Thursday, November 30, 2017

WAZIRI MKUU ATAKA UDAHILI ELIMU YA JUU UONGEZWE

                 
 *Ashuhudia mkewe akitunikiwa Shahada ya Uzamili OUT


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uchumi wa kati na wa viwanda hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23.

“Hivi sasa, kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni asilimia nne. Kiwango hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, ambao licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda mrefu, wamefikia asilimia saba,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Singida na mikoa jirani waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida,

Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba karibu nchi zote washirika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu na kwa maana hiyo zimeizidi Tanzania.

Amesema, Chuo Kikuu pekee chenye kanuni za udahili (open entry), chenye kufundisha, kujisomea na hata kutathmini maendeleo ya wanafunzi (assessment on demand) ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 

“Naungana na Mheshimiwa Rais kuwaomba mtumie fursa hiyo, kuisaidia nchi yetu kuongeza kiwango cha udahili wa wananchi wake katika elimu ya juu, kwa haraka na kasi itakayotuwezesha kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati na wa viwanda, ifikapo 2025.”

“Kwa kushirikiana na Baraza la Elimu Masafa Afrika (African Council for Distance Education (ACDE), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na hata vyuo vikuu vingine ndani na nje ya nchi yetu, ongezeni ubora na panueni wigo wa udahili, kwenye programu za sasa na zingine mtakazoziongeza,” alisisitiza. 

Aliwataka wahakikishe kuwa siku zote, mfumo wao wa utoaji elimu, yaani elimu huria na masafa (Open and Distance Learning (ODL) unajitanabaisha kama mfumo wa kisasa na mahiri katika kutoa elimu na mafunzo yenye ubora unaokubalika na kutambulika kitaifa, kikanda na kimataifa. 


“Kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendelelo na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu, ijikite katika maeneo yaliyoainishwa, chini ya mwanvuli wa kaulimbiu ya Chuo “elimu bora na nafuu kwa wote.”

Waziri Mkuu amesema katika kutambua umuhimu wa elimu huria na masafa kwa maendeleo ya elimu hapa nchini, Serikali inaunga mkono azma ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalumu kwa ajili ya kuimarisha Mfumo wa Elimu Huria na Masafa.

“Kupitia hafla hii, ninaagiza dawati kama hilo lianzishwe pia katika Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zao za ithibati zinazingatia na kukidhi matakwa ya viwango vya mfumo wa Elimu Huria na Masafa,” alisema Waziri Mkuu. 

“Ninaungana na Waziri mwenye dhamana kuagiza kuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) washirikiane na TCU na NACTE kuhakikisha kuwa taratibu za ithibati zinatekeleza azma ya Serikali kama ilivyoainishwa kwenye Sera ya Elimu ya Mafunzo 2014, hususan juu ya suala la kuwatambua watu waliopata ujuzi bila kupitia mfumo (rasmi) wa elimu na mafunzo,” alisisitiza.

Waziri Mkuu pia alishuhudia mke wake, Mary Majaliwa akitunukiwa Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Masters’ of Education in Administration, Planning and Policy Studies) na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Waziri Mstaafu, Mizengo P. Pinda.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.