WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa
maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo
zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.
Amesema pamoja na uwepo wa
sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga
kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika
kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, wakati
akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa
(2022).
Nyaraka nyingine ni Mkakati wa
Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya
Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na
Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa
Makuu (2022).
Amesema miongozo na mipango
hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo
taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi
wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.
Waziri Mkuu amesema nchi bado
inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu,
hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya
kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.
“Nitoe rai kwa Watanzania
wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya
kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze
kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea
ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea
kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na
maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya
usimamizi wa maafa.
Pia, Waziri Mkuu amezielekeza
wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha
kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao.
“Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na
Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti
katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”
Waziri Mkuu amesema viongozi
hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya
hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote
zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa
msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.
Kwa upande wake, Muwakili
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi Veronica
ameihakikishia Serikali kuwa UNDP pamoja na wadau wengine wa maendeleo
wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na maafa.
Amesema nyaraka hizo
zilizozinduliwa leo zitasaidia katika upatikanaji wa taarifa za maafa kwa
wakati na hivyo kuwawezesha wahusika kuchukua hatua haraka.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.