Imeelezwa kuwa, jitihada za
kuendelea kuokoa maisha baada ya ajali ya mgodi kutokea eneo la Nyandolwa Mkoani
Shinyanga zinaendelea usiku na mchana ambapo hadi kufikia Leo Agosti 21,2025
mafundi 10 kati ya 25 waliokuwa wamekwama chini ya ardhi wameokolewa, huku
wanne wakiwa hai, mmoja kati yao akifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa
hospitalini, na saba wakikutwa wamefariki dunia.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini
kwake Mkoani humo ambapo amethibitisha taarifa hizo na kusema kuwa tukio hilo
lilitokea takribani siku 10 zilizopita, likisababisha shughuli za uokoaji
kuendelea kwa muda mrefu katika mazingira magumu.
Amesema ajali hiyo ilitokea
baada ya ardhi kutitia ghafla na kusababisha kifusi kuporomoka katika mashimo
(maduara) matatu tofauti yaliyokuwa yakikarabatiwa na mafundi ndani ya mgodi
huo, unaomilikiwa na kikundi cha Wachapakazi chini ya leseni ya uchimbaji
mdogo.
"Tunaendelea kushirikiana
na taasisi mbalimbali kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama. Hili ni
tukio la huzuni kubwa kwa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla," amesema Mhe.
Mhita.
Kwa upande wake, Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko, ametoa
wito kwa timu ya uokoaji kuongeza kasi na juhudi katika shughuli za uokoaji,
akisisitiza kuwa kila sekunde ina maana katika kuokoa maisha ya waliobaki chini
ya kifusi.
“Natoa pongezi kwa kikosi
kizima cha uokoaji kwa moyo wao wa kujitolea, lakini ni muhimu sasa kuongeza
kasi bila kuhatarisha usalama wa waokoaji wenyewe,” amesema Dkt. Kilabuko.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amefika eneo la tukio na kutoa salamu za pole
kwa familia za marehemu na wote walioathirika na ajali hiyo. Ametoa rai kwa
waokoaji kuendelea kuwa na umakini mkubwa na kutanguliza usalama katika
operesheni ya uokoaji.
“Hii ni ajali ya kusikitisha
mno. Tume ya Madini inatoa pole kwa familia za wahanga, na tutaendelea
kufuatilia kwa karibu kuhakikisha taratibu zote za usalama katika migodi
zinasimamiwa ipasavyo ili kuepusha ajali kama hizi siku za usoni,” amesema Dkt.
Lekashingo.
Aliongezea kuwa, Timu za
uokoaji zinajumuisha maafisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi, Tume
ya Madini, Wizara ya Madini, wachimbaji wenzao, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,
Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Shinyanga, ambao wote wanaendelea kushirikiana
kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama.
Hadi sasa, juhudi za uokoaji
bado zinaendelea katika eneo hilo la mgodi, huku matumaini yakiwa bado
hayajapotea kwa familia na ndugu wa mafundi waliobaki chini ya kifusi. Serikali
imeahidi kutoa usaidizi wa karibu kwa waathirika na kuhakikisha uchunguzi wa
kina unafanyika kubaini chanzo cha ajali hiyo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.