Serikali imesisitiza utoaji wa
elimu kwa jamii namna ya kuzingatia masuala ya lishe nchini ili kuwa na Taifa
lenye afya bora na kujiletea maendeleo yake.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Doroth
Gwajima wakati akimwakilisha Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa wakati wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Wadau
wa Lishe nchini uliofanyika uwanja wa shule ya Msingi Mukendo Wilaya ya Musoma Mkoani Mara.
Akizugumza kuhusu Mkutano huo
alisema, umewezesha washiriki kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa afua za
lishe kwa kipindi cha mwaka wa kwanza (2021/2022) wa utekelezaji wa Mpango
Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa Lishe (2021/22 - 2025/26) na kusema kuwa
tathmini hizo ni za muhimu kwani ndio kipimo cha kujua hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa Mpango.
Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka
huu ni“KUONGEZA KASI KATIKA KUBORESHA HALI YA LISHE KWA MAENDELEO YA RASILIMALI
WATU NA UCHUMI” .
Waziri alisema katika
kutekeleza mpango Juishi wa Lishe suala la elimu lina umuhimu wa kipekee kwa
kila mmoja ili kufikia malengo.
Alifafanua kuwa Serikali
itaendelea kutoa kipaumbele juu ya jamii kupewa elimu ya namna ya kuzingatia
lishe bora ili kuweza kuepukana na udumavu kwa watoto na kuwa na afya bora.
“Ili kupata matokeo chanya
katika kuboresha hali ya lishe nchini ni muhimu kuendelea kuhamasisha jamii
kuhusu masuala ya lishe. Pamoja na uhamasishaji kufanyika kabla ya mkutano na
wakati wa mkutano huu, natoa rai kwa
Taasisi ya Chakula na Lishe na wadau wengine kuhakikisha tunabuni mikakati
zaidi ya kufikisha elimu sahihi ya lishe kwa umma ili kusaidia jamii kuelewa
changamoto,”Alisisitiza Dkt. Gwajima
Aliekeza kuwa,
upo umuhimu wa
kuwa na jitihada za makusudi ili kuhakikisha wadau wa
sekta binafsi wanashirikishwa na kuwa na utaratibu mzuri wa kuchangia
utekelezaji wa afua za lishe.
Aidha, Serikali chini ya
uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imeendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuifanya nchi
yetu kuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda ambapo alieleza kuwa
Maendeleo haya hayawezi kupatikana iwapo hatutaimarisha kasi ya kujenga na
kulinda kizazi chenye nguvu, afya njema na uwezo wa kufikiri.
Kwa upande wake Naibu Waziri
wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde aliasema Wizara yake itaendelea kutoa kipaumbele
katika kutenga fedha nyingi kwenye masuala ya lishe na kuimarisha kilimo cha
umwagiliaji ili kuchagiza ongezeko la upatikanaji wa chakula nchini.
"Uwekezaji katika kilimo
utaleta matokeo chanya katika lishe, lazima tuwekeze katika uzalishaji wa
mbegu, huduma za ugani, umwagiliaji na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ili
kufikia malengo kama yalivyotarajiwa," alisema Mhe. Mavunde
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alisema kumekuwa na chagamoto ya ulaji kwa kutozingatia kauni za lishe bora inayosababisha changamoto
za kifya kwa wengi.
“Takwimu zinaonesha kuwa
kiwango cha ulaji wa nyama kwa wastani wa mtu mmoja kwa mwaka ni kilo 15 wakati
kiwango kinachopendekezwa na FAO kwa mtu mmoja kwa mwaka ni wastani wa kilo 50,
upande wa ulaji wa samaki wastani wa kilo nane na nusu kwa mtu mmoja kwa mwaka,
kiwango hichi kipo chini kulinganisha kiwango kinachopendekezwa cha kilo 23 kwa
mtu mmoja kwa mwaka, aidha ulaji wa mayai na kuku bado si wa kuridhisha,"
alisisitiza Ulega.
Aidha wizara imeendelea kutekeleza afua mbalimbali
za kuhamasisha hali ya ulaji nchini ambapo wanahamasisha ulaji na utumiaji
mazao ya mifugo kwa kushirikina na wadau mbalimbali sambamba na kuongeza
uzalishaji nchini.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.