Serikali
imesisitiza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele cha pekee
kwa ushiriki wa vijana katika maendeleo, kwa lengo la kuinua vipaji, uwezo, na
ari yao katika kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na
Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi,
leo jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la kwanza la kisayansi la
vijana kuhusu VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jinsia na masuala mtambuka. Kongamano
hilo limeandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Akizungumza
katika hafla hiyo, Prof. Kabudi alisisitiza kuwa dhamira kuu ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2050 ni kujenga taifa lenye nguvukazi iliyoelimika, yenye ujuzi na
maono.
"Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele kwa vijana kwa kutumia vipaji na
uwezo wao katika kufanikisha maendeleo endelevu. Nguvukazi hii itajengwa katika
misingi imara ya ubunifu, ujasiriamali, na uwajibikaji," amesema Prof.
Kabudi.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kabudi amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika
kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia na afya ya akili.
Ameeleza
kuwa, serikali imeanzisha madawati maalum ya ulinzi katika maeneo mbalimbali,
ikiwemo shuleni, vyuoni, na kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha huduma za
kinga na msaada zinawafikia wahitaji kwa wakati.
Awali,
akimkaribisha Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,
Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, amebainisha umuhimu wa
kongamano hilo kwa ustawi wa vijana.
"Kongamano
hili ni chachu ya mabadiliko ya fikra na utendaji, tunatarajia elimu
watakayopata itakuwa mwanzo wa safari ya kujenga jamii yenye afya, matumaini,
na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wao," amesema Dkt. Kilabuko.
Kongamano
hilo la siku mbili linaongozwa na kaulimbiu; ‘’Kuunganisha Sayansi na Ubunifu
katika Kukabiliana na Janga la VVU, Afya ya Uzazi na Jinsia, Kukuza Ustawi
Kuelekea Dira 2050”.
.jpeg)
.jpeg)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.