Friday, February 3, 2023

KATIBU MKUU KASPAR MMUYA ATETA NA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU

 


Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wametakiwa kutumia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali pamoja na Busara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Hayo yamesema na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bw. Kaspar Mmuya.

 

Bw. Mmuya alisema ameitumikia Ofisi hiyo na kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa lengo la kuleta matokeo chanya.

 

“Kwa majukumu ya Ofisi hii jinsi yalivyo yalitupa nafasi sisi wengine ya kujua wizara nyingine zinafanya nini katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ujumla,”alisema Katibu Mkuu huyo.

 

Pia amewahimiza  watumishi wa Ofisi hiyo kuishi kwa upendo na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu hatua itakayochochea maendeleo ya Taifa na shughuli za Serikali kufanyika katika hali ya ubora na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Sambamba na hilo, Bw. Mmuya alimshukuru Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu kwa kumfundisha, kumuongoza na kumpa ushirikiano wakati wote alipokuwa akitumikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu katika ofisi hiyo.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  Dkt. John Jingu alisema kuwa Katibu Mkuu Mmuya alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa matokeo hivyo  watumishi kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa  kufanya kazi kama timu katika kuitumikia Nchi, kuishi na watu vizuri.

 

 “Tujitahidi kila wakati kufanya kazi kwa matokeo, uliyaishi matokeo na unaendelea kutukumbusha tuyaishi hayo, kila mtu ana nafasi yake lakini lazima kuheshimiana na kujua umuhimu wa kuwajibika, tuendelee kufanya kazi kwa matokeo weledi ushirikino na nidhamu sisi ni timu moja tushirikiane.” Alisisitiza Dkt. Jingu.

 

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Katibu wa  TUGHE tawi la  Ofisi hiyo Bw. Dotto Kyaolang amemshukuru Katibu Mkuu Mmuya kwa kutoa dira ya utendaji kazi na kumtakia afya njema na utendaji mwema katika kituo chake kipya cha kazi.

 

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.