KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wadau kushirikiana na
Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya kuenea
kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Amesema ulaji usio faa na
mitindo mibaya ya maisha vimechangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya
kuambukiza jambo linalohatarisha maendeleo ya Taifa.
Dkt. Yonazi ameyasema hayo
jijini Dar es salaam leo katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe
unaoendelea katika kituo cha mikutano cha APC Bunju.
Dkt. Yonazi amesema tafiti zinaonesha kuwa
uzito uliozidi na uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya
kuambukiza yakiwemo kisukari, moyo, figo
na baadhi ya saratani.
“Napenda kukumbusha wadau,
taasisi na wataalam kushirikiana na serikali kufanya tafiti zitakazosaidia
kuleta majibu ya changamoto za lishe, pamoja na kusaidia watu kubadili tabia za
ulaji na mtindo wa maisha ili kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza
yanayohusiana na ulaji usiofaa na ambayo ni tishio kwa Taifa letu,”alisema Dkt.
Yonazi
Dkt.Yonazi ameongeza kuwa Takwimu zinaonesha licha ya hali ya lishe nchini kuendelea
kuimarika bado kuna changamoto hususani kwenye uzito uliozidi na kiriba tumbo
hii kutokana maendeleo tunayoyapata na mabadiliko ya mtindo wa maisha
hususani ulaji usiofaa hivyo jitihada za
pamoja kati ya wadau na serikali zinahitajika ili kukabiliana na tatizo hili.
Akizungumza kuhusu mkutano huo
Dkt. Yonazi amesema lengo ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji
wa afua za lishe kwa kipindi cha Mwaka wa Tatu 2024/2025 katika maeneo mahsusi
yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).
Vilevile amesema mkutano huo
unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika,
changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki
cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26.
Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi
mkutano huo unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe
miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
“Uwepo wenu hapa, ni
uthibitisho tosha wa ushirikiano mlionao na utayari wenu katika kuhamasisha
uboreshaji wa hali ya lishe kwa Watanzania, hususani makundi yanayoathirika
zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake
wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi,”amesema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi amewashukuru wadau wote walitoa mchango wa fedha na
ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na
amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau ili
kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.