Sunday, November 5, 2017

WATAKAOKWAMISHA MALIPO YA KOROSHO KUKIONA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote watakaokwamisha malipo ya wakulima wa zao la korosho.

“Hatutamuacha mtu yeyote atakayesababisha wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao. Tutawakamata wote na kuwachukulia hatua stahiki.”

Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mbekenyera wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu alisema wakulima hao ni lazima walipwe fedha zao kwa wakati na asitokee mtu wa kuzitamani fedha hizo.

“Mkulima amelima mikorosho mwenyewe, ameokotoa na kukodoa mwenyewe wao wamepewa dhamana ya kuziuza, hivyo wahakikishe wanawapelekea fedha zao na wala wasizitamani.”

Pia Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya Ushirika vya Msingi wahakikishe mkulima hakosi sh. 3,500 katika kilo moja ya korosho atakayoiuza baada ya kukatwa michango.

Alisema bei ya juu ya korosho katika minada ya mkoa wa Lindi sh. ni 3,970 na ya chini sh. 3,800. “Vyovyote itakavyokuwa mkulima hawezi kukosa sh. 3,500, viongozi wa AMCOS mnisikie.”

 Waziri Mkuu alisema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa bei ya zao la korosho pamoja na kupungua kwa makato ya mkulima ambapo kwa sasa hayazidi sh. 300 katika kilo moja ya korosho.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.