Amani,
mshikamano, kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea ni kati ya mambo yaliyosisitizwa
na Rais wa Tanzania, Mhe.Dkt John Pombe Magufuli katika hotuba yake ya
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.
Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Miaka 58 ya Uhuru na
Miaka 57 ya Jamhuri: Uzalendo, Uwajibikaji ni Msingi wa Ujenzi wa Uchumi wa
Taifa letu”
Sherehe hizo zilizofanyika kitaifa kwa mara ya
kwanza katika Kanda ya Ziwa mkoa wa Mwanza , zimehudhuriwa na viongozi wakuu wa
kitaifa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Mhe.
Dr. Ali Mohamed Shein.
Aidha, Viongozi Wakuu Wastaafu wakiwemo Marais,
Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu ni miongoni mwa walio hudhuria sherehe hizo. Pia, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi
mbali mbali za Serikali na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini ni miongoni
mwa waalikwa walioshriki sherehe hizo.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba
leo Jumatatu Desemba 9, 2019, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli amesema Serikali imejipanga
na itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kulinda amani na utulivu.
“Mshikamano na
umoja wa Kitaifa ni nyenzo ya kufanikiwa zaidi. Serikali inawahakikishia
wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani hiyo. Kazi ya kuendeleza Taifa
sio lelemama. Viongozi na waasisi wa Taifa hili wamefanya mengi kwa mafanikio
makubwa licha ya changamoto nyingi,” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais,
katika hatua nyingine amepongeza juhudi ambazo serikali za awamu zote zilizotangulia
kuiongoza nchi hii zilizozifanya kwa mafanikio makubwa katika kuboresha nyanja za Kiuchumi na Kijamii ili kuhakikisha
nchi yetu inajitegemea, ameongeza kuwa serikali ya awam ya tano inaendelea kuboresha
na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, na nishati ya umeme kwa kuwa ni
muhimili wa ujenzi wa viwanda kwa ustawi wa uchumi wa nchi.
“Katika kipindi
cha miaka 58 ya Uhuru, Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa katika Nyanja za kiuchumi
na kijamii, wakati tunapata uhuru tulikuwa na shule za msingi 310 kwa sasa zipo
shule 17,379, shule za sekondari zilikuwa 41 na sasa hivi zipo 4,817, tulikuwa na
chuo kikuu 1 kwa sasa vipo vyuo vikuu 48”
“Tulikuwa na madaktari
wazalendo 12, Kwa sasa tunao madaktari 9,400, wahandisi wazalendo walikuwa 2 kwa
sasa wapo wahandisi 19,164 walio sajiliwa, vituo vya kutolea huduma za Afya vilikuwa 195
leo hii vipo vituo vya kutolea huduma za
Afya 7,293, Barabara za kiwango cha lami za kuunganisha mkoa na mkoa pia wilaya na
wilaya zilikuwa kilometa 360 tu, leo hii tunazo kilometa 12,679.55” Amesisitiza Mhe.Rais Magufuli.
Mhe. Rais amebainisha
kuwa katika kuhakiksha nchi inakuwa na uchumi imara serikali ya awamu ya tano
imeendelea kujenga viwanda ambapo kwa sasa tayari vimejengwa viwanda 4,000, Pia ameitaja
miradi ya maendeleo ambayo serikali ya awamu ya tano inaendelea kuitekeleza kwa
lengo la kuimarisha ustawi wa uchumi kuwa ni pamoja na kujenga reli ya kisasa,
kujenga bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za Umeme, Kujenga
viwanja vya ndege 11, kununua ndege 11
na kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania.
Aidha, katika
kusherehekea Maadhinisho ya siku ya Uhuru, Mhe.Rais wa Dkt, Magufuli, ametangaza
kuwaachia huru wafungwa 5,533 ambao walikuwa wamefungwa katika Magereza
mbalimbali nchini.
"Nilitembelea Magereza
nikashuhudia kuna mlundikano wa wafungwa, mpaka leo kuna Wafungwa 17,547 na
Mahabusu 18,256, hii ni idadi kubwa, kwa hao wafungwa kuna baadhi wamefungwa kwa
makosa madogo, " amesema Mhe. Rais Magufuli
"Hali ya pale Butimba
ilinihuzunisha sana, kwa kutambua Dini zote zinatufundisha tusamehe na kuamini
wafungwa wengi wanajutia makosa yao, kwa mujibu wa Mamlaka niliyonayo ya Kikatiba, nimewasamehe
wafungwa 5,533" ameongeza Mhe. Rais
Magufuli
Mhe.Rais, Magufuli akimalizia hotuba yake hakusita
kuipongeza Kamati ya Maandalizi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kuratibu
Sherehe hizo, Kupitia Idara ya Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa, ambapo
amempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, kwa kumsaidia vyema Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa wa sherehe hizo. Pia
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Bi.Dorothy
Mwaluko ambaye amekuwa akifuatilia maandalizi ya kila siku ya sherehe hizo
kupitia Idara ya Maadhimisho na sherehe za Kitaifa.
Awali Sherehe hizo zilipambwa na Gwaride la askari wa majeshi ya Ulinzi na
Usalama nchini pamoja na onesho maalum
la pamoja lilojumuisha Sungusungu wapatao
1200, sambamba na makundi manne ya manju
na ngoma ya mang’ombe ga Kijiji.
Aidha Vikundi vya burudani vya Wasanii pamoja na wanamziki wa Kizazi kipya na ngoma za asili kutoka mikoa ya Mwanza,
Kagera na Mara wametumbuiza na kuburudisha wananchi waliohudhuria.
Katika sherehe hizo, kabla ya kuhitimisha hotuba
yake Mhe. Rais, alimkaribisha Rais wa Zanzibar, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu
wa staafu na Viongozi wa vyama vya siasa nchini. Katika salamu zao viongozi hao
kwa pamoja wamesisitiza, Amani,
mshikamano, kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kuwa na uchumi imara kama
ambavyo Mhe. Rais ameweza kuimarisha uchumi huo kwa kipindi hiki cha utawala
wake.
MWISHO
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.