Kama inavyoeleweka kila
tarehe 3 Desemba ya kila mwaka jamii ya kimataifa ikiwemo Tanzania huadhimisha
siku ya watu wenye ulemavu Duniani. Kwa kutambua hilo serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na nchi ya Kuwait wamezindua Mpango wa kuwasaidia watu wenye
ulemavu nchini.
Mpango huo
utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni moja utafadhiliwa na serikali ya
Kuwait na utatekelezwa Tanzania Bara na Tanzania visiwani kwa kuyashirikisha
mashirika yasiyokuwa ya serikali na asasi za kijamii.
Akiongea wakati wa
kuzindua mpango huo leo tarehe 30, Novemba 2017, katika Chuo cha Ufundi Yombo
kwa Watu wenye Ulemavu, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama
alifafanua kuwa serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuboresha ustawi wa watu
wenye ulemavu nchini kwa kushirikiana na wadau wote.
“Ninatoa wito kwa Taasisi
za serikali na zisizo za serikali kila ziendelee kushirikiana na wizara yangu
pale wanapo ona wana nafasi kidogo katika kuwasaidia watu wenye Ulemavu nchini
ili waweze kuishi na kuhudumiwa katika shughuli zote ambazo ni haki zao kwa
mujibu wa katiba ya nchi yetu” alisema Mhagama
Mhagama aliishukuru
nchi ya Kuwait kwa dhamira yake ya kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini ambapo
wamezindua mpango huo kwa kutoa vifaa vya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika
Chuo cha Ufundi Yombo kwa Watu wenye Ulemavu.
Kwa upande wake Balozi
wa Kuwait nchini Tanzania Jassem
Al-Najem alifafanua kuwa nchi yake inatambua juhudi za serikali ya awam
ya tano katika kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na kwa kulitambua
hilo wameamua kuwa na mapango huo ili kutambua mchango wa watu wenye ulemavu.
“Leo nazindua mpango
kwa kutoa msaada wa kwanza kwa wanafunzi wenye ulemavu katika kituo hiki kwa
kusaidia viti vya maringi, magongo vifaa vya kusaidia watu wenye udhaifu wa
kusikia na miwani na fimbo kwa wasiiona,
ni matumaini yangu kuwa mpango huu utakuwa na manufaa kwa wote” alisema
Al-Najem.
Awali akiongea katika
makabidhiano ya vifaa hivyo Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Yombo kwa Watu wenye
Ulemavu, Mariam Chelangwa alieleza kuwa anashukuru kwa kuwa watu wa kwanza wa
kunufaika na mpango huo kwa kupata msaada wa vifaa vya kuwasaidia wanafunzi
ambavyo vitawasaidia kupata mafunzo bora.
Serikali imeendelea na
juhudi za kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki stahiki nchini ambapo
tangu mwaka 2004 serikali iliandaa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa
watu wenye Ulemavu, pamoja na sheria na. 9 ya mwaka 2010 inaweka msisitizo wa
haki za watu wenye ulemavu katika ajira, afya na shughuli za kiuchumi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.