Serikali imeridhishwa na
maandalizi ya miundombinu ya michezo Zanzibar kuelekea Mashindano ya Mataifa ya
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), huku Uwanja wa Amaan Complex ukitajwa
kuwa katika viwango vya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu
wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, mara baada
ya kuongoza Kamati ya Makatibu Wakuu kukagua maandalizi ya CHAN katika visiwa
vya Zanzibar.
“Tumejionea hali halisi ya miundombinu, hasa
Uwanja wa Amaan. Uko katika viwango vya kimataifa, na tunaamini Zanzibar ipo
tayari kuwa sehemu ya mashindano haya muhimu kwa bara letu la Afrika,” amesema
Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi alieleza
kuwa hatua hiyo inaonesha utayari wa Taifa kuandaa mashindano ya kimataifa,
huku akisisitiza kuwa mashindano ya CHAN ni fursa kubwa ya kuimarisha michezo
na kukuza uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (SMZ), Mhe. Fatma Hamad Rajab,
alieleza kuwa Uwanja wa Aman Complex tayari umekidhi vigezo vyote vinavyohitajika
na Zanzibar iko tayari kuwapokea wachezaji, mashabiki na wageni kutoka mataifa
mbalimbali.
Kamati hiyo ya Makatibu Wakuu
inafanya ziara katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani ili kukagua
maandalizi ya CHAN na AFCON 2027.
Mashindano ya CHAN
yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 2 Agosti 2025 yakihusisha wachezaji wanaocheza
ligi za ndani kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.