kwenye shughuli za kiuchumi ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa
kuanzisha miradi au shughuli za uzalishaji mali zenye tija zitakazowawezesha
kuchangamkia na kusimamia ipasavyo fursa mbalimbali za kukua kiuchumi na
kuchangia pato la taifa.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kaspar Mmuya ameyasema hayo Januari 6, 2022 wakati wa Ufungaji wa Mafunzo ya
Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kiteto Mkoani Manyara.
Naibu Katibu Mkuu alieleza
kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
inasimamia utekelezaji wa afua za kushughulikia mahitaji ya makundi maalum ya
vijana wakiwemo vijana kutoka jamii ya wafugaji kama ilivyoanishwa kwenye Ibara
ya 3.25 ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, hivyo kupitia
afua hiyo vijana hupatiwa mafunzo ya ujuzi tepe kulingana na mahitaji yao
ambapo huhamasishwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali na kuunganishwa kwenye
fursa za uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia asilimia 4% ya mapato ya
Halmashauri na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana.
“Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inatambua mchango wa vijana katika kukuza uchumi wa nchi, hamasa kubwa
imekuwa ikitolewa na viongozi kwa vijana wazawa kuanzisha viwanda, makampuni na
shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zenye tija zitakazowafanya wanakuwa
kiuchumi na kujiletea maendeleo katika jamii zao,” alisema Naibu Katibu Mkuu
Mmuya
“Hapa Kiteto mnaongoza kwa
uzalishaji wa mahindi bora na alizeti, hiyo ni fursa kwenu vijana kuanzisha
viwanda vidogo vidogo vitakavyo zalisha bidhaa zinazotokana na mazao hayo,”
alisema
Alifafanua
kuwa, Serikali inatambua vijana ni kundi kubwa linalofanya nguvukazi ya taifa,
kwa mujibu wa taarifa za Shirika la
takwimu la Taifa (NBS) inakadiriwa kuwa idadi ya vijana nchini ni Milioni 17.7 sawa
na ailimia 31.5% ya Idadi ya watu wote nchini ambapo kati ya vijana 17.7 vijana
wenye uwezo wa kufanya kazi ni Milioni 14.2 Sawa na asilimia 80.3% (Ripoti ya
Matokeo ya utafiti wa Nguvu Kazi ya mwaka 2020/2021).
“Asilimia kubwa ya vijana wanaishi vijijini ambapo
wanajishughulisha na kilimo na ufugaji katika kuendesha Maisha yao, hivyo
kutokana na takwimu hizo, Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha mazingira
katika sekta ya kilimo na ufugaji ili vijana wengi waweze kushiriki kikamilifu
katika kukuza uchumi na kujiletea maendeleo,” alieleza Mmuya
Aliongeza kuwa lengo la
mafunzo haya ni kubadilisha mitazamo ya vijana katika kuchangamkia fursa
mbalimbali za kuichumi ndio maana mwitikio wa vijana katika Halmashauri ya
Kiteto kushiriki mafunzo hayo ni mkubwa sana.
“Katika Mkoa huu wa Manyara, Halmashauri
ya Kiteto ambapo mafunzo haya yamefanyika vijana wameonesha uhitaji mkubwa wa
kupatiwa mafunzo haya. Hali hii inaashiria kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu
kwa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa mafanikio na tija.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mmuya
alitumia fursa hiyo kuhimiza Halmashauri zote nchini kuwezesha vijana kiuchumi
kupitia kupitia mikopo inayotolewa kwa Vijana asilimia 4%, Wanawake asilimia 4%
na Watu wenye Ulemavu asilimia 2%.
Sambamba na hayo aliwataka Maafisa
Maandeleo ya Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweka mifumo na utaratibu
mzuri wa ufuatiliaji wa vikundi vya vijana vinavyopatiwa mikopo na Halmashauri
ili kupata matokeo yenye tija ya maendeleo ya fedha hizo za serikali
zinazotolewa moja kwa moja kwa wananchi. Pamoja na hayo amewataka vijana
kutumia fursa hiyo kujifunza kwa
umakini mkubwa ili muweze kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika
kuendesha miradi yenu na kujikwamua kiuchumi.
Pia, Naibu
Katibu Mkuu Mmuya alishukuru Shirika
la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kuendelea kusaidia jitihada
za Serikali katika kutekeleza programu mbalimbali za Maendeleo ya vijana
nchini.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Julius Tweneshe alisema
kuwa mafunzo hayo ni sehemu
ya jitihada za Serikali za kuyafikia na kuyawezesha kiuchumi makundi yote ya
vijana yanayojumuisha waliopo mijini, vijijini, wenye mahitaji maalumu ikiwemo vijana
wa kike na kiume, Vijana wanaotoka katika jamii za wakulima na wafugaji na
vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana tumeweka
mikakati ya kuwasaidia vijana kwa kuhakikisha kuwa tunayafikia makundi yote
maalumu ya vijana likiwemo kundi lenu hili la vijana kutoka kwenye Jamii ya
Wafugaji,” alisema
Akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Kiteto, Bi. Beatrice Rumbeli ambaye ni Afisa
Mipango alisema kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa katika shughuli za kuwezesha
wananchi kiuchumi ikiwemo kutoa mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na
Wenye Ulemavu.
“Katika Mwaka wa fedha
2021/2022 Halmashauri ya Kiteto ilitenga kiasi cha shilingi milioni 183 kupitia
mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya Vijana, Wanawake na Wenye
Ulemavu ambapo hadi sasa jumla ya milioni 120 zimekwisha tolewa kwenye vikundi,”
alieleza Rumbeli
Naye Kijana
Mnufaika wa Mafunzo hayo Bw. Marisix Urasa, aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu
kwa kuwapatia mafunzo hayo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara yaliyoanza
kutolewa katika Halmashauri hiyo ya Kiteto kuanzia tarehe 04 hadi 06 Januari,
2022 ambapo alieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni chachu kwa vijana katika
wilaya hiyo kubadilika kifikra kwa kuanza kurasimisha na kuboresha biashara zao.
“Sisi
vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto tunatambua Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inasimamia utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kitaifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano kuhusu kujenga uchumi shindani na viwanda kwa
maendeleo ya watu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025, hivyo sisi vijana kama nguvukazi ya Taifa tunao mchango mkubwa katika
kufanikisha jitihada hizo za Serikali na za Viongozi wetu wa nchi ili kufikia
malengo ya mpango huo,” alisema Urasa
MWISHO