Ujumbe wa Programu ya
Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Kilimo (IFAD), umesema utaendelea kuwekeza katika uzalishaji na
upatikanaji wa mbegu bora ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Kauli hiyo imetolewa na
kiongozi wa ujumbe huo, Bi. Nester Mashingaidze, alipozungumza na wakulima wa
Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, alipokuwa akikagua utekelezaji wa programu
hiyo inayolenga kuongeza uzalishaji wa mahindi, alizeti, maharage na mimea
jamii ya mikunde.
“Tunalenga kuongeza
upatikanaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na taasisi kama TARI, ASA, na TOSCI
ili kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa wakati,” alisema Bi. Mashingaidze.
Kwa upande wake, Bw. Salum
Mwinjaka – Mratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema AFDP
inatekelezwa katika mikoa 11 ya Tanzania Bara pamoja na visiwa vya Unguja na
Pemba. Alibainisha kuwa programu inajikita katika kilimo kinachohimili
mabadiliko ya tabianchi, lishe na usawa wa kijinsia.
Naye, Mhandisi Enock Nyanda
kutoka TAMISEMI, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wizara za
kisekta kufikisha huduma kwa wananchi kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo.
Wakulima waliopokea mafunzo
kutoka kwenye programu hiyo wamesema imewasaidia kuachana na kilimo cha mazoea
na kuhamia kwenye kilimo chenye tija kwa kutumia mbegu bora na za kisasa.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.