Friday, November 24, 2017

MAJALIWA: TANESCO KAWAHUDUMIENI WANANCHI VIJIJINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liwafuate wananchi walioko katika vijiji vinavyotarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuwahudumia.

Amesema Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nicety hiyo nchini, hivyo ni vema wakawatembelea wananchi katika maeneo yao na kuwahudumia huko huko.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Novemba 24, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo Tunduru, ambapo aliwasisitiza watumishi wa TANESCO kutokaa maofisini na badala yake wakawahudumie wananchi katika vijiji vyao.

Alisema katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza miradi ya kusambaza umeme vijini kupia REA, TANESCO wanatakiwa kwenda vijijini na kuwaandikisha wananchi wanaohitaji huduma hiyo pamoja na kufungua vituo vya muda vya malipo.

Waziri Mkuu alisema hatua hiyo itawapunguzia wananchi gharama za kusafiri hadi kwenye makao makuu ya wilaya kufuata huduma mbalimbali ikiwemo ya kulipia gharama za kuunganishiwa umeme katika nyumba zao.

Alisema Serikali imedhamiria kusambaza huduma ya nishati ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vya wilaya ya Tunduru ambapo wananchi hao wataunganishiwa umeme huo kwa gharama ya sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu aliesema  wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba  lengo la Serikali ya awamu ta tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa.
Waziri Mkuu alisema huduma hiyo ni muhimu kwani mbali ya kutumika katika matumizi ya majumbani, pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati, shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.
Awali Waziri Mkuu alitembea na kukagua shughuli za ujenzi wa mradi wa kituo cha afya kinachojengwa katika eneo la Nakayaya wilayani Tunduru pamoja na kukagua ghala la kuhijfadhia korosho na kisha kupokea taarifa ya kiwanda cha kubangulia korosho cha Korosho Afrocan Limited.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.