Friday, December 22, 2017

VIONGOZI 19 WA USHIRIKA WANUSURIKA KWENDA SELO



*Ni wa Vyama Vikuu vya SHIRECU, NYANZA
*Waziri Mkuu ataka wampe maelezo ya kina upotevu wa mali za mabilioni
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya Shinyanga (SHIRECU) na Mwanza (NCU) kwenda selo na badala yake amewapa siku 23 wampe maelezo yatakayomridhisha juu ya mahali zilipo mali za vyama hivyo viwili.
 
Amefikia uamuzi huo leo (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati akifunga kikao cha siku moja cha wadau wa zao la pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga. Viongozi hao wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya ushirika.
 
“Nataka kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu.
 
“Hawa nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma ifikapo Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisisitiza.
 
Kuhusu tuhuma za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza Cooperative Union - NCU), Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na 2017, kilikuwa jumla ya mali 10 ambazo ziliuzwa kinyemela katika mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi ya mali hizo zilizopo jijini Mwanza.
 
Aliwataja viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni  Murtazar Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo), Bi. Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw. Peter Ng’hingi (aliyekuwa Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa Mhasibu Mkuu - NCU), Bw. George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki - NCU) na Bw. Sospeter Ndoli (aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU).
 
Kuhusu mali za Nyanza zinazoshikiliwa na benki ya CRDB. Waziri Mkuu alisema benki hiyo inaidai NCU mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 2.123 na kwamba benki hiyo inashikilia mali 16 zenye thamani ya sh. bilioni 18.132. Alitaka vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki ya CRDB.
 
Kwa upande wa viongozi wa SHIRECU, Waziri Mkuu alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi ya sh. bilioni 11 ambazo wanadaiwa na benki ya TIB yakiwemo madeni ya mishahara ya watumishi ambayo yanafikia sh. bilioni 1.2.
 
“SHIRECU kwa sasa haina mali zozote kwa sababu mali zote zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,” alisema.
 
Aliwataja viongozi wa SHIRECU ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Bw. Joseph Mihangwa (Meneja Mkuu), Bw. Sillu Mbogo (Kaimu Mhasibu Mkuu), Bw. Maduhu Nkamakazi (Kaimu Mkaguzi wa Ndani), Bw. James Kusekwa (Kaimu Meneja Uendeshaji) na wajumbe wa Bodi ya SHIRECU.
 
Wajumbe hao wa Bodi ni Bw. Robert Mayongela (Mwenyekiti), Bi. Mary Mabuga (Makamu Mwenyekiti), Bw. Sigu Maganda (Mjumbe), Bw. Clement Bujiku (Mjumbe) na Bw. Charles Lujiga.
 
Waziri Mkuu ambaye aliwasili mkoani humo leo asubuhi, alikwenda kwanza kukagua kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha JOC na kisha kurejea ukumbini kuendelea na kikao cha wadau wa pamba ambacho kimeshirikisha wakuu wa mikoa 16, wabunge, ma-RAS, wakuu wa wilaya, wakulima, wanunuzi wa pamba na wenye viwanda.
 
Waziri Mkuu ameondoka Shinyanga kuelekea Ruvuma ambako atakuwa na ziara ya siku moja.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.