Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe.
William Lukuvi, amewahakikishia Watanzania kuwa dawa za kufubaza makali ya
Virusi vya UKIMWI (ARVs) zinapatikana kwa asilimia 100 nchini na zinatolewa
bila malipo kwa watu wote wanaoishi na VVU (WAVIU).
Amesema
hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambapo kwa mwaka 2025 yamefanyika chini
ya kaulimbiu: “Imarisha Mwitikio, Tokomeza UKIMWI”.
Waziri Lukuvi amesema upatikanaji wa dawa hizo
umeendelea kuimarika, huku idadi ya WAVIU wanaotumia Dawa za ARV ikiongezeka
kutoka asilimia 98 mwaka 2024 hadi asilimia 98.5 mwaka 2025, hatua inayochochea
kupungua kwa athari za UKIMWI na kuboresha afya za wananchi.
Aidha, Waziri Lukuvi amebainisha kuwa Serikali
imeongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa WAVIU ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI nchini. Vituo hivyo
vimeongezeka kutoka vituo 7,805 mwaka 2024 hadi vituo 8,203 mwaka 2025.
Ameongeza kuwa, huduma za ufuatiliaji wa
matibabu kwa WAVIU zinaendelea kuimarishwa, huku serikali ikiboresha
upatikanaji wa huduma za maabara kwa kuongeza mashine za kupima wingi wa VVU
mwilini. Kwa sasa, zipo mashine kubwa 50 kutoka 43 mwaka 2024, na mashine ndogo
127, hivyo kufanya kuwa na jumla ya mashine 177 zinazoendelea kutoa huduma
nchini.
Katika tamko lake, Waziri Lukuvi amesisitiza
kuwa Siku ya UKIMWI Duniani ni muhimu kwa kutathmini hali na mwelekeo wa
kudhibiti VVU na UKIMWI nchini na kimataifa, kuhamasisha jamii kushiriki
kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya, kuwakumbuka waliopoteza
maisha kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, na kuwaenzi watu wanaoishi na VVU pamoja
na yatima wanaotokana na athari za UKIMWI.
Amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa ajenda ya kudhibiti UKIMWI inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi zote za uongozi na utungaji sera


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.