Friday, December 1, 2017

BALOZI SEIF: WAISLAM IMARISHENI UADILIFU

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka Waislam nchini kote kuwa waadilifu kama alivyokuwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Amesema ni vema wakatumia wakati huu wa Maulid kutathmini mienendo ya maisha yao kwa kujiuliza kama maisha wanayoishi  yanafanana na yale aliyoishi Mtume Muhammad.

Balozi Seif ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba Mosi, 2017) alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.

“Kuna vigezo vingi mja anaweza kuvitumia wakati anapojitathmini, ambavyo ni pamoja na tabia ya Bw Mtume ya uadilifu na  wake. Tujiulize kati yetu hapa ni wangapi waadilifu na waaminifu kama alivyokuwa Bw. Mtume.”

Amesema kupungua kwa uaminifu na uadilifu ndiko kulikomfanya Rais Dkt. John Magufuli mara baada ya kuingia madarakani kuanzisha vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, hivyo wanatakiwa kumuunga mkono.


Balozi Seif amesema Waislam waka kila sababu ya kushirikiana na Rais Dkt. Magufuli katika mapambano hayo kwa sababu kupinga vitendo vya rushwa na ufisadi ni ibada kwao.

“Mtume (S.A.W) aliikemea sana rushwa na akasema kuwa amelaaniwa na Mwenyezi Mungu mwenye kutoa na kupokea rushwa na hata Yule mpiga debe. Pia tunaamini kuwa dini zote duniani zinapinga rushwa, hivyo tuiiepuke”

Pia amewaomba viongozi wa dini zote nchini waendelee kushirikiana na Seikali kwa kuhubiri  amani, utulivu na mshikamano ili kujenga umoja kwa Watanzania wote. “Siku zote mmekuwa mkitusaidia sana kupitia mahubiri yenu kwa kujenga umoja kwa Watanzania wote bila ya kujali dini zao,rangi wala kabila. Nawaomba muendelee na moyo huo.”

Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Bin Zubeiry alisema aliwaasa Watanzania wote waendelee kuidumisha na kuitunza amani kwa sababu hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana bila ya kuwepo kwa amani.

Alisema suala la kudumisha amani, kuheshimiana na kushirikiana miongoni mwa waislamu na wasiokuwa waislam limehimizwa sana katika dini ya kiislam na dini nyingine, hivyo wananchi hawana budi kuendeleza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza Sheikh Mkuu kwa uongozi wake mzuri wa  Baraza la WaislamTanzani (BAKWATA) ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na dini zote bila Ubaguzi.

Alisem serikali itaendelea kufanya kazi na dini zote na kwamba Rais Dkt. Magufuli amezipa kipaumbele shughuli za dini zote ziendelee kufanyika nchini.

Baraza hilo lilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Zubeiry, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya.

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Maji Bw. Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Nishati Bibi Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri, Bibi Stellah Ikupa Alex, Naibu Waziri wa Madini Bw. Stansilaus Nyongo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bibi Maimuna Tarishi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Bibi Shamim Khan, Mkunge wa Kibiti Bw. Ally Ungando, Mbunge wa Liwale Bw. Zubeiry Kuchauka, Mbunge wa Nachingwea Bw. Hassan Masalla, Mbunge wa Lindi Mjini, Hassan Kaunje Mbunge wa Viti Maalumu Bibi Hamida Abdallah.

Wengine ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Bruno Ngonyani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Alhikma, Kiongozi Mkuu wa Kiroho wa Dhehebu la Shia Ithnasheri, masheikh wa mikoa yote pamoja na wananchi wa Lindi pamoja na mikoa mbalimbali nchini.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.