Watendaji
wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekumbushwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa
weledi, ufanisi na kujituma ili kuhakikisha wanachangia kikamilifu katika
kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050, hususan katika maeneo ya sera,
uratibu na usimamizi wa utekelezaji wake.
Wito
huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na
Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba J.A. Kabudi, wakati akizungumza na
watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kuwasili rasmi na kupokelewa na uongozi
na watumishi wa Ofisi hiyo katika Jengo la Ngome Jijini Dodoma.
Prof.
Kabudi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubunifu miongoni mwa watumishi ili
kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
“Ni
muhimu tushirikishane mawazo na kufanya kazi kwa pamoja ili kumsaidia
Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanikisha adhima ya maendeleo
yenye kuleta ustawi na furaha kwa Watanzania," alisema Prof. Kabudi
Aliongezea
kuwa upo umuhimu wa kushikamana ili kuendelea kuimarisha utendaji wetu ili
kumwezesha Mheshimiwa Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Aidha,
Waziri Kabudi alibainisha kuwa mazingira ya kazi yenye mshikamano na mahusiano
ya kifamilia hayapaswi kuwa chanzo cha uzembe au utovu wa nidhamu, bali yawe
kichocheo cha kuongeza uwajibikaji na kufikia viwango vya juu vya utendaji.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kabudi aliwataka watumishi kuendelea kumuombea aliyekuwa
Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Marehemu William Vangimembe Lukuvi, ili
Mwenyezi Mungu amrehemu na kumpa pumziko la milele.
“Nitaendeleza,
kadri nitakavyoweza, misingi na jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wangu
katika kuijenga Ofisi hii,” aliongeza.
Awali,
Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Ummy Nderiananga, alimpongeza Prof. Kabudi kwa
kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo, akiahidi
ushirikiano wa dhati kutoka kwa watumishi wote katika utekelezaji wa majukumu
yake.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye
Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, naye alimpongeza Waziri Kabudi kwa uteuzi huo na
kusisitiza kuwa watumishi wako tayari kuongozwa na kushirikiana naye katika
kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.